Menu
RSS

Christine Manyenye: Ulemavu umeninyima uongozi Arusha

*‘Wenye ulemevu tunakosea  kujinyanyapaa’

Na Rachel Gabagambi
MIONGONI mwa makundi ya watu ambao wameachwa pembezoni katika mambo mbalimbali likiwamo suala la uchaguzi wa kisiasa, ni pamoja na hili la watu wenye ulemavu ambao kimakosa, watu wengi wanaamini kuwa, hao hawawezi kushika nafasi yoyote ya uongozi wala kuongoza.

 

Hata hivyo, serikali na wadau mbalimbali kikiwamo Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) kwa ufadhili wa shirka la kimataifa la kushughulikia wanawake la UN- WOMEN na wadau wengine, iimeweka msukumo mkubwa kuhakikisha vijana, wanawake na watu wenye ulemevu wanawekewa mazingira rafiki kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 kwa uhuru na haki.

 

Katika mikutano, semina na mafunzo mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Edda Sanga amenukuliwa mara kadhaa akisisitiza kuwa, watu wenye ulemavu hawapaswi kuachwa nyuma katika kupewa nafasi mbalimbali za uongozi eti kwa kigezo cha ulemavu walionao na badala yake, wawezeshwe kushiriki kwa kugombea na kuchagua kwani wana uwezo sawa ama kuliko watu wengi wasio na ulemavu.

 

Katika mikutano, taarifa na mafunzo mbalimbali kwa umma hata kupitia vyombo vya habari, Tamwa imekuwa ikielezea mambo mbalimbali yaliyokuwa vikwazo kwa watu wenye ulemavu na hasa wanawake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu uliopita.

Katika moja ya mikutano hiyo uliofanyika yalipo Makao Makuu ya Tamwa, Sinza Dar es Salaam, Mratibu wa taasisi ya ULINGO, Dk. Avemaria Semakafu, anasema miundombinu mingi haikuwa rafiki kwa wenye ulemavu kupata jumbe za wagombea kwa kuwa wengine ni viziwi na mikutano ya wagombea haikuwa na wakalimani wa lugha za alama.

 

“Miundombinu ilikuwa migumu kwa wenye ulemevu hata wa viuungo hivyo, ilikuwa vigumu kwa wengi wanaowania nafasi za uongozi kuwafikia wapiga kura na pia, unyanyapaa lilikuwa tatizo. Wengi wana dhana potofu kuwa hawawezi kuongozwa na mwanamke au mtu mwenye ulemevu.”

 

Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Amon Mpanju, amekuwa akihimiza watu wenye ulemavu kujihusisha na vyama vya siasa ili wajulikane na kupewa nafasi mbalimbali zikiwamo za kugombea uongozi kwa kuwa vyama vinawafanhamu.

 

Mpanju anazipongeza juhudi za Tamwa na washirika wake akisema zimesaidia kuwafanya watu wengi wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi, ingawa wengi hawakupata, lakini anasisitiza akisema, “Huu ni mwanzo mzuri.”

 

 

Tamwa inahimiza katika chaguzi zijazo, Serikali na jamii kwa jumla waondoe mila na kasumba zinazowabagua vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ili washiriki kikamilifu katika chaguzi kwa kuwa ni haki yao ya kidemokrasia; badala ya kuendeleza mfumo dume, baguzi na kandamizi.

 

Mwandishi wa makala haya amefanya mahojiano na Christine Moses Manyenye anayeishi na ulemavu wa viungo. Huyu, aligombea nafasi ya ubunge wa viti maalum (CCM) katika Mkoa wa Arusha.

 

Mwandishi: Kuna taarifa kuwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, ulikuwa miongoni mwa watu wenye ulemevu waliojitokeza kuwania ubunge. Hali ilikuwaje katika harakati hizo?

 

Christine: Niligombea ubunge wa viti maalum kwa kundi la watu wenye ulemavu mkoani Arusha ingawa mimi ni mzaliwa wa Geita, lakini makazi na shughuli zangu kimaisha nipo mkoani hapa kwa kipindi kirefu sasa ingawa sikufanikiwa.

 

Katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010, pia niligombea nafasi hii. Kwa sasa mimi ni Mjumbe wa Baraza la Wanawake Wilaya ya Meru.

 

Nilishiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka juzi nikafanikiwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Fedha wilayani kwangu.

 

Mwandishi: Mapokeo ya watu wenye ulemavu katika kushiriki kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa kisiasa yakoje mkoani hapo?

 

Christine: Mkoani hapa na hasa wilaya niliyopo bado mwitikio ni mdogo kwani tulijitokeza walemavu wawili pekee kugombea ubunge wa viti maalum.

 

Wengi bado wapo nyuma kiasi kwamba nguvu ya ziada inahitajika ili kuwaleta kundini. Katika ngazi ya udiwani katika Wilaya ya Meru, hapakuwa na mtu mwenye ulemavu hata mmoja aliyejitokeza kugombea nafasi ya uongozi.

 

Kimsingi, bado vitendo vya kuwafungia ndani watu wewnye ulemavu vinaendelea na hii ni hatari sana kwa kuwa kufanya hivyo kunawakosesha haki yao ya msingi ikiwamo ile ya kuchagua na kuchaguliwa.

 

Mwandishi: Unafikiri nini sababu ya ushiriki mdogo wa watu wenye ulemavu katika chaguzi mbalimbali hasa za kisiasa?

 

Christine: Tatizo kubwa lililopo ni kwamba, kwanza,  watu wenye ulemavu wenyewe ‘wanajiwekea ukuta’ kwa kuwa bado wana ile dhana kwamba hawawezi kuchaguliwa wala kuongoza kwa sababu ya ulemavu walionao.

 

Nyingine ni kwamba, jamii inayotuzunguka bado ina mawazo mgando kwa kudhani kuwa mtu kuishi na ulemavu, kuna mfanya akose sifa na uwezo wa kuongoza ndio maana wanatubagua na wakati mwingine kusema waziwazi hawawezi kukubali kuongozwa na “mlemavu.”

 

Mwandishi: Ukiwa mwanamke mwenye ulemavu uliyewania uongozi katika Uchaguzi Mkuu uliopita Mwaka 2015, ulikumbana na changamoto gani katika harakati hizo?

Christine: Changamoto ni nyingi lakini miongoni mwa kubwa zaidi, ilikuwa ni suala la miundombinu ambayo sio rafiki kwetu wenye ulemavu.

 

Kwa mfano, mimi huyu, nilikuwa na wakati mgumu kuzunguka nchi nzima kuwafikia wajumbe ili wanifahamu na wanichague. Miundombinu iliyopo ilinifanya nishindwe kutekeleza azima hiyo.

 

Changamoto nyingine kubwa niliyokumbana nayo katika eneo langu ni ile ya ukabila na ukanda.

 

Niseme wazi kuwa hii nayo ilikuwa sababu kubwa iliyonifanya nisipate nafasi hiyo kwa kuwa mimi ni mzaliwa wa Geita. Jamii iliyonizunguka ilikuwa ikiniambia waziwazi haiwezi kumchagua mlemavu na tena, mtu ambaye sio mzawa wa eneo lao.

 

Changamoto nyingine zilikuwa ukosefu wa fedha kwa ajili ya kampeni kutoka eneo moja kwenda lingine, kutochaguliwa na wenzetu wenye ulemavu wakiwamo wanaoufahamu vema utendaji wetu na badala yake, tukaungwa mkono zaidi na wasio na ulemavu ambao kiuhalisi ni vigumu kutambua uwezo wetu sisi wenye ulemevu.

 

Nyingine kubwa ni ile ya viongozi wazoefu kung’ang’ania nafasi zaidi ya mbili hadi tatu kwa kipindi kirefu pasipo kutoa fursa kwa wengine.

 

Mwandishi: Unauzungumziaje uteuzi wa Rais Dk. John Magufuli kwa watu wenye ulemavu hadi sasa?

 

Christine: Nimefurahishwa sana na uteuzi wake na hasa kwa kutuwekea wizara itakayoshughulika nasi (Wizara ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu) ingawa kuna changamoto ya kutokuwa na mlemavu mwanamke katika uteuzi wake hadi sasa, katika hili tumpe muda kwa kuwa tunaamini atatukumbuka na sisi.

 

Miongoni mwa mambo muhimu kufanyika, ni serikali na wadau wengine kubaini mapungufu taliyofanyika katika Uchaguzi wa mwaka 2015 dhidi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu na kuyatafutia majawabu.

 

Elimu itolewe ili wanawake wawe huru kuunga mkono mgombea au chama chochote bila kutishiwa, kuzomewa wala kutukanwa au kushambuliwa kwa namna yoyote.

 

Kadhalika, elimu zaidi itolewe kwa umma ili watu wajue kuwa, maumbile ya mtu ama kijinsia au kwa hali ya ulemavu sio kigezo cha mtu kushindwa kuongoza kwani kinachotakiwa ni uwezo, uadilifu na busara.

 

Teuzi zinazofanyika, nazo zizingatie usawa wa kijinsia huku wanawake nao wakikumbukwa kwa uwiano sawa wakiwamo wenye ulemavu. Kubwa zaidi, watu wajue kuwa ubaguzi chini ya misingi ya jinsia, dini, kabila na umajimbo, ni sumu ya maendeleo.

 

 End

 

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.