Menu
RSS

Mambo haya hatari katika elimu nchini Featured

KATIKA kipindi cha hivi karibuni vichwa vya watanznia viliweza kukorogwa baada ya kuwepo kwa mkanganyiko wa kauli kuhusu mfumo mpya wa usahihishaji ama wa upangaji wa madaraja kwa wanafunzi wa Sekondari.

Hali hiyo imewatia wasiwasi mkubwa wadau wa elimu na kuielezea kama sehemu ya kuvuruga na kudidimiza kiwango cha elimu nchini kwa sababu wizara nyeti kama hiyo imekuwa ikiyumba katika utoaji wa kauli zake.

Itakumbukwa kwamba Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome alitangaza alama zinaonesha kwamba

 

A=75-100,B+=60-74,B=50-59,C=40-49,D=30-39,E=20-29, na F=0-19,

huku alama endelevu upimaji wanafunzi shuleni yani Continuous Assessment (AC) ikiwa ni 40 huku mtihani wa mwisho ukichangia alama 60.

Na kabla ya Serikali kutangaza alama hizo mpya wizara yenye dhamana na masuala ya Elimu nchini, iliunda Kamati iliyopewa jukumu maalum la kufanya uchunguzi na kuja na mapendekezo ya viwango vipya vya ufaulu na utaratibu wa CA.

Kwa hakika kamati hiyo ilifanya kazi hiyo na kuwasilisha ripoti yake wizarani Septemba mwaka huu ikiainisha kama ifuatavyo: A=80-100,B=70-79,C=50-59,D=40-49,E=35-39 na F=0-34 huku wakitaka CA iwe alama 25.

Hali hii inatajwa na wanazuoni kwamba kwa alama hizo za ufauli Tanzania inaweza kuwa nchi ya kwanza duniani kwa kuwa na alama za chini zaidi za ufaulu.

Aidha jambo lingine ambalo limewachanganya zaidi wananchi na wadau wa elimu ni ile ya kufuta daraja sifuri na kuongeza daraja la tano ama Five.

Lakini Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, bungeni mjini Dodoma, naye alitoa kauli yake akisema kwamba daraja sifuri halijafutwa. 

Ni jambo la kushanga umma hasa katika mustakabali mzima wa ukuzaji na uboreshaji wa kiwango cha elimu nchini kuona kwambna kumekuwan na kauli za kupishana kuhusu jambo hilo.

Ni vizuri masuala hayo ya kitaalam yasiingizwe siasa kwani, ni dhahiri kwamba taifa litapata wataalam ambao hawataleta tija nchini na hatakuwa na ushindani na wenzao na hivyo taifa kuendelea kuwa nyuma.

Hakika hali hii pia itafanya Tanzania isiweze kuwa na watu wenye kugundua vitu na badala yake itakuwa ni watu wanaosoma kwa lengo la kupata ajira na kupokesha mshahara ili maisha yaende.

Kimsingi elimu ndiyo inayofanya taifa lolote lile liwe na maendeleo kwa sababu ya kuwepo kwa wataalama waliobobea, taifa kama Singapore, limeweza kupiga hatua kubwa katika masuala ya maendeleo na teknolojia na kuwa miongoni mwa mataifa yenye kuzalisha bidhaa mbalimbali ni kwa sababu ya kusimama vema katika elimu.

Hivyo Serikali isifanya mzaa na suala la elimu. Itakumbukwa kwamba mwaka huu wanafunzi wa Darasa la saba wamefanya mitihani yao na matokeo yametoka, lakini bado wadau wa elimu wanaendelea kusema kwamba mfumo wa elimu nchini bado hauna matunda ya moja kwa moja katika utoaji wa elimu bora kwa wananchi.

Aidha wadau hao pamoja na mambo mengine wamesema Serikali inatakiwa kuhakikisha inaboresha mfumo wa elimu ili kuwafanya watoto wa maskini waweze kupata elimu bora inayolingana na wanayopata watoto wa vigogo na watu wenye uwezo wanaosomeshwa nje ya nchi.

Kutokana na kutowepo kwa mfumo madhubuti katika sekta ya elimu, taifa linashindwa kupata wataalam wazuri katika kada mbalimbali na badala yake inategemea watu waliosoma nje ndio waje kuwa viongozi ama wataalama kutokana na elimu nzuri waliyoipata nje.

Hali ya watoto wa wakubwa na wenye kipato kikubwa kusoma nje kunadhihirisha wazi kwamba elimu ya Tanzania sio bora na hivyo kutaka watoto wao wasome nje ya nchi ili wapate elimu bora na badaye kuwa viongozi wa nchi.

Kama Tanzania itasimama vema na kutoa elimu bora tutatengeneza hata watu wa nje kuleta watoto wao waje kusoma Tanzania kwa sababu elimu itakuwa bora.

Lakini kama kila mmoja anatamani mtoto wake akasome nje ama shule maalum za International hakika taifa hili litafika pabaya sana, serikali ijipange ifanye maboresho na usimamizi wa karibu katika kutekeleza yale yaliyoamuriwa mambo yatakuwa mazuri.

Nchi kama za Kenya na Uganda ambako Watanzania wengi wanawapeleka watoto wao wakasome huko wamefanya mambo mazuri ya kuwa na mfumo bora ya elimu ikiwemo malipo na posho nzuri kwa walimu jambo linalofanya elimu kuimarika.

 

MPANGO WA BIG RESULT NOW 

Kuhusu Mpango wa Serikali wa kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika mpango wake wa Big Result Now, mpango huo unaweza kuwa wa kisiasa endapo mfumo wenyewe wa elimu hautaboreshwa vema.

Ni vema walimu wakaboreshewa maslahi yao na kutengeneza mifumo mizuri ya elimu hasa suala la miundombinu ili mpango huo uweze kutekelezwa vema.

Sio rahisi kuutekeleza vema mpango huo kama shule zingine wanafunzi wakiendelea kukaa chini huku zikiwa na mwalimu mmoja ama wawili jambo linaloweza kukwamisha mpango huo.

 

SHULE ZA KATA

Haya shule nyingi za Sekondari za Kata zilizoanzishwa katika mpango wa kila Kata kuwa na Sekondari yake, nyingi hali yake katika miundombinu na hata walimu bado hazijasimama vema hivyo zinaweza sisifanye vizuri katika utekelezaji wa mpango wa Big Result Now.

Tuhakikishe walimu wamelipwa madai yao, na wana malupulupu ya kutosha yaliyo bora yatakayowafanya wafanye kazi kwa moyo wa dhati, kwani wapo walimu kutoka Kenya na Uganda wanaofundisha Sekondari hapa nchini wakilipwa vema na kupewa kila kitu na ndiyo maana shule za binafsi zinafanya vizuri. 

Kama haya yatakuwa sawa kabisa hakika kuingiza mpango huo itakuwa wakati muafaka, lakini kama bado shida ipo hii ni sawa na bure.

RUSHWA KATIKA ELIMU

Suala la rushwa isipoangaliwa linaweza likachangia kutopatikana kwa matokeo makubwa kutokana na kuwepo kwa watendaji wasio waaminifu wanaodiriki kuuza mitihani ya taifa ili kujipatia chochote.

Katika ripoti yake Shirika la Transparency International linaonesha kuwa vitendo vya rushwa vimekithiri kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.

Ripoti hiyo pia pamoja na mambo mengine imeonesha kuwepo kwa vitendo vya ufisadi ambavyo vimeshamiri zaidi katika nchi ya Tanzania na Uganda ambapo takribani asilimia 70 ya watu wanaamini kushamiri kwa ufisadi.

Kwa mujibu wa Transparency International, sekta ya elimu ni miongoni mwa maendeo yenye kukabiliwa na vitendo vya rushwa kwa kiwango kikubwa.

Hivyo suala la watu kufaulishwa katika mitihani yao, kwa mtindo wa kutoa rushwa, iwe ya ngono ama fedha ni mambo mabaya yanayoweza kurudisha nyuma juhudi za serikali katika kuboresha elimu.

Na hata wataalama watakaopatikana hawatakuwa watu wa ukweli ambao taifa linaweza kuwategemea, na hali hii inaweza kuchangia majanga mengi kama vile ujenzi wa majengo yasiyo na viwango na barabara ambazo hubomoka baada ya muda mfupi.

Hii ni hali ya hatari ambayo Serikali inatakiwa kuiangalia kwa undani na kuchukua hatua madhubuti katika kunusuri elimu nchini.

Last modified onMonday, 12 January 2015 07:56
back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.