Menu
RSS
Habari za dunia

Habari za dunia (46)

IJUE PAROKIA YA BIKIRA MARIA SALAMA YA WAGONJWA MUHIMBILI

Na Prince Burchad

JIMBO Kuu Katoliki la Dar es Salaam linaundwa na Parokia 85, zinazofanya kazi ya uinjilishaji kwenye jimbo hilo.

Miongoni mwa Parokia hizo ni pamoja na Parokia ya Muhimbili ambayo ilianzishwa kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wanaolazwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbii.

Parokia hiyo ilianzishwa mwaka 1980 ikiwa kama Kigango cha Parokia ya Upanga ambapo mwaka 2008 Kigango hiki kikapandishwa hadhi na kuwa Parokia ya Bikira Maria Salama ya Wagonjwa.

Parokia hii inapatika  katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Waumini wa Parokia hii wengi wao ni wanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Muhimbili, wafanyakazi wa Hospitali na familia zao pamoja na wagonjwa wanaofika hospitalini kwa ajili ya matibabu. 

Parokia ya Bikira Maria Salama ya wagonjwa, ina Jumuiya ambazo uhusika katika kutoa huduma za kikanisa kama ilivyo katika Parokia nyingine, Jumuiya hizi zinaundwa na wanafunzi, wafanyakazi wa hospitali pamoja na wagonjwa kama nilivyokwishataja hapo awali. 

Ziara ya Gazeti ili ilianza kwa kusali pamoja na Jumuiya ya Mtakatifu Kamili Jumuiya inayoundwa na wanafunzi wa Postgraduate, Shahada ya uzamili pamoja na uzamivu katika tasnia ya Udaktari katika Chuo Kikuu Cha  Muhimbili.

Akizungumza na Gazeti Tumaini Letu, Paroko wa Parokia hiyo Padri wa Shirika la Mtakatifu Kamili Fidelis Safari Mushi wakati wa ufafanuzi alianza kwa kusimulia kwa ufupi juu ya Shirika lao chimbuko pamoja na historia ya Somo wa Shirika hilo Mtakatifu Kamili.

Mara baada ya kazi pamoja na historia ya Shirika lake alisimulia kindakindaki juuu ya utendaji kazi wa Parokia hiyo tangu ilipoanzishwa huku akielezea mafanikio, changamoto, pamoja na mikakati ya maendeleo parokiani hapo.

Padri Mushi alisema Parokia  hiyo ina jumla ya Jumuiya saba, Jumuiya hizi zinaundwa na wanafunzi wa Astashahada, Stashahada, Shahada ya uzamili na uzamivu wanaosoma katika Chuo Kikuu Cha Muhimbili pamoja na Jumuiya ya wagonjwa wanafika hospialini hapo kwa ajili ya matibabu.

Aidha alisema kuwa, wanajipanga kuanzisha jumuiya ya vijana wanaotoka katka familia za wafanya kazi wa  hospitali hiyo pindi wanarudi toka masomoni pamoja na wale wanaoishi katika mazingira ya hospitali hiyo.

Pia alizitaja  za Mtakatifu secilia (MCT), Mtakatifu Agatha, Mtakatifu Cosmus na Damiani pamoja na jumuiya ya Mtakatifu Franssco wa Asizi, pia wanajumuiya ya wazazi ya Familia Takatifu.

Akizungumza kuhusu huduma za kiroho katika Parokia hiyo,Padri Mushi alisema wanajitahidi kila siku hasubuhi kuwa na ibada ya pamoja wakati huo huo wametenga siku mbili kila wiki za kusali pamoja na wagonjwa ikiwa ni pamoja na kutoa sakramenti mbalimbali zikiwemo ubatizo, kitubio na sakramenti ya upatanisho kwa wagonjwa  kutokana na maombi yanyofikshwana ofisini.

Pia Padri Mushi ameongeza kutokana na uchache wao mara nyingi wamekuwa wakishindwa kutoa huduma stahiki kama inavyotakiwa hii ni kutokana na uhaba wa mapadre Parokiani hapo.

Sanjari na hayo eneo la hospitali ni kubwa mno hivyo wanajitahidi kadri wawezavyo kuakikisha wanatoa huduma mahitaji ni mengi.

Wakati akiendelea kubainisha changamoto zinazowakabili alisema kuwa , tatizo la kuhamahama kwa wanafunzi , pamoja na wafanyakazi  ni changamoto kwa utume Parokiani hapo, pia alisema kuwa baadhi sakramenti zinahitaji kufahamu kwa undani historia ya mgonjwa kabla ya kutoa huduma husika.

Hivyo kabla hazijatolewa inatakiwa kutafuta taaarifa kutoka Parokiani kwa mgonjwa anapotokea, aidha kuna baadhi ya wagojwa wanahitaji misaada mbalimbali mfano nguo, dawa , vipimo vikubwa kama cityscan, MLI, X –ray, wagonjwa wenye matatizo haya mara nyingi hukimbiwa na ndugu pamoja na familia zao kushindwa kugharamikia matinbabu hayo.

Padri Fidelis alimalizia kwa kutoa salamu za Krismas huku akiwaataka wanafamila wapendane.   

 

Read more...

UJUMBE WA BABA MTAKATIFU (MSTAAFU) BENEDIKTO XVI KATIKA SIKU YA UPASHANAJI HABARI YA 47

Wapendwa Kaka na Dada, 

Kadiri Siku ya Upashanaji Habari 2013 inavyokaribia, ningependa kuwashirikisha tafakari kuhusu hali halisi inayozidi kuwa muhimu kuhusiana na namna watu wanavyowasiliana miongoni mwao siku hizi. Ningependa kutafakari maendeleo ya mitandao ya kijamii ya kidijitali yanayosaidia kutengeneza kile kinachoweza kuitwa “agora” mpya, yaani viwanja vya wazi vya umma ambako watu hukutana ili kubadilishana mawazo, taarifa na maoni, na ambako uhusiano na harakati mpya za jamii huweza kuanzishwa.

Nyenzo hizi za mtandaoni, zikitumika kwa hekima na uwiano mzuri, zinasaidia kulea miundo ya dialojia na mijadala ambayo, kama ikiendeshwa kwa namna yenye heshima na kwa kujali faragha, uwajibikaji na ukweli, inaweza kuimarisha mambo yanayoleta umoja kati ya mtu na mtu na kushajiisha kwa ufanisi mtengamao wa familia ya wanadamu. Kubadilishana taarifa kunaweza kuwa mawasiliano ya kweli, kufahamiana kukua kwa urafiki, na mitandao kujenga udugu. Endapo mitandao hii inaitwa kusaidia kuleta uwezekano huu muhimu, watu wanaojihusisha nayo hawana budi kufanya jitihada za kuwa wakweli hasa kwa kuwa, katika nyenzo za mitandaoni, sio tu mawazo na taarifa zinazosambazwa, bali nafsi zetu wenyewe.

Kuanzishwa kwa mitandao ya kijamii kunadai ahadi ya utayari: watu wanashughulika kujenga uhusiano na kuunda urafiki, kutafuta majibu kwa maswali yao na kuburudishwa, lakini pia katika kutafuta taarifa za kuilisha akili na kushirikishana maarifa na ujuzi. Mitandao hii inazidi kuwa sehemu ya namna jamii ilivyoundwa, hasa kwa vile inawaleta watu pamoja kwa msingi wa mahitaji haya muhimu. Mitandao ya kijamii, kwa hiyo, inalishwa na matamanio yaliyo na asili yake kwenye mioyo ya binadamu.

Utamaduni wa mitandao ya kijamii na mabadiliko katika namna na mitindo ya mawasiliano kunaleta changamoto zinazofikirisha kwa wale wanaotaka kuzungumza kuhusu kweli na tunu. Mara nyingi, kama ambavyo hutokea kila mara katika njia nyingine za mawasiliano ya umma, umuhimu na ufanisi wa njia mbalimbali za kujieleza zinaonekana kuamriwa na umaarufu wake kuliko umuhimu na thamani yake ya asili. Umaarufu, kwa upande wake, mara nyingi inaoanishwa na umashuhuri au kwa mikakati ya kushawishi kuliko mantiki ya ujengaji hoja. Mara nyingine sauti pole yenye kujenga hoja makini inaweza kumezwa na mmiminiko wa taarifa za ghafla na kushindwa kuvuta usikivu ambao badala yake unaelekezwa kwa wale ambao wanajieleza kwa mitindo inayoshawishi zaidi.

Kwa hiyo, vyombo vya habari vya kiraia, vinahitaji ahadi ya utayari wa wote wale wanaotambua thamani ya dialojia, mijadala yenye nguvu ya hoja, na mantiki zinazojengwa kwa hoja; watu wanaojibidisha kujenga mifumo ya majadiliano na njia za kujieleza ambazo zinavuta matamanio mema kabisa ya wale wanaojihusisha katika mchakato wa upashanaji habari. Dialojia na midahalo inaweza kuneemeka na kukua pale tunapowasiliana na kuwachukulia kwa uzito watu ambao fikra zao zinatofautiana na za kwetu. “Kwa kuzingatia uhalisia wa uanuwai wa kiutamaduni, wanachopaswa kufanya watu si tu kupokea uwepo wa utamaduni wa wengine, lakini pia kuamsha ari ya kutaka kuneemeshwa nao na kushirikisha chochote walicho nacho kilicho chema, cha kweli na kizuri” (Hotuba katika Mkutano wa Ulimwengu wa Utamaduni, Bélem, Lisbon, 12 Mei 2010).

Changamoto inayoikabili mitandao ya kijamii kwa maana ya internet, facebook, twiter na Yu Tube ni namna gani iwe ya ukweli yenye uwakilishi mpana: ili kwamba iweze kunufaika kutokana na ushiriki kamilifu wa waumini wanaotamani kushirikisha ujumbe wa Yesu na tunu za utu wa binadamu ambazo mafundisho yake yanalenga kueneza. Waumini wanazidi kutambua kwamba, hadi pale Habari Njema itakapoenezwa katika ulimwengu wa kidijitali pia, vinginevyo haitakuwemo katika yale wanayoyapitia watu ambao kwao nyenzo hizi za mitandaoni ni sehemu muhimu. Mazingira ya dijitali siyo ulimwengu ulio sambamba au unaoelea tu hewani, bali ni sehemu ya maisha ya kila siku kwa watu wengi, hasa vijana. Mitandao ya kijamii ni matokeo ya mwingiliano wa binadamu, lakini kwa upande wao pia wanaunda miundo ya mawasiliano inayojenga uhusiano: uelewa uliotafakariwa wa mazingira haya, ni kwa hiyo, sharti la kuhakikisha uwepo mkubwa katika ulimwengu huo.

Uwezo wa kutumia lugha hizi mpya unahitajika, sio tu ili kuendana na nyakati, lakini hasa kwa ajili ya kuwezesha kuenea kusiko na ukomo kwa utajiri wa Injili katika kutafuta njia za kujieleza zinazoweza kuzifikia akili na nyoyo za watu wote. Katika mazingira ya kidijitali, neno lililoandikwa mara nyingi huambatana na taswira na sauti. Mawasiliano yenye ufanisi, kama ilivyo kwenye mifano ya Yesu, hayana budi kuhusisha fikra pana, vionjo na miguso ya wale unaopenda kuwaalika kukutana na fumbo la upendo wa Mungu. Zaidi ya hilo, tunajua kwamba mapokeo ya Kikristo daima yamekuwa na utajiri wa ishara na alama: Nawaza, kwa mfano, kuhusu Msalaba, vitu, picha za Bikira Maria, sanamu za Kipindi cha Noeli, madirisha ya vioo vyenye picha mbalimbali na michoro katika makanisa yetu. Sehemu kubwa muhimu ya urithi wa kazi za sanaa za binadamu imeandaliwa na wanasanaa na wanamuziki ambao walitaka kuieleza kweli ya imani hii.

Katika mitandao ya kijamii, waumini huonyesha unyoofu wao kwa kushirikisha wengine chanzo muhimu cha matumaini na furaha yao: imani katika Mungu anayesamehe na anayependa kwa kufunuliwa na Yesu Kristo. Kushirikisha huku wengine hakuko tu katika kueleza waziwazi imani yao, bali pia katika ushuhuda wao, katika namna ambayo kwayo wanawasiliana “uchaguzi, mapendeleo na mitazamo inayoshabihiana vyema na Injili, hata kama haitajwi kuwa hivyo moja kwa moja” (Ujumbe katika Siku ya Upashanaji Habari 2011). Njia pekee ya muhimu ya kutoa ushuhuda kama huo ni kupitia utayari wa kujitoa kwa ajili ya wengine kwa kushiriki kwa ustahimilivu na heshima kujibu maswali na mashaka yao kadiri wavyotafuta ukweli na maana ya uwepo wa binadamu duniani. Kuongezeka kwa dialojia au mijadala katika mitandao ya kijamii kuhusu imani na nini watu wanaamini, kunathibitisha umuhimu na umaana wa dini katika midahalo ya umma na katika maisha ya jamii.

Kwa wale waliopokea zawadi ya imani kwa moyo mmoja, jibu la msingi kabisa kwa maswali ya walimwengu kuhusu upendo, ukweli na maana ya maisha – maswali ambayo kwa hakika hayakosekani katika mitandao ya kijamii – yanapatikana katika nafsi ya Yesu Kristo. Ni jambo la kawaida kabisa kwa wale walio na imani kutaka kuwashirikisha wengine, kwa njia za kuwaheshimu wengine na kwa namna iliyo bora, hasa na wale wanaokutana nao katika majukwaa ya kidijitali. Hatimaye, hata hivyo, endapo jitihada zetu za kueneza Injili zitazaa matunda mema, daima ni kwa sababu ya nguvu ya Neno la Mungu lenyewe ambalo hugusa mioyo, hata kabla ya sisi kuchukua hatua hiyo. Imani katika nguvu ya kazi ya Mungu lazima iwe kubwa kuliko kujiamini tunakokuweka katika njia za kibinadamu. Katika mazingira ya kidijitali, pia, ambako ni rahisi sana kukuta sauti zilizochachamaa na zilizogawanyika kukuzwa na ambako utiaji chumvi mara nyingine unaweza kuonekana kushinda, tunaitwa kuwa makini katika kutambua hekima ya ndani ya mang’amuzi.

atika hali hiyo, tukumbuke kwamba Eliya alitambua sauti ya Mungu si katika upepo mkali wenye nguvu, si katika tetemeko la ardhi au katika moto, bali katika “sauti tulivu, ndogo” (1 Wafalme 19:11-12). Hatuna budi kuamini katika ukweli kwamba hamu ya msingi ya binadamu ya kupenda na kupendwa, na kutafuta maana na ukweli – hamu ambayo Mungu mwenyewe aliiweka katika moyo wa kila mwanamume na mwanamke – inawaweka wenzetu wa zama zetu wazi katika kile ambacho Mwenye Heri Kardinali Newman alikiita “mwanga wenye huruma” wa imani.

Pamoja na ukweli kwamba mitandao ya kijamii inaweza kuwa njia ya uinjilishaji, inaweza pia kuwa njia muhimu ya kuleta maendeleo ya binadamu. Kwa kutoa mfano, katika baadhi ya miktadha ya kijiografia na kiutamaduni ambako Wakristo wanajihisi kutengwa, mitandao ya kijami inaweza kuwa njia ya kuimarisha hisia zao za umoja wa kweli pamoja na jumuiya ya waamini kwingineko ulimwenguni.

itandao inawezesha kushirikishana maarifa ya kiroho na kiliturjia, kuwasaidia watu kusali kwa hisia ya ukaribu mpana zaidi na wenzao wanaoshirikiana nao imani moja. Mawasiliano ya dhati na yenye kuleta ubadilishanaji hasa katika maswali na mashaka ya wale walio mbali na imani kunapaswa kutufanya kuwa na haja ya kuneemeka, kwa njia ya sala na tafakari, imani yetu katika uwepo wa Mungu na pia upendo kwa wengine kwa vitendo: “Kama nitazungumza kwa lugha za binadamu na malaika, lakini kama sina upendo, ninakuwa sawa na upatu au kayamba inavyovuma tu” (1 Kor 13:1).

Katika ulimwengu wa dijitali kuna mitandao ya kijamii inayowapa watu wa zama zetu fursa za kusali, kutafakari na kushirikishana neno la Mungu. Lakin mitandao hii inaweza pia kufungua milango ya nyanja nyingine za imani. Watu wengi wanazidi kugundua, hasa asante kwa mawasiliano yaliyofanyika awali kwa njia ya mtando, umuhimu wa kukutana ana kwa ana, maisha ya kila siku ya jumuiya na hata hija, ambavyo ni vipengele muhimu daima katika safari ya imani. Katika jitihada zetu za kuifanya Injili ijipenyeze kwenye ulimwengu wa dijitali, tunaweza kuwaalika watu kuja pamoja kwa sala au adhimisho la liturjia katika maeneo fulani kama parokia na makanisa mengine.

Hakupaswi kutokuwepo kwa mshikamano au umoja katika namna ya kuiishi imani na ushuhuda wetu wa Injili, katika hali halisi yoyote tunayoitwa kuiishi, iwe ya mahali halisi au kidijitali. Tunapojihusisha na wengine, kwa njia yoyote iwayo, tunaitwa kueneza upendo wa Mungu hadi mwisho wa mipaka ya dunia. 

Ninaomba ili kwamba Roho wa Mungu awasindikize na kuwaangazia daima, na kwa moyo mkunjufu ninawapa Baraka zangu, ili mpate kuwa watangazaji wa kweli na mashahidi wa Injili. “Enendeni ulimwenguni kote mkaihubiri Injili kwa viumbe vyote” (Mk 16:15).

 

Kutoka Vatikani, 24 Januari 2013, Sikukuu ya Mtakatifu Francis de Sales.

BENEDIKTO XVI

Read more...

Maaskofu 143 wafariki dunia wakiwemo Makardinali 7

MAKADRINALI 7 na Maaskofu 136 wa Kanisa Katoliki wamefariki dunia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2013.

Katika kipindi hicho kinachoishia Novemba 2, 2013, kwa jumla Makardinali na Maaskofu 143 walifariki dunia na kati yao Maaskofu wakuu na wa kawaida ni 136.

Katika orodha ya Makardinali 7 duniani waliofariki dunia, Kanisa katika Bara la Afrika limempoteza Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Lusaka, Zambia, Mwadhama Medardo Joseph Kardinali Mazombwe, aliyefariki dunia Agosti 29, 2013.

Kati ya Maaskofu 136 waliofariki dunia, 17 ni kutoka Bara la Afrika na kati yao watatu ni Maaskofu katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). 

Maaskofu wa Tanzania ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Aloysius Balina, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Moshi, Amedeus Msarikie na Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Njombe, Raymond Mwanyika.

Maaskofu kutoka mataifa mengine ya Afrika nje ya Tanzania ni 

Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Bulawayo, Zimbabwe, Henry Ernest Karlen, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Kano, Nigeria, Patrick Francis Sheehan na Askofu Mkuu Ambrose Madtha, Balozi wa Vatican Pwani ya Pembe.

Wengine ni Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Ziguinchor, Senegal, Augugustin Sagna, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Sekondi-Takoradi, Ghana, John Martin Darko, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bomadi, Nigeria, Joseph O. Egerega.

Katika orodha hiyo ya Maaskofu waliofariki wamo Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Kara, Togo, Ignace Sambar Talkena, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Umzimkulu, Afrika ya Kusini, Gerald Sithunywa Ndlovu, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Torit, Sudan Kusini, Akio Johnson Mutek.

Wengine ni Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki Antsirabè, Madagascar, Felix Ramananarivo, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Accra, Ghana, Dominic Kodwo Andoh, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Monrovia, Liberia, Michael Kpakala Francis, Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Lichinga, Msumbiji, Luis Gonzaga Ferreira da Silva na Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki la Quelimane, Msumbiji, Bernardo Filipè Governo.

Jumatatu Novemba 4, 2013, Baba Mtakatifu Fransisko, aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kuwakumbuka na kuwaombea Makardinali na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha Mwaka 2013 iliyofanyika kayika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Read more...

Ubalozi wa Vatican washambuliwa kwa makombora

UBALOZI wa Vatican nchini Syria umeshambuliwa kwa kombora Jumanne ya Novemba 5 mwaka huu ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa katika shambulizi hilo.

Balozi wa Vatican nchini Syria, Askofu Mkuu Mario Zenari alisema bomu hilo lilirushwa wakati wa asubuhi muda ambao mara nyingi waamini huwa Kanisani kwa sala ya asubuhi na Ibada ya Misa Takatifu. 

Askofu Mkuu Zenari alisema hakuna madhara makubwa yaliyotokea ubalozini hapo kutokana na shambulio hilo isipokuwa watu walipata wasiwasi mkubwa.

“Kwa kweli hakuna madhara makubwa yaliyotokea kutokana na shambulizi hili isipokuwa watu walipata wasiwasi mkubwa” alisema Askofu Mkuu Zenari.

Alibainisha kuwa hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Ubalozi wa Vatican nchini Syria kutikiswa kwa majanga kama hayo. 

Askofu Mkuu Zenari alisema ingawa katika shambulizi hilo la hivi karibuni hakukuwa na madhara makubwa lakini mashambulizi hayo yanaendelea kuleta athari.

Alisema athari hizo ni pamoja na kuharibu majengo na mali ya Kanisa kama ilivyotokea hivi karibuni kwenye Konventi ya Wafransiskani iliyopo katika Mji wa Alepo.

Askofu Mkuu Zenari alisema hakuna mtu anayefahamu kwa sasa sababu ya mashambulizi dhidi ya maeneo ya Kanisa ingawa mwanzoni maeneo hayo yalikuwa yanaheshimiwa na wananchi wote wa Syria.

Aidha, Askofu Mkuu Zenari alisema ana matumaini kuwa juhudi za kidiplomasia zinazoendelea sasa zinaweza kuzaa matunda licha ya wapinzani nchini Syria kugawanyika.

Read more...
Subscribe to this RSS feed
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.