Menu
RSS
habari za hapa na pale

Sheria mpya ya Maroli yakubaliwa

  • Last modified on Thursday, 02 April 2015 13:34

Madereva wa Mabasi na Malori yaendayo mikoani na nchi jirani nchini,  wameipokea sheria mpya ya udhibiti wa madereva na kudai kuwa sheria hiyo itafanya kazi iwapo Serikali haitaruhusu wamiliki wa magari kuagiza magari yenye uwezo mkubwa wa kukimbia.

Wakizungumza na kituo hiki jijini Dar es Salaam madereva hao wamesema sheria hiyo mpya ya kudhibiti mwendo kasi kwa madereva ni nzuri lakini imeonekana kuwabana madereva pekee na si wamiliki wa magari ambao wao ndio wanaoagiza magari nyenye kiwango cha mwendo usiotakiwa.

Mwenyekiti wa chama cha madereva wa mabasi, maroli, kosta na maroli nchini CLEMENT MASANJA amesema sheria ya kudhitibiti madereva imefanyiwa kazi mapema wakati madereva ambao si waajiri ni vibarua mpaka sasa wamedai kuwekewa sheria ya kuajiri lakini mpaka sasa haijafanyiwa kazi.

Kwa upande wake Katibu wa chama cha madereva ya malori nchini RASHID SALEHE amesema wamewekewa sheria hiyo bila kushirikishwa madereva ambapo serikali imeamua kuwekea kitanzi bila kuangalia kiini cha madereva hao kuendesha magari kwa mwendo kasi ni nini.

Nae mjumbe wa chama hicho ambaye pia ni dereva STELA ARADIN ameitaka serikali kurudisha spid gavana zilizoletwa awali kwa lengo la kudibiti mwendo kasi.

****

Ashura Kishimba

Read more...

Spika ANNE MAKINDA alazimika kuahilisha bunge Dodoma

  • Last modified on Thursday, 02 April 2015 12:05

 

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ANNE MAKINDA, amelazinika kuahirisha kikao cha jana asubuhi cha Bunge hilo baada ya uamuzi wake kuhusu Mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Ubungo, JOHN MNYIKA kukataliwa.

Katika mwongozo aliouomba, MNYIKA alitaka Bunge liache shughuli nyingine ili jadili suala la Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa hasa ikizingatiwa kuwa zoezi la uandikishaji linakwenda taratibu sana.

MNYIKA amesema, ni muhimu kwa Bunge kujadili suala hilo kwa dharura kwa sababu Kura ya Maoni imepangwa kufanyika tarehe 30 ya mwezi huu wakati unadikishaji haujamalizika hata katika mmoja wa Njombe.

Hata hivyo, katika majibu yake, MAKINDA alisema kuwa mwongozo wa MNUKA ulikuwa unafanana na mwongozo ulioombwa kabla na Mbunge mwingine hivyo majibu yake yangetolewa jioni.

Kauli hiyo ya Spika ilipingwa na MNYIKA na wabunge wengine waliodai kuwa suala hilo halikuwa na uhusiano wowote na mwongozo uliotangulia hivyo ulistahili kupata majibu na ndipo mzozo ulipoanza.

 

***

 

Martin Kuhanga


Read more...

Ulaji bora kinga ya ugonjwa wa figo

  • Last modified on Wednesday, 25 March 2015 15:38

Devotha Awato

Kuwa na afya bora ni moja ya mambo msingi na muhimu hasa kwa  kuzingatia kanuni bora za afya ambazo zinazozingatia ulaji borana mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema unamsaidia mtu kupata maradhi ya figo.

Lakini pia hata mtu ambaye amepata athari za figo upo uwezekano mkubwa wa kupunguza kupata madhara zaidi ya kiafya yatokanayo na ugonjwa huo.

Katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo Tanzania inaungana na mataifa yote duniani kutekeleza adhimio la Umoja wa Mataifa  la mwaka 2011 la kuhakikisha linaweka mipango kabambe  kudhibiti magonjwa yasiyo ambukizwa na yanapunguzwakwa asilimia 25 ifikapo  mwaka 2025.

Katika kupambana na ugonjwa huo wa figo ambao unazidi kuwapata Watanzania wengi ambapo asilimia nane hadi 16 watu wote dunianiwameathirika na ugonjwa wa sugu wa figo na kukadiriwa ifikapao mwaka 2023 itafikia aslimia 73 ya watu watakaoathirika na ugonjwa wa figo hasa watu waishio Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mwaka 2011 Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya utafiti na kugundua kuwa Tanzania inashikilia nafasi ya54 duniani ikiongoza kwa vifo vitokanavyo na ugonjwa wa sugu wa figo kutokana na mfumo wa maisha pamoja na kutozingatia lishe bora.

Dk. Muhidin Mahamoud ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili  alisema“Imefikia asilimia 1.6 ya watu hufariki kila mwaka  kutokana ugonjwa huo na  elimu ndogo juu ya ugonjwa huu na gharama kubwa za matibabu  na kusababishia waathirika wa ugonjwa huo kushindwa kuzimudu”.

Akielezea maana ya ugonjwa  Sugu wa Figo anasema ni  kupungua kwa uwezo wa kazi wa figo kuchuja taka sumu zitokanazo na vyakula na vinywaji  kutoka kiwango cha millitre 125 kwa dakika hadi kufikia kiwango cha milita  60  na chini ya hapo mtu huambiwa anamatatizo ya figo na tatizo hilo huanzakuonekana baada ya miezi mitatu.

“Ugonjwa huo wa figo ambao huathiri watu wa jinsia zote na rika zote hutokana na lishe duni  pamoja na vinywaji mbalimbali ambavyo tayari vimeshapita viwandani kuongezewa kemikali ili viweze kukaa kwa muda mrefu”,anasema Dk. Mahamoud.

Ulaji wa vyakula hivi katika jamii maisha yetu ya kila siku huzifanya figo zetu kushindwa kumudu utoaji wa taka sumu mwili kutokana na upatikanaji wa aina mbalimbali za sumu kwenye vyakula hivyo vya kusindikwa kwa muda mrefu.

Ili kuwa na afya bora lazima lishe ya binadamu izingatie vyakula vya asilia ambavyo havina sumu ili kuliwezesha figo kufanya kazi yake vizuri katika hali yake ya kawaida.

Vitu vinavyosababisha ugonjwa huo ni pamoja na ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu,saratani za aina mbalimbali  pamoja na magojwa ya njia ya mkojo.

“Hayo yote hutokana na vishiria vya lishe isiyo bora ambayo hutumiwa na wengi ya wanajamii na kuamini kuwa vyakula vya viwandani ni sahihi  kuliko vya asili ambavyo hubeba virutubisho vyote ambavyo havina viambata vya sumu”,anasema.

Kupitia chama Cha Uuguzi cha Figo Tanzania kimeiomba jamii kwa ujumla kupima afya zao na kujua hali ya viungo vyao vya mwili ili waweze kutibu mapema kabla ya ugonjwa huo kuathiri viungo vingine vya mwili.

“Ingawaje matibabu ya ugonjwa huo ni gharama basi yawapasa kutafuta elimu juu ya masuala ya afya pamoja na kujiunga na mifuko ya jamii ili kujitibia kwa unafuu magonjwa sugu kutokana na gharama wanazochangia katika mifuko hiyo”.

Anasema kuwa dalili za ugonjwa wa figo kwa  mtoto kushindwa kupata haja ndogo ndani ya masaa 48 baada ya kuzaliwa pamoja na kuvimba kwa tumbo, kwa watu wazima kuvimba kwa mwili uso na miguu,kiasi cha mkojo kupungua sana,uchovu wa mwili,kutapika mara kwa mara pamoja na kuwashwa kwa mwili.

Ili kutibu ugonjwa huu hutegemeana na hatua ya ugonjwa ulipofika ambapo kuna hatua tano za ugonjwa  wa sugu ambapo hatua ya kwanza hadi ya tatu hutibiwa kufuata ushauri wa dakatari huku wagonjwa wa hatua ya nne na ya tano wakipatiwa matibabu ya kawaida , haundaliwa matibabu maalum ya ubadilishwaji wa damu na kupandikizwa kwa figo bandia ambayo hutumika kama figo kamili katika kuchuja damu.

Ili kufanikisha kutokomeza ugonjwa sugu wa Figo Chama hicho kimeiomba Serikali kuongeza wataalamu na vifaa mbalimabli vya matibabu vya ugonjwa huo ili watanzania wengi waweze kutibiwa ndani ya nchi ili kuepuka gharma nyingi  zausafirishwaji.

Nalo suala la wataalam wachache juu ya ugonjwa huu ni chanzo cha huduma na matibabu ya ugonjwa sugu wa figo kutibika  sehemu chache  katika hospitali Tanzania ambao Muhimbili yenye madaktari watano ambao hutibia wagonjwa 156  wa ndani na nje na kuwa na shifti zaidi mara tatu ambayo si halali.

Kutokana na changamoto hizo unakuta wagonjwa wengi hushindwa kufika kwa wakati na wengine hufikia hatua za mwisho za ugonjwa huo na kupelekea kushindwa kutibika kwa haraka ambapo gharama zake huwa kubwa.

Dk.Mahmoud  anasema : “Gharama za utenganishaji wa damu inafikia laki mbili na hamsini hadi laki tatu kwa mzunguko mmoja kwa siku ambapo mgonjwa hupaswa kupata huduma mara tatu kwa wiki na kufanya gharama hizo kufika gharama ya laki tisa kwa wiki”.

Kutokomeza ugonjwa huu Serikali haina budi kulipa kipaumbele ugonjwa na kulipatia fungu maalum ili kupunguza gharama kwa waathirika pamoja na kutoa fursa kwa watanzania wanaopenda kusomea taaluma ya figo ili kuwa na wataala wengi na kufanikisha matibabu nchi nzima.

Ugonjwa Sugu wa Figo huadhimishwa  kila ifikapo Alhamisi ya Pili ya Machi, ambapo katika maadhimisho hayo hutolewa elimu juu ya figo na upimaji wa ubora wa figo na kauli mbiu ya Mwaka huu ni Afya ya Figo kwa Wote.

Afya ni hali ya kuwa mzima kimwili kiakili na kijamii na hali kutowepo na ugonjwa ili kuwa na afya bora ni lazima kujumuisha lishe bora na mtindo bora wa maisha ambayo ikifuatwa inaweza kuzuia maradhi ya figo au hata kwa aliyeathirika na ugonjwa figo kupata madhara makubwa ya kiafya yatokanayo na ugonjwa huo.

Ili kuwa na afya bora lazima lishe ya binadamu izingatie vyakula vya asilia amabvyo havina sumu ili kuliwezesha figo kufanya kazi katika hali yake ya kawaida

Katika mwili wa bainadamu  figo ni kiungo muhimu kinchotumika katika utoaji na kuchuja sumu mbalimbali kutoka kwenye vyakula pamoja na vinywaji.

Read more...

Wanaharakati, Wanasiasa watilia mashaka Katiba pendekezwa

  • Last modified on Wednesday, 04 March 2015 10:51

Na Alex Kachelewa

WAKATI Serikali ikiendelea na kazi ya usambazaji wa Katiba inayopendekezwa kwa wananchi ili waweze kuisoma na kushiriki vema zoezi la upigaji kura ya maoni Wanasiasa na Wanaharakati nchini wametilia mashaka zoezi hilo kutokana na kasi ndogo ya kazi ya uandikishaji wapigakura kwenye daftari la kudumu la wapigakura.

Kura ya maoni ya Katika inayopendekezwa imepangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu.

Wakizungumza na Tumaini Letu katika mahojiano maalumu baadhi ya wanasiasa na wanaharakati hao, walisema kuwa serikali imechelewa kugawa katiba inayopendekezwa kwani wananchi watakuwa na muda mdogo wa kuisoma na kufanya maamuzi sahihi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wilaya ya Temeke wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bernard Mwakyembe ameliambia gazeti hili kwamba Serikali imechelewa kusambaza nakala za katiba hiyo kwa wananchi kwani upo uwezekano mkubwa wa zoezi hilo kusuasua.

“Sisi kama wanasiasa tulishaliona hilo na tukatoa angalizo na kueleza kwamba ni vema zoezi hilo la kura ya maoni likaahirishwa na lingefanyika mwaka 2016, kutokana na mambo mengi ambayo yamefuatana kwa mwaka huu lakini tunashangaa serikali inaendelea nalo”,alisema Mwakyembe.

Alisema kuwa mwaka huu una mambo mengi ikiwemo maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ambao unahitaji maandalizi makubwa nay a makini hivyo kuepo kwa kura hiyo ya maoni kunaweza kuathiri baadhi ya shughuli za kufanikisha uchaguzi huo.

Alisema kuwa hata kazi ya kusambaza katiba hiyo inayopendekezwa bado inakwenda kwa kasi ndogo kwani sehemu kubwa ya watanzania hawajafikiwa na katiba hiyo na hata viongozi wa vyama vya siasa hasa ngazi za wilaya hawana, na hata kwenye makaao makuu wamepewa nakala chache.

“Ukiangalia nakala zilizosambazwa ni chache sana kwa vyama vya siasa lakini ukija kwenye wilaya ndo kabisa hatuna nakala hizo hadi makao makuu ambako nako zipo chache”,alisema Mwakyembe.

Kwa mujibu wa Mwakyembe wasiwasi mkubwa wa viongozi wa vyama vya siasa kuhusu kura ya maoni ya Katiba pendekezwa ni zoezi la uandikishaji wananchi kwenye daftari la wapigakura kwani muda uliobakia huenda isitoshe kuandikisha wananchi nchi nzima kwa ufanisi zaidi kutumia teknolojia hiyo.

“Sheria inasema wazi kwamba kila mwananchi anayetakiwa kupiga kura ya maoni lazima awe na kitambulisho sasa hadi sasa zoezi hilo limeanza kule mkoani Njombe na zipo mashine 250 za BvR ambazo hazitoshi sasa sijui itakuwaje”,alisema Mwakyembe.

Kwa upande wake mmoja wa mwanasiasa mkongwe ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alisema Serikali ilitakiwa kuzisambaza nakala hizo mapeza zaidi kama ilivyofanyika wakati wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilisambaza nakala za rasimu mapema na kuwapa wananchi nafasi nzuri ya kusoma na kufahamu nini lichopo ndani yake.

“Jambo la msingi hapa ilikuwa ni kuzisambaza mapema ila sio tatizo ngoja tuangalie hali itakuwaje”,alisema mwanasiasa huyo.

Alisema kuwa hatua hiyo ya kuzisambaza nakala hizo kwa sasa itawapa wakati mgumu wananchi kuzisoma kwani muda uliosalia kwa hali na tabia za watanzania katika suala la kujisomea ni shida kulingana na muda wenyewe.

Mmoja wa wanaharakati jina tunalo, alisema kuwa serikali ilitakiwa kufanya kazi ya usambazaji wa Katiba hiyo inayopendekezwa tangu mwaka jana mara tu baada ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kukamilisha kazi ya utengenezaji wa katika hiyo na kuikabidhi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete mkoani Dodoma ili kuwapa wananchi muda wa kutosha kuipitia.

“Sisi tunadhani ilikuwa jambo jema na la busara zaidi kama nakala za katiba pendekezwa zingesambazwa mapema ili kutoa nafasi kwa wananchi wasome maana huwezi kupiga kura kwa jambo ambalo hujalielewa vema.

Kwa mujibu wa mwanaharakati huyo lengo la wananchi kuisoma katiba hiyo ina maana kubwa kwani walishiriki kwa kiasi kikubwa kutoa maoni yao wakati wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya katiba hivyo itawapa nafasi ya kuangalia pia maoni yao na kuweza kufanya chaguo sahihi.

Read more...

Baba Mtakatifu awatakia matashi mema Wakimbizi nchini Iraq

VATICANCITY, Vatican

Baba Francis amewatakia matashi mema wakimbizi waliyopo kwenye kambi ya Irbil nchini Iraq wakati huu wa Sherehe za Sikuu za Krismasi na Mwaka mpya.

Baba Mtakatifu ametoa matashi hayo kwa njia ya simu alipokuwa akizungumza na wakimbizi hao muda mfupi kabla ya kuanza kwa Ibada ya Misa Takatifu ya Mkesha wa Krismasi iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Aidha Baba Mtakatifu amewapa pole wakimbizi hao kwa kulazimika kuyakimbia makazi yao kutoka na mapigano ya vita yanayofanywa na wanamgambo wa Kundi la Kiislam la IS nchini Iraq.

Akizungumza wakati wa misa Takatifu ya mkesha wa Krismas, baba Mtakatifu amewataka waamini kuhakikisha wanaonesha moyo wa upendo kwa familia zao, ndugu jamaa na marafiki.

Mazungumzo hayo ya Baba Mtakatifu aliyoyafanya kwa njia ya simu kupitia Setelaiti kwenye kambi yab Ankawa pia yalitangazwa moja kwa moja na Televisheni ya Italia.

“Ndugu zangu nipo pamoja nanyi na nimewaweka ninyi ndani ya moyo wangu…lakini kikubwa nawafikiria zaidi watoto na wazee”,alisema Baba Mtakatifu.

"Watoto wasio na hatia wameuawa, nawafikiria wazee ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa sababu ya vita ambao kwa sasa wangeweza kukaa na familia zao”,alisema.

Wanamgambo wa Kundi la IS wamefanikiwa kukimbia kwa maelfu ya Wakristo katika maeneo hayo ya Iraq pamja na watu wa madhehebu mengina na kukimbilia eneo linalomilikiwa na Wakurdi.

 

Read more...

Padri aonya wanaodharau Msalaba

Na Mary Yuda

PAROKO wa Parokia ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda Magomeni Padri  Dk. Joseph Matumaini ameonya watu wenye tabia ya kudharau Msalaba na kuutolea maneno machafu kuacha tabia hiyo kwani ni kumkufuru Roho Mtakatifu.

Padri Matumaini alitoa onyo hilo hivi karibuni katika makabidhiano ya Msalaba na ngao ya imani kutoka Kanda ya Mtakatifu Kizito kwenda Kanda ya Mtakatifu Anatoli Kiligwajo ikiwa ni moja kati ya matukio kuelekea Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Parokia hiyo.

“Ninashangazwa na baadhi ya watu kukashifu msalaba hata baadhi ya wanajumuiya walio na nafasi kukataa msalaba usiingie katika familia zao bado nashindwa kuelewa hawa watu ni wakristu kweli na kama ndio ukristo wao uko wapi kwani kwa kupitia msalaba tulipata wokovu”alisema Padri Matumaini.

Aidha aliwataka waamini hao kuona fahari juu ya msalaba kwa kuwa msalaba ndiyo bendera ya ushindi kwa kila mkristu huku akiwataka kutumia Msalaba huo wa mwaka wa imani pamoja na ngao ya imani kupona katika changamoto mbalimbali ndani ya familia zaokwa kuwa msalaba ni tiba. 

Akitoa taarifa ya mzunguko wa Msalaba na ngao ya mwaka wa imani muda mfupi kabla ya kukabidhi msalaba huo kwa kanda ya Mtakatifu Anatoli Kiligwajo, Katibu wa Kanda ya Mtakatifu Kizito Pascal Katyega  alisema walipokea Msalaba na ngao ya mwaka wa imani Desemba 7, mwaka jana kutoka Kanda ya Mtakatifu Mathias Mulumba na kuanza kuzungusha msalaba huo na ngao ya mwaka wa imani Desemba 8, mwaka jana.

Alidokeza katika mzungo wa msalaba huo  pia kulikuwa na semina kwa kila  Jumamosi zilizokuwa zikitoa mafunzo juu ya msalaba na kwamba wakufunzi katika mafunzo hayo walikuwa ni Katekista Zakaria Mahagire kutoka Parokia ya Pamoja na Katekista Thomas Dismas wa Parokia hiyo.

Akizungumzia changamoto walizokutana nazo wakati wa kutembeza msalaba huo Katyega alisema ni pamoja na baadhi ya wanakanda kukataa kupokea Msalaba, kutoa maneno ya kejeli, pamoja na baadhi ya watu wa imani ya Kiislamu kutema mate msalaba ulipokuwa unapita katika maeneo yao.

Matembezi ya msalaba na ngao ya imani katika Parokia ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda magomeni yanafanyika ikiwa ni maandalizi ya Jubilei ya miaka 50 ya Parokia hiyo inayotarajia kufanyika Agosti mwaka huu.

 

Read more...

Askofu Mdoe: 2015 mwaka wa kufanya maamuzi magumu

• Ataja sifa za Kiongozi ajaye

• Avionya vyama vya siasa

Na Devotha Awato

ASKOFU Msaidizi wa JimboKuu Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Titus Mdoe amewataka watanzania kuuona mwaka 2015 ni wa kufanya maamuzi magumu kuchagua viongozi wazalendo kwa mustakabali wa Taifa.

Askofu Mdoe alitoa rai hiyo wakati akitoa humilia yake  kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya Sherehe za Epifania iliyofanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Anna Hananasifu jimboni humo.

Askofu Mdoe alisema sasa ni wakati muafaka kwa watanzania kuweka uzalendo mbele na kusimamaia masuala yatakayolisongesha mbele taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

 “Kwa sasa tunashuhudia uzalendo kwa Watanzania umepungua kutokana na ukiukwaji wa haki za kimsingi ambazo zimekuwa finyu katika upatikanaji wake”,alisema Askofu Mdoe.

Alisema kuwa kuwepo kwa na utandawazi  ni changamoto kwa viongozi ambao hufanya mambo kibinafsi ikizingatiwa ndio  viongozi wanaopaswa kuwa mbele kuleta maendeleo na kulitumikia taifa kwa uzalendo na mapenzi ya dhati katika matumizi ya rasilimali kwa manufaa ya taifa lao.  

Kwa mujibu wa Askofu Mdoe pia alisema suala la rushwa bado limeendelea kutawala na kuona kuwa ndiyo mahala pekee pa kujiapatia  fedha kwa ajili ya manufaa yao.

 “Uchu wa madaraka na siasa ndivyo vyanzo vya  watu kutotumia taaluma zao kiufasaha kutatua kero za wananchi na kukimbilia  kwenye siasa wakiamini ndiko kwenye ulaji”,alisema Askofu Mdoe.

 Alisma kuwa mwaka uliopita watanzania wameshuhudia taifa likigubikwa na kashfa nzito zilizowashtua wananchi kutoka kwa viongozi waliowachagua  kwa imani ya kuwaleta maendeleo lakini viongozi haop wamekuwa wa kwanza kujilimbikizia mali na kuwaacha wananchi katika hali ngumu ya maisha.

Kutokana na hayo yote Askofu  Mdoe amewaasa waamini nchini kuwa mwaka huu ni wa maamuzi magumu katika Uchaguzi Mkuu kwa viongozi wenye uzalendo na kuweka vipaumbele muhimu kwa wanajamii, taifa na  kuwa chachu ya maendeleo bila ya kujali  ni chama gani anachotoka mgombea.

 Alibainisha kuwa kumekuwa na chaguzi mbalimbali ambazo viongozi wamekuwa wanyenyekevu wanapohitaji kura kutoka kwa  wananchi lakini baada ya kuingia madarakani wanawasahau wapigakura wao na hivyo kukosa uaminifu kwa wapiga kura hao.

“Ndugu zangu wanasiasa mkubali kuwa mmekuwa na ahadi za uongo ambapo imesababisha wananchi kuwaona waongo na kupoteza imani juu yenu”,alisema.

Akizungumza suala la Katiba inayopendekezwa Askofu Mdoe alisema Katiba  hiyo ndio sheria mama kwa taifa lolote duniani, hivyo basi haina budi iwe na mawazo ya wananchi ambayo ndiyo waliyoyapendekeza na  kamwe yasipuuzwe.

 “Kamwe maoni ya wananchi yasipuuzwe wala kubezwa maana ndiyo wanayoyaona yanafaa kuliongoza taifa na siyo maoni ya wachache”,alisema Askofu Mdoe.

Alisema kuwa ili kupata Katiba mpya elimu inahitajika kutolewa kwa waamini kupitia Jumuiya Ndogondogo, kwani ni himu muhimu kuelimishana baadhi yavipengele vyenye utata.

Hata hivyo alisema kuwa Kanisa limepinga vikali baadhi ya vipengele ambavyo katika Katiba inayopendekezwa vinaruhusu utoaji wa mimba, jambo ambalo limekuwakanganya waamini na jumuiya za Kristo na hivyo kushindwa lipi la kufuata.

Aidha Askosu Mdoe amewataka waamini kutowaachia wanasiasa au wanaharakati kuleta mabadiliko ya nchi kwa maaana nchi ni ya watu wote  kwa kupeana elimu kuhusu masuala muhimu.

Alisema ni vema waamini wakadumu katika sala hasa kwa mwaka huu wa familia na kumpokea Yesu Kristo na kubadilisha yale maovu na kumcha Mungu kwa maana wote ni sawa mbele ya uso wa Mungu.

 

Read more...

CHF; Mfuko uliokuja kuwakomboa maskini katika sekta ya afya Manyoni

Na Jumbe Ismailly

MFUKO wa Afya ya Jamii (CHF) ni mfuko unaotoa huduma za afya kwa wananchi wasio katika sekta rasmi.Mfuko huu ulianzishwa kwa sheria ndogo ya serikali za mitaa namba saba ya mwaka 1982 kifungu cha 148.

Kupitia mfuko huu wananchi wasio katika sekta rasmi hutoa fedha kidogo na kisha kupata huduma katika kipindi cha mwaka mzima.

Wilaya ya Manyoni ni moja kati ya Wilaya sita za Mkoa wa Singida ambazo ziliamua kuanzisha mfuko huu ili kuwanufaisha na kuongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wake.

Hadi sasa kiwango cha kuchangia ni shilingi 5,000/= kwa kila kaya ambapo wanakaya sita hupata huduma za matibabu kwa mwaka mzima.

Katika makala hii iliyofadhiliwa na TMF, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Fatma Hassani Toufiq akizungumzia hali halisi ya huduma za afya, hususan Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) anasema tangu kuanzishwa kwake umeleta mafanikio makubwa kutokana na watu kupatiwa huduma za matibabu wakati wote wanapougua na kwa bei nafuu.

“Awali mfuko huu ulipoanzishwa malengo ya uandikishaji wanachama hayakukidhi matarajio ya wilaya kwa kila mwaka kwa kuwa uhamasishaji haukuwa mkubwa sana kwani hawakuwa na fedha za kuwawezesha kwenda vijijini kutoa hamasa hiyo”,anasema Toufiq.

Toufiq ambaye ni mkuu wa wilaya ya Manyoni kwa zaidi ya miaka mitatu sasa baada ya kuona hali ya kusuasua huko alilazimika kubuni mbinu ya kuhamia vijijini kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa wanachama wa mfuko huo.

Ubunifu huo umefanikisha uendeshaji wa CHF katika Halmashauri ya wilaya ya Manyoni kuwa wa kiwango cha juu hivyo kuifanya wilaya hiyo, kuwa na ongezeko la wanachama wa mfuko huo.

Anasema pamoja na kusuasua katika kufanikisha upatikanaji wa wanachama wa CHF, lakini mbinu ya mikutano ya hadhara iliyofanywa na timu ya viongozi mbali mbali aliowaongoza, ilileta mafanikio katika kampeni za chanjo zilizofanyika mwaka huu kwa kuongoza katika Mkoa wa Singida.

“Naomba na wilaya zingine za ndani ya nje ya Mkoa wa Singida zije kuchukua uzoefu kwetu wa namna ya kuhamasisha akina mama na akina baba kujitokeza kwenye huduma za mama na mtoto zinazotolewa kwenye maeneo ya kutolea huduma”anasisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Mkuu wa Wilaya anasema baada ya wao kusuasua katika upatikanaji wa wanachama wa CHF hawakuona haya kwenda kujifunza kwa wenzao wa wilaya ya Iramba, ambao kwa kiasi kikubwa wamebobea katika mfuko huo na kushika nafasi ya kwanza kitaifa.

Toufiq anasema tangu Julai mwaka 2013 hadi Septemba mwaka 2014 kumekuwepo mabadiliko makubwa ya wanachama kujiunga na CHF hadi kufikia 16,816 ikiwa ni sawa na makusanyo ya jumla ya shilingi 84,080,000/=.

“Mabadiliko haya yamechangiwa na uhamasishaji uliofanyika mwezi Juni hadi Septemba mwaka 2013 pamoja na kubadilika kwa gharama za papo kwa papo kutoka Shilingi 1,000/=kwenye zahanati hadi Shilingi 3,000/= na Shilingi 1,500/= hadi 4,500/= kwenye kituo cha afya”,anasema.

Anasema baada ya kupandisha viwango katika zahanati na vituo vya afya, kuanzia Mei huu kiwango cha uchangiaji kwa mwanachama anayetaka kujiunga na mfuko huo kitapanda kutoka shilingi 5,000/= hadi shilingi 10,000/= kwa mwaka.

Kwa upande wake Mratibu wa Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Wilaya ya Manyoni, Michael Mayala anasema ili mafanikio zaidi yaweze kupatikana waliandaa mikakati mbali mbali ikiwemo kutembelea vijiji katika Wilaya na kufanya uhamasishaji kwa wananchi wakiwa na Mkuu wa Wilaya.

“Zoezi hili lilianza Novemba 22, mwaka 2014 hadi Desemba 12, mwaka jana kwa muda wa siku 10 ambapo kiwango cha kuchangia kinatarajiwa kubadilika kutoka Shilingi 5,000/= hadi 10,000/= kwa kila kaya kuanzia mwaka ujao”,anasema.

Anaitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na uhamasishaji wa kila siku kwa wateja wanaohudhuria hospitalini,kituo cha afya na zahanati na kutoa elimu ya usimamizi na matumizi ya fedha za CHF.

Mingine ni kuhakikisha uwepo wa dawa za kutosha na zinazokidhi mahitaji ya wananchi ili kuvutia wateja kujiunga na mfuko wa afya ya jamii na uwasilishaji wa taarifa za CHF kwa Serikali za vijiji na pia kutumia mikutano ya hadhara kuongea na wananchi juu ya umuhimu na faida za kujiunga na CHF kwa kila kaya.

Anasema katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka 2011 hadi Juni mwaka 2012 mfuko huo ulikusanya jumla ya Shilingi 8,725,000/= kutoka kwa wanachama 1,745,wakati kwa mwezi Julai mwaka 2012 hadi Juni mwaka 2013 jumla ya shilingi 11,735,000/= zilikusanywa kwa wanachama 2,347.

Ambapo kwa Julai mwaka 2013 hadi Septemba mwaka 2014 jumla ya Shilingi 84,080,000/= zilipatikana kutoka kwa wanachama 16,816.

Kwa mujibu wa mratibu huyo kati ya Shilingi 84,080,000/= zilizopatikana katika makusanyo ya kuanzia Julai mwaka 2013 hadi Septemba mwaka 2014  ambapo jumla ya Shilingi milioni 40 zimetumika kununulia dawa na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Naye alieykuwa Mratibu wa uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya kati, Timothy Zakaria Kingu anasema serikali haina budi kutoa elimu kwa wazee wanaoishi kwenye maeneo ya vijijini juu ya haki yao ya msingi ya kupatiwa huduma za matibabu bure, badala ya kuendelea na hali iliyopo kwa sasa ambapo bado wazee wanatozwa gharama za matibabu.

Kingu ambaye pia amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Manyoni mkoani Singida na Kibondo mkoani Kigoma licha ya kuishukuru serikali kwa kuanzisha utaratibu wa huduma hiyo kwa wazee,lakini akashauri kwamba ni vyema serikali ikaangalia upya kwa kuziboresha zaidi huduma hizo.

Aidha Kingu anapendekeza pia mabadiliko ya jina linalotumika Hospitalini kutoa huduma kwa wazee hao badala ya kuitwa “Dirisha la wazee” libadilishwe na badala yake liitwe “Matibabu kwa wazee au Huduma kwa wazee”ili kuondoa dhana inayoweza kujengeka kuwa dirisha hilo lipo kwa ajili ya wazee kukaa kwa muda mrefu bila matibabu.

“Jina la dirisha la wazee linaleta maana tofauti na iliyokusudiwa na serikali kwani kwa sasa hivi kutokana na wazee kukaa muda mrefu wakisubiri huduma ya matibabu na wakati mwingine kuondoka bila kupatiwa dawa ni vyema likabadilishwa na kupewa jina la “Huduma za matibabu kwa wazee au Matibabu kwa wazee”.

Hata hivyo anasema huduma za wazee katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni bado haziridhishi kutokana na kutokuwepo daktari maalumu kwa ajili ya wazee na kushauri uongozi wa Hospitali hiyo kuangalia uwezekano wa kuwepo daktari maalumu wa  kutibu wazee na anayeyafahamu magonjwa ya wazee badala  ya ilivyo sasa.

Anasema wakati umefika kwa wataalamu wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kuangalia upya utaratibu wa kuwawezesha wazee hao kuondoka mapema hospitalini badala ya kuendelea kukaa kwa muda mrefu mpaka wanasinzia kwani hivi sasa wao ni watu waliochoka.

Hata hivyo anasisitiza kwamba pamoja na kulitumikia taifa la Tanzania kwa muda mrefu na kwa uaminifu mkubwa, lakini inaonekana bado hawajapewa hadhi yao ikilinganishwa na kipindi chao cha utumishi wao uliotukuka serikalini na hata kwenye mashirika mbali mbali ya umma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Ally Minja anasema upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika wilaya hiyo siyo wa kuridhisha kwa asilimia 100 kutokana na baadhi ya madawa kutopatikana kwenye baadhi ya vituo vya kutolea huduma nje ya Hospitali ya wilaya hiyo.

Anasema hata utaratibu uliowekwa na Halmashauri ya wilaya hiyo kuhusu wazee wasiojiweza,walemavu hususan kwenye makazi ya watu wenye ulemavu Sukamahela na watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupatiwa matibabu bure,bado unapuuzwa na baadhi ya wataalamu kwenye vituo vya kutolea huduma vilivyopo wilayani hapa.

Afisa Mfawidhi Makazi ya Sukamahela, Fredrick Mboya anasema zahanati ya Sukamahela inahudumia walemavu na wananchi walio karibu na makazi haya. Huduma zinazotolewa na zahanati hiyo ni pamoja na huduma ya mama na mtoto,huduma ya wagonjwa wa nje (OPD) na huduma ya uzazi.

Kwa mujibu wa afisa huyo licha ya wazee wa kambi hiyo kulipiwa michango ya uanachama wa Mfuko wa afya ya jamii (CHF) lakini wamekuwa hawanufaiki na huduma za matibabu kutokana na kukosekana kwa dawa muhimu zinazohitajika kwao.

Muuguzi daraja la pili katika zahanati ya Kijiji cha Sukamahela, Sarobe Maula anasema zahanati hiyo inategemewa na vijiji vitatu vyenye zaidi ya wakazi 6,500, jambo linalochangia wazee wa kambi hiyo kutonufaika na michango wanayochanga katika mfuko huo.

Kaimu Afisa Ustawi wa jamii Mkoa wa Singida, Fatuma Malenga anasema kuwa licha ya upatikanaji duni wa huduma za matibabu, vile vile pia upatikanaji wa chakula umekuwa mgumu kwa wazee wa kambi ya Sukamahela kutokana na fedha zinazotolewa na Serikali kutokidhi mahitaji ya kambi.

 

Hata hivyo kwa wakati mwingine hata wazabuni wamekuwa wakiidai wizara kwa muda mrefu hali ambayo inawakatisha tamaa,kutokana na hali hiyo wakati mwingine wanapoweka oda kwa wazabuni hukataa kwa kuamini kuwa hawatalipwa au watalipwa kwa muda mrefu sana. 

 

Read more...
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.