Menu
RSS
habari za hapa na pale

Pato la Taifa lakua kwa kiwango cha chini

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Serikali imewasilisha Bungeni mjini Dodoma taarifa ya hali ya ukuaji wa uchumi inayoonesha kuwa pato la Taifa limekuwa kwa kiwango cha chini ya kiwango kilichokadiriwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu Dk. Mary Nagu alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2014 pato hilo limekuwa kwa asilimia sita nukta nne ikiwa ni chini ya kiwango cha asilimia nane kilichowekwa kwenye Dira hiyo.

Dk. Nagu  ameliambia Bunge kuwa licha ya kiwango hicho kuwa kidogo, bado Tanzania imekuwa miongoni mwa mataifa ishirini duniani ambayo uchumi wake unakua kwa kasi na kuzidi wastani wa ukuaji wa uchumi wa asilimia tano nukta mbili kwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Alibainisha kuwa Sekta ya Huduma ndiyo iliyochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa pato hilo kwa kuchangia asilimia arobaini na moja nukta tatu ikifuatiwa na Sekta ya Kilimo iliyochangia kwa asilimia ishirini na nane nukta tisa.

Alibainisha kuwa Sekta ya Viwanda na Ujenzi imechangia asilimia ishirini na moja nukta saba ya pato hilo huku uzalishaji wa bidhaa za viwandani ukichangia asilimia tano nukta sita.

Akizungumzia hali ya mfumuko wa bei nchini, Dk. Nagu ameliambia Bunge kuwa kiwango hicho kimebakia kwenye ngazi ya tarakimu moja katika kipindi cha mwaka 2014 hadi robo ya kwanza ya mwaka huu.

Dk. Nagu alifafanua kuwa kiwango cha mfumuko wa bei kimeshuka kutoka asilimia saba nukta tisa mwaka 2013 na kufikia asilimia sita nukta moja mwaka 2014.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Suzan Lyimo ameitaka Serikali kusimamia utekelezaji wa Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Elimu nchini (TEA) ili Mamlaka hiyo itekeleze majukumu yake.

 

Suzan alitoa wito huo Bungeni mjini Dodoma alipokuwa anauliza swali la nyongeza kwenda ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

 

Alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria hiyo, Serikali inapaswa kutenga kiasi cha asilimia mbili ya pato la Taifa kwenda TEA ili kiasi hicho kitumike kuimarisha miundombinu ya shule za halmashauri.

 

Alidokeza kuwa endapo kiasi hicho kingepelekwa kama Sheria inavyoelekeza, kungeisaidia Mamlaka hiyo kusimamia utekelezwaji wa shughuli zake ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu hiyo.

 

Hata hivyo akijibu swali hilo kwa niaba ya TAMISEMI, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani ameliambia Bunge kuwa kutengwa kwa kiasi hicho kunategemea ukuaji wa pato la Taifa.

 

 

 

Read more...

DODOMA

  • Last modified on Thursday, 21 May 2015 12:25

Mbunge wa Viti Maalumu {Vijana-CCM}, ESTHER BULAYA amehoji sababu ya Serikali kuchelewesha fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu hadi kusababisha wanafunzi kugoma na kukosa masomo.

BULAYA ametoa hoja hiyo wakati akiomba Mwongozo wa Spika kufuatia mgomo wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam-UDSM, uliosababishwa na kucheleweshewa fedha za kujikimu.

Akijibu mwongozo huo, Naibu Waziri wa Fedha, MWIGULU NCHEMBA amekiri kucheleweshwa kwa fedha hizo kulikosababisha mgomo kwa wanafunzi na usumbufu.

MWIGULU amesema, Serikali imekwishatoa fedha hizo na kuzipeleka kwenye taasisi husika huku akiwataka wakuu wa na wasimamizi wa taasisi hizo kuzitoa fedha hizo haraka bila kusubiri utaratibu wa kawaida ili kuokoa muda wa wanafunzi.

Aidha, Serikali imewaomba radhi wanafunzi hao kwa kucheleweshewa fedha hizo na kwamba kwa sasa Serikali inaweka utaratibu wa kuhakikisha fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja katika taasisi au vyuo ili kuondoa usumbufu.

Frida Manga 

Read more...

Jeshi la Polisi Tanzania latakiwa kuzingatia sheria

  • Last modified on Thursday, 21 May 2015 12:03

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imelitaka Jeshi la Polisi Tanzania, kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Tamko hilo limetolewa baada ya tume hiyo kubaini kuwa jeshi la polisi lilitumia nguvu kupita kiasi katika maandamano ya Chama cha Wananchi-CUF, yaliyofanyika Januari 27 mwaka, Mtoni Mtongani jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa tume, BAHAME TOM NYANDUGE amebainisha hayo jijini Dar es Salaam, wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa tukio uliofanyika kuanzia Februari 3 hadi Mei 15 mwaka huu.

NYANDUGA amesema, mbali na jeshi hilo kutumia nguvu na kusababisha majeraha kwa wanachama wa chama hicho, tume imebaini pia kuwa polisi imewadhalilisha wanachama wawili wa kike wa CUF wakati wakiwa mahabusu.

NYANDUGA ametaja mapendekezo ya ripoti hiyo ya uchunguzi kuwa ni pamoja na taasisi na vyama vya siasa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu za nchi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, tume hiyo imetoa wito kwa chama cha CUF, litafuta namna ya kuboresha mahusiano ma Jeshi la Polisi lakini pia kuzingatia sheria za nchi.

 

***

Mary Yuda {sms}

Read more...

DODOMA.

  • Last modified on Thursday, 21 May 2015 11:39

Kaya laki mbili, elfu sitini, mia moja sabini na tatu {260,173} zimenufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoendeshwa na Mfuko wa Maendeelo ya Jamii Tanzania-TASAF, hadi kufikia Machi 2015.

Hayo yamesemwa bungeni mjini na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Mahusiano na Uratibu, Dakta MARY NAGU, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu {CCM}, FAHARIA SHOMARI HAMISI.

Dakta NAGU amesema, TASAF iliyozinduliwa Agosti mwaka 2012 ikiwa katika awamu ya tatu, imelenga kuzifikia halmashauri mia moja hamsini na tisa {159} kwa Tanzania Bara na Pemba na Unguja kwa Tanzania Zanzibar, zenye kaya masikini milioni moja zenye watu milioni saba.

Amesema, kwa kaya zililzofikiwa na mpango huo, zimefanikiwa kupunguza umasikini kwa kiwango kikubwa kwa kubadili mfumo wa maisha wa kupata milo miwili hadi mitatu kwa siku badala ya mlo mmoja kama ilivyokuwa awali.

Katika swali lake la msingi FAHARIA alitaka kufahamu ni kaya ngapi zimenufaka na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini wa TASAF katika awamu yake ya tatu.

 Frida Manga {TBC live Bunge}

Read more...

DODOMA

  • Last modified on Wednesday, 20 May 2015 13:39

 

Serikali imesema kuwa inatarajiwa kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Kuhudumia Wazee kwa mwaka wa fedha wa 2015, 2016.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, KASSIMU MAJALIWA alipokuwa akijibu swali kwa niaba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Lushoto kupitia Chama Cha Mapinduzi CCM, HENRY DAFA SHEKIFU, MAJALIWA amesema kuwa Serikali inatambua jukumu la kuwatunza na kuwalea wazee ni la kwake na hivyo kupitia Sheria hiyo wazee wataendelea kutunzwa.

Amebainisha kuwa licha ya changamoto zilizopo, bado wazee wameendelea kupatiwa huduma za afya bure ikiwa ni mpango endelevu wa Serikali katika kuwahudumia wazee hao.

Katika swali lake, SHEKIFU alitaka kufahamu muda ambao Serikali itapeleka Bungeni Muswada huo kwa lengo la kuwawezesha wazee kunufaika na huduma mbalimbali za kijamii.

                                                    ***

Frida Manga, Live Bunge

Read more...

DAR ES SALAAM

  • Last modified on Wednesday, 20 May 2015 13:12

Serikali imetangaza kulipuka kwa ugonjwa wa kipindupindu kwenye Kambi ya wakimbizi wa Burundi ya Nyarugusu Mkoani Kigoma na kwamba tayari watu kumi na watano wamefariki dunia kwa ugonjwa huo.

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dakta KEBWE STEPHEN KEBWE amesema watu wote waliofariki dunia kutokana na ugonjwa huo ni wakimbizi wa nchi hiyo wanaokimbia machafuko yanayoendelea nchini humo.

Dakta KEBWE amesema kuwa tayari Wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani WHO imechukua sampuli kutoka kwa wagonjwa kumi na watatu na kwamba wagonjwa kumi na mmoja wamethibitika kuugua kipindupindu.

Amesema kuwa mpaka sasa kuna wahamiaji wapatao laki moja elfu tano mia mbili tisini na wanne wanaotafuta hifadhi na kwamba kati yao wahamiaji mia tano hamsini na wanane wameugua magonjwa ya kuharisha na kutapika huku watu mia mbili thelathini na wawili kati ya hao wamethibitika kuwa na vimelea vya kipindupindu.

Amesema hadi kufikia Mei 19 wagonjwa wapya mia tano themanini na nane wenye dalili za kutapika na kuharisha wameripotiwa.

Dakta KEBWE amedokeza kuwa licha ya Serikali kupeleka dawa, vifaa tiba na vitendanishi ili kukabiliana na ugonjwa huo, bado umeendelea kuenea kwa kasi.

                                                                     ***

Editha Mayemba

Read more...

DODOMA

  • Last modified on Wednesday, 20 May 2015 12:53

 

 

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI, KASSIMU MAJALIWA amesema kuwa mchakato wa kuugawa Mkoa wa Morogoro unaendelea kwa lengo la kuondoa changamoto za kiutawala zinazoukabili Mkoa huo kwa sasa.

Naibu Waziri MAJALIWA ametoa kauli hiyo alipokuwa anajibu swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, SUZAN KIWANGA kwenye kikao cha Bunge la Bajeti kinachoendelea mjini Dodoma.

Ameliambia Bunge kuwa licha ya kuwa jukumu la kuugawa Mkoa wa Morogoro kuwa ndani ya uwezo wa Mkoa huo, Serikali itaangalia namna ya kuzungumza na uongozi wa Mkoa huo ili kuondoa changamoto zinazoyakabili maeneo mengine ikiwemo Wilaya ya Ulanga kabla ya hatua hiyo haijachukuliwa.

Katika swali lake la msingi KIWANGA alitaka kufahamu muda ambao mpango wa kuugawa Mkoa huo utatekelezwa ili kuondoa changamoto zilizopo.

                                                        ***

Frida Manga, Live Bunge

 

Read more...

DAR ES SALAAM

  • Last modified on Wednesday, 20 May 2015 12:21

Imeelezwa kuwa endapo viashiria vya uvunjifu wa amani vitaachwa viendelee, kuna hatari kubwa kwa Taifa la Tanzania kuangamia.

Onyo hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Dakta SALIM AHMED SALIM wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mashauriano kuhusiana na amani, umoja na utulivu wa nchi uliofanyika mjini Dar es salaam.

Dakta SALIM amesema kuwa ni jukumu la kila mtanzania kukemea vitendo vya uvunjifu wa amani vilivyoanza kujitokeza nchini.

Ametaja vyanzo vya vitendo hivyo kuwa ni pamoja na migogoro ya kisiasa na haki kutotendeka kwa wananchi.

Akizungumzia lengo la mkutano huo, Dakta SALIM amebainisha kuwa ni kuzungumzia waziwazi viashiria vinavyohatarisha uwepo wa amani na utulivu nchini na kutafuta mbinu za kuzuia viashiria hivyo kuota mizizi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo JOSEPH BUTIKU amewataka wajumbe wa mkutano huo kutafakari kwa kina vyanzo vya kuhatarisha amani ya nchi ikiwa ni pamoja na maisha ya fujo.

Akizungumza kwa niaba ya vyama vya siasa, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF Profesa IBRAHIMU LIPUMBA ameitaka Serikali kuhakikisha haki inatendeka na kwamba hakuna amani bila haki huku Brigedia Jenerali Mstaafu FRANCIS MBENA ametaka kuheshimiwa kwa wazee kama njia mojawapo ya kudumishwa kwa amani nchini.

Na.Maria Yuda

 

Read more...

Rais FILLIPE NYUSI amelihutubia Bunge Tanzania

DODOMA

Rais wa Msumbiji FILIPE NYUSI ametaka ushirikiano baina ya Tanzania na Msumbiji udumishwe katika nyanja zote kwa manufaa ya nchi hizo mbili.

NYUSI ametoa wito huo alipokuwa akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana June 18,2015 linaloendelea na kikao chake cha Bajeti mjini Dodoma.

Amesema kuwa kwa muda mrefu Tanzania na Msumbiji zimekuwa na ushirikiano wa dhati wa muda mrefu unaotokana na udugu uliopo baina ya pande hizo mbili.

Amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kuzitumia fursa zilizopo nchini Msumbiji kwenda kufanya biashara na kwamba milango iko wazi kwao kufanya hivyo.

Akizungumza mara baada ya NYUSI kulihutubia Bunge hilo, Spika wa Bunge ANNE MAKINDA amemshukuru Kiongozi huyo wa Msumbiji kufanya hivyo na kwamba amekuwa Rais wa kwanza wa Msumbiji kulihutubia Bunge la Tanzania.

Kabla ya kulihutubia Bunge, NYUSI akiambatana na mwenyeji wake Rais JAKAYA KIKWETE amepata fursa ya kukagua gwaride maalum nje ya viwanja vya Bunge na kupigiwa nyimbo za Taifa.

                                                   ***

Frida Manga, live Bunge

Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.