Menu
RSS
Habari za dunia

Habari za dunia (46)

DAR ES SALAAM

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Mhashamu YUDATHADEUS RUWA’ICHI  amesema njia pekee ya kudumisha amani ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anakuwa mdau wa kutunza amani.

 

Mhashamu RUWA’ICHI ameeleza hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Tumaini Media katika mkutano wa mashaurino kuhusu amani, umoja na utulivu nchini.

 

Askofu RWAICHI amesema, kila mmoja katika nafasi yake, hana budi kuheshimu utawala wa sheria  ikiwa ni pamoja na kujituma ili kudumisha amani iliyopo kwani hitaji la amani, utulivu na usalama  ni la kila mtu.

 

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo- CHADEMA, Dakta WILBROAD SLAA amesema, kupotea kwa amani  nchini kumesababishwa na Serikali kusindwa kusimamia katiba iliyopo ya mwaka 1977.

 

Dakta SLAA amesema, kushindwa kufuata katiba iliyopo, kumechangia kupotea kwa misingi ya utu na kuongezeka kwa vitendo vya ufisadi nchini.

Mkutano huo uliowashirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo wazee, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa dini akiwemo Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania-TEC, TARSICIUS NGALALEKUMTWA.

***

 

Mary Yuda

Read more...

wiki ya miito

 

VATICANCITY, Vatican

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya nne ya kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo mchungaji mwema, ya  Aprili26 mwaka huu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kutoka Daraja Takatifu la Upadre, kwa Mashemasi walioandaliwa.

Hii itakuwa niJumapili ya 52 kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, kwani mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache.

Ni siku ambayo waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuombea miito, ili Kanisa liweze kuwapata wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa; watu makini, wema, watakatifu na wachapakazi, ambao daima wako tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Dhamana ya kimissionari na mchakato wa Uinjilishaji ndicho kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa.

Alisema, wito wa Kikristo unajikita katika mang’amuzi ya mtu kutoka katika ubinafsi na undani wake, ili kumwendea Mwenyezi Mungu na kujisadaka kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Huu ni mwaliko wa pekee kwa vijana kutokuwa na woga wa kutoka katika undani na ubinafsi wao, tayari kuanza mchakato wa hija, wakiyaelekeza macho yao kwa ajili ya maskini na watu wanaohitaji kusikia na kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kutoka ni mang’amuzi msingi katika wito, kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 52 ya kuombea Miito mitakatifu ndani ya Kanisa.

Katika Kanisa ambalo kimsingi ni la kimissionari, wito unachipuka, unakua na kukomaa katika mazingira ya kitume, jambo linalowezekana, ikiwa kama mwamini anathubutu kutoka katika ubinafsi wake, kwa kufanya hija, kama ile iliyofanywa na Watu wa Mungu kama yanavyosimulia Maandiko Matakatifu kutoka Misri kuelekea kwenye nchi ahadi, iliyojaa maziwa na asali.

Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kutoka katika utumwa wa ubinafsi ili kuambatana na kupata maisha mapya kwa Yesu Kristo. Hili ndilo Fumbo ambalo linafumbatwa katika historia ya wokovu na mwelekeo wa imani ya Kikristo.

Kutoka ni kiini cha kila wito wa Kikristo anasema Baba Mtakatifu Francisko, kwani hii ni changamoto ya kutoka katika anasa, ukavu wa maisha yanayojikita katika ubinafsi ili mwamini aweze kuyaelekeza maisha yake kwa Yesu Kristo.

Ni kutoka kunakotambua utu wa mtu na kwamba wito wa Kikristo unafumbatwa katika upendo wenye mvuto unaovuka mipaka ya mtu binafsi na kuanza mchakato pevu na wa kudumu ili kutoka katika ubinafsi na kuelekea katika uhuru unaojikita katika sadaka ya mtu binafsi.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa siku ya 52 ya kuombea miito duniani anabainisha kwamba,  kutoka huku kunafumbata dhamana ya kimissionari na uinjilishaji unaotekelezwa na Mama Kanisa.

Hili ni Kanisa linalotoka ili kwenda kukutana na Watoto wa Mungu, katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, ili kuganga na kuponya madonda yao.

Kanisa linaloinjilisha linahamasishwa kutoka ili kukutana na watu, kuwatangazia Habari Njema inayowaletea wokovu; kwa kuwaganga na kuwaponya watu: kiroho na kimwili kwa njia ya neema ya Mungu na kuwafariji maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Wito wa Kikristo ni dhamana inayojikita katika huduma bora na makini kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani sanjari na kujikita katika mshikamano wa udugu na upendo, hususan kwa maskini na wahitaji zaidi.

Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee vijana wa kizazi kipya kutoogopa wala kukatishwa tamaa na wasi wasi kuhusiana na mambo ya mbeleni; yanayoweza kuzimisha ndoto yao kama “kibatari”.

Anawataka vijana kutoogopa kutoka katika ubinafsi wao na kuanza hija ya kufuata nyayo za Yesu, kama alivyofanya Bikira Maria, mfano wa kila wito, ambaye kamwe hakusita kusema, Ndiyo, pale alipoitwa na Mungu, ili aweze kuwa Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Vijana wanakumbushwa kwamba, wito ni mchakato wa kutoka katika ubinafsi ili kumwendea Mwenyezi Mungu na kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Read more...

Kanisa Kenya laainisha changamoto zake

NAIROBI, Kenya.

BARAZA la Maaskofu Katoliki Kenya (Kenya Conference of Catholic Bishops) KCCB, limesema kuwa Kanisa nchini humo kwa sasa linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukata wa rasilimali fedha.

Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza hilo, Padri Daniel Rono alibainisha hayo hivi karibuni wakati ujumbe wa KCCB ukianza hija ya kichungaji mjini Vatican inayofanywa na maaskofu mahalia kila baada ya miaka mitano.

Padri Rono alisema fedha ni moja ya changamoto kubwa kwani zinahitajika kukidhi mahitaji ya Kanisa linaloendelea kukua na kupanuka siku hadi siku.

Alisema, Kanisa linaloendelea kupanuka linahitaji fedha kuweka sawa sawa miundo mbinu yake aliyosema bado imebaki ile ile iliyoanzishwa na wamisionari miaka mingi iliyopita.

“Kanisa la Kenya linaloendelea kupanuka linahitaji fedha kuweka sawa sawa miundo mbinu aliyosema bado imebaki ile ile iliyoanzishwa na wamisionari miaka mingi iliyopita” alisema Padri Rono.

Katibu Mkuu Mtendaji huyo wa KCCB aliitaja changamoto nyingine kuwa ni mafunzo kwa makleri na watawa ili kupata watendaji wengi zaidi katika Shamba la Bwana kwani bila wao hakuna mwendelezo.  

Alisema, kwa sababu hiyo Kanisa lingependa kuwekeza zaidi katika mafunzo makini kwa kundi hilo ili hatimaye wajitoe kwa dhati kwa ajili ya kuihudumia familia ya Mungu ndani na nje ya Kenya.

“Kwa sababu hiyo Kanisa lingependa kuwekeza zaidi katika mafunzo makini kwa kundi hili ili hatimaye wajitoe kwa dhati kwa ajili ya kuihudumia familia ya Mungu ndani na nje ya Kenya” alisema Padri Rono.

Changamoto nyingine kwa mujibu wa Padri Rono ni mawasiliano ya kisasa ili Kanisa liendelee kuwa sauti ya kinabii inayowawakilisha wanyonge na wale waliotengwa kwa kuwafikia watu wengi zaidi na kwa haraka.

Alisema, KCCB inataka kuwekeza maradufu katika mawasiliano ya jamii ili kuwafikia watu wengi watakaoweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima kiroho na kimwili.

Padre Rono alisikitika kutaja changamoto nyingine kuwa ni ubaguzi ulioota mizizi ukijikita katika udini, ukabila na umajimbo lakini pia rushwa na ufisadi.

Alisema mambo hayo yameendelea kuwagawa wananchi wa Kenya, kiasi cha kushindwa kujenga umoja, mshikamano na mfungamano wa kitaifa, kwa ajili ya maslahi ya wengi.

“Mambo haya yameendelea kutumeng’enya na kutugawa wananchi wa Kenya, kiasi cha kushindwa kujenga umoja, mshikamano na mfungamano wa kitaifa, kwa ajili ya maslahi ya wengi” alisema  Padri Rono.

Kwa sababu hiyo Padri Rono alisema Kanisa litaendelea kupaza sauti ili uwepo mgawanyo bora zaidi wa rasilimali na utajiri wa nchi kwa kuzingatia utawala wa sheria na demokrasia.

Baba Mtakatifu Fransisko amewataka wananchi wa Kenya kusimama imara kulinda na kutetea haki za msingi za binadamu, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa.

Katika hija yake iliyoanza Jumatatu Aprili 13 na kumalizika Ijumaa Aprili 17, ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, ulipata fursa ya kukutana, kusali na kuzungumza na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake wakuu mjini Vatican na kutembelea pia kusali kwenye makanisa mbalimbali jijini Roma.

Hija ya maaskofu wa Kenya imefanyika wakati huu, Kanisa linapojiandaa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, uliotangazwa rasmi na Baba Mtakatifu Fransisko, Jumamosi, Aprili 11, 2015.

Read more...

Marekani, Cuba zapongezwa kurejesha uhusiano

NEW YORK, Marekani

BARAZA la Makanisa Ulimwenguni limepongeza hatua iliyofikiwa kati ya Serikali za Marekani na Cuba ya kurejesha uhusiano ya kidiplomasia baada ya uhasama uliodumu kwa zaidi ya miaka 50.

Pongezi hizo zilitolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Duniani (WCC), Dakta Olav Fyske Tveit, wakati wa Mkutano wa VII wa Wakuu wa Nchi za Bara la Amerika uliofanyika nchini Panama.

Dakta Tveit alisema, hizo ni dalili njema kwa jumuiya ya kimataifa kuanza kujikita katika mchakato wa amani licha ya mizozo, migogoro na chuki zilizodumu kwa kipindi kirefu.

Alisema, kwa hakika, amani na upatanisho ni jambo linalowezekana wakati wote iwapo watu wataonesha utashi wa kisiasa na kimaadili kwa kukaa pamoja na kuzungumza.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeendelea kuhamasisha majadiliano na maelewano ya dhati baina ya pande hizi mbili na kwamba maelewano hayo yatadumu.

Wakati WCC ikitoa pongezi hizo, tayari Rais Obama ametangaza kuondoa Cuba kwenye orodha ya nchi zinafadhili ugaidi duniani sanjari na kusitisha vikwazo vya uchumi.

Kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani hatua hiyo ni mojawapo ya juhudi za kujenga upya uhusiano kati ya nchi hizo mbili ulikokuwa mbaya kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Rais Obama katika barua aliyoandikia Baraza la Seneti alisema kuwa katika kipindi cha miezi 6 iliyopita, Cuba haijapata kufadhili shughuli zozote za kigaidi na kwamba imeahidi kuwa itaendelea kuwa hivyo. 

Cuba iliwekwa kwenye orodha hiyo inayozijumuisha pia nchi za Syria, Iran na Sudan kwa miaka 33 na moja ya vigezo vya kuwemo kwenye orodha hiyo ni kuwa na ofisi za ubalozi kwenye nchi hizo.

Tukio la kihistoria la kurejesha uhusiano kati ya Marekani na Cuba lilitangazwa mwezi Desemba na Rais Obama ingawa vikwazo vya kibiashara vitaendelea isipokuwa kama vitaondolewa Baraza la Congress.

 

Read more...

Mashirika ya kitawa yahamasishwa

VATICAN CITY, Vatican

MASHIRIKA ya kitawa na kazi za kitume yametakiwa kuwa na mbinu mkakati ya malezi ya awali na endelevu kuwawezesha watawa kuwa wanyenyekevu wa kweli na wawajibikaji.

Changamoto hiyo ilitolewa hivi karibuni na Sista Claudia Pena Y Lillo, mtawa kutoka Santiago wakati wa kongamano la malezi kimataifa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Sista Claudia alisema, mbinu mkakati hizo zitawafanya watawa wawe na uwezo wa kujenga na kuyafanya maisha yao kuwa mapya kwa kuzunguka Fumbo la Pasaka pamoja na kukumbatia Fumbo la Msalaba.

“Mbinu mkakati hizi zitawafanya watawa tuwe na uwezo wa kujenga na kuyafanya maisha yetu kuwa mapya kwa kuzunguka Fumbo la Pasaka pamoja na kukumbatia Fumbo la Msalaba” alisema Sista Claudia.

Alisema, upya huo wa maisha ya kitawa utakuwa kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu na kuwafanya watawa kumkimbilia Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Aidha, Sista Claudia aliwahamasisha watawa wawe wanasoma maisha yao kwa hekima, wakijitahidi kujifunza mang’amuzi ya maisha ya kila siku, ili kukua na kukomaa kiroho na kiutu.

Alisema, watawa waendelee kujifunza kwa Yesu, mwalimu na mlezi makini aliyefundisha kwa njia ya mifano yake ya maisha, akawaonjesha watu huruma na upendo wa Mungu.

“Sisi Watawa tuendelee kujifunza kwa Yesu, mwalimu na mlezi makini aliyefundisha kwa njia ya mifano yake ya maisha, akatuinjesha sisi wanadamu huruma na upendo wa Mungu” Sista Claudia.

Sista Claudia alisema, Yesu alikuwa na mwono chanya kuhusu maisha ya binadamu, akaonesha kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote waliokuwa wakitengwa, jambo alilosema watawa wanatakiwa kuliiga.

Read more...

Ziara ya Papa kuimarisha majadiliano ya kidini Bosnia

VATICAN CITY, Vatican

BABA Mtakatifu Fransisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Bosnia na Herzegovina, Juni 6 mwaka huu, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani na kujikita katika majadiliano ya kidini.

Kwa mujibu wa Idara ya Habari ya Vatican, majadiliano hayo ya kidini yanalenga kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

 

Ratiba iliyotolewa na Vatican inaonesha kuwa suala la kuimarisha majadiliano ya kidini limepewa kipaumbele kikubwa katika ziara hiyo ya Baba Mtakatifu ikiwa ni ya kwanza kwake kuifanya nchini humo.

Ratiba hiyo inaonesha kuwa katika ziara hiyo ya siku moja Baba Mtakatifu atakutana na viongozi wa dini mbalimbali nchini humo katika Kituo cha Wafransiskani kwa ajili ya wanafunzi kimataifa.

Inaonesha kuwa mazungumzo ya Baba Mtakatifu na kundi hilo yatafanyika saa 11.30 jioni ikiwa ni tukio litakalotangulia mazungumzo yake na vijana wa nchi hiyo saa moja baadaye yaani saa 12.30 jioni.

Kwa ujumla ratiba inaonesha kuwa Juni 6, saa 3.00 asubuhi, Baba Mtakatifu atapokelewa rasmi kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Sarayevo na baadaye atakwenda ikuli kukutana na Rais wa Bosnia na Herzegovina.

Saa 4: 10 asubuhi, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa serikali na wanadiplomasia nchini humo na saa 5:00 anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kosovo.

Baada ya Misa hiyo Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Bosnia na Herzegovina pamoja na kupata nao chakula cha mchana, kwenye Makao Makuu ya Ubalozi wa Vatican nchini humo.

Saa 10. 20 jioni, Baba Mtakatifu atakutana na mapadri, watawa na  waseminari kwenye Kanisa Kuu na baada ya hapo ndipo atakapozungumza na viongozi wa dini mbalimbali saa 11.30 jioni.

Saa 12: 30 jioni, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na kuzungumza na vijana kwenye kituo cha Vijana cha Yohane Paulo II na baadaye, ataelekea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sarajevo, kurejea Vatican kuendelea na utume wake.

Read more...

Baba Mtakatifu ahimiza moyo wa kitume

VATICAN CITY, Vatican

BABA Mtakatifu Fransisko amehimiza moyo wa kitume na uenezaji Injili ili iwe  kiini cha sifa na tabia yote ya wito wa Mkristo ikiwa ni ujumbe wake kwa Siku ya  Kuombea Miito Duniani.

Maneno yanayoongoza ujumbe huo wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya Siku ya Kuombea Miito Duniani itakayoadhimishwa Jumapili ya tarehe 26 ya mwezi huu ni ‘Kutoka, uzoefu msingi katika Miito’.

Baba Mtakatifu amechagua maneno hayo ili kuongoza  Siku ya Kuombea Miito Duniani ambayo kwa mwaka huu yatakuwa maadhimisho ya 52 tangu kuanzishwa.

Katika ujumbe wake huo, Baba Mtakatifu ametoa mwaliko kwa vijana kuacha woga katika kuufunua moyo wazi na kuyatolea maisha yao sadaka, hasa  kwa ajili ya kuwatumikia wahitaji hasa maskini.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu unawatia shime wasitiwe na hofu na hali ya wasiwasi na mashaka katika uhakika wa kutimiza ndoto za maisha ya kila siku, bali wanachotakiwa ni kuwa wazi katika kile wanachotamani katika maisha yao.

Anasema, ni lazima kwanza kutoka na  kuanza  kutembea katika nyayo za Yesu, kama alivyofanya Bikira Maria, mfano wa kila wito, ambaye hakuwa na hofu ya kusema 'Ndiyo’ kwa  wito wa Mungu.

Anawataka vijana, wakati wote na daima kuwa na mtazamo wa kujikatalia utajiri wa kidunia, katika utupu na hivyo kumwendea aliye masikini zaidi, anayehitaji.

Baba Mtakatifu ameandika katika ujumbe huo kuwa katika Kanisa la Kitume “Kimisionari” wito wa  Mkristo hauwezi kuzaliwa tu  ndani ya uzoefu wa utendaji wa kitume lakini hasa ni kwa mtu mwenyewe kujifunua wazi katika ukweli.

Anaeleza katika mzizi wa kila wito wa mkristo, hutoka  katika yote mawili faraja na ugumu binafsi katika kuyaweka maisha kwa Yesu Kristo na kutoka kunakodai  mtu mwenyewe kuyadharau maisha yenyewe na hisia zote za kibinadamu.

Maelezo ya Baba Mtakatifu Fransisko yamefanya nukuu kwa Waraka wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, "Deus Caritas Est" akisema  ni wito wa upendo.

Anasema Baba Mtakatifu huyo mstaafu kuwa wito huo wa upendo ni wenye  kuvutia na kuona zaidi ndani ya nafsi ya mtu mwenyewe na  kuchochea kujifunua wazi na kujiunga katika safari ya maisha ya  kuelekea ukombozi  kwa njia ya kuitoa nafsi, katika huduma kwa wengine.

Read more...

Msimamizi Mkuu mali za Kanisa aapishwa hivi karibuni

VATICAN CITY,

MSIMAMIZI Mkuu wa mali za Kanisa, yaani Camerlengo ameapishwa rasmi na kula kiapo cha utii mbele ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Fransisko.

Camerlengo huyo, Mwadhama Jean-Louis Kardinali Tauran aliapishwa na kula kiapo cha utii mwanzoni mwa mwezi march, 2015 kwenye Viwanja vya Mtakatifu Petro, mjini Vatican.

Kardinali Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini aliteuliwa kushika nafasi hiyo na Baba Mtakatifu Fransisko mwenyewe, Desemba 20 mwaka jana.

Viongozi mbalimbali wamehudhuria tukio la kuapishwa na kula kiapo kwa Kardinali Tauran atakayekuwa na majukumu mengi ikiwemo kutangaza kifo cha Baba Mtakatifu kinapotokea.

Iwapo inatokea Khalifa wa Mtakatifu Petro anafariki dunia, Camerlengo ndiye anayetoa taarifa kwa Makamu wa Askofu Jimbo Kuu la Roma kuhusu tukio hilo naye atatangazakwa familia ya Mungu jimboni Roma.

Camerlengo ana jukumu la kupanga siku ya maziko ya Khalifa wa Mtakatifu Petro baada ya kuwasiliana kwanza na Makardinali wengine watatu.

Yeye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia na kuongoza Baraza la Makardinali akisaidiwa na Makardinali hao wengine watatu, kuhusu masuala yasiyokuwa na umuhimu sana.

Camerlengo ana jukumu la kusimamia na kuratibu shughuli zote zinazofanyika Vatican, Laterano na kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo.

Yeye ndiye mwenye dhamana ya kufunga malango yote yaliyokuwa yanatumiwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro kabla ya kifo chake na kufunguliwa tena mara baada ya maziko ya Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kimsingi Camerlengo ni kiongozi anayesimamia na kuratibu shughuli zote za kipindi cha mpito tangu anapofariki Baba Mtakatifu hadi hadi uchaguzi unapokamilika na hatimaye kutangazwa na kusimikwa kwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki.

Camerlengo ni kati ya viongozi wa Kanisa wanaoendelea na dhamana yao wakiwa chini ya uongozi wa Baraza la Makardinali inapotokea Khalifa wa Mtakatifu Petro yaani Baba Mtakatifu amefariki dunia

Read more...

Serikali yafikia makubaliano na waasi Yemen

Waasi wa madhehebu ya Shia wanaomshikilia nyumbani kwake Rais wa Yemen wamefikia makubaliano na kiongozi huyo anayeungwa mkono na Marekani kukomesha mzozo wa umwagaji damu katika mji mkuu.

Makubaliano hayo yaliofikiwa usiku wa manane ambayo yanawaahidi waasi kuwa na usemi mkubwa katika kuliendesha taifa hilo maskini kabisa katika ulimwengu wa Kiarabu ili waasi hao wawaondowe wapiganaji wao wanaozingira makaazi ya Rais Abed Rabbo Mansour Hadi na maeneo mengine muhimu ya mji mkuu hayakubainisha hasa nani anaongoza nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Yemen SABA waasi hao wa Houthi pia wamekubali kumuachilia huru mshauri mkuu wa Hadi ambaye wamemteka nyara hivi karibuni.

Wahouthi ambao waliudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo na taasisi nyingi za serikali tokea mwezi wa Septemba wamesema walichokuwa tu wakikitaka ni mgao wa haki wa kushirikiana madaraka. Wahakiki wanasema wanataka kuendelea kumbakisha Hadi kama Rais kwa jina tu wakati wakishikilia hatamu za madaraka.

Hadi bado anashikiliwa

 Wapiganaji wa Kihouthi wakiwa katika sare za kijeshi mjini Sanaa.

Wapiganaji wa Kihouthi wakiwa katika sare za kijeshi mjini Sanaa.

Baada ya mapambano ya siku kadhaa na kutekwa kwa Ikulu ya Rais wasaidizi wa Hadi wamesema amekuwa akishikiliwa nyumbani kwake baada ya waasi wa Kihouthi kuwaondowa walinzi wake na badala yake kuwaweka wapiganaji wao.

Mashahidi wanasema wapiganaji wa Kihouthi wameendelea kubakia nje ya kasri la rais na makao yake ya binafsi ambapo mkuu wa nchi ndiko anakoishi hasa .Katika taarifa yake aliyotolewa Alhamisi Rais Hadi amesema Wahouthi wamekubali kuwaondowa wapiganaji wao katika sehemu hizo.

Lakini Mohammed al - Bukhaiti mjumbe wa kamati kuu ya Wahouthi ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba kuondolewa kwa wapiganaji wao na kuachiliwa kwa mkurugenzi wa ofisi ya Hadi, Ahmed Awad bin Mubarak kutoka kizuizini kutafanyika siku mbili au tatu iwapo serikali itatekeleza masharti ya makubaliano yao.

Walichokubaliana

Makubaliano hayo yanamtaka Rais Hadi kuunda upya tume iliopewa majukumu ya kurasimu katiba kuhakikisha uwakilishi mzuri wa Wahouthi.Rasimu hiyo ilikuwa imependekezwa kuundwa kwa serikali ya shirikisho ya majimbo sita jambo ambalo Wahouthi wamelikataa. Makubaliano ya Jumatano yanakusudia kuundwa kwa taifa la shirikisho lakini haikutaja pendekezo la majimbo sita.

 Rasi wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.

Rasi wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.

Wahakiki wanamtuhumu Rais aliyepinduliwa Ali Abdallah Saleh aliyepinduliwa kutokana na uasi wa umma hapo mwaka 2011 baada ya kuwepo madarakani mwa miongo mitatu kwa kuwa na mkono wake katika njama ya Wahouthi kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo.

Akitaka kutumia machafuko hayo kwa faida yake Rais huyo wa zamani wa Yemen hapo Alhamisi ametowa taarifa ya nadra hadharani ambapo amemtaka Hadi kuitisha uchaguzi wa rais na bunge na mapema na kutaka kufutwa kwa vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vilivyowekwa dhidi yake na viongozi wengine wawili wa Kihouthi hapo mwaka jana baada ya Wahouthi kunyakuwa madaraka.

Baadhi ya watu wanahofia kwamba mashambulizi hayo ya Wahouthi yanaweza kusababisha kuvunjika kwa Yemen ambayo imeungana tu hapo mwaka 1990. Mchambuzi wa kisiasa Mansour Hayel amesema kwamba unyakuzi wa madaraka wa Wahouthi katika mji mkuu wa nchi hiyo kunaweza kusababisha kusambaratika kwa Yemen nzima na hali inaweza kuwa mbaya sana kushinda hata ile ya Somalia.

Read more...

Mahmoud Abbas,Netanyahu waandamana

Mfalme wa Jordan na Rais wa Palestinian Mahmoud Abbas ni baadhi ya viongozi kutoka Mashariki ya kati walioshiriki katika maandamo yaliyofanyika mjini Paris Ufaransa kulaani shambulio la kigaidi lililofanyika.

Morocco haijawasilisha uwakilishi wa salam za rambi rambi kutokana na msimamo wake tofauti na mwenendo wa Gazeti la Charlie Hebdo kutokana na vibonzo ambavyo vimekuwa vikichorwa hasa vile vinavyolenga masuala ya kidini.

Rais Hollande aliungana pia na Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu,katika Sinagogi la Grand kuomboleza kwaajili ya waathirika wane wa shambulizi la kigaidi katika Supermarket . Netanyahu alimshukuru mmiliki wa Supermarket iliyoshambuliwa Lassana Bathily kwa jitihada zake katika kuwaokoa mateka waliokuwa ndani ya jingo hilo.

Read more...
Subscribe to this RSS feed
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.