Menu
RSS

AZAKI na kilio cha maboresho ya Rasimu ya Katiba Featured

EU's new banking union will break the link between banks and public debt EU's new banking union will break the link between banks and public debt

MOJA ya vitu ambavyo Watanzania wamekuwa wakililia kwa muda mrefu ni pamoja na kuwepo kwa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania.

Katika hilo Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais wake Dk. Jakaya Kikwete , imesikiliza kilio hicho na kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo pamoja na mambo mengine imefanya kile kinachotakiwa kwa kukusanya maoni ya wananchi na kutoa rasimu ya kwanza ya Katiba.

Kutokana na uamuzi huo, Tume ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 nchini hivi karibuni ilitakiwa kufanya marekebisho katika Sheria ya marekebisho ya Katiba sura namba 83 hususan kuhusu Bunge maalumu la Katiba.

Aidha Tume hiyo ilitakiwa pia kufanya marekebisho katika kipengele cha kura ya maamuzi yaani maoni pamoja na kipengele cha Tume ya marekebisho ya Katiba sanjali na kurekebisha maudhui ya Katiba katika suala zima la Muungano.

Marekebisho hayo yalikuwa ni maazimio ya Muungano wa Asasi za Kiraia 37 za Tanzania (AZAKI) kuhusu mchakato wa Katiba baada ya kongamano la Kitaifa ka Katiba walilokaa Oktoba 27 mwaka huu ambalo walijadili, kuazimia na kutoa tamko lao kuhusu mchakato na maudhui ya Katiba mpya Tanzania. 

Kama inavyofahamika kuwa mchakato wa kupatikana Katiba mpya Tanzania unaendelea huku rasimu ya kwanza ya Katiba ikiwa tayari imekwisha toka na hatua zinazoendelea sasa ni kutolewa kwa rasimu ya pili ya Katiba.

Baada ya kutolewa kwa rasimu ya pili ya Katiba kutafuatiwa na kuundwa kwa Bunge maalumu la Katiba na upigaji wa kura ya maoni ambapo hatua hizi ni muhimu sana na ushirikishwa wananchi kikamilifu imekua moja katika hoja zilizoibua mijadala mikali nchini.

Japokuwa hatua zote hizi zinaongozwa na Sheria lakini baadhi ya Wataalamu wa Katiba, Wasomi mashuhuri, Wanasiasa, asasi za kiraia na Wananchi wameonesha hofu kubwa ya nafasi ya ushirikishwa wananchi kuthaminiwa kikamilifu.

Kuthamini huku kunakuja kufuatia na dosari zilizojitokea tangu kuanza kwa utoaji wa maoni ambapo kulikuwa na malalamiko mengi kufuatia na baadhi ya Watendaji waliopewa mamlaka kuitumia nafasi hiyo kichama na kuambatana na vitendo vya rushwa vya waziwazi.

Washiriki wa Jukwaa la wazi la Semina za Jinsia na maendeleo (GDSS) linaloratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) ilianika uozo uliofanyika katika zoezi zima la mchakato wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya kuanzia ngazi ya mtaa hadi kata.

Jukwaa hilo lilidai kuwa mchakato huo uligubikwa na vitendo vya udini, siasa, rushwa, vitisho na ubaguzi wa kijinsia hali ambayo ilisababisha baadhi watu waliokuwa na sifa za kuwa wajumbe wa mabaraza hao ya Katiba kuenguliwa kimakosa kutokana na utashi na maslahi binafsi ya watu wachache.

Aidha kwa mujibu wa TGNP mchakato huo uligubikwa na vitendo vya ubaguzi na unyanyasaji wa jinsia uliofanywa na baadhi ya viongozi wa mtaa na vyama vya siasa mfano kwenye baadhi ya mtaa wasichana waliokuwa na umri miaka 18 hadi 35 walienguliwa katika kundi la vijana na kuwekwa katika kundi la Wanawake watu wazima kinyume na utashi wa mtu ninafsi.

TGNP ilidai kuwa chakato huo wa kuwapa wajumbe wa baraza la katiba la Wilaya uligubikwa na dhana mzima ya udini baina ya Wakristo na Waislam hali iliyosababisha kuligawa taifa letu kwa misingi ya dini na kama hatua madhubuti hazitachukuliwa za kukabiliana na hili mwelekeo wa nchi yetu utakuwa mbaya.

Kufuatia na dosari hizo Tume mabadiliko ya Katiba haikutaka kurekebisha dosari hizo na badala yake kuendelea na zoezi hilo licha ya wadau hao wa Katiba kutaka mchakato huo usimame.

Aidha wadau waliendelea kulalamikia suala la kuukimbiza mchakato huo ukamilike haraka ili katiba hiyo iweze kutumika katika uchaguzi mkuu ujao kitendo ambacho AZAKI kimedai kuwa ni kuwanyima haki Wananchi kwa kutoshirikishwa kikamilifu.

Kufuatia na hilo la kuukimbiza mchakato huo AZAKI ilidai kuwa muda wa kupeleka elimu kabla ya kupiga kura ya maamuzi hautoshi na hivyo kupendekeza walau Sheria itoe siku 90 ili waweze kuwa na muda wa kutosha wa vipindi vya kutoa elimu.

“Sisi wawakilishi wa asasi za kiraia AZAKI tulikutana katika hoteli ya Double View na tukajadili, kuazimia na kutoa tamko letu kuhusu mchakato wa Katiba hivyo tamko letu katika Bunge maalumu la Katiba tunataka Wajumbe wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wajumbe wote wa baraza la Wawakilishi la Zanzibar wasizidi theruthi moja ya wajumbe wote wa Bunge maalumu”, alisema Usu Millya.

Anasema kuwa Wajumbe wengine ambao idadi yao haitakuwa chini ya theruthi mbili ya Bunge maalumu watoke kwenye asasi za kiraia, makundi yenye mahitaji maalumu katika jamii na kwa kuzingatia usawa wa jinsia.

Aidha anasema kuwa dhana ya usawa na ulinganifu,idadi ya Wabunge wa bunge maalumu la Katiba iwe nusu kwa nusu kati ya Tanganyika na Zanzibar kama ilivyo kwenye Tume ya mabadiliko ya Katiba sanjali na kutaka mchakato uwe wa kidemokrasia na usawa kati ya nchi shiriki.

Akizungumzia kuhusu kura ya maoni Usu alisema kuwa tume zote mbili za uchaguzi ya NEC na ZEC zimekuwa zikilalamikiwa katika kuendesha chaguzi hivyo mamlaka ihakikishe inaweka utaratibu wa kisheria wa kuunda tume maalumu huru ya kusimamia kura ya maamuzi

“Kuhakikisha kunakuwa na vifaa au huduma kwa ajili ya watu wenye ulemavu kuweza kufuatilia na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kura ya maamuzi vikiwemo lugha ya alama, maandishi yaliyokuzwa na yale ya nukta nundu pamoja na vifaa vinginevyo vitakavyohitajika ili waweze kushiriki kikamilifu.

Sisi kama AZAKI tunaoimba tume katika maudhui ya Katiba mpya tuliafikiana muundo wa Serikali tatu lakini bado imeonekana kuwa kuna umuhimu wa mjadala mpana wa kitaifa wa kujadili kuhusu muundo wa Muungano na mambo yanayohusu Muungano ili kuwepo na muafa wa kitaifa ambapo katika rasilimali za taifa tunapendekeza matumizi yatajwe bayana kuwa ni mali ya Watanzania kwa ajili ya kuwanufaisha Watanzania sanjali kuitaka katiba mpya izingatie usawa wa kijinsia”,ansema Usu.

Kwa upande wake Herold Sungusia kutoka kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anasema hadi mchakato umefikia hapa ni wazi kuwa umetumia gharama kubwa hivyo iwapo tume haitakubaliana na matakwa ya Wananchi kuna uwezekano wa katiba hiyo kutokupitishwa.

“Tangu mchakato huu wa katiba mpya uanze ulikuwa na mushkeli masuala ya Muungano yalikuwa yakibishaniwa sana na kama hatutayafanyia kazi yanaweza kutupeleka kama nchi ya Kenya yale yaliyotokea hivyo Wananchi ashirikishwe vizuri:

Kama hawatashirikishwa vyema uko uwezekano wa kukataa kuipitisha Katiba hiyo na hivyo gharama iliyotumika kwenda na maji maana itabidi urudiwe upya huku kiasi kikubwa cha fedha kikiwa kimetumika sisi tunatoa angalizo mapema kuwa Tume isifanye makosa katika hili kwa kuwa hakuna sababu ya kuharakisha mchakato huu maana hata siku tisini zenyewe hazitoshi wanakimbilia wapi kuikamilishga mapema”,alihoji Sungusia.

Kutokana na hilo kuna kila sababu ya kuungana na AZAKI katika kutetea katiba hii mpya kwa kuwa tunaamini kuandika Katiba mpya ni tendo la maridhiano,makubaliano na muafa kati ya makundi mbalimbali ya Kijamii yaliyomo ndani ya nchi.

Hivyo mchakato huu ni lazima uwe shirikishi na maamuzi yasifanyike kwa kutumia mabavu au yasiwe maamuzi yaliyofanywa na kikundi kidogo cha watu kwa kuwa bado yapo malalamiko mengi juu ya mchakato wa Katiba mpya kwa mantiki hiyo tunaamini bado ipo nafasi ya kufikia maridhiano.

Waliosema wengi wape hawakuwa wajinga bali waliangalia kiundani kuwa kuna haja ya kuwapa wengi japokuwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema si kila wanachokidai wengi basi wapewe bali kuna muda wa kuwapa.

Kutokana na hilo Katiba hii imekuja wakati wa wengi kupewa kutokana na kuwa Katiba zilizoundwa na kufanyiwa marekebisho kadhaa Wananchi hawakushirikisha sasa wakati huu umefika wa Wananchi ambao ni wengi kupewa kipaumbele kabla ya Bunge maalumu la Katiba ili kurejesha mchakato wa kupata Katiba mpya yenye muelekeo uliotokana na muafaka kati ya makundi mbalimbali nchini.edss

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.