Menu
Tanzania

Jubilee miaka 50 karismatic katoliki kuadhimishwa Pentekoste Roma

ROMA

Kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Karismatiki Katoliki Duniani kinatarajiwa kufanyika katika Sikukuu ya Pentekoste Dominika hii, katika Jimbo Kuu Katoliki la Roma.

Mtandao wa Vatican umeeleza kuwa adhimisho hilo litatanguliwa na mkesha wa Pentekoste siku ya Jumamosi utakaohudhuriwa na Baba Mtakatifu FRANSISKO, kwenye Uwanja wa Circo Massimo Mjini Roma.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa Baba Mtakatifu anatarajia kuadhimisha kilele hicho na Dominika ya Pentekekoste kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu PETRO, Vatican kuanzia saa 4:30 kwa saa za Ulaya.

Chama hicho cha Kitume nchini Italia pia kinaadhimisha kumbukumbu ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwake jambo ambalo limepewa uzito na makao makuu ya Vatican.

Kwa kutambua uzito wa tukio hilo katika maisha na utume wa Kanisa, Katibu mkuu wa Vatican Mwadhama PIETRO Kardinali PAROLIN, amemtumia ujumbe wa heri na baraka Rais wa Karismatiki Italia Daktari SALVATORE MARTINEZ.

Maadhimisho ya Jubiliei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Chama hicho ni wakati wa kumshukuru Roho Mtakatifu kwa neema nyingi alizolijalia Kanisa na fursa ya kusikiliza shuhuda za wanachama na changamoto walizokabalina nazo kwa kipindi hicho cha Jubilei ya dhahabu.

Utume wa Karismatiki Katoliki ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na tayari wajumbe kutoka ndani na nje ya Italia wameanza kuwasili tayari kushiriki katika semina, makongamano na sala katika makanisa mbali mbali hapa Roma.

***

 

Gaudence Hyera

Read more...

Waleeni watoto katika njia impendezayo Mungu.


 

MOROGORO

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzani(KKKT) Dayosisi ya Morogoro JACOB OLE MAMEO amewataka wazazi na walezi kuwalea watoto kwa kuzingatia misingi ya maadili mema.

Ametoa rai hiyo kwenye maadhimisho ya miaka miwili ya kuwa jimbo kamili ya Kanisa la Moravian Tanzania na kuwahimiza wazazi na walei kutekeleza wajibu wao ili kujenga taifa la watu waadilifu na waaminifu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauru Kuu ya Kanisa hilo Mchungaji SAMWELI MWAISEJE amewatahadharisha Madereva wa vyombo vya moto kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Amekumbusha na kutoa angalizo hilo ili Madereva waweze kukabiliana na matukio ya ajali yanayoendelea kujitokeza na kupoteza maisha ya watu hasa katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Mchungaji MWAISEJE amesema Kanisa limesikitishwa na tukio la ajali iliyotokea wilayani Karatu mkoani Arusha na kusababisha vifo vya  wanafunzi 33 wa shule ya Lucky Vincent, walimu 2 na dereva wao.

Ameongeza kuwa matukio hayo ya ajali yanawezesha kudhibitiwa iwapo watumiaji wa vyombo hivyo watazingatia sheria za usalama barabarani.

Aidha Mchungaji MWAISEJE ameipongeza Serikali kwa jitihada za kuendelea kudhibiti mianya ya udanganyifu wa vyeti yaani vyeti feki kwa watumishi wa umma.

***

Merina Robert

Read more...

Mahujaji 36 wakatoliki Tanzania waondoka ureno kushiriki miaka 100 ya Bikira Maria wa Fatima

DAR ES SALAAM.

        Mahujaji thelathini na Sita kutoka Jimbo kuu Katoliki la Dar es Salaam waondoka  leo Mey 9,2016 kwenda Fatima nchini Ureno kwa ajili ya kushiriki Jubilei ya Miaka Moja ya Tokeo la Bikira MARIA.

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Uchungaji Jimboni humo Padri-Daktari JOSEPH MATUMAINI, Safari hiyo inatarajiwa kuanzia Usiku wa kuamkia Jumatano.

Amesema Mahujaji wote leo wamefanya Tafakari ya mafungo yaliyoongozwa na Katibu wa Jimbo hilo Padri AIDAN MUBEZI katika Ukumbi wa Kanisa kuu la Mtakatifu YOSEFU,Jimboni humo.

Padri MATUMAINI amebainisha kuwa miongoni mwa Mahujaji hao wamo Mapadri wanne, Watawa watatu na Waamini Walei Ishirini na tisa ambao watasafiri kwa pamoja.

Ameongeza kuwa wakiwa Ureno watatembelea Madhabahu ambayo Mama Bikira Maria aliwatokea watoto wa Familia moja Mwenyeheri Sista LUSIA na Watakatifu watarajiwa FRANSISKO na YASINTA.

Padri MATUMAINI ambaye pia ni Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu YOSEFU amesema Jumamosi hii mahujaji hao watashiriki adhimisho la kilele cha hija hiyo pamoja na Baba Mtakatifu FRANSISCO.

Mahujaji hao wote wanatarajia kuanza safari ya kurejea nyumbani Jumanne ijayo Mei 16.

***

Gaudence Hyera

 

Read more...

Askofu apigwa na butwaa waamini kuendelea na shughuli zao Dominika

DAR ES SALAAM

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam Mhashamu EUSEBIUS NZIGILWA amewashangaa waamini wanaoacha Kusali Ibada ya Dominika na kwenda kwenye shughuli nyingine za Kijamii.

Ameonyesha mshangao huo alipokuwa akitoa Mahubiri yake kwenye adhimisho la Misa Takatifu Dominika ya jana iliyofanyika katika Parokia ya Bikira MARIA wa Mateso Msakuzi, Jimboni humo.

Askofu NZIGILWA amewahimiza waamini kumtafuta Mungu badala ya kukimbilia kutafuta mahitaji mengine ya kidunia ambayo yeye anao uweza wa kuwapatia maradufu ikiwa watamtumainia kwa imani.

Katika adhimisho hilo ambalo Askofu NZIGILWA ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana sabini na nane wa Parokia hiyo, amewataka waamini kutambua kuwa wakimkosa KRISTO wajue wamekosa yote.

Amewahimiza vijana waimarishwa kuwa watu wa Sala na kumtegemea KRISTO Mchungaji mwema na kumuomba awe mlinzi katika nyumba wanamoishi kinyume chake watakuwa kama wanaishi Maporini.

Sanjari na adhimisho hilo pia Askofu NZIGILWA amebariki na kuizindua nyumba mpya ya Mapadri iliyojengwa kwa nguvu ya michango ya hali na mali ya waamini wa Parokia hiyo.

Amewapongeza Waamini wote kwa ujumla kwa kufanikisha ujenzi wa nyumba hiyo kwa ajili ya wachungaji wao iliyogharimu zaidi ya shilingi Milioni Mia Tatu Arobaini.

Askofu NZIGILWA aliongoza Harambee ya kuchangia Ujenzi wa Kanisa ambapo zaidi ya shilingi Milioni 13 ikiwa ni ahadi pamoja na Fedha Taslimu zilipatikana.

Kwa upande wake Mkuu wa Shirika la Wamisionari Warosmini Afrika Mashariki Padri ENHART MPETE ameahidi kuongeza idadi ya Mapadri wanaofanyakazi Parokiani hapo ili kuimarisha Uinjilishaji.

***

Editha Mayemba/Gaudence Hyera

Read more...

Shirika la Wasalvatorian lapata viongozi wapya

Na Lawrence Kessy, RCT

SHIRIKA la Mungu Mwokozi (Wasalvatoriani) Provinsi ya Tanzania, limefanya Mkutano wake Mkuu na kuwachagua viongozi wake wapya watakaoliongoza shirika hilo kwa kipindi cha maka mitatu ijayo.

Mkutano huo ulifanyika hivi  karibuni katika Prokura yao iliyopo Kurasini, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na kufanikisha kupatikana kwa viongozi hao.

Mkutano huo ulitanguliwa na semina ya Kiroho iliyoongozwa na Abate Mstaafu wa Abasia ya Hanga, Abate Aqulini Nyirenda, O.S.B ambaye kwa sasa anafanya utume wake mjini Roma, Italia.

Katika Mkutano huo kwa kauli moja wanashirika walimchagua Padri Ponder Paulinus Ngilangwa, SDS kuwa Mkuu wa Shirika akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Padri Africanus Lokilo, SDS aliyemaliza muda wake wa vipindi viwili mfululizo kuliongoza Shirika la Wasalvatoriani Tanzania.

Padri Ngilangwa, kabla ya uteuzi huo, alikuwa anasaidia malezi kwa waseminari, katika nyumba ya malezi ya Shirika Jimbo Katoliki la Morogoro, ambapo katika uongozi wake atashirikiana na washauri wengine wanne ambao ni Padri, Lazarus Vitalis Msimbe, SDS, kama Makamo Mkuu wa Shirika, Padri Eugene Reslinski, SDS, Padri Ayub Mwang’onda, SDS na Bruda Sylvester Chimoto, SDS, ambaye pia ni Mtunza hazina wa Shirika, waliochaguliwa katika mkutano huo.

“Nawashukuru wajumbe wa Mkutano huo kwa imani  na heshima kubwa mlionipa na kuniionesha kwangu, hadi kunipa majukumu makubwa na mazito ya kuliongoza Shirika, hasa kwa kipindi hiki ambacho Shirika letu linakabiliwa  na changamoto nyingi, kama vile za kitume, kimalezi, kielimu na kadhalika,” alisema Padri Ngilangwa.

Alisema aliwataka wanashirika hao kumpa ushirikiano, kwani akishindwa au akifaulu wote watakuwa wamechangia na bila ushirikiano hataweza kufanya miujiza kuleta maendeleo ya Shirika, na hasa suala zima la kuongeza maeneo mengine ya kitume katika Majimbo mbalimbali nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Padri Ngilangwa, SDS, ni wakati sasa kwa wanachama wote, wa Shirika la Mungu Mwokozi, kuchapa kazi kwa bidii na maarifa popote pale walipo, na kuacha kusema maneno bila utendaji wowote ule kwa manufaa ya Shirika zima na kutaka kila mmoja aone kuwa ana majukumu yake na mchango wake katika Shirika.

“Uzuri nawajua wote hapa na majina yenu yapo na ninayo na ninyi ndio mlionichagua na nitaanza na ninyi kuwapangia majukumu. Nitashangaa sana kama nitampa yeyote kati yenu hapa majukumu alafu akataee wakati ninyi wenyewe ndio mlionichagua”, alisema Padri Ngilangwa, SDS.

Padri Ngilangwa ni mzaliwa Juni 3, mwaka 1977 katika Jimbo Katoliki la Njombe na alijiunga na Shirika la Mungu Mwokozi mwaka 2000, akafunga nadhiri za kitawa 07/12/2002, nadhiri za daima 01/01/2009, na daraja Takatifu la Upadritarehe  04/06/2010.

Naye Mkuu wa Shirika hilo duniani kutoka Roma, Padri Milton Zonta, SDS aliwashukuru Wanashirika wote wa Provinsi ya Tanzania, kwa juhudi zao za utume hapa Tanzania na hata wale walioko nje ya Tanzania, kwa kazi nzuri wanazozifanya, kwani ndio lengo na karama ya Mwanzilishi wa Shirika hilo, Padri Francis Maria wa Msalaba Jordan.

 “Ninawashukuru viongozi wote waliomaliza muda wao kwa vipindi viwili, kwa kazi nzuri waliyoifanya kuendeleza majukumu mbalimbali ya Shirika kwa kipindi chote, ingawa mlikutana na magumu na changamoto nyingi, hamkukata tama katika hilo. Mungu awabarikini wote”, alisema Padri Zonta, SDS.

Pia aliwashukuru na kuwapongeza viongozi wote waliochaguliwa, kwa kukubali kwao kuyapokea majukumu makubwa ya Shirika na si kwa Kanisa la Tanzania tu bali, kwa Kanisa lote ulimwenguni, na kuahidi kushirikiana nao, katika kustawisha maendeleo ya Shirika kwa ujumla.

Padri Zonta, SDS aliwatakia Wanashirika wote utume mwema na maisha mema ya jumuiya yenye juhudi, maarifa, na mafanikio tele, kwani wanashirika wengi bado ni vijana ukilinganisha na sehemu nyingine za Shirika kama Ulaya na Amerika. Na kumwomba Roho Mtakatifu awe nao katika utume wao wa kila siku zote.

Shirika la Mungu Mwokozi (Wasalvatoriani) kawa hapa Tanzania, Makao Makuu ya Shirika yako Masasi katika Jimbo Katoliki la Tunduru -Masasi, na wanafanya utume wao katika Jimbo hilo la Tunduru -Masasi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na katika Jimbo Katoliki la Morogoro. 

Read more...

Migogoro ya ndoa inaweza kusuluhishwa kwa kuiga mfano wa Mt. yoseph

DAR ES SALAAM

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam Mhashamu EUSEBIUS NZIGILWA amewataka waamini kuinga mfano wa Mtakatifu YOSEFU katika kutatua migogoro ya familia, ndoa na mahusiano.

Amesema hayo wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Somo wa Kigango cha Mtakatifu YOHANE wa Msalaba, Maramba Mawili iliyoadhimishwa Desemba 18,2016 Parokia ya Mtakatifu PETER CLAVER, Mbezi Luis, Jimboni humo, iliyokwenda sanjari na uzinduzi wa Nyumba wa Mapadri.

Askofu NZIGILWA amesema Mtakatifu YOSEFU alikuwa mtu safi na mcha Mungu na ndiyo maana aliweza kushughulikia mahusiano na Bikira MARIA kwa siri kwani hakutaka mtu anayempenda aumizwe.

Ameongeza kuwa Maandiko matakatifu yanaeleza jinsi Mtakatifu YOSEFU alivyoshughulikia mahusiano yake ya Uchumba na MARIA katika hali ya amani mara baada ya kugundua kwamba ana ujauzito.

Askofu NZIGILWA amewataka waamini hasa akina Baba kuomba Neema ya Mungu kupitia maombezi ya Mtakatifu YOSEFU pindi wanapotaka kushughulikia matatizo yao katika mahusiano, ndoa, kazi, na katika maisha yao ya kila siku.

Amewaasa watu wenye dhamira ya kuwaumiza wanaowakosea kuacha tabia hiyo na kuishi kama alivyoishi Mtakatifu YOSEFU na kwa kufanya hivyo watauona Utukufu wa Mungu katika maisha yao.

Kigango cha Maramba Mawili kinahudumiwa na Wamisionari wa Shirika la Wakarmeli tangu mwaka 2009 yaani Padri VIVIAN MENEZES, Padri IVAN MONTEIRO na Sasa Padri WILFRED PAIS.

***

Frida Manga/ Gaudence Hyera


Read more...

Chuo kikuu SAUT Tanzani kuimarisha umeme wa jua

 

MWANZA

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu AGUSTINO-SAUT, Tanzania Padri Dakta THADEUS NKAMWA amesema Chuo hicho kinatarajia kuimarisha mradi wa Umeme wa jua na kuuza kwenye Gridi ya Taifa.

Amesema hayo mwishoni mwa juma wakati wa Mahafali ya 18 ya Chuo hicho alipokuwa akizungumzia namna Chuo hicho kinavyotumia sehemu ya mapato yake katika maendeleo ya jamii.

Padri NKAMWA amesema Chuo hicho kipo katika hatua za mwisho za kujenga mitambo itakayowezesha kuuza umeme huo ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kuongeza tija kwenye sekta ya nishati hapa nchini.

Amefafanua kuwa ujenzi wa mitambo hiyo itawezesha mradi huo kuzalisha umeme kuanzia megawati nne hadi kumi na itasimikwa katika maeneno ya Wilaya za Sengerema, Mkuranga, Tabora na Bukoba.

Padri NKAMWA amesema Tafiti za awali zimeshafanyika na sasa wapo katika hatua ya kuandaa mikataba na makubaliano na wadau na washirika mbalimbali ikiwemo Serikali.

Amewataja washirika wengine kuwa ni pamoja na Wakala wa umeme vijijini(REA), Mamlaka ya udhibiti na huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Umoja wa Ulaya-EU ambao ndio wafadhili wa mradi huo.

Padri NKANWA amesema mradi huo kwa sasa unahudumia Kaya 80,000 katika Mji wa Ukara, Wilayani Ukerewe na umetoa ajira kwa wahitimu 30 kutoka Chuoni hapo.

Chuo Kikuu cha Mtakatifu AGUSTINO-SAUT chenye Makao yake makuu katika Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza kipo chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania-TEC, kikiwa na matawi yake katika Majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki hapa nchini.

***Gaudence Hyera

Read more...

waamini wa Kanisa Katoliki watakiwa kuwa Imara

DAR ES SALAAM

Paroko wa Parokia ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda, Magomeni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam Padri CHRISTIAN LIKOKO amewataka waamini kusimama imara katika imani yao Katoliki.

Ametoa wito huo juzi Jumamosi kwenye adhimisho la Misa Takatifu ya kumuombea Mmoja wa waamini waasisi wa Parokia hiyo Marehemu LEONARD JOHN SONDOKA aliyefariki katikati ya wiki iliyopita.

Padri LIKOKO amebainisha kuwa Ukristo maana yake ni Mateso, Kifo na Ufufuko hivyo ni lazima kila mwamini apitie njia hiyo ya maisha kama KRISTO mwenyewe alivyoipitia na kufikia Utukufu wake.

Amesema baadhi ya waamini wanajaribu kuishi kwa kukimbia na kuhamahama kwenye makanisa na madhehebu mengine kutafuta faraja jambo ambalo halina maana yoyote isipokuwa kumkufuru Mungu.

Padri LIKOKO ameipongeza familia ya SONDOKA kwa kuonyesha ukomavu wa kiimani na kumtunza baba yao katika kipindi chote cha kuugua kwake bila kutetereka katika Imani.

Adhimisho hilo la Misa Takatifu pia liliwashirikisha baadhi ya Mapadri waliowahi kuhudumu Parokiani hapo akiwemo Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu YOSEFU, Padri Dakta JOSEPH MATUMAINI na Paroko wa Parokia ya Mt. MARTHA, Mikocheni Padri ANDREA MWEKIBINDU.

Mapadri wengine ni Paroko Msaidizi wa Parokia hiyo Padri ISRAEL SLAA na Paroko wa Parokia ya Mlandizi Padri MARTIN DOMINIC ambaye Baba yake mzazi Mzee DOMINO RUTAYEBESIBWA ni rafiki wa Marehemu mzee SONDOKA.

Marehemu Mzee LEONARD JOHN SONDOKA aliyezaliwa Novemba 1, 1927 huko Itaga, Tabora na amefariki Novemba 14, 2016 akiwa na umri wa miaka 89 akiwa kwenye matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

***

Gaudence Hyera

Read more...

Kardinali Pengo atoa sababu za Bagamoyo kuwa Jimbo la Kanisa Katoliki

 


Na Timothy Kahoho

KATIKA makala yaliyohusu Bagamoyo kama kituo cha biashara ya Watumwa, tuliona jinsi Wamisheni wa Shirika la Roho Mtakatifu walivyowasili mwaka 1847 na kujenga Kanisa Katoliki ambalo waamini wake wa awali walikuwa watumwa waliokombolewa katikati ya Bahari ya Hindi kutoka kwa wafanyabiashara wa Kiarabu.  Katika mahojiano, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aelezea sababu za kuwepo kwa Jimbo la Kanisa Katoloki la Bagamoyo.

Swali: Unafikiri ni kwa nini Baba Mtakatifu alikuagiza kuanzisha Jimbo la Kanisa Katoliki la Bagamoyo?

Jibu: Niseme kuwa siyo Baba Mtakatifu aliyeagiza hivyo, bali ni Baraza la Maaskofu la Tanzania (TEC) lililoazimia kwa kuwa Bagamoyo ilikuwa mlango mkuu wa kuenea kwa Kanisa katika Afrika Mashariki na Kati. Kwani Wamisheni wa Shirika la Roho Mtakatifu walikuwa wa kwanza kufika Bagamoyo na kujenga kanisa. Kutoka hapo likawa limeenea kaskazini mwa Tanzania mpaka kusini mwa Kenya hadi Uganda, Rwanda na Burundi. Pia kutoka Bagamoyo likasambaa upande wa magharibi hadi Kigoma na Kalema kwenye Ziwa Tanganyika, na kisha kuelekea kusini hadi kaskazini mwa Zambia na Malawi. Kusema kweli, ni katika kuadhimisha miaka 150 ya Kanisa Katoliki, Baraza la Maaskofu liliamua na mapendekezo yake kupelekwa kwa Baba Mtakatifu kwa kuwa ndiye atakayechagua Askofu wa Jimbo la Kanisa la Bagamoyo.

Swali: Kama wamisheni hao wa kwanza ndio waliojenga Kanisa la awali hapo Bagamayo, ni kwa nini palionekana kudumaa?

Jibu: Ni kweli kabisa, awali makao ya Askofu wa Jimbo la Morogoro yalikuwa Bagamoyo. Mazingira yake yalisababisha kudumaa kwake. Kwanza, nyakati hizo kanisa lenyewe lilizungukwa na Waislam wengi. Na pili, ni watumwa waliokombolewa ndio waliokuwa Wakristo wa kwanza lakini wakaendelea kuwa na mawazo ya utumwa. Hivyo, Kanisa halingeweza kuendelea bila ya kuwepo wenyeji. Kwa hiyo makazi ya Askofu yakahamia Morogoro. Lakini sasa Bagamoyo imebadilika sana.

Swali: Ni kwa nini unasema hivi sasa Bagamoyo imebadilika sana?

Jibu: Hivi sasa Bagamoyo ina wageni wengi ambao wengi wao ni Wakristo na hivyo kuonekana kuwa na uhai. Na sasa watu wengi wanajiona wako huru, labda ni kwa kuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mara baada ya Tanganyika kupata uhuru alitangaza Uhuru na Kazi na baadaye kutamka Uhuru ni Kazi. Waamini wetu wa awali wakati kanisa hilo linaanzishwa hapo Bagamoyo walikuwa watumwa waliokombolewa lakini walikuwa bado wanafikiria hawako huru. Ni lazima waamini wetu watambue katika kujenga uhuru wa kweli ni lazima wafanye kazi.

Swali: Je, unamaanisha watumwa waliokuwa wamekombolewa na kuwa Wakristo hawakuwa na ari ya kufanya kazi?

Jibu:  Ndio, hawakuwa wamekombolewa kimwazo na kwamba sasa wako huru na lazima wafanye kazi.

Swali: Sasa umesema Baraza la Maaskofu ndilo lililoazimia katika kuadhimisha miaka 150 ya Kanisa liwepo Jimbo la Kanisa Katoliki la Bagamoyo. Je, ni maeneo gani yatakuwa upande wa jimbo hilo jipya?

Jibu: Jimbo hilo jipya litahusisha parokia 8 zilizoko katika Wilaya za Bagamoyo na Chalinze, ikiwa ni pamoja na Parokia za Ngerengere, Mandela na Rugoba. Kadhalika, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, itamegwa ambapo parokia 9 za upande wa kaskazini mwa Mto Tegeta zitakuwa upande wa jimbo hilo jipya.

Swali:  Je, unatoa wito gani kwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini katika kuliwezesha Jimbo la Bagamoyo?

Jibu: Kwanza kabisa, zinahitajika kiasi cha Sh. 400 milioni kukamilisha ujenzi na uwekaji wa miundombinu ya makazi ya Askofu atayeteuliwa na Baba Mtakatifu kuongoza Jimbo la Kanisa Katoliki la Bagamoyo. Na pili, ninawaomba waamini kutambua wazi kuwa Bagamoyo ina sifa ya kuwa kitovu cha kuenea kwa Kanisa Katoloki katika Tanzania na Afrika ya Mashariki na Kati kwa ujumla. Kwa hiyo, litahitaji misaada na maombezi ya waamini wote ili liweze kushamiri katika kueneza Neno la Mungu.

 

Mwaandaji wa mafundisho maalum ya binafsi anapatikana kwa barua pepe ya: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.">This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it. na namba 0769 989164 na 0654 886079

 

 


 

Read more...

TUMIENI KARAMA MLIZOPEWA VIZURI -MONSINYORO MBIKU

 

DAR ES SALAAM

 

Waamini wametakiwa kuzitumia vizuri kwa matendo karama na vipaji walivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu badala ya kuvificha au kuviacha huku wakilalamika kuwa hakuna mtu yeyote asiye na karama.

Wito huo ulitolewa na Monsinyori Deogratius Mbiku wakati akitoa mahubiri kwenye Misa takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Avila, Kibwegere Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Alisema mkristo kulalamika au kukana kuwa hana talanta ni kumtukana Roho Mtakatifu na kujitafutia laana na kwamba wajibu mkubwa wa mkristo ni kumuuliza huyo Roho Mtakatifu.

"Kila Mtu amepewa kipaji au Talanta au karama. ukijiona huna basi wewe ni mzembe, au umekificha kipaji chako na umepewa ukitendee kazi kwa kuwa usipokitendea kazi kipaji chako unajipatia laana Mt 25:14-30".

Amewataka pia waamini kutambua kuwa bila kumwalika Roho Mtakatifu katika sala na maombi yao hawatafanikiwa kamwe kwani ni kusali bila kumuomba Roho Mtakatifu ni sawa na kutamka tu maneno.

"Utalia sana ooh nimesali novena ngapi sijui, nimesali sala ngapi sijui sijapata kitu, ndugu yangu hukusali ulikuwa unatamka tu maneno. Paulo Mtume kwa Warumi 8:26, akufundishe Mtume paulo kusali, lazima umwalike Roho Mtakatifu, mwambie Roho Mtakatifu nisaidie kusali, sali nami, sali kwa ajili yangu, utaona utakavyofanikiwa" Alisisitiza.

alisema

Aliwakumbusha kuwa mkristo yeyote ataonesha ukristo wake kwa kusali, tena kusali daima siyo mara moja moja na hilo ni agizo la Yesu Mwenyewe Mt 26:41 na Lk 18:1, War 12:12 Salini daima ili uwe Mkristo na uokoke na kusali huko siyo kutamka tu maneno bali kuinua nafsi yako yote kumwelekea Mungu", alisema.  

Katika hatua nyingine Parokia ya Mtakatifu Theresia w Avila inatarajia kukiimarisha Kigango cha Kidimu ili kiweze kutimiza vema kazi ya uinjilishaji katika eneo hilo lililo mbali na Parokia hali inayowafaya wamini wa eneo hilo kushindwa kuhudhuria Misa Takatifu kila Dominika.

Akizungumza na Tumaini Media, Paroko wa Parokia hiyo Padri EVODIUS NACHENGA amesema kuwa kwa muda mrefu wamini wanaoishi katika vitongoji vya Lumumba na Kidimu wamekuwa wakipata shida kufuata huduma za kichungaji Parokiani hivyo Parokia imeona vema kuweka mkakati wa kukiimarisha kigango hicho.

Amewataka waamini kuhamasika na kushiriki kikamilifu kwa kuwa sasa wamesogezewa huduma karibu na kwamba kuanzia mwakani watoto wa mafundisho ya Kumunyo ya kwanza na kipaimara watakuwa wakifanyia mafundisho huko huko.

Sanjari na hilo, Padri NACHENGA amesema kuwa mkakati wa Parokia ni kuhakikisha wanamafundisho hao wanapatiwa mafundisho katika Kanda zake ili kuepusha usumbufu kwa watot wanaoshindwa kufika kwa wakati mafundishoni na kuchelewa kurudi majumbani kutokana na umbali uliopo.

Amesema walimu watakuwa wakitoa mafundisho kwenye Kanda hizo kadiri itakavyofaa.

Akizungumzia suala la uchumba sugu, Padri NACHENGA amesema kuwa mkakati uliopo ni kushirikiana na Wawili katika Kristo- CFC ili kuhakikisha wakaa uchumba wote wanapewa mafundisho ili watambue faida na madhara ya kuishi bila kufunga ndoa wakiwa wakristo.

Amesema kuwa lengo ni kuhakikisha ndoa nyingi iweekanavyo ziungwe mwakani kwa kuwa katika Parokia hiyo wanaoishi uchumba ni wengi kuliko waliofunga ndoa kitu ambacho ni hatari wa ustawi wa Kanisa.

 

 ***

 

Editha Mayemba

 

 

 

Read more...
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.