Menu
RSS

Kardinali Pengo atoa sababu za Bagamoyo kuwa Jimbo la Kanisa Katoliki

Kardinali Pengo atoa sababu za Bagamoyo kuwa Jimbo la Kanisa Katoliki

 


Na Timothy Kahoho

KATIKA makala yaliyohusu Bagamoyo kama kituo cha biashara ya Watumwa, tuliona jinsi Wamisheni wa Shirika la Roho Mtakatifu walivyowasili mwaka 1847 na kujenga Kanisa Katoliki ambalo waamini wake wa awali walikuwa watumwa waliokombolewa katikati ya Bahari ya Hindi kutoka kwa wafanyabiashara wa Kiarabu.  Katika mahojiano, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aelezea sababu za kuwepo kwa Jimbo la Kanisa Katoloki la Bagamoyo.

Swali: Unafikiri ni kwa nini Baba Mtakatifu alikuagiza kuanzisha Jimbo la Kanisa Katoliki la Bagamoyo?

Jibu: Niseme kuwa siyo Baba Mtakatifu aliyeagiza hivyo, bali ni Baraza la Maaskofu la Tanzania (TEC) lililoazimia kwa kuwa Bagamoyo ilikuwa mlango mkuu wa kuenea kwa Kanisa katika Afrika Mashariki na Kati. Kwani Wamisheni wa Shirika la Roho Mtakatifu walikuwa wa kwanza kufika Bagamoyo na kujenga kanisa. Kutoka hapo likawa limeenea kaskazini mwa Tanzania mpaka kusini mwa Kenya hadi Uganda, Rwanda na Burundi. Pia kutoka Bagamoyo likasambaa upande wa magharibi hadi Kigoma na Kalema kwenye Ziwa Tanganyika, na kisha kuelekea kusini hadi kaskazini mwa Zambia na Malawi. Kusema kweli, ni katika kuadhimisha miaka 150 ya Kanisa Katoliki, Baraza la Maaskofu liliamua na mapendekezo yake kupelekwa kwa Baba Mtakatifu kwa kuwa ndiye atakayechagua Askofu wa Jimbo la Kanisa la Bagamoyo.

Swali: Kama wamisheni hao wa kwanza ndio waliojenga Kanisa la awali hapo Bagamayo, ni kwa nini palionekana kudumaa?

Jibu: Ni kweli kabisa, awali makao ya Askofu wa Jimbo la Morogoro yalikuwa Bagamoyo. Mazingira yake yalisababisha kudumaa kwake. Kwanza, nyakati hizo kanisa lenyewe lilizungukwa na Waislam wengi. Na pili, ni watumwa waliokombolewa ndio waliokuwa Wakristo wa kwanza lakini wakaendelea kuwa na mawazo ya utumwa. Hivyo, Kanisa halingeweza kuendelea bila ya kuwepo wenyeji. Kwa hiyo makazi ya Askofu yakahamia Morogoro. Lakini sasa Bagamoyo imebadilika sana.

Swali: Ni kwa nini unasema hivi sasa Bagamoyo imebadilika sana?

Jibu: Hivi sasa Bagamoyo ina wageni wengi ambao wengi wao ni Wakristo na hivyo kuonekana kuwa na uhai. Na sasa watu wengi wanajiona wako huru, labda ni kwa kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mara baada ya Tanganyika kupata uhuru alitangaza Uhuru na Kazi na baadaye kutamka Uhuru ni Kazi. Waamini wetu wa awali wakati kanisa hilo linaanzishwa hapo Bagamoyo walikuwa watumwa waliokombolewa lakini walikuwa bado wanafikiria hawako huru. Ni lazima waamini wetu watambue katika kujenga uhuru wa kweli ni lazima wafanye kazi.

Swali: Je, unamaanisha watumwa waliokuwa wamekombolewa na kuwa Wakristo hawakuwa na ari ya kufanya kazi?

Jibu:  Ndio, hawakuwa wamekombolewa kimwazo na kwamba sasa wako huru na lazima wafanye kazi.

Swali: Sasa umesema Baraza la Maaskofu ndilo lililoazimia katika kuadhimisha miaka 150 ya Kanisa liwepo Jimbo la Kanisa Katoliki la Bagamoyo. Je, ni maeneo gani yatakuwa upande wa jimbo hilo jipya?

Jibu: Jimbo hilo jipya litahusisha parokia 8 zilizoko katika Wilaya za Bagamoyo na Chalinze, ikiwa ni pamoja na Parokia za Ngerengere, Mandela na Rugoba. Kadhalika, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, itamegwa ambapo parokia 9 za upande wa kaskazini mwa Mto Tegeta zitakuwa upande wa jimbo hilo jipya.

Swali:  Je, unatoa wito gani kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini katika kuliwezesha Jimbo la Bagamoyo?

Jibu: Kwanza kabisa, zinahitajika kiasi cha Sh. 400 milioni kukamilisha ujenzi na uwekaji wa miundombinu ya makazi ya Askofu atayeteuliwa na Baba Mtakatifu kuongoza Jimbo la Kanisa Katoliki la Bagamoyo. Na pili, ninawaomba waamini kutambua wazi kuwa Bagamoyo ina sifa ya kuwa kitovu cha kuenea kwa Kanisa Katoloki katika Tanzania na Afrika ya Mashariki na Kati kwa ujumla. Kwa hiyo, litahitaji misaada na maombezi ya waamini wote ili liweze kushamiri katika kueneza Neno la Mungu.

 

Mwaandaji wa mafundisho maalum ya binafsi anapatikana kwa barua pepe ya: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. na namba 0769 989164 na 0654 886079

 

 


 

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.