Menu
RSS

Wanamuziki kumbukeni kuti la mazoea humuangusha mgema

Wanamuziki kumbukeni kuti la mazoea humuangusha mgema

 

Na Arone Mpanduka

DAWA za kulevya ni tatizo sugu sasa ambalo limeonekana kuitikisa nchi ya Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo Elimu, Michezo, Utamaduni, Sanaa na nyinginezo nyingi.

Kupitia ukurasa huu ninaweza kusema kwamba upande wa sanaa, wimbi la matumizi ya dawa la kulevya limekithiri na kupoteza nguvu kazi ya wasanii wengi wakiwemo wa maigizo na muziki.

Tayari imezoeleka kwamba matumizi ya dawa hizo ni kitu cha kawaida na hadi kufikia wakati baadhi yao kusikika kwenye vyombo vya habari kwamba wanatumia dawa hizo ama waliwahi kutumia.

Hili limejitokeza hasa kwenye muziki wa kizazi kipya ambapo wasanii wengi wanaona kama ni jambo la kisasa ama ujanja hivi kujiingiza katika matumizi ya dawa hizo.

Hivi karibuni msanii wa muziki wa kizazi kipya anayefahamika kama Chidi Benz alijitokeza kwenye kituo kimoja cha televisheni na kuweka bayana kwamba anatumia dawa hizo na ni muathirika mkubwa wa dawa za kulevya.

Mbali na maelezo hayo, Chidi Benz aliamua kuomba msaada kwa Watanzania ili wamsaidie kwa hali na mali kwa sababu matumizi ya dawa hizo yaliathiri utendaji wa shughuli zake za muziki na kumfanya aanze kurudi nyuma kimaisha.

Kwa bahati nzuri mmoja kati ya mameneja wa muziki wa kizazi kipya nchini, Babu Tale alijitokeza kumsaidia kwa kumpeleka kwenye kituo maalum cha kusaidia waathirika wa dawa za kulevya ili warejee kwenye hali ya kawaida.

Si huyo tu, bali hata mwanamuziki mwingine, Rehema Chalamila maarufu kama Ray C, alilazimika kuweka bayana kile kinachomsibu juu ya matumizi ya dawa hizo.

Miaka miwili iliyopita, Ray C alijitokeza na kusema ukweli wake na kuomba msaada ambao ulikuwa ni kumpeleka kwenye kitengo maalum cha waathirika wa dawa hizo kilichopo kwenye Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es salaam.

Ama kwa hakika wimbi la wanamuziki wa Bongo Fleva wanaotumia dawa hizo ni kubwa. Wapo wanaotambulika kwa ushahidi wa kim azingira lakini hawaweki wazi kinachowasibu na matokeo yake muziki wao unazidi kuporomoka na wengine kupotea kabisa kwenye tasnia hiyo.

Kwa mfano Ray C muda mrefu amepotea kwenye tasnia ya muziki wa kizazi kipya huku Chidi Benz naye akianza kutoweka taratibu.

Kibaya zaidi wenyewe kwa wenyewe wanaonekana kufichiana siri wakidhani kwamba ndiyo wanasaidiana kumbe wanazidi kuumizana.

Ninadhani njia pekee ni wenyewe kwa wenyewe kufichuliana maovu walio nayo, jambo ambalo litaisaidia serikali kuwakamata hao watuhumiwa hasa wanaowauzia dawa hizo kupitia vyombo vyake husika.

Tayari wasanii kadhaa wa muziki wa kizazi kipya wametangulia mbele ya haki kwa athari za matumizi ya dawa za kulevya akiwemo Langa Kileo, maarufu kama ‘Langa’ na Albert Mangwea.

Wanamuziki waliobaki wanapaswa kutambua kwamba wanapojiingiza kwenye wimbi la matumizi ya dawa hizo maisha yao huyaweka rehani ikiwemo na fani yao kwa ujumla.

Athari mojawapo ya mtu anayetumia dawa za kulevya ni kutojali kitu chochote, hivyo kama ni mwanamuziki basi hata kazi yake hawezi kuijali na matokeo yake hujikuta muziki wake ukirudi nyuma siku hadi siku.

Kurudi nyuma kwa maendeleo ya muziki huenda sanjari na kufifia kwa kipato na matokeo yake huangukia kwenye umasikini wa kutupwa.

Hali hiyo huchangia kuligharimu taifa kwa ujumla kwa sababu maendeleo ya taifa husababishwa pia na uwezo wa mtu mmoja mmoja, kwa maana ya kwamba kama msanii anafilisika kwa matumizi ya dawa za kulevya maana yake anakuwa mzigo kwa Serikali na taifa kwa ujumla.

Ni jukumu la mwanamuziki mmoja mmoja kukaa na kujitathmini kile anachokifanya na kuhakikisha hajiingizi kwenye wimbi hilo ama kama alianza kutumia dawa hizo ahakikishe anaacha mara moja, vinginevyo anguko lake litakuwa baya.

Na.   Aron Mpanduka.

 

 

 

 

 

 

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.