Menu
RSS

Utapiamlo unavyonyemelea Mataifa Afrika, Asia

Utapiamlo unavyonyemelea Mataifa Afrika, Asia

Na Celina Joseph Matuja

Ulaji duni katika nchi zinazoendelea ni changamoto kubwa katika uboreshaji afya ya jamii na kusababisha utapiamlo, ambao ni hali mbaya ya lishe inaweza kuwa pungufu au iliyozidi.

Nchini Tanzania tatizo la lishe bora ni moja ya changamoto zinazoikabili jamii, hii ni kutokana na jamii kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu lishe, na hali duni ya maisha.

Hizo ni baadhi ya sababu za utapiamlo ili kuzuia utapia mlo ni muhimu kufahamu sababu hizo ambazo ni pamoja na ulaji duni wa chakula unaotokana na kula milo michache na kiasi kisichotosheleza mahitaji ya virutubishi mwilini, ikiwa ni pamoja na kutokuwanyonyesha watoto ipashavyo.

Magonjwa ya mara kwa mara huondoa hamu ya kula, husababisha ufyonzwaji duni wa virutubishi na huongeza mahitaji ya virutubishi mwilini.

Magonjwa hayo ni pamoja na kuharisha, malaria na magojwa ya mfumo wa hewa.

Utapiamlo huathiri afya kwa ujumla, uzalishaji mali na maendeleo katika jamii, nyingine ni kupungua kwa uwezo wa akili kwa watoto na kumfanya mtoto kuchelewa kuanza shule, kurudia rudia darasa sababu hana uwezo wa kufikiri haraka na kudaka mambo.  

Zaidi ya asilimia 40% ya viwango vya utapiamlo katika maeneo ambayo watoto walio chini ya miaka mitano nchini wanakabiliwa na hali ya utapiamlo, hasa katika mikoa ya Dodoma, Kagera, Njombe, Iringa, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Katavi na Geita takwimu hizo ni kwa  mujibu wa Taasisi ya chakula na lishe nchini Tanzania.

Kwa Mama anayenyonyesha ni muhimu kumnyosha mtoto ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa, anyonyeshwe kila wakati usiku na mchana, na aendelee kunyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila hata maji katika miezi sita ya mwanzo.

Imekuwa ni mazoea kusikia maziwa ya mama ni muhimu kwa mtoto mchanga hadi miezi sita, na kufanya wamama wengi kupuuza kauli hiyo ambayo inaelimu ndani yake ili kumkinga mtoto na hali ya utapiamlo.

Mazoea mengine miongoni mwa jamii yanatakiwa kuyaachwa mfano kumpa mtoto maji akingali mchanga ili hali wataalamu wa afya wanashauri kumnyonyesha mtoto maziwa pekee kwa kuwa maziwa hayo yanavirutubisho vyote ikiwa pamoja na asilimia kubwa ya maji ndani ya maziwa ya mama.

Tena yana maji yanayoweza kutosheleza kukata kiu ya mtoto wake kwa miezi sita ya mwanzo.

Katika kupambana na hali ya utapiamlo miongoni mwa jamii wapo wamama wengine  ni wafanyakazi maofisini wakati huo wananyonyesha ni vema na busara pia mwajiri kutekeleza sheria na miongozo inayolinda haki za wanawake wanaonyonyesha.

Mama anayenyonyesha anastahili kupewa siku themanini na nne (84) za likizo ya uzazi pamoja na likizo yake ya mwaka. Aidha mwenza wa mama aliyejifungua anastahili kupewa siku tatu (3) za likizo ya uzazi hii ni kwa mujibu wa Taasisi ya chakula na lishe  Tanzania.

Kazi inatafsiriwa kwa upana ikijumisha kazi ya kuajiriwa, kujiajiri ,kazi za muda mfupi au mikataba na kazi zisizo za kulipwa kwa mfano kazi zilizo katika mazingira ya nyumbani  zikiwemo kazi za shamba, mifugo na kutunza familia.

Tunapoelekea kumaliza mwaka tukiwa pia katika uongozi mpya wa awamu ya tano hatuna budi kulitupia macho suala hili la utapiamlo ambalo kwa kiasi Fulani huwezi kuona iwapo hujishughulishi na mambo ya lishe.

Taasisi ya chakula na lishe Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine wa masuala ya lishe wamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu na matamko mbalimbali ili kuwafikia wanajamii popote Tanzania, na kwamba kwa pamoja kutokomeza utapiamlo inawezekana.

Tangu mwaka 2000 wataalamu wa mambo ya lishe walipitia upya na kuridhia kanuni namba 183 ya shirika la Kazi Duniani( ILO) na mapendekezo namba 191 juu ya ulinzi wa haki za uzazi ya mwaka huo wa 2000.

Hatua hiyo imesaidia kuboresha stahili za wanawake wakati wa uzazi na mipango yenye lengo la kutetea sheria, lakini taasisi ya chakula na lishe Tanzania hivi karibuni ilidokeza kuwa juhudi katika kuboresha utoaji wa msaada kwa upande wa wanawake mahali pa kazi katika sekta zisizo rasmi, majumbani na mashambani hazirizishi, na mifumo ya jamii haijaimarishwa ipasavyo kusaidia wanawake waweze kunyonyesha watoto wao.

Tunapoelekea kufunga mwaka, yapo mambo mengi ya kuzingatia na kuyaendeleza, ili kuiokoa jamii yetu na janga la utapiamlo, la kwanza linaweza kuwa ni kutambua kulinda na kuthamini kazi za nyumbani ambazo sio ajira rasmi zinazofanywa na wanawake wanaonyonyesha.

Serikali kutenga bajeti ya kutosha katika kutoa elimu ya lishe, kwa wananchi hasa waliomijini na vijijini, pia katika kilimo ili kuinua kilimo cha mtu wa hali ya kawaida ili aweze kuzalisha mazao yanayoweza kupatikana katika eneo lake.

Pia kuboresha elimu ya ufugaji, na kilimo cha matunda na mboga mboga kwa kufanya hivyo Tanzania ambayo iko katika hatu yakuridhisha kwa sasa katika kiwango cha utapiamlo itakuwa imepiga hatua.

Mwaka 2015 kwa mujibu wa Taasisi ya chakula na lishe Tanzania umekuwa mwaka wa kupima utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia na kuanza utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu (Sustainable Development Goals).

Malengo hayo yanajumuisha kiashiria cha unyonyeshaji watoto maziwa ya mama pekee” ili kuhakikisha kuwa suala la unyonyeshaji linapewa nafasi katika mpango wa maendeleo katika sekta ya afya na lishe nchini. 

Shirika la Kimataifa la utetezi wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama tangu mwaka 1993 limetoa ufafanuzi wa kazi za mwanamke kwa upana wake kuanzia ajira yenye malipo, kujiajiri mwenyewe, kazi za msimu na za mkataba hadi kazi zisizo na malipo za nyumbani na kuhudumia familia.

Taasisi ya chakula na lishe nchini inasema suala la utetezi wa mwanamke na majukumu ya nyumbani ni changamoto kubwa, kwa kuwa mwanamke hufanya kazi nyingi lakini mara nyingine anakabiliwa na ubaguzi wa kijinsia, kupigwa na unyanyaswa.

Kwa upande mwingine Taasisi hiyo inamwangalia mwanake kuwa ndio mtu muhimu wa kuelimishwa na kuwezeshwa kwa majukumu mbalimbali yakiwemo ya elimu juu ya lishe kwani mwanamama akiwa na elimu atasaidia ulaji bora wa familia na kuepukana na tatizo la utapia mlo ambalo ni janga linaloweza kuzidi iwapo mama hatakuwa na elimu ya kutosha.

Hata hivyo kwa wale wasio katika mfumo rasmi na walio nyumbani, wanahitaji kufahamu haki zao za afya ya uzazi, chakula na usalama, haki ambazo zimeainishwa katika mikataba mingi ya Kimataifa na Kitaifa.

Mpango wowote unatakiwa kuoanisha ajira na kazi zisizo na malipo na uzazi, ni lazima  umwezeshe ili asiwe mtu wa kutegemea misaada, bali awezeshwe na kusaidiwa.

Jamii inatakiwa kuzingatia na kusikiliza mahitaji wa mwanamke na kuheshimu mawazo yao katika uzalishaji, malezi ya watoto na kuwasaidia bila chuki, upendeleo au maslahi ya kibiashara.

Mtoto ni malezi.

End 

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.