Menu
RSS

Utalii unavyoongeza mapato ya Taifa

·       Kituo kipya cha watalii chafunguliwa Kilwa

Dk. Felician Kilahama

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na mema mengi anayonitendea hadi sasa.

 

 Kwa kweli Mwenyezi Mungu ni mwema sana kwetu na tunaendela kuishi tukipata riziki zetu au mkate wetu wa kila siku wakati mwingine kwa huruma yake Mungu kwetu maana hali kimaisha inazidi kuwa ngumu kila kukicha.

 

Hivyo ni jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kila wakati na kila mahali tutakapokuwa katika harakati za kujipatia riziki zetu za kila siku. Vilevile, namshukuru Mungu Mwenye enzi yote kwa kunijalia fursa na uwezo wa kutembelea Mkoa wa Lindi hususani Wilaya ya Kilwa.

 

 Nilikuwa wilayani Kilwa tangu tarehe 10 hadi 20 Januari 2016 na kufikia Mji Mdogo: Kilwa Masoko ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kilwa. Ingawa siyo mara yangu ya kwanza kufika Kilwa Masoko, lakini siku za nyuma sikuwahi kupata muda wa kutembelea maeneo kadhaa ndani ya Mji Mdogo Kilwa Masoko. Safari hii niliona ni vema kuweza kutenga muda kidogo na kuweza kuzuru sehemu mbalimbali katika eneo la Kilwa Masoko.

 

Kilwa ni moja ya Wilaya sita katika Mkoa wa Lindi na mpaka wake kwa upande wa Mashariki ni Bahari ya Hindi (Indian Ocean). Wilaya ilianzishwa wakati wa ukoloni mwaka 1942 wengi wetu tulikukwa hatujazaliwa na wakati ule taifa lilijulikana kama “Tanganyika” chini ya utawala wa Waingereza.

 

Kabla ya vita vya Dunia vya kwanza (First World War: 1914 hadi 1918) eneo la Africa Mashariki lilikuwa likitawaliwa na Wajerumani na lilijulikana kama “Dutch Oustefrica” likihusisha mataifa ya sasa Kenya na Uganda. Hata hivyo Tanganyika ilipata uhuru kutoka kwa Waingereza tarehe 9 Desemba 1961 na mwaka mmoja baadaye (tarehe 9 Desemba 1962) ikawa Jamhuri ya Tanganyika.

 

Tarehe 26 April 1964 mataifa ya Tanganyika na Zanzibar yaliungana na kuwa taifa moja la Tanzania (Jamhuri ya Muungano Tanzania) chini ya Serikali moja (United Republic of Tanzania-URT). Wilaya ya Kilwa ina ukubwa takribani hekta 1.4 millioni (1,390km2) za ardhi inayofaa kwa kilimo, ufugaji, pia kuna rasilimali nyingine kama maji, misitu, wanyamapori na kwa sensa ya watu ya 2012, Kilwa ina watu wapatao 171,000 wengi wao wakiishi vijijini.

 

Ilikuwa ni wiki ya pili ya mwezi January 2016 nikiwa Kilwa Masoko nikawa natembea hapa na pale ndipo nikaona jengo moja karibu na soko na stendi ya mabasi nikavutiwa na hivyo kuweza kufika hapo lilipojengwa.

 

Nilikuta wajenzi wanafanya kazi za kukamilisha ujenzi niliwauliza jengo ni mali ya nani na kwa shughuli gani? Jibu likawa ni mali ya Halmashauri ya Kilwa na litatumika kama kituo cha kuwapatia taarifa mbalimbali wageni na hasa Wataalii watakaotembelea Kilwa.

 

Kusema kweli baada ya maelezo hayo nikavutiwa na lengo hilo la kuweka kituo hicho hapo Kilwa Masoko maana vituo kama hivyo katika Wilaya za Mikoa ya Kusini mwa Tanzania ni nadra sana kuviona. Hii ina maana ni kituo cha aina yake kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara pengine hata Mkoa wa Ruvuma. Baada ya hapo nilionana na Mratibu wa ujenzi wa Kituo hicho Bi Tatu Magina, ambaye alinifahamisha kuwa kituo kitazinduliwa rasimi tarehe 15 Januari, 2016 iwapo nitakuwa bado nipo Kilwa Masoko basi ninakaribishwa kushuhudia uzinduzi huo.

 

Hivyo niliona ni fursa nzuri kushiriki uzinduzi na kuweza kujifanza mengi kuhusu na masuala ya utalii katika Wilaya ya Kilwa na Wilaya jirani katika Mkoa wa Lindi na Mtwara mfano, Wilaya ya Newala inayopakana na Msumbiji pengine kupitia Mzumbiji tunaweza kupata Watalii na wageni wengineo wakaja wakatembelea Kilwa Masoko.

 

Ufunguzi rasimi wa Kituo cha Utalii Kilwa Masoko ulifanyika tarehe 15 Januari 2016 na Mgeni rasimi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mheshimiwa Juma Njoway ambaye aliongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kilwa Bwana Hamidu Mtemekela.

 

Vilevile alikuwepo Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji Mdogo-Kilwa Masoko Bwana Ismail Slim na Mkuu wa Ofisi za Mambokale Kilwa Bwana Revocatus Bugumba. Wageni wengine mashuhuri waliohudhuria na pamoja na Bwana Olivier Coupleux, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Urtawala katika Muungano wa Nchi za Ulaya (European Union Delegation to Tanzania).

 

Vilevile alikuwepo Bwana Philippe BonCour, Conseiller de cooperation et d’Action Culturelle ambaye aliwakilisha Ubalozi wa Ufaransa. Wizara ya Maliasili na Utalii iliwakilishwa na Bwana John Kimaro ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi, Uhifadhi na Teknolojia, Idara ya Mambokale.

 

Wizara ya Fedha na Uchumi iliwakilishwa na Bwana Godlove Stephen ambaye ni Naibu Muidhinishaji (Deputy National Authorising Officer). Wakati huo Bodi ya Utalii Nchini (Tanzania Tourist Board- TTB) iliwakilishwa na Maafisa Waandamizi wawili kutoka Makao Makuu, Dar-Es-Salaam.

 

Mamlaka ya Kilwa Masoko pamoja na Halmashauri ya Wilaya kwa pamoja wameweza kujenga kituo hicho kwa msaada wa fedha na utalaam kutoka European Union Delegation in Tanzania pamoja na Ubalozi wa Ufaransa. Ujenzi wa kituo hicho uliafikiwa baada ya kuona kuwa Wilaya ya Kilwa inavyo vivutio vingi sana kwa ajili ya Watalii na wageni wengine.

 

Kwa mathalani, Kilwa kuna maeneo mazuri ya ufukweni mwa Bahari yanayofaa kwa watalii kuweza kupumzika, kuvinjari hapa na pale na hata kuogelea na kuvua samaki kiutalii siyo kibiashara. Vilevile, Kilwa kuna magofu ya Kale katika maeneo ya Songo Mnara, Kilwa Kisiwani na Kilwa Kivinje.

 

Maeneo hayo ni vivutio vizuri vya Utalii na tangu mwaka 1981 maeneo ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara yaliwekwa chini ya Urithi wa Dunia baada ya kuyatambua kuwa ni maeneo nyeti kihistoria na yanafaa kuhifadhiwa kitaifa na kimataifa kupitia Shirika na Umoja wa Mataifa (UN) la UNESCO.  

 

Kwa mwaka 2015 Halmashauri ya Kilwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mji Mdogo-Kilwa Masoko pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii pia kupitia uhisani wa Muungano wa Nchi za Ulaya (EU) waliweza kundaa Jarida: Karibu kilwa (Kilwa District Heritage Resources) lenye kurasa 75.

 

Jarida hilo limesheheni maelezo na picha zinazoonyesha rasilimali na urithi wa mambokale katika Wilaya ya Kilwa. Kupitia taarifa hiyo Watalii watakaotembela Kilwa Masoko na viunga vyake watapata mahali pa kuanzia kwa kupewa taarifa muhimu na kamili juu ya urithi asilia na vivutio vingine vinavyopatikana Kilwa.

 

Kilwa ni moja ya Wilaya za zamani sana katika nchi yetu na inapakana na Bahari ya Hindi (Indian Ocean) kwa upande wa Mashariki. Wageni kutoka Mashariki ya Kati na Mashariki ya Mbali hasa nchi za Uarabuni mfano, Oman, waliwahi kukaa Kilwa hata kabla ya Waingereza kuitawala Tanganyika (ambayo kwa sasa inajulikana kama Tanzania baada ya kuungana na Zanzibar na kuwa taifa moja.

 

Wakati huo Waarabu waliweza kufanya biashara ya kununua na kuuza Dhahabu na Meno ya Tembo (gold & ivory) trade). Ili kufanya shughuli za kibiashara vizuri waliweza kuanzisha na kutumia fedha ya Kilwa (Kilwa coins) ambayo ilirahisisha malipo husika. Baadaye ikaongezeka na biashara ya Watumwa na Kilwa Masoko ikawa sehemu maarufu Duniani.

 

Kilwa Masoko inaaminika kuwa ilianza kukaliwa na watu katika karne ya tisa (9). Kulingana na maelezao ya Bwana Olivier Coupleux, European Union waliweza kutoa msaada wa  500,000 Euros kwa ajili ya kujenga Kituo pamoja na kundaa Jarida lenye kuonyesha vivutia vinavyopatikana kwenye Wilaya ya Kilwa na mahali (locality) vinapopatikana).

 

 Aliongeza kuwa msaada huo kwa Wilayani Kilwa ni sehemu ya kiasi cha Euro millioni 10 zilizotengwa kwa ajili ya kusaidia Serikali kadhaa katika Bara la Africa ikiwemo Tanzania kuziongezea nguvu ya kuhifadhi na kuendeleza rasilimali kale na vivutio vya utalii. Kwa niaba ya Serikali yetu nawashukuru EU kwa msaada huo uliowezesha Mamlaka za Kilwa Masoko kujenga kituo cha kuhabarisha watalii na wageni.

 

Mwakilishi wa EU katika maelezo yake wakati wa kufunguliwa Kituo alisema kuwa Kilwa ina utajiri mkubwa wa rasilimali asilia na pia wa kihistoria. Hivyo akasema kuwa ifikapo mwaka 2025 namba ya Watalii watakoakuwa wanakuja kuitembelea Tanzania wakafika zaidi ya million nane.

 

Watalii wengi watapenda kufika Kilwa kwa sababu hata miundombinu itakuwa imeboreshwa sana. Kwa mfano, barabara pamoja na huduma za kiutalii kama hoteli na wakala wa kusafirisha na kuongoza watalii vitakuwa vimeboreshwa sana pamoja na kupatikana taarifa mbalimbali kwa Watalii. Kwa sasa inakadiriwa kuwa tunapata watalii karibu million moja kwa mwaka na wachache sana  wanaotembelea Kilwa.

 

Watu wengine muhimu ambao wamewahi kuitembelea Kilwa Masoko ni pamoja na Balozi wa Ufaransa Her Excellency Malika Berak, ambaye aliwahi kusema kuwa “the Kilwa heritage site holds extraordinary capital, both natural & cultural, for the local populations. It is on this capital that the sustainable development of the district must be built to make the ownership & today France takes part in project of sustainable development for Kilwa”.

 

Kwa Kiswahili alimaanisha kuwa Kilwa kuna urithi usio wa kawaida ikiwa ni pamoja na urithi wa kiasilia na kiutamaduni. Kwa urithi huo itakuwa rahisi kuwepo maeledeleo endelevu na sasa Ufaransa inashiriki katika harakati za kuleta maendeleo endelevi Wilayani Kilwa.

 

Kwa upande mwingine, Balozi wa Muungano wa Ulaya (the European Union Ambassador in Tanzania) His Excellency Filliberto Ceriani Sebregondi, kwenye Utangulizi wa Jarida la Karibu Kilwa (Kilwa District Heritage Resources) ambalo limeainisha maeneo mbalimbali yenye urithi asilia na utamaduni mahususi kwenye Wilaya ya Kilwa asisema: “cultural heritage preservation, creative industries, sustainable tourism management, and assistance for people to set up small & medium enterprises”.

 

Maneno haya ni ya kutia moyo kwa minsingi kwamba tukihifadhi utamaduni wetu, tukawa na ubunifu wa kiviwanda pamoja na kusimamia shughuli za utalii kwa misingi endelevu na kuwezesha jamii kuanzisha na kuendesha shughuli ndogo na za kati kijasilia mali tutaweza kuiona Wilaya ya Kilwa ikisonga mbele kijamii, kiuchumi na kimaendeleo kwa kutumia urithi wa tamaduni na rasilimalia asilia bila kuathithiri ubora wa mazingira.

 

Vilevile, Balozi Filliberto Ceriani Sebregondi aliongeza na kushauri kuwa: “the visitors who flock to Kilwa and enjoy the pristine beaches must prolong their stay for the people of Kilwa to fully benefit from their presence. Providing them with a diversified offering of natural & cultural attractions and increased tourist infrastructure will definitely contribute to this”.

 

Hapa Mheshimiwa Balozi ameshauri kuwa Watalii watakaopata fursa ya kutembelea Kilwa waweze kukaa muda wa kutosha; isiwe kufika leo na kesho kuondoka ili watu wa Kilwa waweze kunufaika na kuwepo Watalii wengi. Ili kufanikisha lengo hilo lazima tuhakikishe kuna vivutio vya kutosha vipo na vinafahamika kidunia.

 

Mfano, fukwe zenye mandhali nzuri kiasilia zitunzwe vizuri na kuwepo na miundombinu iliyoimara na bora ili Watalii waweze kupata huduma nzuri sawa na thamani ya fedha zao watakazolipa.

 

Kwa Kufanya hivyo wakazi wa Kilwa kwa kushirikiana na Serikali pamoja na sekta binafsi watafanikiwa na kupiga hatua mbele kimaendeleo kutokana na shughuli za Utalii endelevu.

 

Wakati wa ufunguzi wa Kituo cha kuendeleza Utalii Wilayani Kilwa Mgeni Rasimi  alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Juma Njoway. Alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Kilwa watunze vizuri rasilimali za asili na utamaduni wao ili viweze kuwa vivutio tosha kwa Watalii na wageni watakaotembelea Kilwa kutoka sehemu mbalimbali duniani.

 

Vilevuile, aliwataka watakaosimamia Kituo hicho wahakikishe kinakuwa salama na kuendelezwa kila wakati ili kiendelee kuwa sehemu muhimu kwa Watalii na wageni wengineo kwa kuwapatia taafira muhimu watakazozihitaji.

 

Awali ya yote Mratibu wa shughuli za ujenzi wa Kituo Bi Tatu Magina, alitaarifu kuwa karibu asilimia 90 ya vifaa vilivyotumika kujenga Kituo vilitoka Wilayani Kilwa. Vilevile, Fundiwashi wote walitoka Kilwa na wamefanya kazi nzuri kama jengo linavyoonekana katika picha (sura ya nje na ndani ya jengo).

 

(Photos)

 

 Suala hili linaonyesha kuwa kwa namna moja au nyingine wakazi wa Kilwa wamenufaika na ujenzi wa Kituo. Kwa hiyo sehemu kubwa ya msaada uliotolewa na EU pamoja na Ufaransa (takribani Euro 500,000) zimetumika na kuwanufaisha wakati za Kilwa.

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT), Bwana John Kimaro, Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Mambokale, aliwashuru EU na Ubalozi wa Ufaransa kwa msaada wao wa fedha na utaalam hadi kuwezesha kupata jengo litakalotumika kwa shughuli za Mambokale na Urithi asilia na rasilimali Utamaduni katika Wilaya ya Kilwa.

 

Vilevile, alipongeza Uongozi wa Wilaya na Halmashauri pamoja na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kilwa Masoko kwa ushirikiano wao mzuri kwa kufanikisha mradi huo na aliongeza kuwa Wizara iko pamoja nao katika kuhakikisha kuwa Kituo hicho kinafanikisha malengo yake kwa kuzingatia utaratibu wa kisera, kisheria na kanuni.

 

Kituo sasa kimeanza na Waongoza Watalii sita (six Tour Guides) wanaume watano na mwanamke mmoja kiongozi wao akiwa Bwana Abdallah Ahmad. Wote wamepata mafunzo juu ya shughuli za kuongoza Watalii na wanafahamu lugha ya Kiingereza kiasi cha kuweza kumudu kazi zao za kila siku.

 

Hata hivyo litakuwa jambo jema kwa Kituo kuongeza Wataalam zaidi kadri namba ya Watalii itakavyoongezeka. Kituo pia kiweke utaratibu mzuri wa kuratibu shughuli za kiutalii kwa wananchi wanaokizunguka ili hatimaye waweze kunufaika na uwepo wa Kituo hicho Kilwa Masoko.

 

Pengine na Halmashauri ya Wilaya pamoja na Mamlaka ya Mji Mdogo Kilwa Masoko zitenge bajeti ambayo itasaidia kuendeleza shughuli za kituo hicho kila mwaka ikiwa ni pamoja na kukifanyia matengenezo ya mara kwa mara ili kuhakikisha kinakuwa imara na bora wakati wote.

 

End 

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.