Menu
RSS
Habari za dunia

Habari za dunia (46)

Vatican yasisitiza mazungumzo kukabiliana na itikadi kali

 

ABU DHABI, Falme za Kiarabu

 

 

BARAZA la Kipapa la Majadiliano ya Dini Mbalimbali, limesisitiza kuwa majadiliano kati ya waamini wa Dini mbalimbali ndiyo njia pekee ya kukabiliana na itikadi kali za imani.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Padri Miguel Angel Ayuso Guixot, alipokuwa akitoa mada katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Wanazuoni wa Kiarabu lililofanyika nchini Abu Dhabi.

Akizungumza katika kongamano hilo lililofanyika kwenye Kituo cha Mataifa ya Kiarabu cha Mafunzo Maalum na Utafiti (ECSSR), Padri Miguel alisema hakuna njia nyingine ya kukabilianaa na itikadi kali zaidi ya kuzungumza.

Alisema, viongozi na waamini wa Dini na madhehebu mbalimbali wanatakiwa kujielekeza kwa dhati katika majadiliano ya kweli na ya wazi kati yao ili kukomesha kabisa misimamo mikali ya kidini.

“Viongozi na waamini wa Dini na madhehebu mbalimbali tunatakiwa tujielekeze kwa dhati katika majadiliano ya kweli na ya wazi kati yetu ili kukomesha kabisa misimamo mikali ya kidini” alibainisha Padri9 Miguel.

Alisema, Baba Mtakatifu Fransisko anaamini kuwa msingi wa majadiliano ya kidini unatakiwa kujikita katika wajibu wa pamoja wa kupatikana kwa haki na amani.

Padri Miguel alisema, haki na amani ndiyo misingi mikuu ya kubadilishana mawazo, uzoefu na mang’amuzi katika majadiliano ya kidini kati ya Dini na madhehebu mbalimbali.

Alisema, majadiliano hutengeneza shule ya utu wenye kujali wengine hivyo kuwa chombo cha umoja kinachosaidia kujenga jamii bora zaidi iliyojiunda kwa kuzingatia urafiki wa kweli, udugu na kuheshimiana.

“Majadiliano hutengeneza shule ya utu wenye kujali wengine hivyo kuwa chombo cha umoja kinachosaidia kujenga jamii bora zaidi iliyojiunda kwa kuzingatia urafiki wa kweli, udugu na kuheshimiana” alisisitiza Padri Miguel.

Aidha, katika kongamano hilo, Padri Miguel alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa ECSSR, Dk. Jamal Sanad Al Suwaidi, kwa kuialika Vatican kwenye tukio hilo muhimu.

Alisema, kwa mwaliko huo, Dk. Suwaidi anaungana na Kanisa katika mtazamo wake kwamba majadiliano ya kina, wazi na ya kweli yataondoa tofauti za kiimani zilizopo katika Dini na madhehebu mbalimbali.

Washiriki katika Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Wanazuoni wa Kiarabu walikuwa wataalamu, wasomi na viongozi wa Dini kutoka sehemu mbalimbali duniani waliokutana kushirikishana kuhusu umuhimu wa majadiliano ya kidini kwa lengo la kuwa na dunia yenye amani zaidi, haki, umoja na ushirikiano.

ROMA, Italia

KATIBU Mkuu wa Vatican, Mwadhama Pietro Kardinali Parolin amesema, amesikitikia pengo kubwa kati ya maskini na matajiri na kusema kuwa ni matokeo ya uchumi usiojali.

Kardinali Paroli alibainisha hayo kwenye mkutano wa kimataifa wa siku mbili kuhusu mchakato wa ujenzi wa uchumi shirikishi na endelevu uliofanyika jijini Roma, Italia kuanzia Januari 17 hadi 18.

Alisema, pengo kati ya matajiri na maskini linazidi kuongezeka kila kukicha, hivyo kusababisha watu wengi kuendelea kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato.

Kardinali Parolin alisema, uchumi hauna budi kujielekeza katika kusaidia kukidhi mahitaji ya msingi ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini.

“Uchumi hauna budi kujielekeza katika kusaidia kukidhi mahitaji ya msingi ya binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini” alisema Kardinali Parolin.

Alisema, kwa sababu hiyo, upo umuhimu wa kujenga madaraja ya watu kukutana na kujadiliana kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Fransisko, ili sera na mikakati ya kiuchumi ilenge kweli kudumisha maslahi ya wengi, mshikamano, huruma na mapendo.

Kardinali Parolin alisema, kutokana na changamoto hizo, ipo haja ya kujenga uchumi shirikishi na endelevu unaotoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi.

Alisema, mataifa makubwa yenye nguvu ya uchumi yanatakiwa kukutana kujadiliana kuhusu kuanzisha mchakato wa sera na uchumi  shirikishi na endelevu.

Kardinali Parolin alisema, majadiliano kama hayo yataweza kusaidia kwa namna ya pekee kutambua kwa uwazi mahitaji halisi ya watu katika maisha yao ya kila siku.

Majadiliano kama haya yataweza kusaidia kwa namna ya pekee kutambua kwa uwazi mahitaji halisi ya watu katika maisha yao ya kila siku” alibainisha Kardinali Parolin.

Alisema, Baba Mtakatifu Fransisko anaziona changamoto mbalimbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo na kwamba yote hayo ni matokeo ya uchumi usiowajibika wala kuguswa na mahangaiko ya binadamu.

Katibu Mkuu huyo wa Vatican, aliwakumbusha wajumbe kwamba uchumi unaojali ni moja ya mambo makuu aliyoyasisitiza Baba Mtakatifu Fransisko alipolihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Read more...

Baba Mtakatifu akutana na Mabalozi na kutoa wito

VATICAN CITY, Vatican

BABA Mtakatifu Fransisko, amezitaka Serikali za mataifa duniani kutumia mizozo inayojitokeza sehemu mbalimbalikama fursa ya kudai kupatikana kwa muafaka kwa njia ya amani.

Alitoa wito huo Jumatatu, Januari 11, 2016 alipokuatana na Mabalozi na Wawakilishi nchini Vatican, kwa nia ya kutakiana mema kwa Mwaka Mpya, ikiwa ni utaratibu wa kawaida wa kila mwanzo wa mwaka, kwa Baba Mtakatifu.

Baba Mtakatifu alisema, ana matumaini kwambamizozo iliyojitokeza inaweza kuwa nafasi ya pekee ya kupaza sauti zaidi kwa ajili ya ujenzi wa amani na utayari wa kufikia muafaka kwenye migogoro. 

“Nina matumaini kwambamizozo iliyojitokeza inaweza kuwa nafasi ya pekee ya kupaza sauti zaidi kwa ajili ya ujenzi wa amani nakufikia muafaka” alisema Baba Mtakatifu.

Alitolea mfano wa mafanikio yaliyopatikana katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jamhuri wa Afrika Kati (CAR), akisema ni ishara nzuri ya kutembea pamoja ili kufikia umoja kamili wa kitaifa.

Aidha, Baba Mtakatifu aliitaka jumuiya ya kimataifa kutatua migogoro inayoendelea katika nchi nyingine duniani ikiwemo Cyprus na Colombia,Syria na Iraq.

“Naiomba jumuiya ya kimataifa kutatua migogoro inayoendelea katika nchi nyingine duniani ikiwemo Cyprus na Colombia na Syria na Iraq” alisisitiza Baba Mtakatifu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu aliwataka watu wa mataifa yenye mizozo kuacha ghasia na kurejesha moyo wa mapatano na umoja kwa manufaa ya mataifa yao.

Baba Mtakatifu aliomba mwaka 2016 uwe mwaka wa majadiliano na maridhianoilikuimarisha yaliyo mema kwa wote, hasa katika mataifa yanayopambana na migawanyiko ya kisiasa kama Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Sudan Kusini na Ukraine.

Alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa,nchi binafsi na mashirika ya misaada, kujitokeza kwa wema zaidi, kusaidia mataifa hayo yaliyozingirwa na mizozo na ghasia.

Katika mkutano huo, Baba Mtakatifu aliwakumbuka Mabalozi na Wawakilishi waliofariki dunia mwaka uliopita, Rodney Alejandro Lopez Clemente wa Cuba na Rudolfo P. Von Ballmoos wa Liberia.

Karibu Mabalozi na Wawakilishi wote walihudhuria mkutano huo na kukutana na Baba Mtakatifu wakiongozwa na Dekano wa Mabalozi, Balozi wa Angola, Armindo Fernandes do Espirito Santo Veira. 

Caritas yasikitikia kuuawa kwa maelfu Syria

 

VATICAN CITY, Vatican

 

SHIRIKISHO la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, (Caritas Internationalis), limesema, linasikitikia kuuawa kwa maelfu ya watu nchini Syria, tangu kuanza kwa machafuko nchini humo.

 

Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Michel Roy, alibainisha hayo wakati akizungumzia nafasi ya Caritas katika kuwahudumia waathirika wa machafuko eneo la Mashariki ya Kati.

 

Roy alisema katika kipindi cha miaka mitano ya machafuko na mizozo ya kijamii nchini Syria, mbali na maelfu ya watu kupoteza maisha, mamilioni wenginewamelazimika kukimbia kwenda kuishi kwenye mazingira yenye hatari au nje ya nchi.

Alisema, kutokana na hali hiyo, mwaka 2016 unatakiwa kuleta mabadiliko kwa Syria ili kuacha vita na kuanza kutilia maanani misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Roy alisema, taarifa zinaonesha kwamba, wapo watu wanaoendelea kupoteza maisha kwa kukosa mahitaji muhimu ya kibinadamu ikiwemo chakula kwa sababu ya baa la njaa na kukosa mavazi.

Alisema, katika kipindi cha miezi kumi na mbili ijayo, Caritas Internationalis inataka kuendesha kampeni yenye lengo la kujenga na kudumisha misingi ya amani nchini Syria kwa kuwahusisha wadau mbalimbali.

Roy alisema, kampeni hiyo ilitokana na changamoto iliyotolewa na wajumbe wa Caritas Internationalis kutoka Ukanda wa Mashariki ya Kati, wanaowahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria.

Alisema, watu wanataka kuona msingi wa amani ukijengwa na kudumishwa nchini Syria kwani hiyo ndiyo kiu ya watu wa nchi hiyo kwa wakati huu na kwamba hawahitaji jambo lingile zaidi.

Katibu Mkuu huyo wa Caritas Internationalis alisema, kutokana na ombi la kilio cha amani Mashariki ya Kati, shirika hilo limeamua kutoa kipaumbele cha pekee kwa kilio hicho hadi amani itakapopatikana Syria.

Syria imekuwa katika vita vya wenyewe tangu mwaka 2011 yaliyoanzia na vuguvugu la kisiasa la kuiondoa madarakani Serikali ya Rais Bashar Al Assad na kisha kuanzishwa makundi ya waasi.

Vatican yaendelea kuimarisha uhusiano wa Kidiplomasia

 

ROMA, Italia

UHUSIANO wa kidiplomasia wa Vatican umezidi kuimarika huku takwimu zikionesha kuwa hadi kufikia mwaka 2016, zipo nchi 180 zenye uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican.

Taarifa iliyotolewa wakati Baba Mtakatifu akikutana na Mabalozi na Wawakilishi nchini Vatican Januari 11, 2016, inaonesha kuwa licha ya nchi hizo 180, yapo pia mashirika ya kimataifa.

Takwimu hizo zinayataja mashirika hayo yenye uhusiano na Vatican kuwa ni Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Kimataifa la Malta na Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina.

Ongezeko lingine katika masuala ya kimataifa kwa kipindi cha mwaka 2015 ni katika Balozi na Mashirika ya Kimataifa yenye makao yake mjini Roma yaliyofikia 86.

Idadi hiyo ilifikiwa baada kufunguliwa kwa ofisi za nchi za Belize, Burkina Faso naEquatorial Guinea, pia Tume ya Kudumu ya Serikali ya Palestina, Umoja wa Nchi za Kiarabu na Shirika la kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR).

Pia katika kipindi hicho cha mwaka 2015, Vatican imejiunga na Jumuiya ya Caraibi (CARICOM), kuanzia Juni 4, 2015na kuwa mwanachama mtazamaji wa jumuiya hiyo.

Aidha, taarifa hiyo inaonesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2015, Vatican iliridhia mikataba minne ukiwemo kati yake na Serikali ya Italia kuhusu masuala yakodi, uliotiwa saini Juni 10.

Mikataba mingine ni pamoja na uliotiwa saini Juni 26, kati ya Vatican na Serikali ya Palestina na kati yake na TimorMashariki kuhusu maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini humo, uliotiwa saini, Agosti 14.

Mkataba wa nne ulitiwa saini Juni 22, 2015 kati ya Vatican na Serikali ya Chad kuhusu masuala ya maisha na utume wa Kanisa nchini humo na Septemba 10, Sektretarieti ya Vatican ilitiliana saini Mkataba wa Maelewano na Serikali ya Kuwait kuhusu masuala yanayotakiwa kufuatiliwa na nchi hizo mbili.

 

 

Read more...

Vatican yaanzisha Mfuko wa Elimu.

VATICAN CITY, Vatican

BARAZA la Kipapa la elimu Katoliki limeanzisha Mfuko wa Elimu ya Kikristo ili kusaidia mchakato wa waamini kupata elimu, ujuzi na maarifa ya kisayansi ili kuendeleza Elimu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia.

Mfuko huo umeanzishwa baada ya Baba Mtakatifu Fransisko kuridhia, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha tamko kuhusu umuhimu wa Elimu ya Kikristo (Gravissimum educationis).

Baada ya kutoa idhini, Baba Mtakatifu pia aliamua Makao Makuu ya Mfuko wa Elimu Katoliki yawe katika mazingira ya Vatican na kwamba utaongozwa na kusimamiwa kwa sheria, kanuni na taratibu zote za Mji wa Vatican.

Tamko kuhusu umuhimu wa Elimu ya Kikristo lilichapishwa Oktoba 28, 1965, likikazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa elimu katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Lengo la elimu hiyo katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia, ni kuwawezesha waamini kufaidika na urithi wa kitamaduni na maisha ya kiroho lakini pia kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya kijamii.

Kwa kuanzisha mfuko huo, Baba Mtakatifu Fransisko alilipongeza kwa namna ya pekee Baraza la Kipapa la elimu Katoliki kwani litasaidia kuendeleza Elimu Katoliki sehemu mbalimbali duniani.

Alisema, Kanisa linatambua kwamba, elimu ni sehemu ya haki za msingi za binadamu kwani kila binadamu ana haki ya kupata elimu bora inayoambata pia na elimu ya Kikristo.

 

Read more...

RAIA 29 WASHITAKIWA AFRIKA KUSINI

Cape Town

Raia ishirini na tisa {29} wa Afrika Kusini wameshitakiwa kwa kuhusika na vurugu zilizoanzishwa na maandamano makubwa ya wanafunzi nchini humo ambayo hajawahi kutokea tangu yale yaliyofanywa wakati wa kupinga ubaguzi wa rangi uliomalizikia mwaka 1994.

Polisi nchini humo imelazimika kutumia gesi ya kutoa machozi kwa lengo la kuwatawanya wanafunzi walioandamana na kukusanyika kwenye viwanja vya Bunge mjini Cape Town.

Maelfu ya waamdanamaji wengine pia walikusanyika kwenye Makao Makuu ya Chama tawala kinachoongoza Serikali ya Afrika Kusini kwenye mji Mkuu wa Johannesburg.

Wanafunzi hao wenye hasira walifanya maandamano hayo kwa lengo la kupinga Muswaada wa ongezeko la gharama ya fedha za malipo kwa masomo ya ziada iliyopendekezwa na serikali nchini humo.

Maandamano hayo yalianza tangu wiki iliyopita katika Chuo Kikuu cha Witwatersrand na kueneea kwenye vyuo vingine zaidi ya kumi {10}, wakishinikiza kusitishwa kwa mpango huo.

Jeshi la Marekeni laokoa maelfu ya watu waliotekwa - IS

HAWIJA

Majeshi ya Marekani nchini Iraq yamefanikiwa kuwaokoa maelfu ya watu waliokuwa wakishikiliwa na vikosi vya wanamgambo wa kundi la Kiislam la Islamic state-IS nchini humo.

Tarifa za jeshi hilo iliyotolewa na makao makuu ya Jeshi nchini Marekani Pentagon imeeleza kwamba katika operesheni hiyo wanajeshi kadhaa wa Marekani walijeruhiwa na wengine kupoteza maisha tangu operesheni hizo zilipoanza rasmi mapema mwaka uliopita dhidi ya IS.

Aidha jana Alhamisi majira ya asubuhi majeshi hayo yamefanya operesheni nyingine katika enelo lililopo karibu na mji wa Hawija Kaskazini mwa Iraq.

Marekani imesema kuwa katika zoezi hilo wanamgambo watano wa IS walikamatwa huku wengine wakiuawa wakati walipokuwa wakiwadhibiti wanamgambo hao.

Maofisa wa ulinzi wa Marekani wamesema kuwa watu zaidi ya sabini {70} wamekamatwa, ikiwemo wa jamii ya Sunni, wenye uraia wa Iraq ishirini {20} ambapo katika operesheni hiyo hakuna mtu wa jamii ya kikurd aliyeokolewa.

***

Imetafsiliwa kutoka-BBCNews

Read more...

Baba Mtakatifu kutembelea Kenya, Uganda wakati mmoja

NAIROBI, Kenya

BARAZA la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB) limetangaza rasmi kuhusu ziara ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Fransisko itakayokwenda sanjari na ziara kama hiyo katika nchi nyingine ya Afrika Mashariki, Uganda.

Tangazo la ujio wa Baba Mtakatifu nchini Kenya lilitolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mhashamu Askofu  Philip Anyolo, aliyesema kuwa ziara ya Baba Mtakatifu itakuwa Novemba 2015.

Katika barua yake ya kichungaji kwa waamini aliyoitoa kwa niaba ya Maaskofu wenzake, Alhamisi ya Agosti 27, 2015, Askofu Anyolo alibainisha kuwa wakati umefika wa kuijandaa kwa ajili ya ugeni mkubwa nchini Kenya.

Askofu Anyolo wa Jimbo la Homabay aliandika wazi kwenye barua hiyo kwamba Baba Mtakatifu amekubali mwaliko wa Maaskofu wa Kenya kuitembelea nchi hiyo mwezi Novemba 2015.

“"Baba Mtakatifu amekubali mwaliko tuliotoa Maaskofu wa kuitembelea nchi yetu na atafanya hivyo baadaye mwezi Novemba mwaka huu” alibainisha Askofu Anyolo.

Alisema, ziara ya Baba Mtakatifu ni ziara ya kichungaji, hivyo Kanisa nchini humo litashirikiana na Serikali ya Kenya, katika maandalizi kuhakikisha inafanikiwa.

Aidha, Askofu Anyolo aliomba sala za waamini na msaada wa hali na mali kutoka kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ili kufanikisha ziara hiyo ya Baba Mtakatifu nchini humo.

“Tunaomba sala zenu na msaada wa hali na mali kutoka kwenu waamini na watu wote wenye mapenzi mema ili kufanikisha ziara ya Baba Mtakatifu nchini mwetu” ilieleza barua hiyo ya Askofu Anyolo.

Mwaliko kwa Baba Mtakatifu kuitembelea Kenya ulitolewa na Maaskofu wa nchi hiyo wakati wa ziara ya kitume ya maaskofu mahalia inayofanywa kila baada ya miaka mitano mjini Vatican waliyoifanya Aprili, 2015.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Fransisko kuitembelea Kenya tangu alipochaguliwa kuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Machi 2013.

Hata hivyo, hiyo itakuwa ni ziara ya nne kufanywa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani nchini Kenya, tatu za kwanza zikifanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II Mei 1980, Agosti 1985 na Septemba 1995.

Katika ziara hiyo ya kwanza kwa Baba Mtakatifu Fransisko kuzuru Bara la Afrika, mbali na kuitembelea Kenya na Uganda, atakuwa na ziara nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).

Read more...

Kanisa lasikitikia mashambulizi ubalozini

 

 

ROMA, Italia

 

BABA Mtakatifu Fransisko amesema vitendo vya kigaidi mahali popote vinapotendekea duniani havina budi kulaaniwa na watu wote wenye kupenda amani popote walipo. 

Wito huo wa Baba Mtakatifu umo katika salamu zake alizomtumia Rais wa Misri, Abdel Fattah El Sisi, kufuatia shambulizi la bomu lililotokea mapema Julai , 2015 kwenye Ubalozi wa Italia nchini Misri.

Katika salamu zake hizo zilizoandikwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa Vatican,  Mwadhama Pietro Kardinali Parolin, Baba Mtakatifu alisema, ugaidi ni hatari.

Alisema, mbali na kulaani ugaidi, jumuiya ya kimataifa haina budi kusimama imara na pamoja kukabiliana na wale wote wanaofadhili na kutekeleza vitendo hivyo vya kinyama.

Baba Mtakatifu katika salamu zake alisisitiza kuwa, ugaidi popote unapofanyika, unahatarisha mafungamano na mshikamano wa kitaifa na kimataifa. Kwa salamu hizo za kulaani shambulizi lililofanyika Ubalozi wa Italia nchini Misri,  Baba Mtakatifu alikuwa ameungana viongozi wengine kulaani shambulizi hilo.Miongoni mwa viongozi waliolaani shambulizi hilo la kigaidi la Cairo ni  Rais wa Italia, Sergio Mattarella na Waziri Mkuu wake, Matteo Renzi. Katika shambulizi hilo lililofanyika nje ya Ubalozi wa Italia nchini Misri, mtu mmoja alifariki dunia na wengine kumi kujeruhiwa na mali kadhaa kuharibika.

Kutokana na shambulizi hilo, Waziri Mkuu wa Misri Ibrahim Mahlab alisema kuwa nchi hiyo kwa sasa ni sawa na vile ipo vitani na hivyo Serikali itaelekeza nguvu zake kukabiliana na makundi yoyote yanayohatarisha amani.    

Read more...

Idadi ya Makardinali yapungua kwa kifo cha Kardinali Biffi

 

VATICAN CITY.

 

IDADI ya makardinali wa Kanisa Katoliki duniani imefikia 221 hadi kufikia Jumamosi Julai 11, 2015 baada ya mmoja wao, Mwadhama Giacomo Kardinali Biffi, kufariki dunia.

Kwa mujibu wa Idara ya Habari ya Vatican, Kardinali Biffi ,Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Bologna nchini Italia, alifariki dunia mapema Julai 2015, akiwa na umri wa miaka 87. 

Kwa kifo cha Kardinali Biffi, kati ya makardinali waliobaki, 120 ndiyo wenye haki ya kupiga kura kumchagua Baba Mtakatifu mpya iwapo itatokea sababu ya kufanya hivyo na 101 hawana haki hiyo.

Katika makardinali hao waliobaki, Bara la Afrika lina makardinali 20, kati yao watatu hawana haki ya kupiga kura kumchagua Baba Mtakatifu mpya iwapo itatokea sababu ya kufanya hivyo.

Marehemu Kardinali Biffi, alizaliwa  Milan nchini Italia Juni 13, 1928, na baada ya malezi ya kipadri alipewa Daraja Takatifu la Upadri Desemba 23, 1950.

Baada ya utume wake akiwa Padri kwa miaka 25, aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Milan Desemba 7, 1975, na kuwekwa wakfu Januari 11 1976.

Aprili 19, 1984, aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Bologna kufuatia kifo cha Askofu Mkuu Enrico Manfredini na mwaka uliofuata yaani Mei 25, 1985, akateuliwa na kutangazwa kuwa Kardinali. 

Marehemu Kardinali Biff aliyekuwa pia mwanzilishi wa Taasisi ya  Kichungaji ya Lombardy, aliliongoza Jimbo Kuu la  Bologna kwa karibu miaka 20, hadi Desemba 16, 2003, alipostaafu.

Katika  maisha yake kwa mara kadhaa aliitwa kuhubiri wakati wa mafungo ya Papa na wasaidizi wake katika Idara za Curia ya Roma na alifanya hivyo wakati wa utawala wa Baba Mtakatifu Yohana Paulo II na pia wakati wa Kwaresma ya mwaka 2007 mbele ya Papa Benedict XVI. 

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Fransisko, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Kardinali Biffi wakati huo akiwa katika ziara ya kichungaji nchini Paraguay, moja ya nchi alizozitembelea huko Amerika Kusini.

Katika salamu zake, Baba Mtakatifu alisema, kwa huzuni nyingi, amemkumbuka marehemu Kardinali Biffi, aliyeweza kuishi kwa utulivu na ujasiri wa imani, akijiweka chini ya mapenzi ya Bwana, licha ya afya yake kuwa mbovu kwa muda mrefu.

Alisema, yupo pamoja na waamini wa Jimbo Katoliki la Bologna katika majonzi hayo ya kuondokewa na mpendwa Kardinali Biffi, aliyeitangaza kwa furaha, hekima na ushupavu  Injili ya Kristo.

 

Read more...

Kanisa lataka waandishi wa habari walindw

 

NEW YORK, Marekani

MWAKILISHI wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa (UN), Mhashamu Askofu Mkuu Bernardito Auza, amesema waandishi wa habari wanastahili kulindwa wakati wanapotekeleza majukumu yao.

 

Askofu Mkuu Auza alitoa wito huo mjini New York, Marekani wakati akichangia mada kuhusu umuhimu wa kuwalinda waandishi wa habari wanaotekeleza majukumu yao kwenye maeneo ya vita.

Alisema, waandishi wa habari wana umuhimu mkubwa katika kutoa habari zinazohusu vita, maamuzi yanayotolewa na kubainisha mikakati inayoweza kutumika kwa ajili ya kukomesha vita lakini bahati mbaya hawalindwi.

Askofu Mkuu Auza alisema, wakati huu wa kukua kwa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, watu wengi wana hamu ya kupata habari kutoka maeneo ya vita, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa kimataifa na watu walioathirika na vita kwa kuwapatia msaada wanaohitaji na kwamba mbali na habari hizo za vita, watunga sera nao hupata wakati mgumu kupata habari za uhakika kutoka kwenye maeneo ya vita.

Kuhusu hujuma dhidi ya waandishi wa habari, Askofu Mkuu Auza alisema kwa mwaka 2014 pekee, waandishi wa habari 69 walipoteza maisha na wengine 221 kufungwa gerezani kutokana na kazi yao.

Alisema, kwa mwaka 2015 hadi sasa wapo waandishi wa habari 25 waliuawa na wengine 156 kufungwa gerezani, jambo alilosema linasikitisha kutokea kwa watu muhimu katika jamii katika kupasha habari.

Askofu Mkuu Auza alisema, kutokana na hali hiyo, pande zote zinazohusika hazina budi kuhakikisha zinawalinda waandishi wa habari ili waweze kutekeleza wajibu wao ipasavyo bila vikwazo vyovyote.

Alisisitiza kuwa waandishi wa habari hawana budi kulindwa wanapokuwa katika maeneo ya vita na kwamba ipo haja ya kuangalia iwapo sera na mikakati ya kuwalinda waandishi wa habari kwa sasa inakwenda na wakati.

Askofu Mkuu Auza alisema, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha waandishi wa habari wanalindwa na jumuiya ya kimataifa kwa upande wake ihakikishe inasaidia kuwagharimia waandishi wa habari katika masuala ya fedha na uchumi.

Hata hivyo, alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari wenyewe kuwa wa kwanza kujilinda wanapokuwa vitani, kwa kujielekeza katika ukweli na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiutu, kitamaduni na imani.

Aidha, Askofu Mkuu Auza alisema, waandishi wa habari hawana budi kujikita katika kutangaza ukweli kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba, wahusika wa mauaji ya waandishi wa habari wafikishwe kwenye mkondo wa sheria kuwezesha haki kutendeka.

Read more...

Taasisi ya amani yaundwa Maziwa Makuu

Bukavu, DRC.

SHIRIKISHO la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati ( ACEAC), limeanzisha Taasisi ya Amani Maziwa Makuu kwa lengo la kuharakisha mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano.

Katibu Mkuu wa ACEAC Padri Edouard Mobili, alisema, taasisi hiyo ni muhimu kwa kuwa ukanda wa Maziwa Makuu umekuwa ni uwanja wa machafuko ya kila aina.

Padri Mobili alisema, kituo hicho kitakuwa msaada mkubwa kwa mchakato wa haki, amani na upatanisho hasa kwa nchi zinazounda ACEAC, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).

Alisema, nchi za Maziwa Makuu zinahitaji chombo makini kisicho na mamlaka ya utawala kushughulikia mizozo na migogoro katika mataifa ya ukanda huo akitolea mfano wa mzozo wa sasa wa kikatiba nchini Burundi.

Padri Mobili alisema mzozo nchini Burundi hauwezi kutatuliwa kwa mabavu na mapigano bali utashi wa kweli wa viongozi wa kisiasa na msaada wa usuluhishi wa taasisi mbalimbali yakiwemo makanisa.

Alisema, Makao Makuu ya taasisi hiyo yatakuwa Bukavu, Kusini mwa Jimbo la Kivu nchini DRC ambako ni kitovu cha migogoro na vita vya muda mrefu nchini humo.

Padri Mobili alisema, taasisi hiyo itakayoendesha mafunzo yake kwa lugha za kiingereza na kifaransa, itafanya shughuli zake katika Seminari Kuu ya Bukavu na kwa sababu hiyo itakuwa ikishirikiana kwa karibu na taasisi nyingine ikiwemo Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Bukavu.

Alizitaja taasisi nyingine kuwa ni Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha DRC, ofisi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) DRC, Chuo Kikuu cha Rwanda na Chuo Kikuu cha San Diego cha Marekani. 

Read more...
Subscribe to this RSS feed
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.