Menu
RSS
Tanzania

Parokia Yombo Kiwalani yazawadia Jumuiya zake

Na Bruno Bomola

UONGOZI Parokia ya Mtakatifu Kamili Yombo Kiwalani Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam imetoa zawadi ya Mbuzi kwa Jumuiya tatu za parokia hiyo zilizofanya vizuri katika kipindi cha mwaka jana kwa  kujitoa katika michango mbalimbali parokiani hapo.

Parokia ya Mtakatifu Kamili ina jumla ya jumuiya ndogo ndo go 44 zilizokuwa zikichuana kuchangia michango mbalimbali hatimaye zikapatikana jumuiya tatu zilizofanikiwa kupata zawadi ya Mbuzi.

Kwa mujibu wa Kamati tendaji ya Walei wa Parokia hiyo, zoezi hilo la kutoa zawadi ya Mbuzi lilitakiwa kufanyika kila mwaka ili kuleta ushindani na kuwajengea waamini na viongozi wanao hamasa ya utoaji michango mbalimbali ya Kanisa.

Jumuiya zilizopata zawadi ya Mbuzi ni Jumuiya ya Mtakatifu Kamili Kariagogo, Mtakatifu Francis wa  Asiz, na Jumuiya ya Mtakatifu Luka Mwinjili zilizochuana kuchangia michango mbalimbali kwenye Parokia hiyo, ikiwemo zaka, ulinzi, harambee, tegemeza Jimbo na kadhalika.

Jumuiya ya Mtakatifu Kamili Kariagogo waliibuka kidedea na kushika nafasi ya kwanza,  na kuzibwaga jumuiya 43 zilizoburuza mkia.

Jumla kuu ya michango yote  iliyotolewa na Jumuiya hiyo ni Shilingi 6,669,000 kwa mwaka mzima ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Robert  Bamwebuka.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Francis wa Asiz chini ya Mwenyekiti wake, Rugemamu Kashura  iliyofanikiwa kutoa kliasi cha Shilingi 5,775,250 kwa mwaka  mzima.

Huku nafasi ya tatu ikishikwa na Jumuiya Mtakatifu Luka chini ya Mwenyekiti Gaspary Mhegele, waliotoa Shilingi 5,550 ,650, kwa mwaka mzima wa 2015.

Akizungumza baada ya hafla ya utoaji wa zawadi hizo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mtakatifu Luka, Gaspary Mhegele alisema kuwa zipo changaoto zinazowakabili lakini waamini wake waliweza kuchangia michango mbalimbali ya Kanisa  na kufikisha kiasi hicho cha fedha.

“Tukifanya kazi ya bwana kwa kushirikiana pasipo kuwa na maneno ya pembeni tunaweza kufanikiwa lakini mtu akisikia kuna mchango anaanza kunung’unika kiasi kwamba kama ile pesa anayotoa inakwenda kuliwa na sio kufanya kazi ya bwana …. tunatakiwa kujitoa kutoka mioyo yetu pasipo kusema sema”, alisema Mhegele.

Kwa upande wake  Katibu Msaidizi wa Parokia, Veronica  Obaganga alisema kuwa zoezi hilo limeanzishwa kwa ajili ya utoaji wa zawadi kila mwaka kwa washindi lina lengo la kuongeza uhamasishaji kwa waamini kuendelea kuchangia Kanisa.

Parokia ya Yombo Kiwalani, ilikusanya zaka kwa mwaka mzima wa 2015 ilikushilingi 26,361,900 pamoja na ulinzi shilingi 8,588,650,harambee Shilingi  19,273950, tengemeza  jimbo Shilingi 13,852,500 pamoja  na michango mingine ya parokia hiyo, kwa mwaka 2015, ambayo ilikuwa Shilingi 87,538,050.

Read more...

Parokia Yombo Kiwalani yazawadia Jumuiya zake

Na Bruno Bomola

UONGOZI Parokia ya Mtakatifu Kamili Yombo Kiwalani Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam imetoa zawadi ya Mbuzi kwa Jumuiya tatu za parokia hiyo zilizofanya vizuri katika kipindi cha mwaka jana kwa  kujitoa katika michango mbalimbali parokiani hapo.

Parokia ya Mtakatifu Kamili ina jumla ya jumuiya ndogo ndo go 44 zilizokuwa zikichuana kuchangia michango mbalimbali hatimaye zikapatikana jumuiya tatu zilizofanikiwa kupata zawadi ya Mbuzi.

Kwa mujibu wa Kamati tendaji ya Walei wa Parokia hiyo, zoezi hilo la kutoa zawadi ya Mbuzi lilitakiwa kufanyika kila mwaka ili kuleta ushindani na kuwajengea waamini na viongozi wanao hamasa ya utoaji michango mbalimbali ya Kanisa.

Jumuiya zilizopata zawadi ya Mbuzi ni Jumuiya ya Mtakatifu Kamili Kariagogo, Mtakatifu Francis wa  Asiz, na Jumuiya ya Mtakatifu Luka Mwinjili zilizochuana kuchangia michango mbalimbali kwenye Parokia hiyo, ikiwemo zaka, ulinzi, harambee, tegemeza Jimbo na kadhalika.

Jumuiya ya Mtakatifu Kamili Kariagogo waliibuka kidedea na kushika nafasi ya kwanza,  na kuzibwaga jumuiya 43 zilizoburuza mkia.

Jumla kuu ya michango yote  iliyotolewa na Jumuiya hiyo ni Shilingi 6,669,000 kwa mwaka mzima ikiwa chini ya Mwenyekiti wake Robert  Bamwebuka.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Francis wa Asiz chini ya Mwenyekiti wake, Rugemamu Kashura  iliyofanikiwa kutoa kliasi cha Shilingi 5,775,250 kwa mwaka  mzima.

Huku nafasi ya tatu ikishikwa na Jumuiya Mtakatifu Luka chini ya Mwenyekiti Gaspary Mhegele, waliotoa Shilingi 5,550 ,650, kwa mwaka mzima wa 2015.

Akizungumza baada ya hafla ya utoaji wa zawadi hizo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mtakatifu Luka, Gaspary Mhegele alisema kuwa zipo changaoto zinazowakabili lakini waamini wake waliweza kuchangia michango mbalimbali ya Kanisa  na kufikisha kiasi hicho cha fedha.

“Tukifanya kazi ya bwana kwa kushirikiana pasipo kuwa na maneno ya pembeni tunaweza kufanikiwa lakini mtu akisikia kuna mchango anaanza kunung’unika kiasi kwamba kama ile pesa anayotoa inakwenda kuliwa na sio kufanya kazi ya bwana …. tunatakiwa kujitoa kutoka mioyo yetu pasipo kusema sema”, alisema Mhegele.

Kwa upande wake  Katibu Msaidizi wa Parokia, Veronica  Obaganga alisema kuwa zoezi hilo limeanzishwa kwa ajili ya utoaji wa zawadi kila mwaka kwa washindi lina lengo la kuongeza uhamasishaji kwa waamini kuendelea kuchangia Kanisa.

Parokia ya Yombo Kiwalani, ilikusanya zaka kwa mwaka mzima wa 2015 ilikushilingi 26,361,900 pamoja na ulinzi shilingi 8,588,650,harambee Shilingi  19,273950, tengemeza  jimbo Shilingi 13,852,500 pamoja  na michango mingine ya parokia hiyo, kwa mwaka 2015, ambayo ilikuwa Shilingi 87,538,050.

Read more...

Watu wenye ulemavu, wanawake hawaoni uchaguzi huru, haki.

Na Sabinus Nyasenso

KATIKA Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2015, Jesca Kishoa ambaye sasa ni Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) alishiriki kampeni za uchaguzi akiwa na ujauzito wa miezi minane na ilipofika wiki tatu kabla ya kampeni kumalizika, akajifungua.

 

Hali hiyo ilikuwa moja ya changamoto kubwa wanazokumbana nazo wanawake wengi katika harakati za uchaguzi wa kisiasa kwani kampeni zikianza hazisubiri mtu amalize kipindi cha ujauzito au kunyonyesha.

 

Alinukuliwa akisema, “Kwa kuwa niliwaahidi Wanairamba kuwa nao bega kwa bega baada ya kumaliza siku saba za uzazi, nilirejea kwenye mapambano na kichanga changu (mtoto mchanga) kikiwa na siku 10 tu, licha ya kupitia mazingira magumu yasiyoelezeka maana mwanamke anapotoka kujifungua anapitia changamoto nyingi.”

 

Anaitaja changamoto ya jinsia kuwa kubwa kwani katika mchakato uchaguzi, baadhi ya wanasiasa na wafuasi walitumia nguvu kushawishi wananchi wasimchague kwa kuwa ni mwanamke.

 

“Mungu alinipa ujasiri nikasimama imara kuelimisha wananchi wangu kujua kuwa hata wanawake wana uwezo sawa na wanaume kiutendaji na ndio maana wamepewa nafasi mbalimbali tena wakafanya vizuri hata zaidi ya wanaume,” anasema.

Mbali na hilo, sura ya mfumo dume kuifanya njia ya kuelekea uchaguzi huru na wa haki hadi kwa wanawake na watu wanaoishi na ulemavu kuwa nyembamba isiyoonesha uhuru wala haki, inaonekana hata katika teuzi mbalimbali.

 

Ali Thabiti ni Mwanahabari wa Kituo cha Radio cha Jogoo FM kilichopo Songea mwenye ulemevu wa kutoona. Akiwa Dar es Salaam anasema uhuru, haki na usawa kwa wanawake na watu wenye ulemavu ni kitendawili katika jamii nzima tangu watu wa ngazi za chini hadi juu.

 

Anazungumzia usawa wa kijinsia akirejea uteuzi wa hivi karibuni alioufanya Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kwa mawaziri, naibu waziri, makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu.

 

Anasema, “Rais hajazingatia jinsia katika uteuzi wake maana hata idadi kubwa ya mawaziri na manaibu waziri ni wanaume licha ya kuwa alimteua Samia Suluhu kuwa Makamu wa Rais…Samia pekee hatoshi.”

 

Akaungana na mwandishi mwingine ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu na usawa wa kijinsia, Rachel Gabagambi kumshauri Rais kuwakumbuka wanawake wakiwamo wenye ulemavu katika uteuzi wa nafasi zilizosalia zikiwamo za ubunge, ukuu wa wilaya na ukuu wa mikoa.

 

Katibu Mkuu wa Sauti ya Wanawake Wenye Ulemavu Tanzania (Swauta), Stella Jailos mwenye ulamavu wa kutoona anasema, “Nampongeza Rais Magufuli maana amekuwa Rais wa kwanza Tanzania kuonesha ujasiri wa kuwathamini wenye ulemavu na kuwateua katika Serikali yake.”

 

 “Fursa hizi zisiishie tu kwa wenye ulemavu wanaume, bali ziwafikie pia wanawake wenye ulemavu maana wana changamoto nyingi na nzito za kipekee kwanza, kama wanawake na pia , kama wanawake wenye ulemavu.”

 

Akaongeza, “Nawashukuru Tamwa (Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania) na UN-WOMEN kwa elimu ambayo wamekuwa wakiitoa kwa umma maana imesaidia sana kuongeza uelewa wa watu kuhusu wanawake na watu wenye ulemavu na imewafanya wengi kujitokeza kushiriki katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita ama kwa kushiriki kampeni na kuchagua viongozi, au kwa kugombea wenyewe…”

 

Jailos ambaye ni mmoja wa wanasiasa chipukizi aliyewania nafasi ya Ubunge wa Viti Maalum mkoani Dodoma, anasema changamoto kubwa inayowakabili wagombea chipukizi wakiwamo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ni hasa rasilimali fedha ambayo imewakwamisha kwa kiasi kikubwa tofauti na wabunge waliopata mafao yao na kushiriki katika kinyang’anyiro hicho.

 

Anasema wabunge wanapopata mafao ya kustaafu kisha wakaruhusiwa kugombea, wengi wanatumia nguvu ya pesa walizopata kuwashawishi wapigakura ili wawachague kwa mara nyingine.

 

Katika teuzi hizo, Rais Magufuli amemfanya Dk. Abdallah Possi mwenye ulamavu wa ngozi (albinism) kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), Profesa James Epifani Mdoe kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Amon Mpanju kuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Sheria na Katiba.

 

Kimsingi, katika mfumo wowote baguzi kijinsia wanawake na watu wenye ulemavu wanateseka sana, lakini, wanawake wenye ulemavu wanateseka zaidi hivyo, wanastahili uwakilishi maalumu ili kujenga na kuimarisha usawa kama Tamwa inavyosisitiza.

 

Mpanju kwa upande wake anamshukuru Rais Magufyuli kwa kuwakumbuka wenye ulemavu akisema katika utendaji wake (mpanju) hatamwangusha Rais.

 

Anazishukuru Tamwa, UN-WOMEN na Shivyawata (Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu) kwa juhudi zao kuelimisha umma kuhusu umuhimu na nafasi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika mchakato wa uchaguzi wa kisiasa huku akiwaasa watu katika makundi hayo kutojibagua na kubweteka, bali wajihusishe katika mambo mbalimbali ya kijamii na kisiasa ili vyama viwatambue na kuona mchango wao na hatimaye, vyama viwape nyadhifa.

 

Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015, Tamwa kwa ufadhili wa UN-WOMEN imeweka nguvu kubwa kutetea haki za binadamu na usawa wa kinjisia ikisisitiza umuhimu wa wanawake, vijana na watu wenye ulemevu kupata fursa sawa na za haki katika kushiriki kikamilifu mchakato wa Uchaguzi wa kisiasa.

Hili linahusisha ushiriki wao katika kugombea, na au katika kujiandikisha, kushiriki mikutano ya kampeni na kujitokeza kupiga kura bila hofu.

 

Mratibu wa taasisi ya ULINGO, Dk. Avemaria Semakafu anazungumzia changamoto na kero walizokumbana nazo wanawake katika Uchaguzi Mkuu uliopita  akisema kulikuwa na vitisho, udhalilishaji, kuzomewa na hata kutukanwa na kushambuliwa kwa wanawake waliokuwa na mtazamao tofauti na baadhi ya watu.

 

“Siasa za vyama zilikuwa si rafiki kwa wanawake na zilikuwa ngumu. Zilitumia makundi ya vijana kuzuia uhuru wa wanawake wengi kushiriki kampeni sawasawa hasa waliovaa sare za vyama vingine. Kimsingi, wanawake waliteseka sana.”

 

Hii ni moja ya sababu kuu za watu wenye ulemavu na wanawake kutokuuona uchaguzi ulio huru na haki.

 

Mpanju, Jailos  na Gidion Mandesi (aliyewania Ubunge katika Jimbo la Muleba Kusini), wanasema kasumba ya kuwabagua, kuwapuuza na kuwanyanyapaa  wanawake na watu wenye ulemavu katika mchakato wa uchaguzi wa kisiasa, ni doa na mtazamo unaopaswa kuondolewa katika jamii haraka.

 

Wanasema jamii nyingi zinatumia lugha mbaya dhidi ya mwanamke au mtu mwenye ulemavu anayegombea huku watu wengine wakisema wazi, “Huyu mwanamke, kilema au kipofu atamwongoza nani?” Hili si jambo jema.

 

Mazingira kama hayo ya baadhi ya makundi ya watu kumnyimwa fursa sawa za kushiriki katika uwakilishi na ngazi za maamuzi ndiyo yamemfanya Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga kusema kuwa nafasi za uwakilishi za wanawake kupitia viti maalumu vya udiwani na ubunge, hazilengi hasa kumtendea haki mwanamke na kwamba, ni kiini macho kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 hairuhusu Mbunge asiye wa kuchaguliwa jimboni kuwa waziri mkuu.

 

Sanga anasema, “Kupitia viti maalumu, ni ndoto mwanamke kuwa Waziri Mkuu na hali hii itachukua muda mrefiu kuiondoa… Ikumbukwe kuwa sisi wanawake ni zaidi ya nusu ya Watanzania na ndio wapiga kura wengi; tungepewa nafasi hizi kwa wingi na hata sheria baguzi zirekebishwe.”

 

Anaongeza, “Ndiyo maana Tamwa tunasisitiza uwakilishi utokane na wanawake wenyewe, au watu wenye ulemavu wenyewe kuchaguana kupitia taasisi zao sio kupitia vyama vya siasa ambavyo vinaonekana wazi vina agenda zao.”

 

Sanga anasema kutokana na viongozi wa vyama vya siasa kuwa na maslahi yao, hata katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa Oktoba 25, mwaka 2015, wanawake wengi walijitokeza kugombea udiwani na ubunge, lakini baadhi ya viongozi wakawalazimisha kujitoa na kusubiri kuteuliwa katika viti maalumu.

 

End 

Read more...

Abate ataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii.

Na John Liveti

Abate wa Abasia ya Hanga, Abate Thadei Mhagama, amewataka watanzania kufanya kazi kwa bidii kumuunga mkono Rais wa awamu ya tano Dk. John Pombe Magufuli, huku wakiishikilia imani yao kama walivyofanya Wafiadini wa Pugu.

Abate Mhagama aliyasema hayo hivi karibuni katika adhimisho la Misa Takatifu ya kuwakumbuka Wafiadini wa Pugu iliyoenda sanjari na kusimikwa kwa Msalaba, kubariki Kanisa la Hija, kuoneshwa kwa Sanda ya Yesu Kristo na uzinduzi wa Mwaka wa Huruma ya Mungu kijimbo.

Katika Misa hiyo iliyoongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Eusebius Nzigilwa, Abate Mhagama alisema, waamini wanatakiwa kufanya kazi kwa kuwa Wafiadini wa Pugu walikuwa na falsafa hiyo inayohimiza kufanya kazi kwa bidi.

Watanzania natakiwa kumuunga mkono Dk. MAgufuli kwa kauli mbiu yake ya ‘hapa Kazi Tu’ inayohimiza kazi aliyosema ilianzishwa miaka mingi iliyopita na Mtakatifu Benedikto, ‘Sala na Kazi’.

Abate Mhagama aliwataka waamini kuzingatia sala kila waanzapo kazi na kuishi imani hata ikiwagharimu kutoa maisha yao kama walivyofanya wamisionari wa kwanza Wafiadini wa Pugu.

Aidha, Abate Mhagama aliwataka waamini kujenga ushirikiano na waamini wa Dini na madhehebu mengine kwa matendo mema hasa katika maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu.

Abate Mhagama  alisema mmonyoko wa amaadili ulijitokeza hasa katika taifa letu  ni kutokana na watu kufanya kazi pasipo kujikabizi kwa Mungu na nadio maana mambo yalikwenda vibaya.

Alisema  waamini wa Kanisa Katoliki katika kipindi hiki hasa tunaposherehekea Jubilei ya Huruma ya Mungu inawapasa kujirudi kwa Mungu  kuwa watu wa msamaha  na watu wa kutenda  matendo mema ili kujipatanisha na baba na hasa kuwa watu wa imani.

“Tukumbuke kuwa ili kuwa na imani thabiti lazima tuingie gharama  kama vile walivyoingia gharama hawa wafiadini wa Pugu ambao walijitoa katika maisha  yao kutoka huku Ulaya na kuja kueneza habari njema ya  neno la Mungu”,alisema.

Alisema katika masumbuko na mateso ambayo waliyapata imeleta mwelekeo bora  kwa jamiii kwani wamisioanri walijikita zaidi kulea watoto yatima waliokuwa wakiletwa na na jamaa mbalimbali.

Hivyo aliwataka waamini kujitahidi kujenga mahusiano bora na watu wa Dini nyingine ili  kuwe na uelewano na mshikamano katika taifa la Tanzania.

Wakati huo huo, katika adhimisho hilo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, aliyekuwa amelazwa katika katika Hospitali ya Tifa Muhimbili kwa Siku 9, alihudhuria na kuwashukuru waamini kwa sala na maombi yao. 

End 

Read more...

Waamini tengenezeni njia ya Bwana-Askofu

Na John Liveti

Waamini wa Kanisa Katoliki nchini wametakiwa kuitengeza njia ya Bwana na kuyanyoosha mapito yao wakati huu kanisa linapojiandaa kufanya kumbukumbu  ya kuzaliwa  Mkombo wao Yesu Kristo.

 

Akizungumza katika azimisho la Misa Takatifu iliyofanyika katika Parokia ya Roho Mtakatifu Segerea Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu  Eusebius Nzigilwa alisema ujumbe uliotolewa na Yonane Mbatizaji  unagusa zaidi maisha ya waamini hao ya sasa,baadaye na yaliyopita.

 

Alisema ni wazi ukiutafakari kwa kina ujumbe huo kifalsafa una umuhimu katika maisha kwani ipo sehemu hasa kuharibu njia zao na hivyo zinahitaji kusawazisha.

 

Askofu huyo alisema katika mwaliko huo kila mmoja anatakiwa kujitafiti kwa upande wa pili ndani ya Roho kwa kuangalia anatenda yaliyo katika kipindi cha majilio na kutenda mema.

 

“Mkristo anapswa kujitafiti ndani ya moyo  wake katika kuzingati mambo makuu matatu ili aweze kufanikisha  kuwa ni kweli anaiteneza njia  ya bwana na kuyanyoosha mapito yake”,alisema Askofu Nzigilwa.

 

Alisema jambo la kwanza la kuzingatia  kuhakikisha njia inatengezwa ni waamini kufanya maisha  ya toba  na msamaha  kwani mtua anayeishi maisha ya toba na msamaha daima huwa na moyo wa msamaha.

 

Jambo la pili amablo aliwaasa waamini hao kuzingatia ni kuwa watu wa kuishi fazila  za upole na unyenyekezu hayo yanaenda na lile la kwanza kwani toba na msamaha  zinamfanya mtu kuwa mpole na mnyenyekevu.

 

Askofu Nzigilwa alisistiza katika hatua hiyo mwamini anapaswa kuwa mshiriki hai wa msakramenti mbalimbali ya Kanisa  hasa sakramenti ya upatanisho yaani Sakramenti ya kitubio.

 

Aidha Askofu huyo aliendelea kusema kuwa jambo lingine linalotakiwa kufanywa na waamini hao ni kufuata ujumbe wa Yohane Mbatizaji unapsema itengenezeni njia ya bwana ni ile amri ya upendo.

 

“Hapo tunapswa kutambua kuwa hii ni amri kuu ambayo Kristo aliwaachia mitume wake nao wamisambaza hadi kwetu hivyo ni lazima kuwa na upendo kwani bila upendo  mambo hayawezi kwenda vizuri”,alisema Asofu Nzigilwa.

 Alibainisha kuwa “Ili tuweze kufanikiwa na kuishi katika mahali pa usalama na  kudumisha hali ya amani iendelee kustawi  ni lazima kuzingatia mmbo hayo matatu ambayo yatamfanya kila mmoja  amwone mwenzake kuupitia uso wa Mungu”.

 

Aidha katika azimisho ambalo lilikwenda sanjari na kubariki Groto ya Mama Bikira Maria, Askofu Nzigilwa, aliwapongeza waamini kwa majitoleo yao mazuri  na kufanikisha ujenzi wa Groto hiyo, na kuwataka kuaacha majivuno.

Read more...

Ukiona mwenzio ananyolewa, wewe tia maji

Siku chache tu baada ya kula viapo pale mjengoni Dodoma makao Makuu ya Tanzania, baadhi ya Wabunge, walidiriki kuwa watovu wa nidhamu kwa kuzomea na kutamka maneno yasiyoendana na maadili ya viongozi, hususan walioapa au kuthibitisha kwamba watakuwa waaminifu,  kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na kuitumikia kwa moyo wote na kwamba watahifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa Sheria iliyowekwa.

Tukio hili lilitendeka muda mfupi kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Magufuli, kulihutubia Bunge Jipya la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.

Hali hiyo, ilimlazimu Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwaomba wabunge  walioshiriki kutoka nje ya ukumbi ili kuruhusu taratibu zingine ziendelee kwa mujibu wa ratiba. Hali ambayo  waheshimiwa hao waliiheshimu.

Walikuwa radhi kukosa kuwawakilisha watanzania waliowachagua katika kusikiliza yale ambayo Rais wa Awamu ya Tano, Dk. Magufuli aliongea na Watanzania kupitia kwa mabalozi wao ambao ni waheshimiwa wabunge.                                                                                           

Iwapo kwa namna moja au nyingine, mpiga kura wako hakupata fursa ya kufuatilia kilichojili siku hiyo, lakini akafarijika kwamba, maadam nina mwakilishi wangu mheshimiwa mbunge atanipasha angalau yale ya muhimu. Utamjibu nini.                                                                                                                         

Tanzania ni nchi kubwa sana,ambayo bado asilimia kubwa ya wananchi wake wanaishi vijijini ambako waheshimiwa wanatoka, hili halina ubishi.

Kati ya watanzania hao wapo waliobahatika kuwa na vyombo kama radio kuweza angalau kupata taarifa ya habari tu. Zipo sababu nyingi zinazodhihirisha hili.

Katika makala yangu ya ijumaa Novemba, 20 – 26, 2015, katika gazeti hili, niliwasihi waheshimiwa wabunge kuhusu kuvienzi viapo vyenu. Niliwakumbusha umuhimu wa maandalizi kabla ya kula viapo, hususan vile vinavyomhusisha Mwenyezi Mungu.  Niliwaomba kutafakari  kwa kina kabla na baada ya kuapa, na kwamba kupata tathmini kamilifu ya  nini maana ya kuapa.

Kutozingatia haya, ni kujifunga kitanzi ambacho kukifungua kutahitaji nguvu za ziada. Sasa mjiulize wangapi mnazo nguvu hizo.

Mtakubaliana nami pia kwamba katika makala hiyo, niliwaasa Waheshimiwa Wabunge kwamba, amtangulizaye Mwenyezi Mungu katika mwanzo wa  utekelezaji wa azma yake anatafuta Baraka.

Ni wazi kwamba atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi wa hali ya juu, kwa vile amesafisha mapito yake kwa kuyatakasa yasiingiliwe na pingamizi lolote.

Na kwamba haya yatakuwa hivyo, iwapo tu mtu hataapa kimzahamzaha. Hataapa kwa minajili ya kutekeleza ratiba iliyopangwa. Hataapa kujifurahisha nafsi yake, wala ya wale wanaomsikiliza kupitia redio au kumtizama kupitia runinga . La hasha. Aaminiye hivyo, amejidanyanga na atahitaji nguvu za ziada kufungua kitanzi alichojifunga mwenyewe.

Hapa namaanisha kwamba, waheshimiwa walioanza safari yao kwa kutoenzi kile walichoapa, pale walipodharau mamlaka iliyopo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tayari wameanza safari yao vibaya, na nathubutu kuwaeleza kwamba huenda wakahitaji nguvu za ziada kusafisa upya mapito yao. Safari hii ndefu ya kutembea kilomita za miaka mitano sijui nani anaweza kuleta jumla ya hesabu yake.

Bila kuzingatia hilo,Mheshimiwa umethubutu kuuvunja utii huo. Na mbaya zaidi unasahau kwamba,uvunjifu huo wa utii, ulishuhudiwa na wanaokutegemea.

Mheshimiwa Baba Mbunge, mkeo, wanao, wazazi wako, ndugu zako, marafiki zako, jirani zako bila ya kuwasahau watanzania waliokuchagua ukawe kisemeo chao, walifuatilia kwa makini ulichokuwa ukikiwakilisha.  

Kadhalika wewe Mheshimiwa Mama Mbunge, mumeo, wanao, wazazi wako, ndugu zako, marafiki zako, jirani zako bila ya kuwasahau watanzania waliokuchagua ukawe kisemeo chao, wakifuatilia kwa makini ulichokuwa ukikiwakilisha.

Nina imani mlio wengi hamkueleweka na wale mnaowawakilisha, na sidhani kama waliamini kuwa wanachoona au kusikia ndicho hicho au walikuwa ndotoni.

Wabunge mlioshiriki zoezi hilo la kudharau mamlaka iiliyowekwa madarakani na watanzania wapatao milioni hamisini (50), mlishindwa kujipanga mkatafuta utaratibu wa busara, wa kueleza yale mliyokuwa nayo mioyoni mwenu.                                                                                                                

Nina imani hali hiyo imewakwaza wengi wenu, hasa hivi sasa mnapobaini kuwa, utaratibu mlioutumia haukuwa na mashiko. Na kwamba, Rais wenu Dk. John Magufuli ni msikivu na kwamba  angeliwasikiliza  iwapo mngempa nafasi awahutubie, baadaye hata kama sio siku ile ile mumwombe kuongea naye, mumweleze yaliyo mioyoni mwenu.

Kwa ushauri tu , ni wakati mwafaka kwenu kutafuta fursa ya kuonana na Rais Mteule, Dk. Magufuli, kupitia kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kwa nia ya kuungama utovu wenu wa nidhamu na kumweleza kilichojili mioyoni mwenu na kupelekea  kuchukua uamuzi huo, ili Rais awaelewe.                                                                                                            

Nina imani, inawezekana, yaliyo mioyoni mwenu si mabaya, na kwamba kwa namna moja au nyingine, yatamwezesha Rais  Magufuli kuona mbele kwa jicho la tatu.

Ni muhimu pia Rais  akawapa fursa hiyo, iwapo mtatumia njia adilifu kwanza kwa kukili mapungufu yenu, na pili kwa kuomba msikilizwe.

Sina utafiti wa kutosha kuhusu kinachoendelea miongoni mwa watanzania takribani milioni hamsini (50) kuhusu safari mpya iliyoanzishwa na Rais Dk. Magufuli ya Tanzania ya 2015/2020. 

Kama mwanahabari, nafuatilia kila aina ya chanzo cha habari. Nikiongeza  vyanzo binafsi,  Rais Dk. Magufuli, amekubalika. Na watanzania wanamuunga mkono katika kuenzi utaratibu aliouanzisha.

Natoa angalizo kwamba, iwapo waheshimiwa Wabunge hamtaenzi viapo vyenu, kibao kinaweza kuwageukia. Kile mlichokionyesha  kule Dodoma, mtakipokea katika majimbo yenu.

Hata kama si wakati huu,  nimeshaeleza awali ya kwamba safari mliyoanza ni ndefu. Urefu wa kilomita za kipindi cha miaka mitano si mchezo mnaweza kushindwa kutoa jumla ya hesabu yake.

Miongoni mwa  walioonyesha utovu wa nidhamu, wamo tunaowagetemea kushika nyadhifa zingine. Kuna nafasi za Mawaziri, Makatibu Wakuu na kadhalika. Ina maana, mtakula viapo vingine kwa ajili ya nafasi hizo.                                                                                                                                                

Ni budi mkajiandaa vilivyo ili yasiwatokee yaliyopita. Ni vema mkaona umuhimu wa kuvienzi viapo, hasa vile vinavyogusa uwepo wa Mungu Mwenyezi. Na muanze kuamini kuwa jina la Mungu halichezewi na kwamba  halifanyiwi mzaha.

VIAPO

Katika Biblia Takatifu, Yoshua Bin Sira 23: 7 –

Kuhusu Viapo anasema:  Wanangu sikilizeni utawala wa kinywa; aushikaye hatakamatwa. Mwenye dhambi katika midomo yake atapatwa, na mshutumu na mwenye kiburi atajikwaa. Anaendelea: Usikizoeze kinywa chako kuapa, wala usifuate desturi ya kulitaja jina lake Mtakatifu. Yaani, mtumishi akichapwa daima hakosi kuchubuka; hivyo aapaye na kumtaja Mungu daima hawezi kusafika dhambi.

Mtu mwenye viapo vingi atajaa uovu. Wala adhabu haitaondoka nyumbani mwake.Akikosa dhambi yake itakuwa juu yake; akitoa kuiangalia ametenda dhambi maradufu. Akiwa ameapa bure hatahakikishwa, kwa maana nyumba yake itajaa misiba.

Read more...

Magufuli akosa mawaziri Fedha, Utalii, Elimu, Ujenzi

Na Waandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli  ametangaza Baraza jipya la Mawaziri huku nafasi nne za Wizara zikiwa bado hazijajazwa.

Akitangaza Baraza hilo mbele ya waandishi wa habari, Dk. Magufuli ametaja Wizara ambazo Mawaziri wake bado hawajapatikana kuwa ni pamoja na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Fedha, Uchumi na Mipango, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara yaa Elimu, Teknolojia na Ufundi Stadi.

Katika Baraza hilo lenye Wizara kumi na tisa na Mawaziri 14 mpaka sasa, Mawaziri saba wa zamani ndio waliorejea tena kwenye Baraza hilo huku Wizara zingine zikiunganishwa.

Mawaziri hao ni pamoja na George Simbachawene aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora ambaye kabla ya uteuzi huo mpya alikuwa Waziri wa Nishati na Madini.

Waziri mwingine kwenye ofisi hiyo aatakuwa Angela Kairuki ambaye kaabla ya uteuzi huo mpya alikuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.Naibu Waziri katika Wizara hiyo ameteuliwa Suleiman Jafo.

Mwingine ni January Maakamba aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na Naibu wake akiteuliwa Luhanga Mpina.


Naye Jenister Mhagama aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu na Bunge kwenye Serikali ya awamu iliyopita amebaki kwenye nafasi hiyo huku Wizara hiyo ikiongezewa majukumu ya kushughulikia maasuala ya vijana, kazi, ajira na walemavu akiwa na Manaibu Mawaziri wawili ambao ni Dk. Abdallah Posi ambaye ameteuliwa pia kuwa Mbunge na Anthony Mavunde.

Naye aliyekuwa Waziriwa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwenye Serikali iliyopita William Lukuvu amebakia kwenye nafasi hiyohiyo akisaidiwa na Naibu Waziri wake Angelina Mabula.

Nafasi ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi imechukuliwa na Mwigulu Nchemba ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa Fedha kwenye Baraza lililopita huku akisaidiwa na William Ole Nasha kama Naibu Waziri wa Wizara hiyo.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini kwenye Serikali iliyopita Profesa Sospeter Muhongo ambaye alilazimika kujiuzulu kutokana na kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow amerejea tena kwenye nafasi hiyo akisaidiwa na Naibu wake Dk.Medard Kalemani.

Dk. Harrison Mwakyembe aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria huku Profesa Makame Mbarawa Mnyaa aliyekuwa Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia akiteuliwa kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Naibu wake Injinia Isack Kamwela.

Waziri mwingine aliyebakia kwenye nafasi yake ileile ni Dk. Hussein Mwinyi aliyebakia kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa JKT.


Mbali na Kairuki na Mwigulu waliopanda ngazi moja kutoka Manaibu Mawaziri na kuwa Mawaziri kamili, Manaibu Mawaziri wengine wa zamani waliopanda nafasi ni pamoja na aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Ummy Ali Mwalimu aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia ameteuliwa Dk. Hamis Kigwangala.

Mwingine ni Charles Mwijage aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Naye aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Charles Kitwanga ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Mawaziri wapya walioteuliwa kuingia kwenye Baraza hilo wakiwemo walioteuliwa kuwa wabunge ni pamoja na Balozi Dk.Augustino Mahiga aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashaariki, Kikanda na Kimataifa na Naibu Waziri wake ni Dk. Suzan Alfonce Kolimba.

Naye Nape Nauye ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo huku Naibu wake akiwa Anastazia Wambura.

Hata hivyo licha ya kutoteua Mawaziri kwenye Wizara nne, Dk. Magufuli ameteua Manaibu Mawaziri kwenye Wizara hizo.

Manaibu hao ni Dk. Ashatu Kijaji aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango huku Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii akiteuliwa Injinia Ramo Matala Maakani.

Naye Injinia Stellah Manyanya ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi akiteuliwa Injinia Edwin Amandus Ngonyani.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amefuta Semina Elekezi iliyopangwa kufanyika kwa Mawaziri wapya walioteuliwa kuingia kwenye Baraza la Mawaziri.

Akizungumza kabla ya kutangaza Baraza lake jipya la Mawaziri Dk. Magufuli alisema kiasi cha shilingi bilioni mbili kilichopangwa kutumika kugharimia semina hiyo kitatumika kugharimia shughuli zingine muhimu za kijamii na kutolea mfano ununuzi wa madawati.

Dk. Magufuli alibainisha kuwa kiasi hicho cha fedha kitajumuishwa na kiasi cha fedha kilichopaswa kulipwa kwa Mawaziri ambao wangeteuliwa katika kipindi cha mwezi mmoja.

Alisema kuwa Mawaziri hao wataelekezana kazi hukohuko mbele ya safari na kuwataka Mawaziri hao kufanya kazi zao vizuri.

Alidokeza kuwa kuchelewa kutangazwa kwa Varaza hilo kumesaidia kuokoa kiasi fulani cha fedha ambacho kingetumika kuwalipa mishahara Mawaziri hao.

Akizungumzia udogo wa Baraza lake la Mawaziri, Dk. Magufuli alisema hatua hiyo italisaidia Baraza hilo kufanya kazi zake vizuri na kwa muda wote sanjari na kuokoa kiasi cha fedha endapo Baraza hilo lingekuwa kubwa.*****

Read more...

Hongera Rais Magufuli lakini…

Na Dk. Felician Kilahama

“HAYAWI HAYAWI HUWA” Kweli hayo ndiyo mapenzi yake Mwenyezi Mungu. Ulimtanguliza mbele wakati wa kampeni zako na sasa yametimia.

Kusema kweli kumtanguliza na kumweka mbele Mwenyezi Mungu kuna faida nyingi. Nimezoea kuwaambia watoto wangu kuwa “ kama baba awahurumiavyo watoto wamchao” ndivyo na Mwenyezi Mungu awavyowahurumia wamchao”.

Kumcha Mungu ni chanzo cha maarifa. Napenda nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kumuinua Mheshimiwa Dk. Magufuli kuwa kinara wa nchi yetu kati ya wagombea wanane kwa kiti cha Urais kupitia vyama vyao.

Sifa na Utukufu tumrudishie yeye aliye hai daima na mwenye uwezo kwa mambo yote Duniani na Mbinguni; yeye aliye Mfalme wa Amani. Naamini kuwa kupitia Dk. Magufuli, akiwa Rais wa awamu ya tano ya utawala wa nchi yetu, amani itaendelea kutawala maana ataliongoza taifa kwa mapenzi makubwa kwa watu wote bila ya ubaguzi wala upendeleo wa aina yoyote. Hongera sana Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Baada ya utangulizi huo, niseme kwamba katika harakati za kampeni ulitoa ahadi nyingi sasa ni kuzifanyia kazi tu. Chamsingi ni kuziweka katika vipaumbele mbalimbali kwa maana kwamba ipi uanze nayo na zipi zifuate na hatimaye kuweza kufanikisha.

Kwa mtazamo wangu elimu ni ufunguo wa maisha na kumwezesha kila mtanzania kufanya mengi anapokuwa ameelimika. Hili ndilo la kuvalia njuga kwanza yaani elimu kwa ngazi zote; waalimu na vifaa shuleni.

Kuna suala la usaalama wa chakula. Tunataka kila mwenye nguvu afanye kazi hakuna kuzembea.  Hii itawezekana iwapo mtu ana uhakika wa kupata chakula. Lakini asiye fanya kazi basi asile.

Wavivu wasipewe nafasi au wazururaji hovyo nao ni adui kwa maendeleo yetu. Kuna suala la upatikanaji wa maji ya kutumia katika nyumba zetu yaliyo safi na salama; tunahitaji maji kuzalisha umeme, tunahitaji maji kwa umwagiliaji na hili linaendana na usalama wa chakula; tunahitaji maji kwa viwaanda vyetu; tunahitaji maji hospitalini, vituo vya afya, kwenye zahanati; tunahitaji maji kwa ajili ya mifugo yetu; tunahitaji maji kwa ajili ya wanyamapori wetu.

Suala la upatikanaji wa maji pia liunganishwe na suala la kuhifadhi Misitu ya asili ambayo ni muhimu sana kwa upatikanaji wa maji nchini.

Hali ya misitu kwa sasa siyo nzuri na ndiyo maana ukame unatuandama. Chemichemi, vijito na mito sehemu kadhaa nchini ni tupu maana hakuna hata tone la maji ni kavu.

Miti inakatwa hovyo, matumizi ya mkaa yamekuwa makubwa sasa usimamizi katika misitu yetu ni duni sana. Ili mazingira ya nchi yetu yasiendelee kuharibika utashi wa kisiasa hasa kwa ngazi za juu kama aliyoipata Dk. Magufuli ni budi uwepo: Misitu Ni Uhai - Tuitunze, Itutunze.

Kuna suala la afya na matibabu ni jambo la msingi sana. Pia uliahidi viwanda ili kupatikane ajira kwa vijana na wasomi wetu na hatimaye kuboresha maisha kwa watanzania wote ikiwepo akina mama ntiliye na wamachinga katika sehemu mbalimbali za Tanzania Bara. Kwa upande wa miundombinu wewe ni mjuzi sana katika eneo hilo. 

Yapo mengine mengi uliyoyaahidi kuyatekeleza na miaka mitano siyo mingi. Utaona kwa maisha ya kila siku yaani “funga (jioni) fungua (asubuhi)” miaka imekwisha na kama hukujipanga vizuri unabaki kushanga nimefanya kitu gani? Usiwape mwanya wapinzani na maadui wako kuweza kupenya na kwa maneno yako; “SASA KAZI TU” tusonge mbele na iwe mbele kwa mbele kurudi nyuma mwiko.

Nimalizie pongezi zangu kwa kuyasema masuala matatu: Moja msingi wa maendeleo ni kwa kila mtu kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Hili liwekewe mkazo sana maana kwa nyakati hizi wengi tumekuwa wavivu tunakimbilia kupata fedha kirahisi (easy money). Usomaji magazeti katika ofisi nyingi za umma unachukua nafasi kubwa kuliko kazi. 

Nidhamu kazini pia imedorora kwa kiasi fulani na hii inasababishwa kwa kuajiri watumishi kwa kujuana, kupendeleana, wakubwa kushinikiza watoto wao au ndugu zao wa karibu waajiriwe wakati hawana ujuzi wa kazi husika au elimu ya kutosha hawana.

Udanganyifu umeongezeka hivyo ukweli katika utendaji wetu umepotea; bora uongo katika siasa kuliko kuongopa katika shughuli za utendaji. Mheshimiwa Rais Mteule, msemo wako: “SASA NI KAZI TU” uwe ndiyo msingi wa kuimarisha utendaji serikalini.

Viongozi wote wawajibike ipasavyo bila ya kuwa na woga au kumwonea mtumishi na watumishi wote watimize wajibu wao ipasavyo. Asiye na kazi za kumtosha apewe kazi za kutosha.

Matumizi ya simu za mkononi wakati wa kazi yaangaliwe maana kupoteza muda mwingi kwa ku-chart na matumizi ya mitandao ya kijamii bila kufanya kazi ni mbaya kwa uhai wa taifa letu na watu wake.

Jambo la pili ni kupambana na mafisadi na wala rushwa. Hili ni tatizo la siku nyingi sasa wakati umefika liwe ni jambo la kihistoria. Watanzania wana imani na wewe sasa fanya kweli. Mianya yote ya rushwa na mifereji ya mafisadi vifungwe au kukomeshwa mara moja.

Usione haya katika hili. Wanzania wamekuchagua wewe kama Magufuli na siyo kuchagua chama kama wangeaangalia chama usingepita wengi wanasema wamechoka na chama kutokana na suala la mafisadi, wizi kwa fedha za umma na rushwa lakini pia na suala la dawa za kulevya.

Mateja yamekuwa mengi kutokana na ulegevu katika kudhibiti uingizaji na matumizi makubwa ya dawa za kulevya. Katika kushughulika masuala haya; umuhimu wa matingatinga ndiyo unapoonekana maana utapasua sehemu zilizoshindikana;

Jambo la tatu ni kuimarisha usimamizi katika sekta zote na kwa ujumla wake. Tatizo letu ni kulegalega shughuli za usimamizi. Kwa mfano, Jiji la Dar es Salaam ni chafu karibu maeneo yote kwa nini? usimamizi haupo wala anayejali hayupo mazingira ya Jiji yanaleta kichefuchefu karibu kila mahali. Tabia za kutupa taka hovyo au kumwaga na kutiririsha majitaka zimekithiri sana.

Je, Jiji halinawasimamizi wake? Kama wapo kulikoni huko?  Mimi naamini kwamba kila mmoja wetu akiwajibika ipasavyo, na usimamizi ukaimarishwa pamoja na viongozi kutimiza wajibu wao bila shuruti; hatutaona uchafu katika maeneo yote ya Jiji la Dar es Salaam miji mingine nchini.

Nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akujalie Baraka zake nyingi uwe na busara na hekima kama alivyokuwa Mfalme Suleiman na akaweza kuliongoza taifa la Mungu vizuri. Yote yawezekana  kwake aaminiye.

Nina imani yatawezekana chini ya Uongozi wako. Mwenyezi Mungu akujalie uunde TEAM nzuri ya kukusaidia katika harakati za kuwaletea maendeleo endelevu wanannchi wa Tanzania. Hakuna shaka tutafika bila shida yoyote.

Hapa ni kazi tu” tuchape kazi tusonge mbele ipasavyo,  mwenyezi mungu awe pamoja nawe uweze kuchangia maendeleo endelevu katika nchi yetu”

End 

Rais Magufuli:Uchaguzi umekwisha tuijenge nchi

Na Alex Kachelewa

Rais mpya wa Awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli amewataka watanzania na viongozi wa vyama vya siasa vya kambi ya upinzani kutambua kuwa uchaguzi Mkuu umekwisha na kilichobaki kwa sasa ni kuijenga nchi.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa shukrani zake kwenye sherehe za kumuapisha kushika nafasi hiyo, zilizofanyika kwenye uwanja wa Uhuru.

Alisema kuwa kilichobaki sasa ni kwa watanzania wote wakiwemo wanasiasa kushikamana pamoja ili kuwezesha ujenzi wa Tanzania bila kujali tofauti zao za kisiasa, kidini na kikabila.

“Ndugu zangu wa upinzani nyingi hakukuwa wapinzani bali mlikuwa washidani wangu sasa uchaguzi umekwisha na mimi John Pombe Magufuli ndiyo Rais hivyo tuache itikadi zetu tushirikiane kuijenga nchi”,alisema Rais Dk. Magufuli.

Aidha Rais Magufuli aliwataka watanzania kumtanguliza Mungu ili awezeshe kutekelezwa kwa ahadi zilizoahidiwa katika kipindi chote cha kampeni.

Rais Magufuli alichukua nafasi hiyo kuwapongeza wagombea wengine saba waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kwa changamoto waliyompatia na kwamba amejifunza mengi kutoka kwao.

Alisema kuwa atahakikisha anafanya anafanya kazi zake kwa nguvu zxake zote ili kufikia na kutekeleza ahadi zote aizozitoa wakati wa kampeni, kwa kama inavyotakiwa na kwa haraka.

Aidha Rais Magufuli aliipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NECO) kwa kufanya uchaguzi ulio huru mbali na vyombo vya usalama vilivyoimarisha amani ikwiemo wanahabari kwa kuwaelimisha raia wa Tanzania.

“Sasa ni kazi tu” alitumia pia nafasi hiyo kuwataka viongozi wa upinzani kushirikiana kwa lengo la kuendeleza na kuwahudumia watanzania na kueleza kwamba anatambua  ana jukumu kubwa la kuwafanyia kazi watanzania,lakini hatahivyo  amewataka watanzania wamuweke Mungu mbele ili kutekeleza ahadi hizo.

Nawashkuru watanzania kwa kunichagua kwa kura nyingi ili kuongoza taifa kwa miaka mitano ijayo lakini pia nawashukuru viongozi mbalimbali waliowasili hapa ili kujumuika nami katika sherehe hii muhimu”,alisema Rais Magufuli akitoa shukrani zake.

Mbali na Dk. Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan naye aliapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othman Chande.

VIONGOZI WA DINI WAMUOMBEA

Awali Akitoa sala kwa ajili ya kumuombea Rais huyo mpya na Taifa la Tanzania, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amemuomba Mungu aendelee kuijalia Tanzania ili amani iliyopo kwa sasa izidi kudumu.

Kardinali Pengo alikuwa akiongoza sala ya kumuombea Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Magufuli kwenye sherehe ya kuapishwa kwake iliyofanyika kwenye uwanja wa Uhuru mjini Dar es salaam.

Alisema kuwa ili amani hiyo iendelee kudumu, Mungu awajalie wananchi wa Tanzania waweze kukabiliana na maovu ya ndani na ya nje ya nchi.

Kardinali Pengo alimuomba Mwenyezi Mungu amjalie hekima na busara Dk. Magufuli ili aongoze nchi kwa kufuata mapenzi ya Mungu.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa alimuomba Mungu amjalie rais huyo hekima ya kuliunganisha Taifa la Tanzania na kulifanya liwe moja bila kuzingatia tofauti za kikabila na kidini.

Alisema kuwa Rais huyo pia anatakiwa kutenda kazi zake kwa misingi ya haki, pasipo kuogopa jambo lolote.

Naye Sheikh Mkuu wa Tanzania Abubakar Zuber Ali alimuomba Mungu amuongoze Dk. Magufuli na wasaidizi wake ili aiongoze nchi kulingana na mapenzi ya Mungu.

Sherehe za kuapishwa kwa Dk. Magufuli zilihudhuriwa na viongozi kutoka mataifa kadhaa ya Afrika na dunia kwa ujumla.

Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na                            Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa, ambapo amehudhuria kwenye tukio hilo ikiwa ni siku moja tangu kuzagaa kwa uvumi kuwa alikuwa amefariki dunia.

Rais Mstaafu Mkapa aliyekuwa amekaa karibu na Rais Mstaafu mwingine wa awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi huku akionekana akiwa na afya njema.

Jumatano ya Novemba 4, mwaka huu Serikali kupitia kwa Msemaji wake Assa Mwambene ilikemea taarifa hizo zilizozushwa hususan kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kuhusiana na uvumi huo.

Katika taarifa hiyo Mwambene aliitaka jamii kuacha tabia ya uzushi na kutunga taarifa zisizo na ukweli wowote kwani kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika.

Magufuli ni Nani?

Dk. John Pombe Joseph Magufuli, alizaliwa Oktoba 29, mwaka 1959 wilayani Chato – wakati huo ikiwa Mkoa wa Kagera (sasa Mkoa wa Geita).


Ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia aliyoipata mwaka 2006 – 2009 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka 1991 – 1994, alisoma Shahada ya Uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na baadaye Chuo Kikuu cha Salfordnchini Uingereza.

Mwaka 1985 – 1988, alisoma Shahada ya Kwanzaya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.

Mwaka 1981 – 1982, alisoma Stashahada (Diploma) katika Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.

Mwaka 1979 – 1981, alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Mkwawa, mkoani Iringa.

Mwaka 1977 – 1978, alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza.

Mwaka 1975 – 1977, alisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera.


Mwaka 1967 – 1974, alisoma Shule ya Msingi, Chato.

Mafunzo
Machi 1984 – Juni 1984 alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani Dodoma.

Januari 1984 – Machi 1984 alikuwa JKT Makuyuni, Arusha.
Julai 1983 – Desemba 1983 alikuwa JKT Makutupora, Dodoma.

Uzoefu wa kazi
Mwaka 2010 – hadi anakuwa Rais alikuwa Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato.


Mwaka 2008 – 2010 alikuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki; Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato).

Mwaka 2005 – 2008, alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato).

Mwaka 2000 – 2005 alikuwa Waziri wa Ujenzi, na Mbunge wa Biharamulo Mashariki.


Mwaka 1995 – 2000 alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Biharamulo Mashariki.


Mwaka 1989 – 1995 alikuwa Mkemia Chama cha Ushirika cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.), mkoani Mwanza.

Mwaka 1982 – 1983 aliwahi kuwa Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema (akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati).


Dk. Magufuli amepata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi na ameshiriki na kuongoza mikutano mingi ya Kitaifa na Kimataifa.

End 

Read more...

Wafanyabiashara wawatoa hofu Wakulima

Na Ashura Kishimba

 

Wafanyabishara wa soko la Buguruni jijini Dar es Salaam, wamewatoa hofu wakulima nchini waliyokuwa wakiogopa kuvuna na kusafirisha mazao yao kutokana na harakati za uchaguzi Mkuu kwani hali ilivyo sasa ni shwari.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Tumaini Letu sokoni hivi karibuni wafanyabiashara hao walisema hali ya biashara hivi sasa sokoni hapo ni ngumu kutokana na uchache wa mizigo inayoingia sokoni hapo.

 

Habiba Salumu na Fatuma Hussen ni wafanyabiashara wa nyanya walisema mzigo wa bidhaa hiyo unaoingia sokoni hapo kwa hivi sasa ni kidogo hali inayosababisha biashara kuwa ngumu kwa kuwa wateja wao hawafiki na matokeo yake wanajikuta wakiuza kwa bei ya hasara.

 

Walisema kwa sasa wananunua tenga moja la nyanya kwa shilingi 35,000 hadi 40,000 na wao kwa kawaida huuza kindoo kidogo maarufu kisado kimoja kwa Shilingi 5,000 lakini hivi sasa huuza kwa Shilingi 3,000 au 3,500.

 

Waliwashauri wakulima nchini kutoogopa harakati za uchaguzi kwa kuwa zimekwishapita na kuwataka kupeleka mazao yao kwa wingi sokoni hapo.

 

“Wakulima wasiogope walete tu mazao yao kwa wingi hapa sokoni hali hivi sasa ni swari;” alisema Habiba.

 

Kwa upande wake Hamza Abdalla, alisema biashara hivi sasa imesimama kwa ababu wananchi wengi walinunua vyakula kwa wingi wakahifadhi ndani kwa kuhofia machafuko ya uchaguzi na kwamba wanaojitokeza sokoni hapo kununua bidhaa ni wachuuzi ambao wanakwenda kutembeza barabarani na wengine kwenye magenge yao nyumbani.

 

Abdallah alisema awali walikuwa wakinunu gunia la vitungu kwa shilini 110,000lakini hivi sasa wananunua shilingi 130,000 hadi 160,000.

 

Salumu Hamisina Mwinyi Haogwa ni wafanyabiashara wa matunda wamesema ingawa matunda yameonekana kuanza kuingia sokoni hapo, bado siashara sio nzuri kwabababu wanayanunua kwa bei kubwa robota moja hununua kwa shilingi 70,000 hadi 80,000.

 

Walibainisha kuwa matunda kama maembe hivi sasa wanategemea kutoka Mkoa wa Tabora na Mbeya Pwani Mikoa ya Pwani bado matunda ni machache na hata Mikoa inayoleta matunda hayo inalazimisha lakini matunda yenyewe bado hayajakomaa vizuri.

 

End 

Read more...
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.