Menu
RSS
habari za hapa na pale

Kard. Pengo ataka waamini kuchangia ujenzi nyumba ya Askofu Bagamoyo

Na Editha Mayemba

ASKOFUMkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewaomba waamini wa jimbo hilo na wote wenye mapenzi mema kujitoa kuchangia ujenzi wa nyumba ya Askofu wa Jimbo jipya la Bagamoyo.

Alitoa ombi hilo katika salamu zake za shukrani kwa Mungu kwa kutimiza miaka 45 ya Upadri ambapo Mapadri wa Parokia mbalimbali za jimbo hilo wamempatia shilingi milioni 25 kwa ajili ya kumpongeza.

Kardinali Pengo alitoa kiasi hicho cha fedha alizozawadiwa Juni 20, mwaka huu pamoja na kiasi kama hicho kilichotolewa na watu mbalimbali na kufikia shilingi milioni 50 ili kuendeleza ujenzi wa nyumba hiyo.

Aliwashukuru wote waliochangia ujenzi wa nyumba hiyo na kuwaomba waamini wote bila kujali majimbo yao kutoa michango zaidi ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kwamba yeyote atakayechangia fedha hiyo itatumika kama ilivyokusudiwa.

“Tunao Mradi wa ujenzi wa nyumba ya Askofu, Bagamoyo, ningekuwa kijana kiasi cha fedha nilichopewa na Maparoko ningeweza kununua pikipiki au baiskeli, lakini fedha zote ni nilizozipokea nitazipeleka kwenye ujenzi”

“Juni 19 Padri Valentino Bayo aliniita kwa shughuli ya uzinduzi wa Jiwe la Msingi la ujenzi huo. Tumeshatumia zaidi ya mililioni  500 katika awamu ya kwanza:

Jimbo Kuu la Dar es Salaam liliahidi kutoa sh. Mil 250 na nilikuwa bado sijapeleka hivyo nikijumuisha kiasi nilichokipokea nitawasilisha zote kwa pamoja na kila aliyechangia awe na hakina fedha zote zitatumika kama zilivyokusudiwa.”

Kardinali Pengo alimshukuru Mungu kwa zawadi kubwa ya miaka 45 ya Upadri kwani yeye ni miongoni mwa Mapadri saba walio baki hai kati ya Mapadri 25 waliopewa Daraja ya Upadri pamoja Juni 20, 1971.

“Kwamba nimetimiza miaka 45, siamini mimi mwenyewe naona ni kama tukio lilotokea juzi au jana, lakini nikichunguza wale tulioanza pamoja, tumebaki wachache sana:

Kati ya mapadri 27 tuliopata upadrisho mwaka ule (1971) kwa Tanzania nzima, tulio hai hatuzidi hata saba, wengine wametangulia mbele ya Mungu”, alisema na kuongeza:

“Hii inanipa nguvu kubwa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa Baraka hiyo kubwa. Mwenyezi Mungu anapotoa baraka zake, anatoa na wajibu, najiuliza neema hii aliyonipa Mungu ya miaka 45 ya Upadri je niliyotenda yanalingana na uwingi wa miaka hiyo? Basi namuomba Mungu yale niliyopungukiwa anisamehe pamoja na wenzangu tulioanza pamoja mwaka ule”.

Alisema anaendelea kumuomba Mungu kiasi kilichobakia cha maisha yake hapa duniani aendelee kujitoa bila kujibakiza licha ya kuwa na umri wa zaidi ya miaka 70.

Kardinali Pengo alitumia nafasi hiyo kuwashukuru waamini wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwani katika miaka hiyo yote ametumikia kwa kiwango kikubwa Jimbo hilo tangu akiwa Padri Seminari ya Segerea na hata alipoteuliwa kuwa Askofu.

Aliwahimiza Mapadri kutokata tamaa kwa magumu wanayokutana nayo katika Utume wao na daima wamwombe Mungu neema ya kufurahia Upadri wao kwa kumwadhimisha Mungu daima.

Kardinali Pengo aliwashauri Mapadri kusali Sala ambayo yeye mwenyewe amekuwa akiitumia kwa kuwa sala hiyo itawasaidia kuomba neema ya kuendelea kufanya kazi hiyo katika hali yoyote.

“Katika miaka hiyo 45 hata siku moja sijawahi kujua kwa nini nilikuwa Padri, imekuwa ni chimbuko la furaja japo kuna magumu kadhaa unaweza kupanga kazi lakini haziendi kama ulivyopanga basi nachukulia ni mambo ya kibinadamu”.

“Napenda kuwaambia mapadri wenzangu kwamba, kamwe tusivunjike moyo, tusijutue kwamba kwa nini tuliamua kuwa mapadri, kila siku tuombe neema ya kufurahi upadri wetu hata katika mambo ya kufurahisha na yale magumu yanayoweza kutukatisha tamaa.

“Mimi daima ninayo sala kwa Kristo mwenyewe Kuhani Mkuu, Yesu ‘Ee Yesu mwema unifanyizie niwe Kuhani kulingana na Mapenzi ya moyo wako’ Sala hiyo Padri akiisali kadri iwezekanavyo kwa kila siku, nina hakika nguvu kutoka kwa Kristo zitamsimika kuweza kuendelea hata katika hali inapokuwa ngumu.

Kituo cha Tumaini Media kinamtakia Mwadhama Polycarp  Kardinali Pengo, heri na baraka za Mungu katika kumbukumbu yake ya Upadri, maisha marefu na afya njema alipoadhimisha mapema mwezi wa saba mwaka huu.

end 

Read more...

Wanandoa wanalitia majeraha Kanisa-Askofu Nayisonga

Na Frida Manga

Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda Mhashamu Gervas Nyaisonga amesema Kanisa linapata majeraha na vidonda kutokana na wanandoa kutengana, kushindwa kulea familia na kukosa upendo miongoni mwao.

Kwa mujibu wa Askofu Nyaisonga, wanandoa na waamini wanapokosa upendo na kuwa na migogoro miongoni mwao Kanisa la Mungu nalo linapata majeraha na kudhoofika.

Askofu Nyaisonga aliyasema hayo wakati akitoa homilia yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu ya Somo wa Parokia ya Mtakatifu Antoni wa Padua, Mbagala Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, iliyokwenda sanjari na utoaji wa sakramenti ya Ndoa Takatifu kwa ndoa Jozi 26.

Aliwataka wanandoa hao kuishi maisha ya upendo, kuvumiliana na sala kila wakati na kwamba hiyo ndiyo silaa pekee ya maisha ya ndoa kwani hakuna njia nyingine ya kuponya ndoa hizo zinapokumbwa na changamoto.

Alieleza kuwa tendo la kufunga ndoa si jambo ndogo na la mzaha, bali ni utayari wa kimwili na kiroho kwa watu wawili kukubali kuishi pamoja katika uhai wa maisha yao yote watakayojaliwa na Mwenyezi Mungu.

“Ndoa ni Uhai wa muunganiko wa watu wa wawili ya Mke na Mume, utengano hauna uhai, lakini pia ni dhambi panapotokea utengano katika kile kilichounganishwa na Mungu”,alisema Askofu Nyaisonga.

Kwa mujibu wa Askofu huyo, hata Maandiko Matakatifu yanasema kupitia Mtume Paulo anasema kiungo kikubwa katika kinacholeta uhai ni upendo hivyo amewataka wanandoa  hao kuwa na  upendo wa dhati.

Alibainisha kuwa ikiwa kila mwanandoa na familia ya Mungu kwa ujumla ikatenda matendo mema ya dhati ataliimarisha Kanisa la Mungu na ndoa zitapata kupona.

Askofu Nayisonga alisema Kanisa linawategemea wanandoa hao katika kupeperusha Bendera ya Kristo katika Fumbo la Upendo, Uvumilivu na uchaji wa Mungu.

Aliwakumbusha wajibu wao wa kusaidia kutibu majeraha ya vidonda vya kristo katika Kanisa la Mungu kwa kushinda vishawishi, na kuzishinda changamoto zinazojitokeza ndani ya ndoa zao.

Hata hivyo Askofu Nyaisonga amewataka wanandoa hao kufahamu kuwa changamoto zipo na kwamba ushujaa ni kuzipokea na kuzikubali na kwamba upendo utawapa majibu ya changamoto zinazozitokeza mbele yao.

Aliwataka wanandoa hao kutobabaishwa na kuyumbishwa na changamoto hizo bali kumtumaini Kristo na kubeba silaha ya upendo kama ngao ya kupambana na changamoto hizo.

Kwa upande Paroko wa Parokia hiyo, Padri Jemms Mwapongo alisema changamoto inayowakabili ya waamini kuishi maisha ya mke na mume bila Sakramenti Takatifu ya ndoa, wameikubali na kwamba wanaweka mikakati ya kusaidia waamini kuondokana na hali hiyo.

Padri Mwapongo mbali na kueleza hilo, amewataka wazazi na walezi kujitambua na kutambua wajibu waliopewa na Mungu katika kulea na kuwatunza watoto waliopewa na Mungu.

Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Francis Gwankisaalisema changamoto kubwa inayowakabili ni kuwa na idadi kubwa ya waamini wanaoishi maisha ya mke na mume bila Sakramenti Takatifu ya Ndoa.

Parokia hiyo inawastani wa waamini elfu tisa na zaidi, ina Vigango Viwili, ambavyo ni Chamazi na Majimatitu, Jumuiya 116 Kanda 43 inamiradi miwili ya kiuchumi, Shule ya Awali na ukumbi ambao hata hivyo haujakamilika lakini wameaza kuona matunda yake.

Gwankisa ametaja changamoto nyingine inayowakabili ni uhaba wa Makatekista, na kwamba katika kukabiliana na hilo tayari wameweka mpango wa kuwapeleka masomoni Vijana wakapate mafunzo ya Ukateksita.

 

Mwisho.

 

Read more...

kongamano la huruma Mungu linaendelea -Emaus ubungo hadi Mei 8,2016

DAR ES SALAAM

Kongamano kubwa la Huruma ya Mungu Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam limeanza linaendelea katika Kituo cha Emaus, Ubungo na linatarajiwa kufikia kilele Dominika ya Mei 8 Mwaka huu.

Akizungumza na Redio Tumaini Katibu wa Karismatiki Katoliki Jimboni humo amesema Kongamano hilo limefunguliwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo Mhashamu EUSEBIUS NZIGILWA.

BANZI amebainisha kuwa Kongamano hilo linasimamiwa na Idara ya Utume wa Walei Jimboni humo chini ya uratibu wa Mkurugezi wake Padri VITALIS KASEMBO.

Amesema Ratiba ya Kongamano hilo itaanza saa nane adhuhuri kila siku ikiwemo siku za Dominika ambapo muda wa asubuhi utatumika kwa ajili ya ushauri, Baraka na maombezi binafsi.

Amewataja Watoa Mada katika Kongamano hilo kuwa ni pamoja na Askofu EUSEBIUS NZIGILWA, Mapadri na baadhi ya Waamini Walei kutoka Jimboni humo na nje ya nchi.

BANZI ambaye ni Mjumbe wa kamati ya maandalizi ya Kongamano hilo amewataka Waamini kutoka Parokia zote Jimboni humo kuzingatia Mwaliko uliotolewa wa kushiriki Kongamano hilo.

Amesisitiza kuwa ni nafasi muhimu kwa kila mmoja kuonja Huruma ya Mungu isiyo na mipaka kupitia kwenye Kongamano hilo ambako kutatolewa Maombi, Baraka na Rehema.

***

Gaudence Hyera

Read more...

KONGAMONO LA HURUMA YA MUNGU KUZINDULIWA APRILL 22 UBUNGO DSM.

DAR ES SALAAM

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam Mhashamu EUSEBIUS NZIGILWA, anatarajiwa kufungua Kongamano kubwa la Huruma ya Mungu Ijumaa Aprili 22 Mwaka huu.

Akizungumza na Redio Tumaini Katibu wa Karismatiki Katoliki Jimboni humo amesema Kongamano hilo litafanyika katika Kituo cha Emaus, Ubungo na linatarajiwa kufikia kilele Mei 8 Mwaka huu.

BANZI amebainisha kuwa Kongamano hilo limeandaliwa na uongozi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam na linasimamiwa na Mkurugezi wa Utume wa Walei Jimboni humo Padri VITALIS KASEMBO.

Amewataja Watakaotoa Mafundisho kuhusu Huruma ya Mungu kuwa ni pamoja na Askofu NZIGILWA, baadhi ya Mapadri na baadhi ya Waamini Walei kutoka Jimboni humo na nje ya nchi.

Amesema Ratiba ya Kongamano hilo itaanza saa nane adhuhuri kila siku ikiwemo siku za Dominika ambapo muda wa asubuhi utatumika kwa ajili ya ushauri, Baraka na maombezi binafsi.

BANZI ambaye ni miongoni mwa wajumbe wa kamati ya maandalizi ya Kongamano hilo la kipekee kwa mwaka huu amewataka Waamini wote Jimboni humo kuzingatia Mwaliko huo wa kushiriki Kongamano hilo.

Amesisitiza kuwa ni nafasi muhimu kwa kila mmoja kuonja Huruma ya Mungu kupitia kwenye Kongamano hilo ambako kutatolewa Baraka mbalimbali, Sala na Rehema.

 

***

Gaudence Hyera

Read more...

WADAU WA MUZIKI MTAKATIFU TOENI ELIMU YA KATEKESI KWA WALIMU WA MUZIKI

DAR ES SALAAM

Askofu wa Jimbo Katoliki la Ifakara Mhashamu SALUTARIS LIBENA amesema Watunzi na Walimu wa Muziki Mtakatifu wa Kanisa wanapaswa kupewa Elimu ya Katekesi ya Kanisa Katoliki.

Amesema hayo katika Mkutano wa mwaka wa Kamati ya Taifa ya Muziki Mtakatifu wa Kanisa uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania-TEC.

Askofu LIBENA ambaye ni Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia ya TEC, amesema Katekesi hiyo itawawezesha wahusika kutunga na kufundisha nyimbo kwa kufuata taratibu za utunzi zilizowekwa na Kanisa.

Ameongeza kuwa Elimu hiyo itawasaidia kutunga kuendana na mazingira na nyakati na umuhimu wa kutunga nyimbo kufuatana na maandiko matakatifu.

Askofu LIBENA amefafanua kuwa kukosekana kwa Elimu ya Teolojia kunawafanya watunzi wajikite katika vionjo zaidi ili kuchangamsha waamini badala ya kuzingatia Ibada na Uchaji.

Amebainisha kuwa na kipaji pekee hakitoshi kuwa sifa ya utunzi wa Muziki Mtakatifu bali Teolojia na Katekesi ni lazima itolewe ili nyimbo zao zifuate misingi ya Kanisa Katoliki.

Askofu LIBENA amewakumbusha na kuwahimiza wanamuziki wa Kanisa wawe na Roho ya Liturujia, kujifunza vizuri utamadunisho na kuelewa  miongozo ya Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani kuhusu Muziki wa Kanisa ili wawasaidie Waamini kusali vizuri.

 

***

Gaudence Hyera


 

Read more...

ILI KUKUZA AMANI NA UPENDO SALA INAHITAJIKA: BALOZI WA PAPA TANZANIA

KAHAMA

Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Askofu Mkuu FRANCESCO MONTECILLO PADILLA amewataka Waamini kuwa na Moyo wa Ibada na Sala na kukuza upendo na amani katika Kanisa na jamii.

Ametoa rai hiyo wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya kubariki na Kutabaruku Kanisa jipya la Parokia ya Ekaristi Takatifu, Kabuhima, Jimbo Katoliki la Kahama katika ziara yake mwishoni mwa juma lililopita.

Askofu Mkuu PADILLA amesema Kanisa ni mahali pa Sala hivyo kila mwamini anapaswa kuwa chumvi na mwanga wa Dunia ili kukuza mapendo kwa Mungu na kwa majirani katika maisha ya kila siku.

Amelitaka Kanisa liwasaidie waamini kupendana na kuwa karibu na Mungu kwa sala, kujenga mshikamano na amani na kuishi udugu kwa sifa na utukufu wa Mungu.

Balozi huyo wa Vatikani anayemaliza muda wake hapa nchini amemshukuru Askofu wa Jimbo la Kahama Mhashamu LUDOVICK MINDE kwa mwaliko wake na mapokezi makubwa Jimboni humo.

Askofu Mkuu PADILLA amempongeza Paroko wa Parokia ya Kabuhima Padri SALVATORE GUERRERA ambaye ni Mmisionari kwa jitihada zake na ushirikiano baina yake na Waamini.

Ameitakia Parokia hiyo mshikamano endelevu wa Sala uliofanikisha ujenzi wa Kanisa jipya lenye uwezo wa kuchukua waamini 1500 na pia ameliombea Baraka Jimbo la Kahama liendelee kudumu katika Imani.

Askofu Mkuu PADILLA amatumia ziara hiyo kuwaaga waamini wa Jimbo la Kahama baada ya hivi karibuni kuteleuliwa na Baba Mtakatifu FRANSISKO kuwa balozi Mpya wa Kuwait na Kisiwa cha Kiarabu.

***

Gaudence Hyera

DAR ES SALAAM

Read more...

RAIS MAGUFULI,AMETUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA KIFO CHA ASKOFU MSTAAFU DODOMA.

DAR ES SALAAM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta JOHN POMBE MAGUFULI ametuma salamu za rambirambi kwa Kanisa Katoliki nchini kufuatia Kifo cha Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Mhashamu MATHIAS JOSEPH ISUJA.

Katika Salamu hizo alizozituma kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania-TEC Mhashamu TARCISIUS NGALALEKUMTWA, Rais MAGUFULI amesema amepokea kwa huzuni kubwa taarifa za kifo cha Askofu MATHIAS ISUJA.

Rais MAGUFULI amesema Askofu Mstaafu ISUJA alikuwa mzalendo wa kweli Askofu Mstaafu ISUJA ambaye kazi yake na huduma yake kwa jamii ya Watanzania ni vigumu kuipima.

Ameongeza kuwa Askofu ISUJA atakumbukwa kwa namna alivyokuwa alikuwa kipenzi cha watu, aliyejitolea kwa Moyo wake wote na aliyefanya kazi kubwa ya kuwajenga watu Kimwili na Kiroho.

Amebainisha kuwa Serikali yake na Watanzania kwa ujumla kamwe hawatasahau mchango mkubwa wa Askofu ISUJA katika mandeleo ya Elimu, Afya na malezi ya watoto.

Dakta MAGUFULI amemuomba Rais wa TEC Askofu TARCISIUS NGALALEKUMTWA kufikisha salamu zake kwa Baraza la Maaskofu, Waamini wa Kanisa Katoliki na wote walioguswa na Msiba huo.

Marehemu Askofu Mstaafu MATHIAS JOSEPH ISUJA alifariki Dunia juzi Alfajiri katika Hospitali ya Mtakatifu GASPAR iliyopo Manyoni Singida alikokuwa amelazwa kutokana na Maradhi ya Saratani ya Tumbo.

Askofu huyo aliyekuwa mzalendo wa kwanza kuliongoza Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, aliwekwa Wakfu kuliongoza Jimbo hilo Mwaka 1972 na kustaafu mwaka 2005, amefariki akiwa na umri wa miaka 87.


Wakati huo huo, Mapadri waliobahatika kufanya utume na Askofu ISUJA, wamesema alikuwa ni mfano kwa kuwa alikuwa mtu mwenye kutoa mawazo, ushauri mwenye kupenda masikilizano bila upendeleo wowote.

Paroko wa Parokia ya Kanisa Kuu Padri SEBASTIAN MWAJA amesema Askofu ISUJA atakumbukwa kwa mengi aliyofanya katika jimboni humo ikiwemo harakati za kuhamasisha vijana kujiunga na miito mitakatifu.

Padri MWAJA amesema Askofu ameyapokea mashirika mengi ya kitawa na kuyapa fursa za kufanya kazi za utume katika jimboni Dodoma kwa kipindi alichokuwepo madarakani.

Kuhusu elimu na huduma za jamii, amesema ilikuwa kazi ya mashirika mbalimbali ya kitawa na ilikuwa jitihada zake yeye mwenyewe kwani alikuwa ni msimamizi na mwelekezaji kuhusu shughuli mbalimbali zilizotakiwa kufanywa na mashirika hayo.

Padri MWAJA amesema, Askofu ISSUJA alikuwa ni tegemeo kubwa katika kanisa hususani katika ujenzi wa kanisa la mungu, kwani alikuwa akitafuta hata wafadhili kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbalimbali za Mungu.

Kwa Upande wake Paroko wa Parokia ya Mpwapwa, Padri DAVID NGIMBA Mpwapwa amesema amepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Askofu ISUJA kwani alikuwa mshauri na mlezi wake katika makuzi yake yote ya kikasisi na hata alipokuwa paroko wa kanisa kuu la Kiaskofu la jimbo kuu katoliki Dodoma.

Naye Paroko wa Parokia ya Kiwanja cha ndege Dodoma JOHN MAZENGO marehemu Askofu ISUJA mara nyingi alikuwa chachu ya maendeleo ya kimwili na kiroho.

 

 

***

 

 

Ashura Kishimba, Gaudence Hyera


 

Read more...

TAFRANI MV. MAGOGONI KIGAMBONI TANZANIA

DARA ES SALAAM

 

Wananchi wa Wilaya ya Kigamboni na maeneo mengine jijini Dar es Salaam leo wamekumbwa na taharuki baada ya Kivuko cha MV Magogoni kupata hitilafu na kupoteza mwelekeo hali iliyosababisha kupumzishwa kwa takribani saa mbili na kuongeza tatizo la usafiri kati ya Kigamboni na Feri.

 

Wananchini wa Wilaya ya Kigamboni na maeneo mengine jijini dar es salaam leo wamekubwa na Taharuki baada ya Kivuko cha MV Magogoni kupata hitilafu na kupoteza mwelekeo hali iliyosababisha kupumzishwa kwa takribani saa mbili na kuongeza tatizo la usafiri kati ya Kigamboni na Feri.

 

Hali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa abiria na magari hasa kutokana na kulazimika Kivuko Kimoja kufanya kazi na kushindwa kumudu kupunguza msongamano huo.

 

Baadhi ya wananchi waliokwama wamekiambia kituo hiki kwamba hata kivuko hicho kikubwa kilipoanza kazi kilizidiwa kutokana na muda wa asubuhi kuwa na idadi kubwa ya watu na magari wanaovuka kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine kama inavyoonekana.

 

Hali hiyo imemlazimisha Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Dakta FAUSTINE NDUNGULILE kuitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kukifanyia ukarabati Kivuko cha MV Magogoni ili kisilete maafa kwa wananchi wanaokitumia hasa baada ya kuwa kibovu kwa muda mrefu.

 

Katika taarifa yake Dakta NDUNGULILE amesema amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi wa Kigamboni wanaodai kwamba kivuko hicho ni kibovu na huchukua muda wa zaidi ya nusu saa kuvuka kati ya Kigamboni na Feri ambapo asubuhi ya Alhamisi Februari 11 kilipoteza mwelekeo na kusababisha taharuki kubwa.

 

Aidha Dakta NDUNGULILE amesema wananchi hao wamedai kuwa injini za kivuko hicho zimekuwa zikizima mara kwa mara na kukifanya wakati mwingine kipoteze mwelekeo kikiwa majini kama ilivyotokea Februari 10 mwaka huu na ambapo kivuko hicho kilipoteza mwelekeo na kuelekea Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere

 

Amesema kutokana na malalamiko hayo yeye kama Mbunge ameamua kumwandikia Barua ya tatu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kumkumbusha barua ya awali yenye kumbukumbu no KIG/FER/VOL.ya Januari Mosi Mwaka huu inayoeleza kutoridhishwa na huduma za Kivuko cha Kigamboni na kuitaka wizara kuchukua hatua mara moja kwani tangu barua hiyo ilipowasilishwa hakuna jitihada zilizoonekana za kuondoa adha inayowakabili wananchi wa Kigamboni.

 

Mashuhuda wanadai kuwa vilio na kelele zilisikika pale maji yalipoanza kupanda ndani ya kivuko kutokana na kuzidiwa na idadi ya watu wakati kivuko hicho kikubwa kilipoanza tena kufanya kazi hali iliyowafanya abiria waanze kujitosa ndani ya maji kwa wale wanaojua kuogelea.


***

Editha Mayemba

 

Read more...

Serikali imeombwa kusimamia sheria ili Jiji la Dar es Salaam liwe Safi

DAR ES SALAAM

 

Serikali imeombwa kusimamia sheria na kuwachukulia hatua watu wenye tabia za kujisaidia ovyo kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kandokando ya barabara ili kuweka mazingira katika hali nzuri.

 

Hayo yamesemwa na baadhi ya wananchi wakati wakizungumza na kituo hiki katika maeneo ya Buguruni na Tabata Matumbi kuhusu baadhi ya watu kujenga tabia za kujisaidia ovyo.

 

Wamesema kuwa kuwepo kwa tabia hiyo ya kujisaidia ovyo inachangia kwa kiasi kikubwa kuchaguzi wa mazingira na kusababisha kuwepo kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa kipindipindu.

 

 

 

 

Read more...
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.