Menu
RSS

Riba kwenye Taasisi za fedha

 

Na Dk. Felician Kilahama

Awali ya yote inanibidi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema mengi anayotutendea katika maisha yetu. Vilevile, nikiri kwamba mimi sina utaalam wa masuala ya fedha au shughuli za kiuchumi.

Uelewa wangu ni mdogo kiasi kwamba yote nitakayoyasema hapa niombe radhi pale nitakapokuwa nimekosea. Inawezekana msomaji wa Makala hii akasema kuwa: iwapo huelewi au huna elimu ya kutosha juu ya masuala ya fedha na uchumi kwa nini usiulize ukaeleimishwa na wenye elimu hiyo? Mtazasamo wa namna hiyo ni sahihi hasa kwa yeyote anbaye nia yake ni kujifunza kwa faida yake binafsi.

Naelewa wako wengi wenye hali kama yangu na pengine wanahitaji kuelimishwa kwa namna moja au nyingine ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika harakati za kujiletea maendeleo endelevu kama mtu binafsi, familia au hata kijamii.

Nimeonelea ni vizuri niyatoe mawazo yangu kupitia fursa hii ili atakayeguswa na jambo hili aweze kunielimisha na kwa kufanya hivyo inawezekana tukanufaika wengi kutokana na ukweli kwamba “elimu haina mwisho”.  Vilevile, nashukuru Uongozi wa gazeti hili kwa kukubali kuchapisha Makala hii kwa faida yetu sote.

Natambua kwamba binadamu hulazimika kuchukua hatua iwapo ataona kuna changamoto inayomkabili katika maisha ya kila siku. Mfano, kama kuna misitu au  miti ya kutosha siyo rahisi watu wengi, kwa utashi wao wenyewe, wakaamua kupanda miti. Iwapo itatokea watafanya hivyo msukumo wa ziada lazima utoke kwa wenye mamlaka juu yao na kwa kutumia nguvu ya sheria.

Kwa upande mwingine, iwapo hakuna miti na hali inakuwa ngumu kimaisha mfano kushindwa kupika chakula kwa sababu upatikanaji kuni au mkaa ni shida; haishangazi kuona wengi wanachukua hatua za kupanda miti ili hatimaye wapate chanzo cha nishati ya kupikia.  Hali ndivyo ilivyo kwa suala hili ninalolieleza hapa.

Kabala sijapata shida ya kujihusisha na vyombo vya fedha hususani benki; nilikuwa siwazii suala la kukopa au riba zikoje. Lakini baada ya changamoto ya mahitaji ya fedha kutugusa kifamilia ndipo hali ya kufikiri namna ya kujikwamua ikapelekea kuwaza kukopa katika taasisi za fedha hasa benki.

Hatua ya kwanza ilikuwa kupata maelezo kutoka benki ni jinsi gani mkopo unavyopatikana iwapo mtu anahitaji kukopa? Ni vigezo gani vinatumika kuweza kumpatia mteja mkopo anaouhitaji? Maelekezo ikawa ni lazima anayetaka kukopa awe na akaunti kwenye benki anayotaka kupata mkopo.

Vilevile, ni lazima afanye mchanganua wa kina namna mkopo utakavyotumika; kuonyesha jinsi utakavyorejeshwa na kuwepo ushahidi wa kuridhisha wa mali isiyohamishika kama shamba au nyumba na hatimiliki.

Shamba au nyumba  pamoja na hatimiliki ndiyo rasilimali ambazo benki itazitumia kama dhamana kwa mkopo. Kadhalika rasilimali hizo thamani yake (value of fixed assets) idhibitishwe kwa taarifa ya Mthamini mali anayeaminiwa na benki husika na atokane na kampuni au taasisi yenye makubaliano na benki kufanya kazi hiyo. Gharama ya kuthamini rasilimali hizo ni jukumu la mkopaji.

Kabla ya kupata mkopo sharti hili lazima litimizwe hata kama utapata mkopo au laa. Huu unakuwa mwanzo kwa mkopaji kupata maumivu ya  aina yake: huna fedha unataka ukope kakini masharti ya kukopa yanakupelekea kuanza kutumia fedha ambazo huna unazipata wapi?.

Ukiyatimiza hayo benki inakuwa iko tayari kujadiliana nawe na ikiridhika na mawasilisho mkopaji anapata fursa ya kukopeshwa kwa masharti ya kurejesha mkopo pamoja na riba kwa muda mtakaokubaliana. Baada ya kupata mkopo hapo ndipo maumivu zaidi yanapoingia kulingana na riba inayotozwa na jinsi ya kuurejesha mkopo.

Kwa waliowengi siyo rahisi kupata mkopo toka benki maana ni vigumu kukidhi masharti yanayotolewa kwa mkopaji. Vilevile, riba inayoambatana na mkopo ni kubwa sana kiasi cha kuwaumiza wakopaji kutokana na jinsi inavyokokotolewa katika mahesabu ya kila siku.

Kwa uelewa wangu mdogo nilitegemea kama nimekopa shilingi milioni 12 kwa kiwango cha riba ya asilimia 20 kwa mwaka na kulipa mkopo kwa muda wa miaka mitatu (miezi 36) ningetegea benki kufanya biashara kifaida lakini pia na mimi mkopaji kuwa na unafuu kidogo.

Kwa mfano nikirejesha kila mwaka shilingi milioni nne (4) pamoja riba isiyozidi shilingi milioni moja (jumla milioni tano) kwa miaka mitatu ningelipa milioni 15. Kwa hali hiyo benki inapata faida na mkopaji ananufaika kwa kutatua changamoto iliyokuwepo au pia kujiongezea kipato kupitia uwekezaji.

Kiuhaliasia mambo ni tofauti sana na matarajio ya mkopaji na ndipo maumivu yanapowakumba wakopaji. Hata kama haujakopa hali hii itakugusa kwa namna moja au nyingine kwa kusababisha gharama za maisha kupanda mara kwa mara (i.e. tunaponunua huduma mbalimbali na bidhaa kwenye soko unasikia bei zimepanda).

Katika hali ya kibenki unapokopa shilingi milioni 12 kwa miaka mitatu unajikuta unalipa zaidi ya shilingi milioni 17 (mkopaji anaizalishia benki shilingi milioni tano kwa miaka mitatu). Vilevile, kwa aliyekopa shilingi milioni 30 kutoka benki mojawapo hapa nchini na kwa kipindi cha miaka mitatu akajikuta analipa shilingi milioni 48 ikiwa ni marejesho ya mkopo na riba.

Cha kushangaza ni kwamba mkopaji analipa liwango hichohicho cha marehesho tangu mwamzao hadi mwisho. Nilitegemea kwa hali ya kawaida nikirejesha mkopo na riba baada ya mwaka nianze kulipa kiwango pungufu na baada ya miaka miwili nilipe kiwango pungufu

zaidi kwa sababu sehemukubwa ya mkopo na riba vimerejeshwa. Lakini kiwango cha marejesho kinabaki kilikile mwanzo hadi mwisho kulikoni?

Mfano mwingine ni aliyekopa shilingi milioni 100 na kutakiwa kurejesha mkopo huo ndani ya miaka miwili. Alianza kurejesha mkopo kwa kulipa shilingi zaidi ya milioni tano na laki saba kila mwezi. Atakapomaliza miaka miwili marejesho yaweyamemalizika na kwa hali hiyo atalipa benki si chini ya shilingi milioni 137.

 

Hii inamaana kwamba ndani ya kipindi hicho cha miaka miwili awe amelipa mkopo (shilingi milioni 100) na tozo ya riba (zaidi ya shilingi milioni 37). Hebu angalia kwa kipindi hicho kifupi mkopeshaji (bank) inapata shilingi milioni 37 kutokana na uwezo wake wa kumpatia mkopaji (mhitaji) shilingi milioni 100.

Iwapo mkopaji atayamudu mazingira magumu ya kibenki lazima awe na nafasi nzuri ya kutoa huduma au kufanya biashara ambayo itamwingizia faida ya kutosha. Mathalani mifano hiyo niliyoitoa biashara au huduma husika viweze kutoa tija ya kutosha kiasi kwamba kila shilingi aliyokopa na kuitumia imzalishie takribani senti hansini: yaani apate shilingi mia moja hamsini. Kinyume cha hapa atakuwa anafanya kazi isiyolipa hivyo hataweza kulipa mkopo na wakati huo atashindwa kujiendeleza.

Hali hiyo inamaanisha kwamba kwa muda wa miaka miwili mkopaji aweze kupata angalau shilingi milioni 150 ili alipe deni na riba na kuweza kupata faida pengine akapanua shughuli zake.  Katika haya yote mwisho wa siku anayeumia ni mlaji au mtumiaji wa huduma zinazotolewa na mhusika (mkopaji).

Hii ndiyo dhana kwamba aliye nacho ataongezewa na mwenye kidogo hata hicho kidogo atanyanganywa. Hivyo walionacho watazidi kutanua (mabenki kugawana mabilioni ya shilingi kama faida) wakati wakopaji wengine wakifilisiwa kwa kushindwa kurejesha mikopo waliochukua kwa kudhani wangejikwamua kutoka kwenye hali ya umaskini na kupiga hatua mbele.

Serikali ya awamu ya tano imedhamira kutuingiza kwenye uchumi wa viwanda. Hii ni nia njema maana kupitia shughuli za viwanda mkulina atanufaika kwa kuona mazao yake yananunuliwa na kusindikwa (hasa mazao yanayoharibika haraka kama matunda).

Wafugaji nao wataweza kupata soko la uhakika kwa bidhaa zitokanazo na mifugo. Pamoja na nia hiyo nzuri ya Serikali iliyopo madarakani ya kutaka kuinua uchumi wetu kwa nchi; mtu mmoja mmoja au familia na jamii; ipo changamoto kwamba baadhi ya wawekezaji wanapata mitaji yao kutoka benki na vyombo vingine vya fedha.

Iwapo hali ya riba ndiyo hiyo (gharama kubwa sana) wanapokopa na kuwekeza, bidhaa/huduma zitakazozalishwa zitauzwa kwa bei kubwa kuliko uwezo wa wanunuzi kwa maana wengi kipato kiko chini.

Hata kama mtu ameajiriwa bado viwango vya mishara viko chini kumwezesha kumudu gharama za maisha ya kila siku. Kwa hali hiyo ni dhahiri kwamba riba kwenye mikopo zikiendelea kuwa kubwa na wakati huo tunahitaji kupata huduma na bidhaa kwa bei nafuu; itabaki kuwa kitendawili kisichoteguliwa mwishowake ni kilio kwa watu wa kawaida wenye kipato cha chini.

 

Kimsingi mwenye madhara ni mnunuzi wa bidhaa au mtumiaji wa huduma takribani kwenye maeneo yote ya uchumi ambayo gharama zake zinalipwa kupitia mlaji au mtumiaji wa huduma husika.

Tumekuwa tunalia kwamba gharama za umeme zinatuumiza kwa sababu ziko juu; lakini wazalishaji wa umeme (TANESCO) na kuusambaza kwa watumiaji hujitetea kuwa gharama za kufanya kazi hiyo ni kubwa. Pengine nao wanakopa kuwekeza kwenye mitambo ya kufua umeme. Sasa riba kwa mikopo inapokuwa kubwa inakuwa vigumu kwa TANESCO kusambaza na kuuza huduma ya umeme kwa bei ya chini. Matokeo yake ni mtumiaji wa umeme kugharamia riba kwa mkopo kupitia bei kubwa tunazolipa kila mwezi.

Tunafahamu fedha zinazolipwa na TANESCO kwa kampuni kama IPTL na nyinginezo ni fedha nyingi sana sijui makubaliano yalivyokuwa lakini lazima walipe. Je, TANESCO fedha za kulipia madeni kama hayo inazipata wapi? Kwa vyovyote vile njia kuu ni kutoka kwa wateja wake ambao ni watumiaji wa umeme.

Wakati mwingine huwa ninafikiri kwamba Serikali itupunguzie makali ya gharama za umeme kwa kuipatia TANESCO ruzuku. Lakini ukija kwa upande mwingine ujiulize Serikali fedha za ruzuku inazipata wapi? Jibu ni kutoka kwa walipa kodi ambao ni watanzania wenye kufanya shughuli mbalimbali zinazowaingizia kipato wapate fedha za kulipa kodi.

Hata hivyo sote tunajikuta tumo katika mzunguko wa shida na changamoto kibao kutokana na mifumo ya benki pamoja na vyombo vingine vya fedha ilivyo. Hata ukiuangalia utaratibu wa kuuza na kununua fedha za kigeni hapa nchini umetoa uhuru sana wa watu kufanya wanavyotaka ili mradi wanufauke wenyewe bila kujali hali halisi ya walio wengi.

Haingii akilini mwananchi ndani ya taifa lake la Tanzania atakiwe kulipa malipo ya ada kwa kutumia fedha za Marekani (US Dollars) hasa katika shule zenye kutumia lugha ya kiingereza. Kwa nini hali iwe hivyo na shilingi yetu ikataliwe ni kwa maslahi ya nani?  Mifumo wa kifedha ilivyo inaweza ikawa kipingamizi mojawapo katika kufanikisha adhma ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Hali hii itaendela mpaka lini?  Ipo haja ya Serikali kupitia Benki Kuu na vyombo vingine vya fedha kuingilia kati suala la riba katika benki ya biashara ili kuwezesha watu wengi kukopa.

Kwa kweli tunahitaji kukopa ili tuweze kusonga mbele lakini iwapo wenye nacho watazidi “kuwakamua” wasionacho ambao ni wakopaji kupitia viwango vikubwa vya riba; maendeleo endelevu kwa jamii ya kawaida itakuwa shida kuyafikia ifikapo 2025 au 2030. Ni vigezo gani vinatumika kuweka riba kubwa kwenye mikopo wataalam wa masala ya fedha na uchumi wanalo jibu.

Pamoja na hayo jinsi mahesabu kuhusu mkopo na riba yake yanavyokokotolewa wakopaji, kwa kufahamu au kutokufahamu, tunajikuta mathalani mkopaji pengine unalipa zaidi ya asilimia 20 ya kile ulichokopa. Utaratibu wa Vikoba nao haujawa na nguvu za kutosha kumkomboa mtu wa hali ya chini.

Kwa kuwa kipato ni kidogo mkopaji kupitia Vikoba haruhusiwi kukopa zaidi ya mara tatu ya kiasi alichoweka kwenye Vikoba. Kwa maana hiyo bado tunahitaji huduma za kibenki

 

zitusaidie tusonge mbele kimaendeleo lakini kwa viwango vya riba vilivyo ni mtihani mgumu.

Maana mtu anaweza kupoteza maisha kutokana na “presha” ya damu (BP) kupanda iwapo benki itaanza kumdai kwa kushindwa kuurejesha mkopo pamoja riba yake. Mwenyezi Mungu atunusuru kwa hili kwa kuwapa hekima na busara viongozi wetu wakuu Serikali ili waweze kushughulikia suala hili kwa faida ya waliowengi.

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.