Menu
RSS
Tanzania

Mwaka wa Huruma ya Mungu uwabadilishe waamini-Padri

Na John Liveti

Paroko wa Parokia ya Matakatifu Kamili Yombo Kiwalani Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam ambaye pia ni Mmisionari wa  Shirika la Mtakatifu Kamili,  Padri Festo Liheta  amelaani vikali tabia za  waamini kujichimbia na kukaa  uchumba sugu  bila  ya kufunga ndoa kwani kufanya hivyo ni kukufuru Mungu na kujitafutia laana  na balaa maishani.

Padri LIheta alisema hayo hivi karibuni wakati wa Adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ya  somo wa Parokia hiyo  Mtakatifu Kamili, iliyofanyika parokiani hapo  na kuwashirikisha waamini wa Parokia hiyo na wengine kutoka nje ya Parokia.

Alisema kuwa kwa muamini wa Kanisa Katoliki hapaswi kujifungia masakramenti yeye mwenyewe kwani Mungu alimuumba mwanadamu akiwa na utashi wa kutambua mema na mabaya.

Alisema katika Jubilei ya Huruma ya Mwenyezi Mungu ni wajibu wa kila muamini kujitafiti kuhakikisha anakuwa mstari wa mbele kushiriki Sakaramenti mbalimbali za Kanisa ili kujichotea neema  kwani Sakramenti hizo hazina masharti yoyote lakini  utakuta watu wanaogopa kutoka na msongo wa dhambi zao inayotokana na matendo maovu wanayofanya ambayo hayampendezi Mungu.

Padri Liheta alisema  katika mwaka huo wa huruma ya Mungu, Kanisa limeaalika kila mmoja kujitafiti lakini kwa namna ya pekee mapadri wamealikwa kuwahurumia  watu kwa  kuwatembelea na kuwafariji wote wanaoteseka  katika shida mabalimbali ikiwemo ya kutopata Sakramenti za Kanisa.

Kwa mujibu wa Padri Liheta, katika Parokia ya Mtakatifu Kamili Yombo,  uongozi wake umefanikisha hayo na kuwa kielelezo katika Jubilei hiyo ya Huruma ya Mungu na Parokia inaposherekea somo wake.

Alisema katika hilo Parokia imeunganisha matukio yote kuhakikisha kuna kumbukumbu za   maalumu ambayo mojawapo ni kuwavua watu walio katika maisha ya  uchumba  sugu ambayo kwa sasa wengine wanaita wanaoishi katika uzinzi  sugu.

Padri Liheta  alisema miongoni mwa watu ambao wanaokata tamaa zaidi ni wanawake ambao hawawahamasishi Wanaume kuingia katika maisha ya ndoa.

Alisema hali kama hiyo ilimtokea mama yake Mtakatifu Kamili ambapo katika maisha yake ya Ndoa na mume wake, Geovani baba yake Mtakatifu Kamili  na mama yake Kamili yaani Kamila waliishi bila kupata mtoto kwa kipindi kirefu  hadi alipofikia miaka 60 ndipo alipopata mtoto jambo lililowashangaza watu wengine.

Alisema katika miaka hiyo yote  mama huyo alitegemea sana Huruma ya Mungu ambayo ilimjalia hadi  wakafanikiwa kupata mtoto ambaye hadi leo Kanisa  linamtumia  kuwa somo wa wagonjwa.

Licha ya Kuwa Mtakatifu Kamili kiasili alikuwa ni Askari Jeshi aliyefanya kazi kuwahudumia wagonjwa  jambo ambalo lilimgusa zaidi kwani awali wagonjwa walikuwa wakihudumiwa na wafungwa.

“Hii ilikuwa kama adhabu kuhudumia wagonjwa lakini katika kuguswa kwake  aliamua kuacha kazi ya Jeshi na na kuamua kuanzisha Shirika kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa jambo ambalo alifanikiwa na Shirika hilo likaitwa la Makatifu Kamili”,alisema Padri Liheta.

Padri Liheta  aliwataka waamini kutoka na historia fupi na maelezo ya familia ya wazazi wake Mtakatifu Kamili waichukue kwa uzito wa pekee  kwa waamini  hasa akinamama kuacha kukata tamaa mapema  kwa kile wanacholalamika kutopata watoto.

Katika azimisho hilo la Misa takatifu  aliwapokea watoto 39 katika Sakramenti ya Ubatizo  na kuwaingiza rasmi kwenye Ukristo  huku akiwataka wazazi wa watoto hao  kuhakikisha wanawalea watoto katika maadili.

Alisema katika ziara za Mapadri  katika Kaya za waamini ndizo zilizoza matunda ya kuibua hayo katika kuwavua hasa hizo jozi 33 kuingia katika maisha mapya ya masakramenti na kuondoka katika dimbwi la kuishi uzinzi sugu.

Alibainisha kuwa miongoni mwa  walifunga ndoa hizo wengi wao wameishi kwa muda mrefu katika uchumba sugu wengine zaidi ya miaka  15.

Read more...

Parokia Chalinze kuadhimisha Jubilee miaka 50

 

Na Bruno Bomola

PAROKIA ya Chalinze Jimbo Katoliki la Morogoro inatarajiwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Parokia ya Mtakatifu Yohane Mwinjili Chalinze ni miongoni mwa Parokia kongwe zilizopo katika Jimbo Katoliki la Morogoro iliyoanzishwa mwaka 1968.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Chalinze, Cosmas Msemwa ameliambia gazeti hili katika mahojiano maalum kwamba Parokia ya Mtakatifu Yohane Mwinjili Chalinze ina jumla ya vigango 16.

Alisema kuwa vigango hivyo vimegawanyika katika Kanda Kuu nne na kati ya vingango hivyo vipo ambavyo vinatarajiwa kuwa parokia.

Msemwa amevitaja Vigango hivyo kuwa ni Kingango cha Bwawani ambacho tayari kimekamilisha nyumba ya ibada na kuendelea hivi sasa na nyumba ya  Mapadri pamoja na Masista na Kigango cha Mdaula ambapo ujenzi wake mkubwa kidogo vyote hivyo vikikamilisha vitu muhimu vitatangazwa kuwa Parokia kamili.                                                  

Hadi sasa Parokia hiyo ina jumla ya kwaya mbili ambazo ni Kwaya ya Mtakatifu Francisco  Ksaveri pamoja na kwaya ya Kristo Mfalme inayoongozwa na Vijana Wakatoliki Wafanyakazi (VIWAWA) zinafanya kazi ya uinjilishaji katika ibada na shughulu mbalimbali za ndani na nje ya parokia.

Akizungumzia suala la maendeleo, Msemwa alisema  parokia hiyo ina shule ya chekechea lakini pia inajiandaa kuanzisha miradi mbalimbali  ya maendeleo.

“Shida iliyopo na inayotupata mapaka sasa walei wa parokia ya Chalinze hatuna mradi wowote wa maendeleo ambao utatuongezea kipato kwa namna moja ama nyingine tulikuwa na mpango endelevu wa kujenga vibanda na kupangisha lakini mabadiliko ya mababa wa kiroho mara kwa mara imekuwa changamoto”,alisema Msemwa.

Alibainisha kuwa parokia hiyo kwa sasa eneo lililopo tayari lipo katika mipango ya kufanya shughuli za kimaendeleo pamoja na kujenga maduka pembeni na shule ya chekechea ambayo yatapangishwa.

Alisema kuwea kwa kupitia michango ya waamini wanajipanga kununua gari gari ambalo litakuwa likitumiwa na mapadri kwani kwa muda wote walishindwa kununua gari kutokana na maparoko waliopita walikuwa wakija na magari yao.

Naye Mweka hazina wa  Parokia hiyo, Peter Mlai alisema kuwa changamoto kubwa linalofanya wasipige hatua ni kuwepo kwa ufinyu wa eneo la kanisa na kuwa na uzio wa kuzunguka kanisa jambo linalofanya kudhorota kwa baadhi ya shughuli za kanisa.

Alisema kuwa waamini tunatakiwa kushikamana na kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanachangia na kuwezesha parokia kupiga hatua na kuwa mfano wa kuigwa.

Mataifa ya Afrika, Asia na changamoto ya lishe bora

Na CELINA JOSEPH.

MOJA ya vitu vinavyoyafanya Mataifa ya Bara la Afrika na Asia kuwa na changamoto ya watoto wenye utapiamlo kwa kiwango kikubwa ni uliji duni.

Bado mataifa ya mabara hayo yana changamoto kubwa katika uboreshaji afya ya jamii na kusababisha utapiamlo, ambao ni hali mbaya ya lishe inaweza kuwa pungufu au iliyozidi.

Nchini Tanzania tatizo la lishe bora ni moja ya changamoto zinazoikabili jamii, hii ni kutokana na jamii kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu lishe, na hali duni ya maisha.

Hizo ni baadhi ya sababu za utapiamlo ili kuzuia utapia mlo ni muhimu kufahamu sababu hizo ambazo ni pamoja na ulaji duni wa chakula unaotokana na kula milo michache na kiasi kisichotosheleza mahitaji ya virutubishi mwilini, ikiwa ni pamoja na kutokuwanyonyesha watoto ipashavyo.

Magonjwa ya mara kwa mara huondoa hamu ya kula, husababisha ufyonzwaji duni wa virutubishi na huongeza mahitaji ya virutubishi mwilini.

Magonjwa hayo ni pamoja na kuharisha, malaria na magojwa ya mfumo wa hewa.

Utapiamlo huathiri afya kwa ujumla, uzalishaji mali na maendeleo katika jamii, nyingine ni kupungua kwa uwezo wa akili kwa watoto na kumfanya mtoto kuchelewa kuanza shule, kurudia rudia darasa sababu hana uwezo wa kufikiri haraka na kudaka mambo.  

Zaidi ya asilimia 40% ya viwango vya utapiamlo katika maeneo ambayo watoto walio chini ya miaka mitano nchini wanakabiliwa na hali ya utapiamlo, hasa katika mikoa ya Dodoma, Kagera, Njombe, Iringa, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Katavi na Geita takwimu hizo ni kwa  mujibu wa Taasisi ya chakula na lishe nchini Tanzania.

Kwa Mama anayenyonyesha ni muhimu kumnyosha mtoto ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa, anyonyeshwe kila wakati usiku na mchana, na aendelee kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila hata maji katika miezi sita ya mwanzo.

Imekuwa ni mazoea kusikia maziwa ya mama ni muhimu kwa mtoto mchanga hadi miezi sita, na kufanya wamama wengi kupuuza kauli hiyo ambayo inaelimu ndani yake ili kumkinga mtoto na hali ya utapiamlo.

Mazoea mengine miongoni mwa jamii yanatakiwa kuyaachwa mfano kumpa mtoto maji akingali mchanga ili hali wataalamu wa afya wanashauri kumnyonyesha mtoto maziwa pekee kwa kuwa maziwa hayo yanavirutubisho vyote ikiwa pamoja na asilimia kubwa ya maji ndani ya maziwa ya mama.

Tena yana maji yanayoweza kutosheleza kukata kiu ya mtoto wake kwa miezi sita ya mwanzo.

Katika kupambana na hali ya utapiamlo miongoni mwa jamii wapo wamama wengine  ni wafanyakazi maofisini wakati huo wananyonyesha ni vema na busara pia mwajiri kutekeleza sheria na miongozo inayolinda haki za wanawake wanaonyonyesha.

Mama anayenyonyesha anastahili kupewa siku themanini na nne (84) za likizo ya uzazi pamoja na likizo yake ya mwaka.

Aidha mwenza wa mama aliyejifungua anastahili kupewa siku tatu (3) za likizo ya uzazi hii ni kwa mujibu wa Taasisi ya chakula na lishe  Tanzania.

Kazi inatafsiriwa kwa upana ikijumisha kazi ya kuajiriwa, kujiajiri ,kazi za muda mfupi au mikataba na kazi zisizo za kulipwa kwa mfano kazi zilizo katika mazingira ya nyumbani  zikiwemo kazi za shamba, mifugo na kutunza familia.

Tunapoelekea kumaliza mwaka tukiwa pia katika uongozi mpya wa awamu ya tano hatuna budi kulitupia macho suala hili la utapiamlo ambalo kwa kiasi fulani huwezi kuona iwapo hujishughulishi na mambo ya lishe.

Taasisi ya chakula na lishe Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine wa masuala ya lishe wamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu na matamko mbalimbali ili kuwafikia wanajamii popote Tanzania, na kwamba kwa pamoja kutokomeza utapiamlo inawezekana.

Tangu mwaka 2000 wataalamu wa mambo ya lishe walipitia upya na kuridhia kanuni namba 183 ya shirika la Kazi Duniani( ILO) na mapendekezo namba 191 juu ya ulinzi wa haki za uzazi ya mwaka huo wa 2000.

Hatua hiyo imesaidia kuboresha stahili za wanawake wakati wa uzazi na mipango yenye lengo la kutetea sheria, lakini taasisi ya chakula na lishe Tanzania hivi karibuni ilidokeza kuwa juhudi katika kuboresha utoaji wa msaada kwa upande wa wanawake mahali pa kazi katika sekta zisizo rasmi, majumbani na mashambani hazirizishi, na mifumo ya jamii haijaimarishwa ipasavyo kusaidia wanawake waweze kunyonyesha watoto wao.

Tunapoelekea kufunga mwaka, yapo mambo mengi ya kuzingatia na kuyaendeleza, ili kuiokoa jamii yetu na janga la utapiamlo, la kwanza linaweza kuwa ni kutambua kulinda na kuthamini kazi za nyumbani ambazo sio ajira rasmi zinazofanywa na wanawake wanaonyonyesha.

Serikali kutenga bajeti ya kutosha katika kutoa elimu ya lishe, kwa wananchi hasa waliomijini na vijijini, pia katika kilimo ili kuinua kilimo cha mtu wa hali ya kawaida ili aweze kuzalisha mazao yanayoweza kupatikana katika eneo lake.

Pia kuboresha elimu ya ufugaji, na kilimo cha matunda na mboga mboga kwa kufanya hivyo Tanzania ambayo iko katika hatu yakuridhisha kwa sasa katika kiwango cha utapiamlo itakuwa imepiga hatua.

Mwaka 2015 kwa mujibu wa Taasisi ya chakula na lishe Tanzania umekuwa mwaka wa kupima utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia na kuanza utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals).

Malengo hayo yanajumuisha kiashiria cha unyonyeshaji watoto maziwa ya mama pekee” ili kuhakikisha kuwa suala la unyonyeshaji linapewa nafasi katika mpango wa maendeleo katika sekta ya afya na lishe nchini. 

Shirika la Kimataifa la utetezi wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama tangu mwaka 1993 limetoa ufafanuzi wa kazi za mwanamke kwa upana wake kuanzia ajira yenye malipo, kujiajiri mwenyewe, kazi za msimu na za mkataba hadi kazi zisizo na malipo za nyumbani na kuhudumia familia.

Taasisi ya chakula na lishe nchini inasema suala la utetezi wa mwanamke na majukumu ya nyumbani ni changamoto kubwa, kwa kuwa mwanamke hufanya kazi nyingi lakini mara nyingine anakabiliwa na ubaguzi wa kijinsia, kupigwa na unyanyaswa.

Kwa upande mwingine Taasisi hiyo inamwangalia mwanake kuwa ndio mtu muhimu wa kuelimishwa na kuwezeshwa kwa majukumu mbalimbali yakiwemo ya elimu juu ya lishe kwani mwanamama akiwa na elimu atasaidia ulaji bora wa familia na kuepukana na tatizo la utapia mlo ambalo ni janga linaloweza kuzidi iwapo mama hatakuwa na elimu ya kutosha.

Hata hivyo kwa wale wasio katika mfumo rasmi na walio nyumbani, wanahitaji kufahamu haki zao za afya ya uzazi, chakula na usalama, haki ambazo zimeainishwa katika mikataba mingi ya Kimataifa na Kitaifa.

Mpango wowote unatakiwa kuoanisha ajira na kazi zisizo na malipo na uzazi, ni lazima  umwezeshe ili asiwe mtu wa kutegemea misaada, bali awezeshwe na kusaidiwa.

Jamii inatakiwa kuzingatia na kusikiliza mahitaji wa mwanamke na kuheshimu mawazo yao katika uzalishaji, malezi ya watoto na kuwasaidia bila chuki, upendeleo au maslahi ya kibiashara.

End 

Read more...

MAASKOFU WATOKA SABABU MIITO MITAKATIFU KUPUNGUA

  • Published in Tanzania

Na Waandishi Wetu

Mwaka huu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam lilizizima kwa shangwe, nderemo na vifijo katika Parokia mbalimbali ambako ziliadhimisha Sakramenti Takatifu ya Kipaimara.

Huenda hii ilikuwa ni mara ya kwanza na itabakia kuwa kumbukumbu kutokana na karibu robo ya idadi ya Parokia za jimbo hilo zilitembelewa na Maaskofu kutoka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini.

Katika siku hiyo Parokia 21za Jimbo hilo ziliweza kuifanya ile siku aliyoifanya Bwana kwa staili ya kipekee kuanzia mapokezi ya Maaskofu, ibada na baadaye tafrifa parokiani na hata majumbani.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Josaphat Luis Lebulu aliadhimidha Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa huruma, Mbezi Beach, ambapo vijana 26, walipokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara na kukabidhiwa tuzo ya vyeti maalum kuthibitisha hatua waliyofikia katika Imani Katoliki.

Askofu Mkuu Lebulu aliwapongeza Waimarishwa wa Sakramenti ya Kipaimara kwa hatua ya kuwa Askari imara wa Yesu Kristo na kuwataka wairutubishe imani yao kwa kujiunga na miito Mitakatifu.

Aliwakumbusha na kuwataka Waamini washiriki vyema Jumuiya ndogondogo za Kikristo ili kujiimarisha kiimani na kujitakatifuza katika malimwengu.

“Mimi mwenyewe ninaamini kwamba Jumuiya ndogondogo ni mhimili muhimu wa Kanisa ambako familia zinashirikishana maisha ya kiroho na kimwili, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”,alisema Askofu Lebulu.

Aliwakumbusha Waamini kutilia mkazo ushiriki wao katika mambo yanayomhusu Mungu zikiwemo Sakramenti za Kanisa badala ya kujielekeza kwenye malimwengu yanayowatenga na upendo wa Mungu. 

Askofu Mkuu Lebulu, aliwashukuru Mapadri na Waamini wa Parokia hiyo kwa mapokezi mazuri na zawadi ambazo hakuzitarajia akiahidi kuziwasilisha kwa wenzao wa Jimbo Kuu la Arusha kwa ajili ya kuliendeleza Kanisa.

Naye Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mama wa huruma Mbezi Beach Padri Timothy Nyasulu Maganga alimshukuru Askofu Mkuu wa Jimbo kuu Katoliki la Arusha Mhashamu Josaphat Lebulu kwa kupeleka baraka zake katika parokia hiyo.

Padri Nyasulu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa (PMS), Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, alimtakia heri na baraka za Mungu Askofu Mkuu huyo katika kazi yake ya kichungaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Walei wa parokia hiyo, Donesta Byarugaba alisema parokia hiyo imepiga hatua kubwa katika maendeleo ya kimwili na kiroho licha ya changamoto zinazoikabili.

Alizitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na waamini wengi hasa akinababa kutoshiriki kwenye Jumuiya ndogondogo za Kikristo na baadhi kuendelea kuishi maisha ya Mume na Mke bila kufunga ndoa.

Byarugaba alimhakikishia Askofu Mkuu Lebulu kuwa uongozi wa Parokia ya BMMH umeweka mikakati thabiti na unafanya jitihada mbalimbali ili kuweza kuondokana na changamoto hizo.

Aliwashukuru Viongozi wa Vigango, Vyama vya Kitume, Kanda na Jumuiya za Parokia hiyo kwa ushirikiano mkubwa katika maandalizi, mapokezi ya Askofu Lebulu na adhimisho hilo la Kipaimara katika Parokia hiyo.

“Natoa shukurani kwa kila mmoja wenu ambaye baada ya kupokea Taarifa ya ujio wa Askofu Mkuu Lebulu, ameshiriki kikamilifu kuanzia maandalizi hadi leo, kwa kweli tumeweza” alisema Byarugaba

ASKOFU MINDE:TETEENI IMANI YENU IKIBI HATA KUFA

Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama Mhashamu Ludovick Minde amewataka waamini Kanisa Katoliki kutetea imani ya Kanisa lao mahali popote bila kuhofia jambo lolote ikimlazimu kufa kwa kutetea imani ya Kanisa.

Askofu Minde alitoa rai hiyo katika adhimisho la Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyofanyika Dominika iliyopita katika Parokia ya Mtakatifu Agustino Salasala.

Alisema baadhi ya waamini wa Kanisa Katoliki wamekuwa waficha imani yao kwa hofu hasa wanapokuwa kwenye mikusanyiko ya watu au wanapokuwa wanakula, wanaogopa hata kusali kwa kufanya ishara ya Msalaba.

Aliwataka waamini hao kutokuwa na waonga wowote na badala yake kusimama imara katika kuipeperusha bedera ya Kristo na kuitangaza imani ya Kanisa Katoliki popote watakapokuwa.

Aidha Askofu Minde aliwapongeza Waimarishwa wa Sakramenti ya Kipaimara kwa hatua ya kuwa Askari imara wa Yesu Kristo na kuwataka wairutubishe imani yao kwa kujiunga na miito Mitakatifu.

Katika adhimisho hilo jumla ya vijana 125 kutoka Parokiani hapo na Vigango vya Parokia hiyo wamepokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara ambapo walikabidhiwa Tuzo ya vyeti maalum kuthibitisha hatua waliyofifikia katika Imani Katoliki.

                                

Askofu lyimo: mtangazani kristo bila uoga

Askofu  Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha Mhashamu  Prosper Lymo amewataka waimarishwa na waamini kumtangaza Yesu Kristo na kuwa askari hodari hata wakati wa mateso na mahangaiko.

Ametoa wito huo kwenye adhimisho la Sakramenti Takatifu ya Kipaimara iliyofanyika Dominika ya 12 ya mwaka C wa Kanisa, katika Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mkuu Mtume Kijitonyama Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Askofu Lyimo  amebainisha kuwa Sakramenti ya Kipaimara bwana anawapaka mafuta anawaimarisha kuwa na nguvu na kueneza  Injili bila kuwa na uwoga.

“Msiogope kumtangaza Kristu na kuwa shupavu pindi mtakapokutana na majaribu msikate tamaa bali mnatakiwa kushikamana na kusonga mbele kwa kumtangaza bwana wetu Yesu Kristo”,alisema Askofu huyo.

Amewakumbusha wazazi na walezi kuwatilia mkazo na kuwakumbusha waimarishwa kumtumikia Mungu katika shughuli mbalimbali za Kanisa kuliko kuwaacha na kupotelea kwenye makundi mbalimbali ya malimwengu.

 Katika adhimisho hilo la jumla ya vijana 40 wamepokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara  na kukabidhiwa tuzo ya vyeti maalum kuthibitisha ukristo wao ndani ya Kanisa Katoliki.

askofu sangu alia na maadili kwa vijana

Askofu  wa Jimbo Katoliki la Shinyanga  Mhashamu Leberatus Sangu amewataka vijana waliopokea Sakaramenti ya Kipaimara kujitahidi kujenga  uadilifu na uaminifu katika yale wanayotenda.

Askofu Sangu alisema hayo kwenye Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Paroki ya Mtakatifu Agostino  Temboni  Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kuwataka waamini kujitafakari wapo na  kuwa chimbuko la upendo.

Askofu Sangu aliwataka  Wazazi kushirikiana na  na watoto wao hasa kuwaelekeza na kuwapatia malezi bora  kwani wapo wazazi ambao wakifika nyumbani hapakaliki na hivyo kuwafanya watoto kujisikia kama wapo kifungoni.

Aliwataka vijana hao kujijenga zaidi  kwa kushikama na mapaji ya Roho Mtakatifu kuhakikisha wanakuwa wajumbe wazuri kwa wengine kwa kuwalisha Neno la Mungu.

Alibainishi katika ulimwengu wa leo una chanangamoto nyingi hivyo wanatakiwa kusimamamia ukweli wa imani kwa kuyaishi maadili ya Kanisa.

Adhmisho hilo la Misa takatifu lilikwenda sanjari na utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa Vijana 131 kutoa parokiani hapo na  Kigango cha Mzingwa.

Akizungumza na viongozi mbalimbali wa Jumuiaya vyama  vya Kitume  na Kamati ya Kigango cha Msingwa na Kamatiti tendaji ya Parokia ya Temboni, Askofu Sanguali alitumia nafasi hiyo kuwataka viongozi hao kusimamia na kuongoza vyema kwa  wale wanaongoza hasa kuhakikisha wansimamia ukweli  kwa kuwafundisha mafundisho yaliyo sahihi ya Kanisa katika Mwaka huu wa Huruma ya Mungu.

Askofu Sangu  aliwataka Viongozi hao pia kuwa Mabalozi wazuri kuahakikisha watu  wanazaliana ili kuliongoza Taifa la Mungu  kwani itafika wakati kutakuwa hakuna Miito Mitakatifu kutokana hali ya watu kutopenda kuzaa watoto wengi katika nyakati  za sasa.

Alisema bila kuzaliana ni kazi bure kwani Mungu aliumba wanadamu ili waweze kuzaa na kuijaza nchi ili kazi za Mungu ziweze kufanyaka  lakini kwa sasa jamii imeiga tabia za wageni kutoka nje kwa kuweka uzazi wa mpango hilo si sahihi.

Habari hii imetayarishwa na Alex Kachelewa, Bruno Bomola, John Liveti na Gaudence Hyera.

 

Read more...

Viongozi watakiwa kushirikisha wananchi kufanya maamuzi.

Na Janepher John, UDSM

 Viongozi wa nchi zinazoendelea wametakiwa kuleta maendeleo yanayolenga kujenga  jamii kujitegemea, kuleta haki katika jamii na kushirikisha wale wanaowatawala katika kufanya maamuzi kwa maendeleo ya nchi.

Hayo yamesemwa na viongozi wa nchi mbalimbali, wasomi, watu mashuhuri na wanadiplomasia katika Kongamano la nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimun Nyerere, Profesa Penina Mlama alisema kongamano la Mwalimu Nyerere limekuwa likisaidia kuenzi fikra za Mwalimu katika kuleta maendeleo kwenye nchi zinazoendelea.

Kongamano hili la nane linaenda na kauli mbiu isemayo “Mwalimu Nyerere na mtazamo wa kimaendeleo uliojikita katika misingi ya watu” na kongamano la mwaka jana lilikuwa na kauli mbiu isemayo “ubinafsishaji na haki za jamii kwa wanyonge”,alisema Mwenyekiti huyo.

Naye kwa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alimzungumzia Mwalimu Nyerere kuwa ni kiongozi ambaye alitoa haki kwa watu wote, mpinga matabaka, mkombozi, mpenda umoja kati ya nchi zinazoendelea na alihimiza kujitegemea mambo ambayo yanapaswa kuigwa na viongozi wote  wa nchi za dunia ya tatu.

Mkapa alisisitiza kuwa uongozi wa zamani waliokuwa nao kina Nyerere na Nkwame Nkurumah ni uongozi ambao viongozi wa Afrika na nchi nyingine zinazoendelea wanatakiwa wafuate nyayo zao ili kuleta maendeleo kwa watu.

“Makubaliano ya mabadiliko yako pale na yanajulikana vizuri lakini hatutaona mababiliko yoyote kwa sababu nchi zilizoendelea hazitayaruhusu”,alisema Rais Mkapa.

Alisema kuwa nchi nyingi za dunia ya tatu hazipendi mitazamo ya nchi zilizoendelea lakini haziko tayari kupiga hatua zenyewe bila kutegemea nchi zilizoendelea na kufuata sera kwa manufaa ya nchi zote zinazoendelea.

Aidha Mkapa alikiri kuwepo kwa madhaifu mbalimbali katika uongozi katika nchi za Afrika na nyingine zinazoendelea hususan Tanzania kuhusu suala la uwekezaji.

 “Ilikuwa ni kipindi kigumu cha ubinafsishaji {Privatization}, lazima tuwe na Instrument lakini wakati huo haikuwa na mamlaka na isingeweza yenyewe kufuatilia maendeleo ya privatization tulifanya makosa:

Lakini hio lilichukuliwa sio kodi ya kuzuia privatization” alisisitiza kuwa uwekezaji wa ndani lazima uongezeke na tuache kulalamika na kulaumu serikali, tukusanye nguvu ili tuweze kushindana na wawekezaji kutoka nje”,alisema.

Aidha Mkapa alikiri kuwa kiongozi  lazima asikilize wale anaowaongoza ili kuleta maendeleo katika nchi kwani marehemu Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo mkubwa wa kusikiliza watu wasomi na wasiosoma na hii ilisaidia kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

 Mkapa aliongezea kuwa licha ya kuwa kiongozi lazima asikilize lakini watu wengi wanapenda kuzungumza wao badala ya sera na kuwataka  wasomi, vijana na viongozi kama wabunge waache kulalamika na kutupa kila mzigo kwa serikali na kusema kila mtu kwa nafasi yake anawajibu wa kujenga nchi.

Naye , Profesa Mugira Mwase Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM), anasema kuwa uwajibikaji wa viongozi sio lazima Rais aseme lakini viongozi wa kawaida kama Meya na Madiwani lazima wafuatilie mambo katika maeneo yao.

Aidha uwajibikaji wa viongozi uliungwa mkono na Generali Ulimwengu aliyesema “ naona na ninabaini sasa kwamba viongozi wetu kwa bahati mbaya wanapata busara baada ya kuacha nafasi zao za uongozi”.

Naye mwanasiasa mkongwe Abdulrahaman KInana anasema kuwa sio sahihi kudai kuwa wewe ndio unamiliki ukweli, hekima na haki lazima uwe tayari kusema nadhani hapa nilikosea.

Kinana alisema kuwa Mwalimu Nyerere alipokuwa akitoka madarakani alisema “Watanzania mmeajiri kwa miaka 24 lakini ninahakika nilifanya makosa mengi ama kwa kutojua ama kwa kushauriwa vibaya nawaomba radhi. Kinana alisema viongozi tuwe na ujasiri wa kuomba radhi pale tunapokosea”.

Naye Balozi wa Venezuela nchini, Jhony Balza alisema kuwa “ninaishi kusini na ninaamini katika nchi za Kusini kwamba zinaweza kuvunja ukuta na kutengeneza maendeleo yake na kuwa na huru na kujitegemea bila kutegemea wengine kwa kufuata misingi iliyowekwa na viongozi wetu kama Nyerere.

Alisema kuwa Nyerere alisaidiana na nchi nyingine zinazazoendelea duniani na kujenga umoja miongoni mwa viongozi wa nchi kama Brazil, Cuba na Venezuela.

Nao wanafunzi chuoni hapo akiwemo,  Irene Ishengoma Makamu wa Rais Mstaafu chuoni hapo alisema “mwalimu aliamini katika kuwasikiliza watu ili kuleta maendeleo, aliwapa watu uhuru wa kuongea lakini katika kipindi hiki hakuna uhuru wa kuongea vijana wanaambiwa wawe wazalendo lakini hawapewi uhuru wa kuongea.

Kwa upande wake Japheth Japheth alisema kuwa “viongozi wetu tatizo lao, wengi wapo kwaajili ya masirahi yao wenyewe na si kwaajili ya kuhudumia wananchi kama mwalimu alivyokuwa akifanya, kama tunataka maendeleo lazima viongozi waamue kufuata nyayo za mwalimu kwa vitendo.

Read more...

Wanandoa wanalitia majeraha Kanisa-Askofu Nayisonga

Na Frida Manga

Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda Mhashamu Gervas Nyaisonga amesema Kanisa linapata majeraha na vidonda kutokana na wanandoa kutengana, kushindwa kulea familia na kukosa upendo miongoni mwao.

Kwa mujibu wa Askofu Nyaisonga, wanandoa na waamini wanapokosa upendo na kuwa na migogoro miongoni mwao Kanisa la Mungu nalo linapata majeraha na kudhoofika.

Askofu Nyaisonga aliyasema hayo wakati akitoa homilia yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya Somo wa Parokia ya Mtakatifu Antoni wa Padua, Mbagala Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, iliyokwenda sanjari na utoaji wa sakramenti ya Ndoa Takatifu kwa ndoa Jozi 26.

Aliwataka wanandoa hao kuishi maisha ya upendo, kuvumiliana na sala kila wakati na kwamba hiyo ndiyo silaa pekee ya maisha ya ndoa kwani hakuna njia nyingine ya kuponya ndoa hizo zinapokumbwa na changamoto.

Alieleza kuwa tendo la kufunga ndoa si jambo ndogo na la mzaha, bali ni utayari wa kimwili na kiroho kwa watu wawili kukubali kuishi pamoja katika uhai wa maisha yao yote watakayojaliwa na Mwenyezi Mungu.

“Ndoa ni Uhai wa muunganiko wa watu wa wawili ya Mke na Mume, utengano hauna uhai, lakini pia ni dhambi panapotokea utengano katika kile kilichounganishwa na Mungu”,alisema Askofu Nyaisonga.

Kwa mujibu wa Askofu huyo, hata Maandiko Matakatifu yanasema kupitia Mtume Paulo anasema kiungo kikubwa katika kinacholeta uhai ni upendo hivyo amewataka wanandoa  hao kuwa na  upendo wa dhati.

Alibainisha kuwa ikiwa kila mwanandoa na familia ya Mungu kwa ujumla ikatenda matendo mema ya dhati ataliimarisha Kanisa la Mungu na ndoa zitapata kupona.

Askofu Nayisonga alisema Kanisa linawategemea wanandoa hao katika kupeperusha Bendera ya Kristo katika Fumbo la Upendo, Uvumilivu na uchaji wa Mungu.

Aliwakumbusha wajibu wao wa kusaidia kutibu majeraha ya vidonda vya kristo katika Kanisa la Mungu kwa kushinda vishawishi, na kuzishinda changamoto zinazojitokeza ndani ya ndoa zao.

Hata hivyo Askofu Nyaisonga amewataka wanandoa hao kufahamu kuwa changamoto zipo na kwamba ushujaa ni kuzipokea na kuzikubali na kwamba upendo utawapa majibu ya changamoto zinazozitokeza mbele yao.

Aliwataka wanandoa hao kutobabaishwa na kuyumbishwa na changamoto hizo bali kumtumaini Kristo na kubeba silaha ya upendo kama ngao ya kupambana na changamoto hizo.

Kwa upande Paroko wa Parokia hiyo, Padri Jemms Mwapongo alisema changamoto inayowakabili ya waamini kuishi maisha ya mke na mume bila Sakramenti Takatifu ya ndoa, wameikubali na kwamba wanaweka mikakati ya kusaidia waamini kuondokana na hali hiyo.

Padri Mwapongo mbali na kueleza hilo, amewataka wazazi na walezi kujitambua na kutambua wajibu waliopewa na Mungu katika kulea na kuwatunza watoto waliopewa na Mungu.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Francis Gwankisaalisema changamoto kubwa inayowakabili ni kuwa na idadi kubwa ya waamini wanaoishi maisha ya mke na mume bila Sakramenti Takatifu ya Ndoa.

Parokia hiyo inawastani wa waamini elfu tisa na zaidi, ina Vigango Viwili, ambavyo ni Chamazi na Majimatitu, Jumuiya 116 Kanda 43 inamiradi miwili ya kiuchumi, Shule ya Awali na ukumbi ambao hata hivyo haujakamilika lakini wameaza kuona matunda yake.

Gwankisa ametaja changamoto nyingine inayowakabili ni uhaba wa Makatekista, na kwamba katika kukabiliana na hilo tayari wameweka mpango wa kuwapeleka masomoni Vijana wakapate mafunzo ya Ukateksita.

 

Mwisho.

 

Read more...

Fao la matibabu NHIF linavyowakuna wastaafu

Na Frida Manga

Tafsiri ya uzee inachukuliwa kama hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana hadi uzee, na inatofautina kutoka nchi moja hadi nchi nyingine

Kwa Tanzania Sera ya taifa ya Afya na Sheria ya utumishi wa umma inazingatia umri ya miaka 60 kuwa ndio kigezo cha uzee kwani nguvu za kufanya kazi zinakuwa zimepungua.

Aidha wazee nchini wamegawanyika katika makundi mbalimbali, ambapo lipo kundi ya wazee Wastaafu, Wazee Wakulima, Wafugaji, Wavuvi na Wazee wasio na ajira, makundi yote ya wazee yanatofautiana kimatatizo na kimahitaji kutoka kundi moja hadi jingine.

Licha ya ukweli kwamba mzee anapozeeka nguvu za uzalishaji zinapungua, lakini kundi hili ni muhimu kwani ni hazina kubwa ya taifa kwa sababu wao ndio wamejenga misingi bora ya Taifa.

Wazee wanakabili wa changamoto kubwa ya maradhi yanayoelezwa na wataalamu kuwa yanatokana na uzee wao, hivyo huduma bora za afya na za haraka kwao ni jambo la muhimu sana.

Licha ya sera ya Taifa kutamka wazi kwamba Wazee wote nchini wanapaswa kupewa matibabu bure, bado wanakabiliwa na changamoto ya mapokeo kwa wato huduma za afya.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na Tatizo la upatikananji wa Dawa/ Matibabu ya Magonjwa yanayowasibu wazee (NCDs), Kisukari, Moyo, Miguu, Macho n.k.utolewaji wa Lugha zisizo rafiki kwa wazee.

Ukosefu wa pato kulipia gharama za usafiri kwenda Hospitali kununua Dawa. Matibabu bila malipo kuwa kwenye Hospitali za Serikali tu.

Kwa upande wa wazee wastaafu hali iko tofauti kidogo, kwani wao wanapata matibabu bure kwa kupitia kadi ya Matibabu ya kustaafu ya NHIF.

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF ulianzisha Fao la Matibabu kwa Wastaafu mwaka 2007 lengo ikiwa ni kuwapunguzia wazee changamoto wanazokutana nazo katika kupata huduma za matibabu.

Eugin Mikongoti ni Mkurugenzi wa Mfuko wa Jamii (NHIF) anasema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa kuona umuhimu na kuthamini uzee ulianzisha Fao la Matibabu kwa wastaafu ili kuongeza uhai wa kuishi kwa wazee ikiwa watapata huduma bora na salama za afya.

Anasema kabla ya hapo Mwanachama mstaafu alikuwa akitibiwa kwa muda wa miezi mitatu tu, baada  ya kutoka kwenye utumishi wa umma.

Anaeleza kwamba kuanzishwa kwa huduma hiyo kulizingatia maoni ya wadau wakiwemo wanachama wa mfuko na mahitaji, hali ya matibabu kwa wastaatu ambao wametumia muda mrefu wa maisha yao na nguvu kujenga Taifa.

Anasema wanaamini huduma hiyo itasaidia kuongeza muda wa kuishi kwa wastaafu unaokadiriwa hadi kufikia Desemba mwaka 2015 Mfuko ulisajili wanachama wastaafu 27,056 ambapo Mwanachama mstaafu pamoja na mwenza wake anapata matibabu bure

Nchini Tanzania Sera ya Taifa ya Afya, imewaka wazi kwamba wazee wapaswa kupata huduma bure za matibabu ingawa Wazee wanasema uwepo wa sera hii inawafanya wakose huduma kwa kile wanachoelezwa kuwa wao ni bure.

Licha ya kuwepo kwa sera hiyo, Wazee nchini Tanzania wanaeleza kukerwa na usumbufu wa Watumishi wa Afya kutoelewa vizuri mahitaji ya Kiafya ya wazee, Upungufu wa Madawa na huduma nyinginezo katika Vituo vya Afya au Hospitali za Serikali.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na shirika la kimataifa la Help Age International takribani asilimia 90 ya wazee Tanzania ambao ni maskini wanaishi maeneo ya vijijini.

Tanzania kwa sasa inakadiriwa kuwa na idadi ya wazee milioni 2.4 ambayo ni sawa na asilimia 5.7 ya watanzania wote, ambapo hata hivyo  wazee hao wanaelezwa kutunza asilimia 53 ya watoto yatima.

Lakini Wazee wastaafu wanazungumziaje uwepo wa Fao hilo la Matibabu kwao, Clementi Nyikui licha ya kupongeza mfuko huo kwa uwepo wa fao hilo wametaka NHIF kuzungumza na watoa huduma katika vituo vya Afya kuanzisha Madawati maalumu kwa ajili ya Wazee ili kuwapunguzia Wazee adha ya kukaa kwenye foleni muda mrefu.

Anasema tayari miili yao imeshachoka kutokana na maradhi na umri wao hivyo uwezo wa kukaa kwenye foleni muda mrefu ni sawa na kuongeza maumivu kwenye maradhi yao na kwamba inapaswa kuwa na dawati la ambalo halitahusiana na wagonjwa wengine.

“Wakati nikiwa kazini sikuona umuhimu wa Kadi ya Bima ya Afya ya Matibabu, kwa sababu nilikuwa na pata vijisenti na hivyo kumudu kujigharamia matibabu hata katika vituo vya afya vya binafsi”,anasema  Antony Teye ambaye pia ni mstaafu.

Anasema mara baada ya kustaafu ndipo alipogundua umuhimu wa kadi hiyo mara baada ya kusumbuliwa na maradhi ya macho na hivyo kutumia kadi hiyo katika kipindi chote cha matibabu.

Pia anataka mfuko kuweka utaratibu utakao wasaidia watoto yatima kupata ama kunufaika na matibabu bure, kwani asilimia 50 ya wazee nchini wanalea wajukuu ambao hawana wazazi hivyo uwepo wa utaratibu huo utawapungunzia mzigo wazee.

“Tumesha sataafu hivyo hatuna tena uwezo wa kuzalisha, lakini pia tunalea wajukuu ambao ni yatima hatuna kipato cha kuwasaidia kimatibabu hivyo kama NHIF itaweka utaratibu wa kuwasaidia watoto hao itakuwa vinzuri sana” Alisema Mzee Teye.

Ni ukweli kwamba wazee wanasumbuliwa na maradhi mengi, na kwamba mengi kati ya maradhi hayo yanatokana na sababu za umri wao, lakini pia kukaa bila ya mazoezi mara baada ya kustaafu.

Ikumbukwe pia miili yao ilizoea kufanya kazi, na kwamba sasa haifanyi kazi, hivyo kukaa tu bila kujishughulisha huwenda kukachangia kuleta maradhi ndani ya mwili wa mzee.

Anashauri Mfuko kupana wigo zaidi ili kuwafikia watanzania wengi ili kila mtanzania anufaike na huduma za matibabu zinazotolewa na kuwapungunzia mzigo wananchi kwani huduma za matibabu kwa sasa ni gharama zaidi.

Kwa upande wake, Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Kamanda, Jamal Rwambow anatoushauri kwa wazee, kufanya mazoezi walau mara mbili kila siku ili kujiepusha maradhi yanayoweza kuepukika kwa kufanya mazoezi.

“Pindi wazeewatakapokuwa wamejinusuru na maradhi yanayoweza kuzuilika kwa kufanya mazoezi pia watakuwa wameisaidia serikali kuondokana na mzigo wa madeni yakuhudumia wazee wastaafu”,alisema Kamanda Rwambow.

Read more...

Yatupasa kuwa na matendo mema kwa kumjua Kristo

Na Martin  Fabian 

Maana  ya ukristo katika kumfuata Yesu kristo ni kuishi  maisha mapya kwa kumjua Yesu kristo kumjua huko kupo kwa maana nyingi tofauti tofauti kama vile kumjua Yesu kama Mungu.

 

Kumjua kama mwana wa Mungu na kumjua kama  wa Mungu na kumjua kama mtu kamili. Katika kumjua Yesu kwa maana zote hizo yapo matendo mema  yanayotakiwa tuwe nayo  kama watu tunaemjua Mungu.

 

 KUMJUA YESU KAMA MUNGU

1Yohana 5:20 inasema nasi twajua ya kwamba mwana wa Mungu amekwisha  kuja na metupa akili  kwa tumjue yeye aliye wa kweli,  nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya mwana wake Yesu Kristo.

 

Huyu  ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele. Nasi tunajua mwana wa Mungu amekwisha kuja na ametupa sisi akili.Tafisri nyingi za Biblia za kiingereza  zimeandika neno Understand kwa  maana ya uelewa.

 

Lakini tafsiri za Biblia za Kiswahili zimetaja neno  akili. Neno akili limetumika kama uelewa au  utimamu yani misimamo ya kufuata . Kwa  maana zote hizo kwetu katika kumjua Yesu Kristo tumepewa  akili kwa maana ya uelewa katika kufuata misimamo thabiti.

 

Kwa  kumjua Yesu kama Mungu kunatufanya tupate kuachana na  miungu ya uongo na kuachana na tabia  zote mbaya katika  kuzitenda. Maana miungu imebeba tabia mbaya kama  vile uchafu na uzinzi na zinaa na uasherati na uongo na tabia  zinginezo zilizo mbaya Warumi 1:24-31 kwa ajili ya hayo  Mungu  aliwaacha kwa tamaa za, waufuate uchafu , hata wakavunjiana heshima miili yao.

 

Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya muumba  anaye himidiwa milele  Amina. Hivyo Mungu aliwaacha  wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake  wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume wao  vivyo hivyo waliyaacha  matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyowapasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.

Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye  yasiyowapasa.

 

Wamejaa na udhalimu wa kila namana , uovu na tamaa na ubaya ; wamejaa na husda, wenye kusengenya, wenye kusingizia,  wenye kumchukia Mungu , wenye jeuri, wenye  kutakabari, wenye  majivuno, wenye kutunga  mabaya, wasiowatii wazazi wao,wasio na ufahamu, wenye kuvunja maagano,  wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema ;ambao  wakijua sana  hukumu ya Mungu na kwamba wayatendayo hayo wamestahili mauti , wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana  nao  wayatendayo.

 

Haya ndiyo wayafanyao  watu wasiomjua mungu  na wale wanaomjua Mungu lakini wana  uwezo wa kumkataa Mungu kwa akili zao zisizo za maarifa  yani zisizowafaa . Lakini kwetu  sisi  tunaomjua Mungu wa kweli aliyejifunua katika  Yesu Kristo.

 

Mungu ametupa akili katika mwanawe Yesu kristo kwa kumjua yeye aliye wa kweli na uzima wa milele .Sasa katika kumjua huyo Yesu kristo  aliye Mungu wa kweli na uzima tunakuwa na akili kwa kuelewa yatupasayo katika kuyaishi na ndiyo yanayotufanya tuwe hai  katika yeye mwokozi  wetu.

 

2Petro 1:3-9  inasema kwa kuwa uweza  wake wa uungu umetukirimia vitu vyote  vipaavyo uzima na utauwa , kwa kumjua yeye  aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.

 

Tena kwa hiyo ametukirimia ahadi kubwa mnoza thamani ili  kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu  ya tamaa Naam na kwa sababu hiyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yetu tieni na wema na katika wema wenu maarifa na  katika maarifa  yenu kiasi na katika kiasi chenu saburi na katika saburi yenu utauwa na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo.

 

Maana mambo haya yakiwa kwenu na kujaa  tele yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na  matunda , kwa kumjua Bwana wetu Yesu kristo.   Kwa sababu ya kumjua Yesu kwa maana ya kuwa Mungu  kunaleta kwetu kuwa na akii  katika kuishi yatupasayo . Lakini pia na kuwa na tabia za uungu na  kuzaa matunda mema.

 

MATUNDA MEMA KATIKA KUMJUA MUNGU

Ni pamoja kfahamu suala la imani, wema, maarifa,kiasi,saburi,utawa,upendanowa, udugu,upendo.

 

Hivyo basi  unatakiwa kuishi katika  upya kwa kumjua Yesu kuwa ni Mungu  kwa yale aliyetupa yaani uelewa katika maarifa ya kweli na yenye uzima wa milele . Na katika kushiriki tabia za  uungu yaani tabia za rohoni na kuzaa matunda katika kumjua  mungu wa kweli na wa uzima wa milele.

 

2. KUMJUA YESU KAMA MWANA WA MUNGU.                                                                                                                                                                                                                                                            

Kuna maanisha katika hali ya upya kwa kutokufa tena . Yeye ameshinda kifo na mauti . Nasi ametufanya tuwe wapya kwa kutokufa ( kwa dhambi )  kwa kuwa tumeungana naye.

kwa  sakramenti ya ubatizo na hapo tume kuwa ni wana wa Mungu kwa huyo Roho wa kristo aliye ndani yetu. Hivyo tu wana wa Mungu kwa kuwa kristo yupo ndani yetu ( kwa sakramenti zake) , miili yetu  imekufa kwa sababu ya dhambi.

 

Yaani dhambi haihesabiwi kwetu  bali roho zetu zi hai katika kutenda haki, Kwa sababu ya uwepo wa  roho wake kristo ndani yetu,yeye aliyemfufua kristo katika wafu ataihuisha  na miii  yetu inayokufa kwa Roho wake anayekaa ndani yetu, yani dhambi  haitakuwa na nafasi ya kutushinda.

 

Yesu kuitwa  mwana wa Mungu  ni kwa maana ya cheo cha kimo cha utimilifu wake. Kristo  Yesu ni mwana wa Mungu kwa maana   ya katika roho ya uweza , utakatifu na kwa ufufuo wa wafu. 

 

UWEZA WAKE – Sababu  ya kwanza Yesu  kuitwa mwana wa Mungu ni uweza uliokuwepo ndani  yake. Aliishi  katika uweza wa kimungu katika nguvu ya kutenda  kitu hata kikawa. Uweza huo alitupatia  sisi tunamjua yeye  kuwa ni mwana wa Mungu  na kumwamini tazama Yohana 1:12 inasema  Bali wote  waliompokea aliwapa uweza wa kufanyika watoto wa Mungu, ndiyo wale waliiaminio  jina lake.

 

Kwa hiyo basi kwa kumkubali Yesu nasi  tunafanyika watoto wa Mungu kwa uweza ule ule wa Kimungu  katika maisha yetu . Uweza wa ufahamu , uweza wa kutazama na kufanya yale  Uwezo wa kufanya kitu kikawa  2. UTAKATIFU  – Sababu ya pili inayofanya Yesu aitwe mwana wa Mungu . Utakatifu katika kuishi maisha ya kumpendeza Mungu. Nasi akatufanya tuishi utakatifu kwa  damu yake ya thamani.

 

Tazama Waefeso 1:3-5 Atukuzwe  Mungu , baba wa Bwana wetu Yesu  kristo aiyetubariki kwa baraka  zote za rohoni , katika ulimwengu wa roho , ndani yake  kristo ; kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuweka misingi ya ulimwengu , ili tuwe  watakatifu,watu wasio na hatia mbele zake katika wasio na hatia mbele zake  katika pendo.

 

UFUFUO WA WAFU - Sababu ya tatu Yesu kristo kuitwa mwana wa Mungu , yeye ndiye wa kwanza  kwetu  (mwanadamu wote ) kufa na kufufuka  kutoka wafu.  Mauti haikumweza yeye kwa kuwa ni mwana wa Mungu .  Naye ndiye wa kwanza kwetu kanisa kutoka kwa wafu  tazama Wakolosai  1:17- 18  Inasema  naye amekuwapo kabla ya vitu vyote na vitu vyote  hushikana katika yeye . 

 

Naye ndiye kichwa cha mwili , yaani kanisa ; naye ni mwanzo,  ni mzaliwa wa kwanza  katika wafu , ili  kwamba awe mtangulizi katika yote.

 

3. KUMJUA YESU KWA MAANA KUWA MTU KAMILI

Kuna  leta kwetu maana ya kujifunza kuishi  utii na unyenyekevu na uvumilivu hata  kufukia utukufu wa Mungu tazama Wafilip 2:5-11.

 

KWA MAWASILIANO  WASILIANA NAMI  KWA SIMU 0676- 146822

                                                   End 

Read more...

UDHALILISHAJI WANAWAKE SOKO BUGURUNI WALALAMIKIWA- dsm TANZANIA

DARA ES SALAAM

 

Baadhi ya wafanyabiashara wanawake katika soko la Buguruni jijini Dar es salaam, wamelalamikia vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanaofanyiwa na wafanyabiashara wenzao wanaume sokoni hapo.

 

Wakizungumza na Tumaini Media iliyotembelea sokoni hapo akina mama hao wamedai kuwa hufanyiwa vitendo vya udhalilishaji mara kwa mara wanapokuwa katika biashara zao hali inayowafanya kukosa Amani na kujisikia vibaya.

LEMIFRIDA PAULO na ZAINA MUSA ni wafanyabiashara wa matango wao wanasema wamekuwa wakikumbana na vitendo hivyo vya udhalilishaji lakini wanashindwa kupeleka kwenye uongozi wa soko kwa madai kuwa wakiwashtaki wanajijengea uadui na viongozi wao wa vitengo kwa kuwa kesi hizo zinapofika katika baraza la usuluhisi mlalamikiwa hutozwa faini ya shilingi elfu hamsini.

 

Wamefafanua kuwa fedha hizo hutolewa na kitengo husika cha biashara na hivyo huwajengea hofu hali inayowafanya wanyamaze na kuendelea kufanyiwa vitendo hivyo kila siku na baadhi ya wanaume wasio waadilifu. 

 

Wanaume hao wamedai kuwa wakati mwingine vitendo hivyo husababishwa na tabia za baadhi ya wanawake kujitiheshimu wawapo sokoni hapo huku wengine wakidai hufanya kwa lengo la utani na kwamba hawakusudii kuwadhalilisha.

Akijibu tuhuma hizo katibu Mkuu wa Soko la Buguruni FURAHISHA KAMBI, amesema katika kipindi cha hivi karibuni hajapokea malalamiko yoyote ya udhalilishaji wanaofanyiwa wanawake hao wanapokuwa katika shughuli zao sokoni hapo isipokuwa katika kipindi cha nyuma vitendo hivyo vilishamiri.

Amebainisha kuwa kutokana na kushamiri huo uongozi uliunda Kamati maalum ya kufuatilia kwa kina na kuwachukulia hatua wale wote ambao wamekuwa wakilalamikiwa hali iliyofanya vitendo hivyo kupungu.

 

Ashura Kishimba & Valeria Mwalongo

Read more...

TAHARIRI ..

Rasilimali hizi  kunufaisha wa Tazania.

UTENDAJI kazi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli, unaonesha wazi kwamba keki ya taifa italiwa na wananchi wote.

Hali hii inajidhihirisha kutoka na ukweli kwamba mambo msingi ya jamii, ikiwemo huduma za afya, elimu na mambo mengine yameanza kufanyiwa kazi na hivyo kuna uwezekano wa wananchi wa kawaida kunufaika na huduma hizo.

Kama inavyofahamika katika miaka ya hivi karibuni wananchi wengi hasa wanaoishi karibu na maeneo yenye uwekezaji wa madini katika Mikoa mbalimbali nchini wamekuwa na maisha duni yasiyoendana na rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao.

Tumeshuhudia maeneo kadhaa yenye madini ya dhahabu, Tanzanite na almas yakiendelea kudorola hasa kwa wananchi wake kutokana na kutowepo kwa mfumo mzuri wa kuwawezesha wakazi wake kufaidi uwepo kwa madini hayo, lakini kwa utendaji wa serikali ya Amuwa ya Tano hakika hayo yaliyokosekana yatapatikana na kuwanufaisha wananchi.

Hali hii ilikuwa ikiwaumiza zaidi wananchi na kuwafanya wawekezaji kuendelea kunufaika zaidi huku wakiyaacha maeneo hayo kubaki na mashimo wanapomaliza kuchimba, hali inayowatia uchungu zaidi wananchi.

Wananchi wanaoishi maeneo yenye kuchimbwa madini ya aina mbalimbali wamekuwa wakikumbwa na athari kadha wa kadha kemikali zinazotumika kufanikisha uchimbaji wa madini hayo ama kusafishia pamoja na maji yanayotiririshwa kwenye makazi ya watu na kuwadhuru.

Lakini kwa sasa tumeona tarawi Wizara yenye dhamana ikiwemo NEMC, inafuatilia kuona athari zinazowapata wananchi kutokana kuwepo kwa madai ya kemikali hizo.

Hakika wakati uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na wananchi sasa umefika kwani Serikali imedhamiria kutengeneza mazingira bora ili wananchi wanufaike na rasilimali za nchi.

Lakini pia sisi tunashauri kwamba Serikali iwabane wawekezaji ili wananchi katika maeneo yenye uwekezaji wa mali kama vile madini, miradi ya gesi asilia na uchimbaji mafuta nao wafaidike kwa kiasi kikubwa.

Tumeshuhudia mara nyingi rasilimali za nchi zimekuwa zikitoroshwa kwenda nje ya nchi huku watu wachache wakifaidi keki hiyo ya taifa na wengi wakitaabika utadhani kama vifaranga vya kuku visivyo na mama, lakini tunaamini Serikali iliyopo itasimamia hilo.

Tunajua kwamba wananchi wengi waliopitiwa na miradi ya ina hiyo wengi wao wanapata shida huku mali hizo zikienda kuwaneemishe wageni, jambo ambalo ni baya mbele za mwenyezi Mungu.

Sisi tunadhani kwamba Tanzania ina mali nyingi sana za asili lakini kutokana na utaratibu na usimamizi mbovu wa mali hizo, zilizotolewa na Mungu, wengi hawanufaiki nazo na badala yake wachache wakiendelea kujineemesha, tunaomba sasa ule mpango wa kunufaika wachache umalizwe bali wengi wanufaike na keki hiyo ya Taifa.

Sisi tunaipongeza Serikali kwa kuvutia wawekezaji na kuja kuwekeza katika nyanja mbalimbali nchini, lakini tunatao angalisho kwamba ni vema malengo ya miradi hiyo ya uwekezaji ikazingatiwa na kutekelezwa kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Tunasema hivyo kutokana na ukweli kwamba mara nyingi kumekuwa na malalamiko mbalimbali ya wananchi waliopitiwa na miradi hiyo ya uwekezaji lakini wamejikuta wakichiwa makovu huku wageni wakiendelea kupeta.

Kama inavyofahamika kwa sasa Tanzania inachimba madini ya aina mbalimbali, ikiwemo rubi, dhahabu, almasi, Ulanga na madini mengine kadha wa kadha, lakini hakuna mtanzania anayenufaika na madini hayo hata wanaoishi kando kando ya migodi husika zaidi ya kusikia kiasi fulani cha madini kimetoroshwa nje hii ni hatari, hivyo serikali idhibiti jambo hilo.

Tunaiomba Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Wizara ya Mali Asili na Utalii, Wizara ya Nishati na Madini kwa ujumla wake kuhakikisha inaweza sera madhubuti ili kila mtanzania anufaike na mali hizo.

Lakini kuendelea kuwachekea wawekezaji na kuwapa mikataba inayowasaidia wao na kuwaneemesha watu wachache walio madarakani ni jambo baya ambalo hata Mwenyezi Mungu halipendi, kwa sababu ni unyonyaji.

Umefika wakati kila mtu aifaidi keki ya taifa, inayoliwa na wachache kwa miaka mingi bila ya kuona huruma viumbe wa Mungu wanavyoendelea kusaga lami kila kukicha, wakisaka mkate kwa kufanya kazi ngumu na nzito zenye kipato kidogo.

Tunaamini kuwa sio rahisi kila mtu kuona moja kwa moja matunda ama manufaa ya uchimbaji wa madini hayo kwa kupatiwa fedha mkononi mwake, lakini kupitia uboreshaji wa huduma za jamii ikiwemo miundombinu, huduma za afya na elimu hilo litaonekana, na hakutakuwa na mtu wa kulalama.

Mungu Ibariki Tanzania.

 

Read more...
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.