Menu
RSS

Mzee Cheka ‘atia chokaa kwenye unga’

BABA mzazi wa bondia Francis Cheka, mzee Boniface Cheka ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutokubali mwanae apande ulingoni Mei 30 mwaka huu.

Francis Cheka anatarajiwa kuzichapa na Kiatchai Singwancha kutoka nchini Thailand kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam badala ya Mganda anayeishi nchini Marekani Kassim Ouma.

Lakini wakati maandalizi ya pambano hilo yakidaiwa kwenda vizuri, baba mzazi huyo wa Cheka amesisitiza kwamba anahisi promota wa pambano Kaike Siraju hajafuata taratibu husika ikiwemo ya kuitaarifu mahakama juu ya uwepo wa pambano hilo.

Akizungumza na Tumaini Letu, Mzee Boniface Cheka alisema mwanae anatumikia kifungo cha nje kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii anazopangiwa na mahakama hivyo anatakiwa kuombewa ruhusa kwa kila kitu anachotaka kukifanya.

Mzee huyo alisema anahisi promota analeta ubabaishaji kwa sababu awali alizungumza naye na kumuhakikishia kwamba amemalizana na taratibu za mahakama lakini baadae ikagundulika kwamba hakufanya hivyo.

Alisema wasiwasi wake ni kuona siku moja mwanae anarejeshwa tena jela kwa kosa la kutofuata taratibu kama hizo ambazo kwa mtazamo wa haraka zinaonekana kama hazina mashiko.

“Yule kijana ananitia wasiwasi mkubwa sana, mimi hadi sasa bado ninamuhitaji sana mwanangu na sitaki nimpoteze kwa uzembe wa mtu mmoja. Kitu anachoniudhi  ni kwamba analeta ubishi katika masuala ya msingi na hata wakati mwingine simu zangu hapokei,”alisema.

Alisema jambo baya zaidi kuna wakati alipigiwa simu kutoka Morogoro akiulizwa mahali alipo mwanae kwa sababu hakutokea kwenye eneo lake la kazi alilopangiwa na watu wa Ustawi wa Jamii.

“Nilichukizwa sana na ile hali, nilipochunguza nikaambiwa kwamba Cheka alisafirishwa kinyemela kuja Dar es salaam kusaini mkataba wa mapambano yake na nilipompigia promota hakupokea simu yangu,”alisema Mzee huyo.

Alisema endapo akajiridhisha kwamba taratibu zote zimefuatwa, mwanae atapanda ulingoni kupigana vinginevyo hatoruhusu apigane.

Kwa upande wake promota Kaike alikanusha  madai hayo na kusema kwamba taratibu zote amezifuata hivyo hakuna tatizo lolote litakalotokea.

“Mimi siyo mtoto mdogo hadi niamue tu kumpandisha ulingoni Cheka wakati ninajua kabisa anatumikia kifungo, nilichofanya nimemtaarifu Afisa wa Ustawi wa Jamii pamoja na mahakama,”alisema Kaike.

Ubabaishaji mwingine

Ilifahamika kwamba Cheka angepigana na Kassimu Ouma lakini katika hali ya kushangaza zilitoka taarifa kwamba Ouma hana vigezo, swali likaibuka, je, wakati wanatangaza pambano hilo hawakufuatilia rekodi za mpinzani wa Cheka?

Kufuatia hali hiyo inaonyesha dhahiri kwamba promota hakujipanga na kukurupuka kwa minajili ya kuangalia pesa zaidi kuliko vitu vingine.

Jambo baya zaidi hata maelezo yaliyotolewa na promota Kaike kuhusiana na suala hilo hayakuwa na mashiko.

Hiyo pia si mara ya kwanza kwa Cheka kubadilishiwa mpinzani kwani hata mwaka 2013 aliwahi kubadilishiwa mpinzani katika pambano la kuwania ubingwa wa WBF.

Katika mwaka huo Cheka alibadilishia mpinzani kutoka Findley Derrick hadi Mmarekani Phil Williams.

Kwa mujibu wa Rais wa Oganaizesheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBO-Limited), lililosimamia pambano hilo, Yassin Abdallah 'Ustaadh' alisema Derrick ameondolewa kwa kukosa sifa za kupigana na Cheka.

Ustaadh alisema baada ya kupitiwa kwa rekodi za mabondia wote ilionekana Cheka amemuacha mbali Derrick na hivyo WBF ikamteua Williams anayeshikilia nafasi ya 45 duniani kati ya mabondia zaidi ya 900 wa uzito wa Super Middle kupigana na Mtanzania huyo.

Wakati huo Cheka alikuwa nafasi ya 34 duniani katika uzito huo tofauti na ilivyokuwa kwa Derrick aliyekuwa anashikilia nafasi ya 95 kati ya mabondia 1220 wa uzani wa kati, kitu ambacho kingempa nafasi nzuri Cheka kumshinda kirahisi mpinzani wake kwa wasifu na vigezo hivyo.

Last modified onWednesday, 29 April 2015 12:29
back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.