Menu
RSS

Askofu Mdoe;Mchungaji mwenye karama kuinua miito ya Vijana

Askofu Mdoe;Mchungaji mwenye  karama kuinua miito  ya Vijana

Na Alex Kachelewa

UKUAJI wa Utume ndani ya Kanisa Katoliki Tanzania na duniani kwa ujumla bado unaendelea licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali, kwani kanisa hilo linahitaji watendakazi wengi zaidi kwa ajili ya kuwachunga kondoa wa Bwana wasipotee.

Kutokana na hilo Kanisa Katoliki limekuwa likiendelea na shuguhli zake za utume, kwa kuwawezesha wanaamii wake kuimarika kiimani, kiroho na kimwili, kupitia utoaji wa huduma zake mbalimbali za kimwili na kiroho.

Huduma hizo ni pamoja na Afya, Elimu hasa ya Msingi, Sekondari  na Seminari pamoja na vyuo Vikuuu kwa ajili ya kuwaandaa watu katika maadili mema lakini pia kupata watendakazi kwenye shamba la bwana.

Hilo linakwenda sanjari na kukuza miito kupitia Wakurugenzi wa Miito kwenye Majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini.

Miongoni mwa Watendakazi hao aliyeshiriki vema katika suala zima la ukuzaji wa miito hiyo na aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Titus Mdoe, ambaye kwa sasa ni Askofu wa Jimbo la Mtwara.

Hakika uteuzi wake uliofanywa na Baba Mtakatifu Fransiko wa kumteua Askofu Mdoe kuwa Askofu wa Mtwara, umeongeza chachu ya ukuzaji na uendelezaji wa imani katoliki nchini.

Itakumbukwa kwamba Askofu Mdoe, anayekwenda kufanya utume jimbo Mtwara wakati huo akiwa Padri, na akiwa Mkurugenzi wa Miito kwenye Jimbo Katoliki la Tanga alifanya kazi nzuri ya kutengeneza vijana wengi kuingia kwenye miito ya Upadri.

Lakini pia akiwa jimboni Dar es Salaam, kazi yake imeonekana miongoni mwa waamini.

Je, Akiwa Mkurugenzi wa Miito na Vijana kwenye Jimbo Katoliki la Tanga, Askofu Mdoe alifanya nini katika kuwaandaa vijana kwenye miito hiyo?

Askofu Mdoe enzi hiyo, aliweza kufanya mengi, kwani hali ya miito kwenye jimbo la Tanga ilikuwa chini lakini askofu huyo alijitahidi kuwaandaa vema vijana katika miito.

Kama inavyofahamika Askofu Mdoe alifanya kazi kubwa ya kuwahamasisha vijana kuingia kwenye miito mitakatifu ya Upadri kwa sababu alikuwa akijishusha na kushirikiana nao kwa ukaribu zaidi na hivyo wengi wakavutika huko.

Moja ya mambo yaliyowavuta zaidi vijana na kuingia kwenye wito wa upadri katika kipindi cha miaka 1988 wakati huo Askofu Mdoe akiwa Mkurugenzi wa miito ni hatua ya askofu huyo kuwa karibu na kushirikiana vema na vijana huku akiwashauri mambo mbalimbali ikiwemo maendeleo na suala zima la miito ndiyo maana wakati huo miito ilikuwa mingi.

Lakini pia askofu huyo alikuwa mtu wa michezo hivyo jambo hilo limeweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuwavuta vijana wengi kwani muda mwingi alikuwa nao na hivyo vijana wakavutika.

Tukiangalia Jimbo tanga ambako Askofu Mdoe ndiko alikotokea, historia ya Ukristo jimbo humo, ni ndefu ambapo, mwaka 1893, Ukristo uliingia kwenye Jimbo la Tanga eneo la Chumbageni na wakati huo ilikuwa ikiitwa Vikarieti ya Kilimanjaro.

Mwaka 1958, Jimbo la Tanga lilianza rasmi chini ya uongozi wake Askofu Eugen  wa Shirika la Mapendo aliyefanya utume jimboni humo.

Ilipofika mwaka 1969 Afya ya Askofu Eugen ilianza kuwa mbaya zaidi  jambo lililosababisha ajiuzulu wadhifa huo na kupisha wengine waendeleze utume huo.

Kufuatia kujiuzulu kwake mwaka 1970, Kanisa lilimpeleka Askofu Maurus Komba kutoka Jimbo Kuu la Songea kuliongoza Jimbo la Tanga, lakini ilipofika mwaka 1987 naye alijiuzulu kwa sababu ya kiafya pia.

Kanisa halina mwisho na halikati tamaa katika uinjiishaji. Kufuatia kujiuzulu kwa Askofu Komba, mwaka 1988 Askofu Telesphory Mkode ambaye kwa sasa ni Askofu wa Jimbo la Morogoro, alipelekwa jimboni Tanga kufanya utume ambako alifanya kazi ya uinjilishaji kwa kipindi cha miaka mitano.

Lakini kutokana na aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Morogoro kwa wakati huo, Mhashamu Andrea Mkoba kukabiliwa na hali mbaya ya kiafya, Askofu Mkude alipelekwa Morogoro kufanya utume ambako anaendelea hadi leo.

Baada ya hatua hiyo, mwaka 1994, Jimbo la Tanga akaletwa Askofu Anthony Banzi kutoka Morogoro pia ili aendeleze utume kwenye jimbo hilo ambapo anafanya kazi ya utume hadi anapatikana Askofu Titus Joseph Mdoe.

Askofu Mdoe, alifanya utume wake Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam kama Askofu Msaidizi, hadi anateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Mtwara.

HALI YA UKRISTO JIMBO TANGA

Inaelezwa kwamba hali ya Ukristo kwenye Jimbo la Tanga tangu mwaka 1975 ni nzuri kwa kiasi kwani tangu kipindi hicho hadi sasa kuna Seminari moja tu ya Soni.

Jambo hilo linaashiria kwamba hali ya miito bado iko chini ambapo juhudi zaidi ikiwemo sala na maombi mbele za Mwenyezi Mungu zinahitajika ili kukuza miito ya utawa na upadri.

Seminari hiyo imeelezwa kufanikiwa kutoa Mapadri 50, wanaofanya kazi  katika shamba la bwana, Akiwemo Askofu Mdoe.

Aidha Mashirika ya Kitawa yanayofanya kazi ya uinjilishaji jimboni humo ni 15, ikiwemo Shirika la Wabenediktini na Shirika la Masista wa Usambara.

Kwa sasa Askofu Mdoe anakwenda kufanya utume wake Jimboni Mtwara, ambako waamini wanatakiwa kumpa ushirikiano ili yale yaliyoachwa na Mtangulizi wake, Askofu Gabril Mmole, anayestaafuy kutokana na sababu ya kiafa yaweze kuendelezwa.

UTEUZI

Askofu Mdoe alitangazwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam na Baba Mtakatifu Mstaafu, Benedikto XVI Februari 16, 2013 kupitia Mwakilishi wa Baba Mtakatifu nchini, ikiwa ni siku tatu tu Baba Mtakatifu huyo alipotangaza kujiuzulu kwa sabau za kiafya.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, alitangaza kustaafu Februari 13, mwaka huu, 2013, na kustaafu rasmi Februari 28,  mwaka 2013.

Askofu Mdoe aliteuliwa akiendelea na utume katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), tawi la Mtwara akiwa Mkurugenzi wa Utawala na Fedha.

Lakini mwaka 2015 Baba Mtakatifu Fransisko, alimteua kuwa Askofu wa Jimbo la Mtwara, ambapo amesimikwa kuwa Askofu wa jimbo hilo, Januari 17, mwaka 2016.

 

 

HISTORIA YAKE

Askofu Mdoe alizaliwa Machi 19, mwaka 1961 eneo la Ngulu, Parokia ya Gare wilayani Lushoto, Jimbo Katoliki la Tanga na alipata  elimu ya msingi katika Shule ya Kongei kati ya mwaka 1968 na 1974.

Mwaka 1975 hadi1978 alipata elimu ya Sekondari katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Petro  Jimbo Katoliki la Morogoro kati ya mwaka 1975 na 1978.

Mwaka 1979 hadi mwaka 1981 alipata elimu ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Kibosho  Jimbo Katoliki la Moshi.

Baadaye Askofu Mdoe alipata elimu ya Teolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, Segerea Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam kati ya mwaka 1981 na 1986 na kupewa Daraja Takatifu la Upadri, Juni 24, mwaka 1986.

Baada ya kupewa daraja hilo la Upadri alitoa  huduma za kiroho katika Parokia mbalimbali Jimbo Katoliki la Tanga ikiwemo Parokia ya Gare aliyoitumikia akiwa kama Paroko msaidizi kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka 1987.

Mwaka 1987 hadi 1989 alikuwa pia Paroko msaidizi katikaParokia ya Kilole hadi alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Miito na Vijana wa Jimbo  Katoliki la Tanga mwaka 1989 hadi mwaka 1992.

Mwaka 1992 hadi 1994 alifanya kazi za kichungaji katika Parokia ya Mtakatifu Theresia akiwa kama  Paroko Msaidizi na Mkurugenzi wa miito na vijana ambapo mwaka 1995 hadi 2000 alikuwa Paroko wa Parokia ya Hale.

Mwaka 2008 hadi 2009 aliondoka parokiani hapo kwenda masomoni nchini Marekani kuchukua masomo ya Elimu ya Juu.

Aliporejea Tanzania aliteuliwa kuwa mwalimu wa Seminari ndogo ya Soni Jimbo Katoliki la Tanga alikofanya kazi ya kufundisha na pia Mkuregenzi wa miito na vijana kazi aliyoifanya kuanzia mwaka 2009 hadi 2010.

             Mwisho.

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.