Menu
RSS
habari za hapa na pale

Vifo vya Maaskofu wastaafu Nkalanga na Shija ni pigo kubwa kwa TEC.

Na Martin Kuhanga

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limepata pigo kubwa baada ya Maaskofu wake wawili wastaafu kufariki dunia katika kipindi kisichozidi siku tisa.

Maaskofu hao ni mhashamu Askofu Mathew Shija, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Kahama aliyefariki dunia Desemba 9, 2015 na Placidius Gervas Nkalanga, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, aliyefariki dunia, Ijumaa usiku, Desemba 18. 

Vifo vya Maaskofu wastaafu Nkalanga na Shija ni pigo kubwa kwa TEC kwa kuwa vinafanya idadi ya Maaskofu wastaafu Tanzania kupungua hadi sita.

Maaskofu wastaafu waliobaki baada ya kufariki dunia kwa maaskofu hao wawili ni Askofu Mathias Isuja wa Dodoma, Askofu Nestory Timanywa wa Bukoba na Askofu Mkuu Norbert Mtega wa Songea.

Wengine waliobaki ni Mhashamu Askofu Emmanuel Mapunda wa Mbinga, Askofu Gabriel Mmole wa Mtwara na Askofu Jacob Koda wa Same.

Askofu Nkalanga aliyezaliwa Askofu Nkalanga aliyezaliwa Juni 19, 1919 huko Ruti, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 96, anatarajiwa kuzikwa Jumanne, Desemba 29, 2015, katika Abasia ya Hanga, Jimbo Kuu Katoliki la Songea.

Alipewa Daraja la Upadri Julai 15, 1950 na Aprili 18, 1961 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane XXII kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba na kuwekwa wakfu Mei 21, 1961.

Baadaye, Machi 6, 1969 akasimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba baada ya Mwadhama Laurian Kardinali Rugambwa kuteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Askofu Nkalanga liendelea kuwa Askofu wa Jimbo la Bukoba hadi alipojiuzulu Novemba 26, 1973 na kujiunga na Wamonaki wa Shirika la Wabenediktini, Abasia ya Hanga, Songea alikoishi kwa miaka 42 hadi alipofariki dunia.

Akiwa Askofu wa Bukoba, Askofu Nkalanga alibahatika kuhudhuria Sinodi ya Pili ya Maaskofu iliyofanyika kati ya mwaka 1962 na 1965, akakosa awamu ya pili pekee iliyofanyika Septemba 29, 1963 hadi Desemba 4, 1963.

 

Kati ya Februari 1966 na Mei 29, 1969, Askofu Nkalanga alikuwa Msimamizi wa Kitume wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Kabale, Magharibi mwa Uganda, mara tu lilipoanzishwa.

 Askofu mstaafu Shija aliyefariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuungua kwa muda mfupi ingawa alikuwa akikabiliwa na magonjwa ya mara kwa mara kutokana na umri wake mkubwa.

Maziko ya Askofu Shija alizaliwa Aprili 17, 1924 huko Puge Jimbo Kuu Katoliki la Tabora na kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 91, yalifanyika jimboni Kahama, Alhamisi Desemba 17, 2015.

Askofu Shija alipata Daraja Takatifu la Upadri Januari 17, 1954 na miaka 30 baadaye, Febuari 26, 1984 akasimikwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Kahama baada ya kuteuliwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, Novemba 11, 1983.

Askofu Shija alistaafu kuliongoza Jimbo hilo Aprili 24, 2001 akiwa na umri wa miaka 77 na nafasi yake kuchukuliwa na Askofu wa sasa, Mhashamu Ludovick Minde aliyesimikwa Agosti 5, 2001.

 

end 

Read more...

Safari ya Orchestra Safari Sound {29}

Na Fred Mosha

 

TUNAKUTANA Tena tukiendelea kusafiri pamoja na bendi ya Orchestra Safari Sound OSS, mojawapo ya bendi zilizojizolea umaarufu mkubwa hata kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki.

 

Katika safu iliyopita ya kusafiri na Orchestra Safari Sound kwa namna moja ama nyingine tuliangalia baada ya nyimbo zilizoutambulisha mtindo wa Power Iranda nini kiliendelea ndani ya bendi hiyo na hapa nakiri kusema kuwa tunaanza kushuka mwishoni mwa safari hii ya OSS.

 

Pia tuliangalia kuhama bendi kwa mwanamuziki mkongwe Muhidin Maalim Gurumo ambaye paamoja na mpiga gitaa la bass Charles John Ngosha waliaamua kurejea ndaani ya DDC Mlimani Park japo Gurumo alikaa Sikinde kwa kipindi kifupi kidogo.

 

Aidha tuliaangalia ujio wa mara ya pili wa mwanamuziki Maxmillian Bushoke ndani ya OSS mara baada ya kuchukuliwa kutoka Sikinde na kufanywa kuwa Kiongozi wa bendi lakini pia pamoja na ujio wa mwanamuziki Suleiman Mwanyiro ambao hata hivyo hawakukaa sana ndani ya bendi hiyo.

 

Sasa leo hebu tuangalia hatua nyingine inayochukuliwa na OSS baada ya baadhi ya wanamuziki wake kuanza kuhama na kujiunga na bendi zingine lakini kabla hatujaendelea basi naa tujikumbushe nini tulichokiangalia kwenye sehemu iliyopita.

 

Gurumo anaamua kuachana na OSS

 

Baada ya kuitumikia bendi hiyo kwa takribani miaka sita akiwa kama Kiongozi wa bendi hiyo hatimaye Mwanamuziki mahiri Muhidin Maalim Gurumo alitangaza kuachana na OSS na kwa maelezo yake aliyoyatoa wakati anachukua uamuzi huo ni kuwa ati alitaka kupumzika shughuli za muziki kwa muda kabla hajarejea tena.

 

Haikuwa hatua ya kushtua sana kwa Gurumo kuchukua uamuzi huo hasa kutokana na nafasi yake wakati huo ndani ya OSS hiyo ya Power Iranda kuanza kuonekana finyu hasa baada ya kuvuliwa uongozi wa bendi na kupewa Benno lakini pia kutoshiriki nyimbo nyingi za Power Iranda wakati huo.

 

Gurumo alitangaza kuchukua uamuzi huo huku mkononi akiwa tayari na wimbo Usia kwa watoto aliotungia na kufanyia mazoezi akiwa na OSS lakini kwenye kurekodi nyimbo hizo za Power Iranda alikataa wimbo wake usirekodiwe.

 

Kumbe wakati huo anatangaza kupumzika, Mzee Gurumo alikuwa anafanya ‘mambo yake’ kimyakimya kwani juma moja baada ya kutangaza habari hiyo, zikaja taarifa za gwiji huyo kurejea kwenye bendi yake ya zamani ya DDC Mlimani Park ‘kwa sababu maalum’

 

Nimetaja ‘sababu maalum’ kwa kuwa mipango ya kurudi kwake Sikinde ilifanyika kwa hila ili amshawishi Hassan Bitchuka aliyekuwa Mlimani siku hizo warejee wote JUWATA, jambo lililofanikiwa.

 

Hata hivyo Gurumo hakuondoka OSS peke yake aliondoka na Charles John Ngosha na kurudi wote ndani ya Sikinde kaabla ya Gurumo na Bitchuka hawajarejea JUWATA kwa kadiri ya mipango ilivyokuwa.

 

Baadhi ya wanamuziki wanaanza kuondoka OSS

 

Inaonekana kuwa kuondoka kwa Gurumo kuliwashtua baadhi ya wanamuziki wa ndani ya OSS kiasi kuwa walianza kuona mustakabali wao sio mzuri licha ya wengine kudai kuwa waliondoka kutokana na kile walichodai kuwa ni kutotimiziwa kwa makubaliano waliyoahidiwa walipokuwa ndani ya OSS.

 

Baadhi ya wanamuziki hao ni pamoja na Bennovilla aliyejiunga na Vijana Jazz, Maneno Uvuruge aliyejiunga na JUWATA Jazz, Muhina Panduka aliyeamua kurejea Washirika, Shaw Hassan Shaw aliyejiunga na Washirika na Mohamed Shaweji aliyejiunga na Sikinde kabla ya ‘kufukuzwa’ na mashabiki kwa madai kuwa sauti yake ilikuwa haiendani ya mirindimo ya Sikinde.

 

Max Bushoke ndani ya Power Iranda

 

Kutokana na hali ya mambo kuanza kwenda kombo ndani ya OSS, kwa akili ya harakaharaka Abel Baltazar aliamua kumfuata Max Bushoke ambaye kwa wakati huo alikuwa karejea Sikinde ili ajiunge tena na OSS na safari hiyo akiwa kama Kiongozi wa bendi, jambo aliloafikiana nalo na kujiunga tena na bendi hiyo, mkononi akiwa na wimbo Messanger kawa Supervisor.

 

Ikumbukwe kuwa kabla ya wimbo huo, Max alikuwa tayari ana wimbo wa Visa vya Messanger ambao alianza kuutunga akiwa ndani ya OSS kabla hajahama nao na kwenda Bima Lee.

 

Alipojiunga tena na OSS safari hii akapendekeza achukuliwe pia na Suleiman Mwanyiro ambaye ndio kwanza alikuwa karejea nchini akitokea Japan alikokuwa anafanya shughuli zake za kimuziki ambapo naye alikubali na kujiunga na OSS kwa mara ya pili.

 

Akiwa OSS Mwanyiro ndiko alikoutungia wimbo Kauka nikuvae kwa mara ya kwanza ambao arrangement yake imetofautiana kwa kiasi fulani na ile aliyoifanya akiwa na OTTU ambapo katika wimbo huo wa Msondo, kipande ambacho Bitchuka alikiimba ‘Naona aibu watoto viraka vimewajaa kama matangazo gazetini nawe kazi huna’

 

Max aliimba ‘Naona aibu watoto viraka vimewajaa vikubwa kama gazeti la Daily News’ ingawa asilimia kubwa ya maneno yaliyokuwemo ndani ya wimbo wa OSS ndio hayohayo yaliyotumika ndani ya wimbo wa OTTU.

 

Hata hivyo baada ya muda mchache, Max alifukuzwa ndani ya OSS kwa sababu za utovu wa nidhamu ambao siwezi kuuandika hapa huku Mwanyiro akichukuliwa sasa na Msondo na muimbaji mwingine Tino Masinge akijiunga na DDC Mlimani Park na kuondoka na wimbo wake wa Arawa aliouanzia mazoezi OSS na kupigwa kwenye kumbi za starehe.

 

Sasa tuendelee

 

Nguza Vicking ndani ya OSS

 

Naweza kusema lilikuwa tukio la kushtua kidogo lililotokea mwishoni mwa mwaka 1991 pale uongozi wa OSS ulipoamua kwa kauli moja kumchukua mpiga gitaa nguli na mtunzi Nguza Mbangu Vicking ambaye kwa wakati huo alikuwa ametokea kwenye bendi ya Sambulumaa.

 

Hakuna hata mtu mmoja aliyetarajia kuwa Nguza angekuwa mwanamuziki wa OSS kipindi hicho hasa ikizingatiwa mazingira aliyoondokea Maquis wakati huo huku wengi wa mashabiki wakidhani kuwa Sambulumaa ilikuwa bendi yake kabisa lakini la kushangaza ni kuwa iweje tena Nguza aiache bendi yake mwenyewe naa kurejea tena kwenye maisha ya kuajiriwa??

 

Labda pengine majibu yaake anayo Nguza mwenyewe lakini ukweli ndio ulikuwa huo, Nguza kajiunga na OSS, bendi ambayo siku za nyuma ilikuwa naa upinzani mkali sana na Maquis ambayo Nguza ndiye alikuwa Jemedari wake na yeye mwenyewe ndiye aliyeongoza mapambano dhidi ya OSS iliyokuwa na Ndala Kasheba wakati huo.

 

Hata hivyo mashabiki wa muziki wa dansi walikuwa na hoja kuwa hakuna jambo lisilowezekana kwa Nguza kujiunga na OSS, hasimu wa zamani wa Maquis wakati mwaka 1985, Kasheba ambaye aliongoza Jeshi la Dukuduku dhidi ya Maquis aliamua naye kujiunga na Maquis!!

Basi hivyo ndivyo ilivyotokea na mara tu baada ya kujiunga na OSS akafanywa kuwa Kiongozi wa bendi huku Abel Baltazar ‘Bwana Mipango’ akiteuliwa kuwa Meneja wa bendi hiyo.

 

Kabla ya kufanya lolote lile, Nguza alifanikiwa kutengeneza na kurekodi wimbo wa harakaharaka uliozungumzia masuala ya uzazi kabla ya kuamua kuwa OSS isimamishe maonesho yake ya muziki na isukwe upya sanjari na kuchukua wanamuziki wapya.

 

Naam!! Ndivyo ilivyokuwa kwani OSS iliamua kusimamisha maosho yake na mchakato wa kutafuta wanamuziki wengine wapya kwa ajili ya kujiunga na bendi hiyo ukaanza na safari hii Nguza na Abel ndio waliosimamia jambo hilo.

 

Tofauti na ilivyotarajiwa na wengi kuwa labda pengine, mtazamo wa Nguza na Abel ungekuwa kwa bendi za hapahapa Tanzania wakati wa mchakato wa kuchukua wanamuziki hao haikuwa hivyo licha ya kuwepo kwa baadhi ya wanamuziki wachache waliotoka bendi za hapahapa nchini waliochukuliwa kipindi hicho.

 

Safari hii Nguza alisafiri mpaka Zambia ambako huko aliwachukua baadhi ya wanaamuziki wenye asili ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo DRC waliokuwa wakifanya kazi zao nchini humo na vikundi tofauti na kuwashawishi kuja Tanzania na kujiunga na OSS.

 

Ndio!! Nguza alifanikiwa kuwachukua wanamuziki kadhaa ingawa hawakuwa wengi ambao ni pamoja na muimbaji mwenye sauti tamu Edwars Chibangu ‘Eddy’ ambaye ana uwezo mkubwa wa kutunga, kupanga muziki, kuelekeza, kuimba na pia ni mpigaji mzuri wa gitaa hasa solo.

 

Huyu Eddy Chibangu ndiye aliyemfundisha Omari Mkali, kuimba na kuachana na upigaji wa tarumbeta aliokuwa akiufanya wakati wa OSS hususan walipokuwa wote ndani ya bendi ya Tango Stars iliyokuwa na maskani yake kwenye hoteli ya Vatican Sinza.

Mbali na Eddy Chibangu, mwanamuziki mwingine aliyechukuliwa ni muimbaji Baldwin Kazoka ambaye kwa sasa ni marehemu aliyekuwa na sauti nzuri sana wakaati huo na ndiye aliyeimba nakala asilia ya wimbo Salima ambao huohuo aliurudia Papy Kocha.

 

Wengine waliochukuliwa ni pamoja na muimbaji na Rapa Chibangu Chichi ambaye baadaye alikwenda MK Group, pia mpiga kinanda ambaye namkumbuka kwa jina moja la Patrick ambao wote hawa walikuja Tanzania na kuungana na wanamuziki waliokuwa ndani ya OSS kwa wakati huo.

 

Kwa upande wa wanamuziki wa hapa nyumbani, OSS kupitia kwa Abel ilifanikiwa kumrudisha kundini mpiga sax mahiri King Maluu aliyekuwa Tancut Almasi nyakati hizo pamoja na kuwachukua wanamuziki wengine kama mpiga gitaa Omary Makuka ambaye zamani aliwahi kuwa na Maquis, mpiga drums Hatibu Said maarufu kama Kish Nyapara aliyewahi kuwa na TOT enzi za Banza Stone na pia alijumuishwa mpiga kinanda gwiji Abdul Salvador ‘Fadher Kidevu’ aliyechukuliwa kutokea Washirika Tanzania Stars.

 

Mtindo wa Rashikanda Wasaa

 

Ndio gia aliyoingilia Nguza ndani ya OSS, mtindo mpya wa Rashikanda Wasaa uliochukua nafasi ya Power Iranda pamoja na kuubadilisha kabisa muziki wa OSS na kuanza kupiga soukouss, muziki uliotawala kipindi hicho cha mwanzoni mwa miaka ya 1990.

 

Kwa ujumla wake OSS ikawa imezaliwa kwenye enzi mpya kuanzia wanamuziki hadi aina ya muziki uliokuwa ukipigwa ikiwa ni pamoja na kuingiza vionjo vya moja kwa moja vya soukouss kupitia Rapa wake wa wakaati huo Chibangu Chichi lakini pia hata mpangilio waa muziki wake.

 

Nyimbo karibu zote za Rashikanda Wasaa wakati huo zilikuwa zimeathiriwa moja kwa moja na Soukouss hili jambo lililowafanya mashabiki wa OSS kuukosa muziki waliouzoea kuanzia nyakati za Ndekule hadi hiyo Power Iranda na hivyo kuzalisha changamoto mpya ya kutafuta mashabiki wapya kwa vionjo vipya.

 

Inawezekana kabisa kuwa hatua hiyo ilichukuliwa hasa ikitiliwa maanani kuwa muziki wa aina hiyo ndio uliokuwa kwenye soko nyakati hizo na kuvuma kwa wanamuziki Kanda Bongoman, Pepe Kalle, Aurlus Mabele na Loketo yake, Alain Konkou, bendi ya Soukouss Stars na wanamuziki na vikundi vingine vya aina hiyo ndiko kulikozifanya baadhi ya bendi za Tanzania kipindi hicho nazo kukumbwaa na mkumbo huohuo.

 

Tutaendelea toleo lijalo

 

 

Read more...

Serikali itupie jicho kero hii

Na Mwandishi Wetu

KUTOKANA na mizozo ya ardhi kuzidi kuongezeka kila kukisha, ni vema Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli, kumulika ufisadi kwenye eneo hilo kwani wengi wamepoteza maisha kwa migogoro hiyo.

Kama inavyofahamika ardhi ni bidhaa muhimu katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa ambapo, asilimia kubwa ya raia wa nchi hii wanategemea ardhi kama nyenzo kuu ya ustawi wao.

Hivyo masuala yanayotokana na miliki na matumizi ya ardhi yana uzito wa kipekee katika maisha ya watu wote pamoja na Taifa kwa ujumla.

Katika kipindi cha Ukoloni umiliki wa ardhi nchini ulikuwa wa kibaguzi ambapo ardhi kubwa na yenye rutuba ilimilikiwa na Wakoloni.

Mara baada ya Uhuru wa Tanganyika, Desemba 9, mwaka 1961, ardhi yote iliwekwa chini ya umma na mtu mmoja mmoja kuruhusiwa kumiliki wa ajili ya matumizi maalum kwa muda maalum na masharti maalum.

Hata hivyo kutokana na ongezeko la watu na kuzidi kuongezeka kwa miji sambamba na kasi ya kukua kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile Kilimo, ufugaji, uchimbaji wa madini, ujenzi, tumeshuhudia tatizo la migogoro ya ardhi ambayo ikitokea siku kwa siku.

Kuwepo kwa migogoro hii kumesababisha uvunjifu wa amani kwa baadhi ya maeneo na hata kusababisha vifo, hasa kwa migogoro inayokutanisha pande mbili tofauti kama vile, wakulima na wafungaji.

Lakini pia tumeshuhudia migogoro baina ya wawekezaji na wazawa, ambayo nayo kimsingi imekuwa ikileta tafrani na uvunjifu wa amani katika baadhi ya maeneo  hapa nchini.

Migogoro inayoumiza kichwa na kuleta tatizo kubwa ni ile ya wananchi kuvamia maeneo ya wazi na kuyaendeleza kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii hatimaye ni kuibuka kwa migogoro ya aridhi baina ya serikali na wananchi.

Huwenda changamoto hizi za migogoro ya ardhi zinatokana na usimamizi mbovu wa sheria, sera kutoka kwa watendaji wanaosimamia sheria hizo au ongezeko la watu na ukuaji wa uchumi unaopelekea watu kukosa ardhi kuendesha shughuli zao za kijamii, kiuchumi.

Tatizo la migogoro ya ardhi na usmamizi wa sheria na mfumo mzima wa ardhi yameleta changamoto kubwa katika jamii na Serikali na hivyo kuchangia wadau mbalimbali kutoa mapendekezo yatakayosaidia kukabiliana na tatizo hilo kwa kupitia upya sheria ya ardhi.

Kuwepo kwa migogoro hiyo kumechangia matatizo makubwa, ambayo hata Serikali kukosa mapato yake kutokana na hata uuzwaji wa maeneo kiholela kwa misingi ya rushwa.

Ila Watanzania wana imani kubwa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli, kwamba ataishughulikia ipasavyo na mafisadi wataonekana wazi.

Moja ya chanzo cha migogoro hiyo kwa namna moja ama nyingine ni Wizara ya Ardhi, kwani wapo baadhi ya watendaji wasio waaminifu kuanza ngazi ya juu hadi vijiji ambako huyauza maendeo kwa misingi ya rushwa na hivyo pande moja kuonewa.

Moja ya suluhu ya migogoro ya ardhi nikufanya mapitio ya mfumo mzima wa usimamizi wa ardhi na sheria za ardhi.

Itakumbukwa kwamba katika miaka mingi sababu kubwa iliyosababisha Tume hiyo kufanya mapitio hayo, ni kutokana kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi licha ya maboresho na mabadiliko mbalimbali ya sheria na usimamizi wa mfumo wa ardhi hapa nchini.

Aidha katika miaka ya nyuma, Mahakama zilikuwa na mamlaka ya kusikiliza mashauri yanayohusiana na migogoro ya ardhi hadi mwaka 1995 ambapo sera ya ardhi ilitungwa na hivyo kupelekea mabadiliko ya Sheria za Ardhi na Sheria zinginezo.

Mabadiliko hayo ya yote yalipelekea kuanzishwa Mabaraza ya Ardhi tangungazi ya Vijiji hadi Wilaya, Sheria inayotoa mamlaka kwa mabaraza hayo kusikiliza mashauri yote yanayohusiana na ardhi kwa lengo la kupunguza mlundikano wa kesi na migogoro ya ardhi.

Katika ngazi ya Mahakama Kuu kilianzshwa Kitengo maalum cha kusikiliza mashauri ya ardhi pamoja na rufaa zote za kesi za ardhi zilizotoka Mabaraza ya Ardhi Kata.

Pamoja na mabadiliko hayo ya sheria yaliyofanyika katika mfumo mzima wa utatuzi wa migogoro ya ardhi, bado inaendelea kutokea na hata kusababisha wananchi wengi kupoteza maisha na mali zao kiwemo ardhi.

Lakini pia Mabaraza hayo yamekuwa na changamoto nyingi ikiwemo kukosekana kwa usimamizi wa Mabaraza hayo tika Mahakam za juu kwani Baraza hayo ya vijiji na Kata yanasimamiwa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) wakati Mabaraza ya ardhi na Nyumba ya Wialaya yanasimamiwa na Wizara ya Ardhi na rufaa zote zinazotoka chini zinasimamiwa na Mahakam kuu na Mahakama ya Rufaa ambayo iko chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

Tume ya Kurekebisha Sheria kwa kutumia mamlaka yake ya kisheria imefanya mapitio sheria na mfumo mzima wa utatuzi wa migogoro ya ardhi nahii ni kufanikisha mapitio ya Sheria na utafiti ambapo Tume iliwahusisha wadau mbalimbali kutoka Mikoa tofauti lengo ni kupata maoni yatakayo saidia kuboresha sheria ya ardhi.

Zipo tafiti zilizofanywa na Tume hiyo, uliolenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa sheria na kubaini mapungufu yanayojitokeza wakati wa kutekeleza sheria hizo na kisha kutoa mapendekezo kwa serikali kwa lengo la kuondoa dosari za kisheria na kiutekelezaji zilizojitokeza ili malengo na makusudio ya sheria hiyo yaweze kutekelezwa kwa ufanisi na mafanikio zaidi kama yalivyokusudiwa.

Tume hiyo ilikuja na mapendekezo yake yanatokana na utambuzi wa uwepo mabadiliko makubwa katika nyanja ya kiuchumi, kisera na kijamii, na kwamba Tume hiyo tayari imekamilisha taarifa ya utafiti yenye mapendekezo na kuiwasilisha kwa Waziri wa Katiba na Sheria mwezi Mei mwaka huu kwa mujibu wa sheria husika.

Katika taarifa yake tume hiyo ilisema kuwa: “Katika utafiti huo, Tume ilibaini mapungufu mbalimbali ya kisheria, kisera kiutekelazaji ambayo yamepelekea migogoro ya ardhi kuendelea kuongezeka na kupelekea wanachi kuanza kukosa imani na mfumo wa utatuzi wa Migogoro ya ardhi uliopo.

Sambamba na hilo, ongezeko la watu, hifadhi za misitu hifadhi za Taifa na wakati mwingine katika hali inayoleta migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya watumiaji.

Lakini pia utafiti huo ulibaini mabaraza hayo machache ya Wilaya yalilemewa na wingi wa rufaa kutoka Mabaza ya Kata, lakini pia utafiti huo ulionyesha kuwa uchache wa majaji wa kitengo cha Ardhi ambao walishindwa kuhimili wingi wa rufaa zilizotoka kwenye mabaraza (38).

Kutokana na mapungufu hayo na mengine mengi Tume hiyo ilitoa mapendekezo na kuyawasilisha serikali ili kusaidia kuboresha sheria ya ardhi na usimamizi wake.

Mapendekezo hayo ni pamoja na kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kuunganisha mabaraza hayo na Mahakama za kawaida ili kuwa na usimamizi mzuri tangu ngazi ya chini hadi ngazi za juu za Rufaa, serikali kuona uwezekano wa kuongeza majaji kitengo cha ardhi lakini pia kufanyamaboresho sambamba na kuboresha mfumo mzima wa utatuzi wa migogoro.

Matatizo yanayohitaji mabadiliko ya sheria kwa mfano kuruhusu Mahakama za kawaida kuendelea kupokea na kusikiliza mashauri pale ambapo mabaraza hayajaanzishwa lakini pia yapo yanayohitaji kufikiriwa upya kisera, pengine kurejesha mfumo mmoja wa utatuzi wa migogoro chini ya mahakama.

Marekebisho na maboresho ya sheria yatasaidia kumaliza ama kuondoa tatizo la migogoro ya ardhi nchini ambayo kwa miaka mingi imeleta matatizo katika jamii.

Migogoro mingi ya ardhi katika masuala ya uvamizi wa maeneo ya wazi inatokana na wananchi kutofahamu sheria na mfumo mzima wa usimamizi wa ardhi hivyo swala elimu kwa umma ni la muhimu ili kuwezesha jamii kuondokana na tatizo hilo.

Utatuzi na usuluhishi wa migogoro ardhi mapema kutadumisha kutachangia ukuaji wa uchumi lakini pia kutadumisha ushirikiano na amani kati ya wakulima na wafugaji na serikali kwa ujumla lakini pia usimamizi mzuri utasaidia kuondoa urasimu uliopo vikwazo na mlundikano wa kesi mahakamani.

Ni matumaini kwamba mapendekezo hayo ya yatasaidia kuondoa tatizo lakini pia yatasaidia kupunguza gharama za kiutawala kwa kuwa na Wizara moja itakayosimamia utatuzi wa migogoro ya ardhi nchini.

End 

Read more...

IGWUTA YAITAKA SERIKALI KUHAKIKISHA WAMILIKI WA VYOMBO VYA HABARI WANATOA AJIRA KWA WATU WAO

Chama cha wafanyakazi wa Viwanda na Sekta mbalimbali IGWUTA kimemtaka Rais JOHN MAGUFULI kuhakikisha wamiliki wa vyombo vya habari wanatoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wake hususani wana habari

Katibu Mkuu wa Chama hicho MICHAEL CHAMBUA ametoa kauli hiyo mjini Dar es Salaam wakti akimpongeza Dakta MAGUFULI kupitia waandishi wa habari mjini Dar es salaam.

 

CHAMBUA amesema kuna haja kwa waandishi wa habari kupewa mikataba ya ajira ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi badala ya kutumika kuficha baadhi ya maovu yanayofanywa na watu wasio waadilifu nchimi.

 

Aidha amempongeza Dakta MAGUFULI kwa utendaji wake mzuri anaoufanya tangu aingie madarakani huku akimtaja Rais MAGUFULI kuwa Rais wa kwanza kuomba aombewe.

 

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi kumuunga mkono na kusema kuwa ana imani na MAGUFULI kuwa atafufua viwanda vilivyokufa na kuongeza ajira na kumkumbusha Kiongozi huyo kutowasahauwatu wa kawaida ili aepuke kujenga urasimu.

 

                                                 ***

 

 

Read more...

UTUME WA FAMILIA WAOMBEA AMANI TANZANIA

  • Last modified on Saturday, 24 October 2015 11:27

 

 

Mkurugenzi wa Utume wa Familia Jimbo Kuu la Dar es Salaam Padri NOVATUS MABULA, jana aliongoza ibada maalum ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea Amani,Haki Kweli na na Utulivu katika Uchaguzi Mkuu, itakayofanyika Jumapili ya Oktoba 25, mwaka huu.

 

Taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Utume wa Familia ya Wanamaridhiano Jimbo Kuu la Dar es Salaam, CHARLES MISANGO, imeeleza kuwa Misa Takatifu hiyo ilifanyika katika Parokia ya Msimbazi kuanzia majira ya saa kumi na moja {11:00} jioni.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa katika kipindi hiki ni muhimu kumwomba Mwenyezi Mungu ili aibariki Tanzania na kuwaongoza watu wake kuendesha uchaguzi kwa amani na usalama hatimaye wapatikane viongozi anaowataka

Misa hiyo imeadhimishwa pia kwa mujibu wa maandiko matakatifu ‘Njooni twende mbele za Bwana kwa kuwa, “Bwana asipoujenga mji, wajengao wafanya kazi bure”.

***

 

Martin Kuhanga 

 

Kard. Pengo ataka waamini kuitegemeza Tumaini Media

Na Princepius Burchard

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka watu wote wenye mapenzi mema  na wenye karama mbalimbali ajitoe kwa ajili ya kuitegemeza Tumaini Media.

Amesema utoaji wa mchango wao wa hali na mali zikiwemo fedha na vipawa walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu utasaidia kutimiza lengo la upashanaji habari kwenye vyombo vya habari vya jimbo hilo ikiwemo Gazeti Tumain Letu, Redio Tumaini na Televisheni Tumaini.

Kardinali Pengo alitoa rai hiyo wakati wa kikao cha Marafiki wa Tumaini Media (UMTUME), kilichofanyika katika ukumbi wa Kardinali Rugambwa katika Parokia ya Mtakatifu Petro, Oyestabay  jijini Dar es Salaam.

Askofu Pengo alisema watu wote wenye mapenzi mema wanatakiwa kuendeleza na juhudi zinazotakiwa katika kuitegemeza  Tumaini Media  pasipo kuchoka huku akiwashukuru Marafiki  wa Tumaini Media kwa moyo wao, waliouonesha hususan kutoa walichonacho ndani ya uwezo wao.

“ Msikate tamaa hata kama mkikutana na wakati mgumu”,alisema Askofu Mkuu Kardinali Pengo.

Kardinali Pengo alihimiza kuhusu kazi njema na nzuri inayofanywa na umoja huo wa Marafiki wa Tumaini Media katika kutimiza moja ya wajibu wao wa msingi ulio katika nguzo nne muhimu, wajibu wa ushauri kila panapostahili. Kardinali Pengo alisema kutimiza wajibu huo kwani utaepusha hatari za sasa zinazoikumba jamii kutokana na upotoshaji wa kutisha uliopo  katika jamii kupitia Vyombo vya Habari, unaokolezwa kwa manufaa ya watu binafsi na si jamii husika.

Kardinali Pengo aliongeza kuwa manufaa hayo yanaweza kuwa ya kisiasa pamoja na kiuchumi kwa maana ya kulenga zaidi biashara kuliko uhalisia wa jambo husika,  na hivyo kupotosha ukweli.

Kwa mujibu wa Kardinali Pengo kuna hatari endapo hali hio isipokemewa kwa sababu inaweza kuingia hata katika Vyombo vya Upashanaji Habari vya Kanisa na kuiathiri jamii.  

Aidha amesisitiza kuwa , daima Askofu hawezi kukaa kando ya Redio pamoja na Terevisheni au kusoma Gazeti Tumaini, ili aweze kuona ni wapi kuna makosa bali kila mmoja katika umoja huo kwa nafasi yake anawajibu kutoa maoni yake endapo anaona mambo yanakwenda mrama. Pamoja na hayo amewashukuru kwa kumsaidia Askofu katika kutimiza jukumu hilo huku akitoa rai kwa marafiki hao kuongezeka ili kusikiliza na kutazama vyombo hivyo vya upashanaji habari.

Naye Mwenyekiti wa umoja huo wa Marafiki wa Tumaini Media (UMTUME), Peter Macha, amekumbushia juu ya majukumu ya msingi yanayotakiwa kutimizwa na marafiki hao kwa mujibu wa katiba ya umoja huo inavyoelekeza ikiwa ni pamoja na kushauri, kushiriki, kuombea na kutegemeza.

Macha alisema majitoleo yao kwa ajili ya kuitegemeza Tumaini Media yamekuwa yakitolewa na Marafiki hao kila mwaka tangu umoja huo ulipoanzishwa mwaka 2011.

Pia ameahidi kuwa wanategemea kutoa jumla ya shilingi za kitanzania milioni 10, wakati wa sherehe ya upashanaji habari itakayoadhishwa katika wiki ya pili ya mwezi wa nane mwaka huu.

Ameongeza kuwa hii itakuwa ni kuelekea katika kutimiza lengo walilojiwekea marafiki hao la kuchanga jumla ya Shilingi za kitanzania milioni 37 kwa ajili ya Tumaini Media.

Read more...

Watu wote mnaalikwa mkutano injili Jangwani Dar es salaam

 

Katibu wa Karismatiki Katoliki Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam MEDARD BANZI amewataka Waamini kuendelea kujitokeza kushiriki Kongamano la Roho Mtakatifu linaloendelea kwenye Viwanja vya Jangwani.

 

Ametoa Wito huo alipkuwa akizungumza na Kituo hiki kuhusu Kongamano hilo lililoanza Julai 10 na linatarajiwa kufikia kilele Dominika ya Upashanaji Habari Agosti 2 Mwaka huu.

 

Lengo la Kongamano hilo ni kufikisha ujumbe wa Injili ya YESU KRISTO kupitia uweza wa Mungu Roho Mtakatifu ikiwa mojawapo mapaji yake yote Saba.

.

Amewataja wahubiri katika Kongamano hilo kuwa ni pamoja na Padri MAXWELL kutoka nchini Ghana, Padri CAMILLIUS kutoka Botswana na Mwinjilishaji ni PAUL LORD’SWILL kutoka Nigeria, na wengine kutoka hapa Tanzania.

 

BANZI amesema wanaendesha Warsha mbalimbali za Uponyaji, kufunguliwa toka mila potofu na kujazwa Roho Mtakatifu zinazofanyika kila siku kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana.

 

Amebainisha kuwa Mahubiri yanafanyika kila siku kuanzia saa 8:00 adhuhuri hadi saa 12:00 jioni ikiwemo nyimbo za kusifu na kuabudu zinazoongozwa na Kwaya ya Ebeneza.

 

Kauli mbiu ya Kongamano la Roho Mtakatifu Mwaka huu ni “ YESU akasimama, akapaza sauti yake akisema, mtu akiona Kiu na aje kwangu anywe” YOH. 7:37.

***

 

Gaudence Hyera

 

Read more...

VIJANA KUSHIRIKI KONGAMANO DODOMA AGOST 11-17/2015

  • Last modified on Wednesday, 22 July 2015 11:29

 

Huduma ya Vijana Karismatiki Katoliki Tanzania imeandaa Kongamano la Vijana linalotarajiwa kufanyika katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo, Dodoma kuanzia Agosti 11 hadi 17 Mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Kongamano hilo ELEUTER MANGE imeeleza kuwa kabla ya Kongamano kutakuwa na Semina ya viongozi wa vijana wa ngazi mbalimbali kuanzia Agosti 5 hadi 10.

 

Amebainisha kuwa Kongamano hilo linatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa vijana ukanda wa Afrika Mashariki na kutoka baadhi ya nchi nyingine barani Afrika.

MANGE amesema Wakufunzi katika Kongamano hilo watakuwa ni Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bunju Padri DOMINIC SOMOLA na Mlei  MICHAEL WABOMBA kutoka Uganda.

 

 

Amewataja wakufunzi wengine kuwa ni SAMWEL POKU kutoka Ghana na FABRICE BASOSILA kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC.

 

 

MANGE amewakumbusha washiriki wote wa Kongamano hilo kuchukua vifaa muhimu vikiwemo Biblia, Madaftari, Kalamu, Shuka za kujifunika, nguo za michezo, nguo za kuogelea na nguo za baridi.

 

Gaudence Hyera.

 

 

 

Read more...

Sherehe ya UMTUME na TUMAINI MEDIA AGOSTI 2,2015

Sherehe ya Umoja wa Marafiki wa Tumaini Media-UMTUME, inatarajiwa kufanyika Dominika ya Agosti 2 Mwaka huu, kwenye Ukumbi wa Kardinali RUGAMBWA ulioko katika Parokia ya Mtakatifu PETRO, Oyterbay.

 

 

 

Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza anzilishi la umoja huo  Rafiki PETER SAKIA MACHA, Mgeni rasmi katika adhimisho hilo anatarajiwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam Mhashamu TITUS MDOE.

 

 

Rafiki MACHA amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kuanza mnamo saa 7:00 mchana siku hiyo ambapo Misa Takatifu itaongozwa na Askofu MDOE kuanzia saa 8:00 adhuhuri.

 

 

 

 

Amewahamasisha Marafiki kutoka Parokia zote za Jimbo hilo kujiandaa kwa michango mbalimbali ili kuwezesha adhimisho hilo pamoja na kununua mahitaji mbalimbali ya Kituo cha Tumaini kama ilivyo kawaida ya kila mwaka ya umoja huo.

 

 

 

 

Mwenyekiti huyo amewakumbusha wana-UMTUME wote kujitokeza mapema Parokiani hapo ili kumpokea Askofu MDOE ambaye  anatarajiwa kuwasili katika Viwanja vya Mtakatifu PETRO Saa 7:00 mchana.

 

 

Hivi sasa UMTUME wapo katika ziara za uhamasishaji kwa Waamini wanaopenda kujiunga na umoja huo na pia kutafuta michango kwa ajili ya kukitegemeza  Kituo cha Tumaini ambacho kinaundwa na Redio Tumaini, Televisheni Tumaini na Gazeti Tumaini Letu.

 

 

 

***

 

Gaudence Hyera

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Read more...
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.