Menu
RSS

Serikali yafikia makubaliano na waasi Yemen

Waasi wa madhehebu ya Shia wanaomshikilia nyumbani kwake Rais wa Yemen wamefikia makubaliano na kiongozi huyo anayeungwa mkono na Marekani kukomesha mzozo wa umwagaji damu katika mji mkuu.

Makubaliano hayo yaliofikiwa usiku wa manane ambayo yanawaahidi waasi kuwa na usemi mkubwa katika kuliendesha taifa hilo maskini kabisa katika ulimwengu wa Kiarabu ili waasi hao wawaondowe wapiganaji wao wanaozingira makaazi ya Rais Abed Rabbo Mansour Hadi na maeneo mengine muhimu ya mji mkuu hayakubainisha hasa nani anaongoza nchi hiyo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Yemen SABA waasi hao wa Houthi pia wamekubali kumuachilia huru mshauri mkuu wa Hadi ambaye wamemteka nyara hivi karibuni.

Wahouthi ambao waliudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo na taasisi nyingi za serikali tokea mwezi wa Septemba wamesema walichokuwa tu wakikitaka ni mgao wa haki wa kushirikiana madaraka. Wahakiki wanasema wanataka kuendelea kumbakisha Hadi kama Rais kwa jina tu wakati wakishikilia hatamu za madaraka.

Hadi bado anashikiliwa

 Wapiganaji wa Kihouthi wakiwa katika sare za kijeshi mjini Sanaa.

Wapiganaji wa Kihouthi wakiwa katika sare za kijeshi mjini Sanaa.

Baada ya mapambano ya siku kadhaa na kutekwa kwa Ikulu ya Rais wasaidizi wa Hadi wamesema amekuwa akishikiliwa nyumbani kwake baada ya waasi wa Kihouthi kuwaondowa walinzi wake na badala yake kuwaweka wapiganaji wao.

Mashahidi wanasema wapiganaji wa Kihouthi wameendelea kubakia nje ya kasri la rais na makao yake ya binafsi ambapo mkuu wa nchi ndiko anakoishi hasa .Katika taarifa yake aliyotolewa Alhamisi Rais Hadi amesema Wahouthi wamekubali kuwaondowa wapiganaji wao katika sehemu hizo.

Lakini Mohammed al - Bukhaiti mjumbe wa kamati kuu ya Wahouthi ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba kuondolewa kwa wapiganaji wao na kuachiliwa kwa mkurugenzi wa ofisi ya Hadi, Ahmed Awad bin Mubarak kutoka kizuizini kutafanyika siku mbili au tatu iwapo serikali itatekeleza masharti ya makubaliano yao.

Walichokubaliana

Makubaliano hayo yanamtaka Rais Hadi kuunda upya tume iliopewa majukumu ya kurasimu katiba kuhakikisha uwakilishi mzuri wa Wahouthi.Rasimu hiyo ilikuwa imependekezwa kuundwa kwa serikali ya shirikisho ya majimbo sita jambo ambalo Wahouthi wamelikataa. Makubaliano ya Jumatano yanakusudia kuundwa kwa taifa la shirikisho lakini haikutaja pendekezo la majimbo sita.

 Rasi wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.

Rasi wa zamani wa Yemen Ali Abdullah Saleh.

Wahakiki wanamtuhumu Rais aliyepinduliwa Ali Abdallah Saleh aliyepinduliwa kutokana na uasi wa umma hapo mwaka 2011 baada ya kuwepo madarakani mwa miongo mitatu kwa kuwa na mkono wake katika njama ya Wahouthi kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo.

Akitaka kutumia machafuko hayo kwa faida yake Rais huyo wa zamani wa Yemen hapo Alhamisi ametowa taarifa ya nadra hadharani ambapo amemtaka Hadi kuitisha uchaguzi wa rais na bunge na mapema na kutaka kufutwa kwa vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa vilivyowekwa dhidi yake na viongozi wengine wawili wa Kihouthi hapo mwaka jana baada ya Wahouthi kunyakuwa madaraka.

Baadhi ya watu wanahofia kwamba mashambulizi hayo ya Wahouthi yanaweza kusababisha kuvunjika kwa Yemen ambayo imeungana tu hapo mwaka 1990. Mchambuzi wa kisiasa Mansour Hayel amesema kwamba unyakuzi wa madaraka wa Wahouthi katika mji mkuu wa nchi hiyo kunaweza kusababisha kusambaratika kwa Yemen nzima na hali inaweza kuwa mbaya sana kushinda hata ile ya Somalia.

Read more...

Mahasimu wa Sudan Kusini wasaini makubaliano

  • Published in Africa

Viongozi wa pande hasimu nchini Sudan Kusini wamesaini makubaliano ya kuimairisha juhudi za kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe mjini Arusha, Tanzania, wakishuhudiwa na viongozi kadhaa wa Afrika.

Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Machar, walisaini makubaliano hayo ambayo sasa yanazileta pamoja kambi mbili zinazopingana ndani ya chama tawala cha Vuguvugu la Ukombozi wa Sudan Kusini (SPLM).

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Benard Membe, aliupongeza "uongozi wa SPLM kwa kufikia makubaliano ya kukiunganisha tena chama chao kwa maslahi ya Sudan Kusini."

Mazungumzo hayo yalikuwa chini ya usimamizi wa Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, huku viongozi kadhaa wa mataifa jirani wakihudhuria kuhakikisha kuwa mahasimu hao wawili wanasaini makubaliano hayo.

Hadi sasa, hakuna taarifa za vipengele vya makubaliano hayo zilizotolewa, lakini makundi hasimu yanayowania udhibiti wa siasa za nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta yameyavunja makubaliano ya kusitisha mapigano mara tano ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

IGAD yaendeleza juhudi za mapatano

 Mkutano wa upatanishi chini ya IGAD mwezi Novemba 2014 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano wa upatanishi chini ya IGAD mwezi Novemba 2014 mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Mazungumzo hayo nchini Tanzania yalikuwa sehemu ya juhudi za pamoja kusaka makubaliano zilizoanzishwa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika (IGAD) kwenye mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Mazungumzo mengine ya IGAD yanatazamiwa kufanyika kandoni mwa mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa mwishoni mwa mwezi Januari.

Kwa mara ya kwanza, mapigano yalizuka kwenye taifa hilo jipya kabisa barani Afrika mwezi Disemba 2013, baada ya Kiir kumtuhumu makamu wake wa zamani, Machar, kutaka kumpindua. Baadaye yakageuka kuwa vita vya kikabila ndani ya SPLM na kuchochea mapigano ya kulipizana kisasi na mauaji nchi nzima yaliyopelekea vifo vya maelfu ya watu na kuirejesha nchi hiyo kwenye ukingo wa njaa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kiir na Machar walikutana kwa mara ya mwisho mwezi Novemba mjini humo, ambako walikubaliana kusitisha mara moja vita, lakini makubaliano hayo yalivunjwa masaa machache tu baadaye.

Mapigano makali yaliripotiwa mapema wikik hii kati ya jeshi la waasi kwenye jimbo la kati la Lakes na siku ya Jumanne, msemaji wa jeshi, Philip Aguer, alivilaumu vikosi vya Machar kwa kukiripua kinu cha kuzalishia mafuta kwenye jimbo la Unity.

Hakuna orodha rasmi ya vita iliyorikodiwa na serikali au waasi au Umoja wa Mataifa, lakini taasisi ya kushughulikia mizozo duniani, International Crisis Group, inakisia kuwa kiasi cha watu 50,000 wameshapoteza maisha hadi sasa.

Read more...

Wauguzi Mweka waula

Na Celina Joseph 

WAHITIMU wa mafunzo ya wauguzi wasaidizi katika Chuo cha Mweka, wamepewa ahadi ya kusaidiwa kupata sehemu ya kufanyika kazi katika baadhi ya hospitali zilizoko kwenye Kata ya Kigogo jijini Dar es Salaam.

Ahadi hiyo ilitolewa na  Afisa Mtendaji  kata hiyo Anthony Ngonyani, hivi karibuni  aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Diwani wa kata hiyo, alipozungumza nao kwenye mahafali ya 10 yaliyofanyika Kigogo.  

Alisema waanguzi wasaidizi wanahitajika sana, ili kuongeza nguvu kwa madaktari  na manesi wanaofanya kazi hiyo.

Ngonyani alisema wahitimu wa kazi ya uuguzi wanapaswa pia kuzingatia maadili ya kazi yao ili kuepusha madhara na vifo kwa wangojwa na kutenda kazi kwa huruma na upendo. 

 Naye Mkuu wa Chuo cha uuguzi cha Mweka Kigogo Dk. Mlangwa, alisema kila mhitimu anapaswa kuzingatia mafunzo kwa umakini na kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya uuguzi. 

Alisema huruma kwa wangonjwa inahitajika zaidi bila kusahau upendo licha ya kumpatia matibatu  mgonjwa kwani kufanya hivyo kutamsaidia mgonjwa kupata afuaeni hata kabla ya matibabu. 

Dk. Mlangwa alisema kwa mafunzo waliyoyapata ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa vitendo katika hospitali mbalimbali wauguzi hao watakuwa wamepata elimu ya kutosha kumhudumia mgonjwa kama wauguzi wasaidizi. 

Aidha Mkuu huyo alikemea tabia ya baadhi ya wauguzi kuwanyanyasa wagonjwa na kuwatolea lugha zisizo rasmi kuwa haifai katika kazi yao kwani wanakiuka maadili ya uuguzi.

Alisema Muuguzi mwenye maadili daima anazingatia, kazi yake na kuwaheshimu watu wote wanaofika kwa ajili ya matibabu kwa kuwa wao ndio wataalamu wa masuala ya afya badala ya kuwakejeli na kutaka rushwa , kuwa tabia hiyo sio nzuri hata kidogo. 

Mkuu huyo wa chuo pia aliwataka waunguzi hao kutokuridhika na elimu waliyoipata bali watafute muda ili kujiendeleza zaidi katika ujuzi huo. 

Alisema elimu waliyoipata sio kwamba haifai bali iwe tiketi ya kwenda mbele kwa mfunzo zaidi ili kuwafanya wagojwa wafurahie huduma itakayokuwa ikitolewa kwa kiwango cha hali ya juu na watu wenye taaluma iliyobobea. 

Alisema vinginevyo badala ya kuhudumia wagonjwa watabaki kutoa lugha zisizo rasmi, kutokuwajibika wakati wa saa za kazi na pengine kutoroka ofisini kwa sababu ya kutokuwa makini.

Kwa upande wake mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, Sista Issabela Mdam wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo wa Mbinga, aliwataka wahitimu wenzake kufanya kazi kwa uadilifu na kufuata kanuni za uuguzi. 

Sista Issabela alisema kazi itakuwa ni rahisi ikiwa wauguzi hao wakifuata kanuni za kazi yao, ikiwa ni pamoja na kumshirikisha Mungu kwa kuwa kazi bila Mungu haiwezi kuwa na mafanikio. 

Alisema mafanikio ya kazi yoyote hayawezi kuja kuwa na juhudi za mtu binafsi hasa katika suala la kujiendeleza kimasomo zaidi na kwamba iwapo muuguzi atakuwa na ujuzi wa kutosha itamsaidia kutoa huduma kwa wagonjwa bila hofu kwa kuwa atakuwa anafahamu nini anafanya, tofauti na ujuzi wa kubabaisha wajue kwamba kosa moja linaweza kugharimu uhai wa Mtu. 

Sista huyo alitoa wito pia kwa jamii inayokuwa ikiwahudumia wagonjwa kwenye hospitali kuwa na moyo wa uvumilivu badala ya kuwalaumi na kugombana na wauguzi jambo linaloweza kuwafanya wagonjwa kukosa imani na waunguzi. 

Alisema kazi hiyo ni nzuri ila inahitaji umakini mkubwa, moyo wa huruma na upendo bila kusahau kumuomba Mwenyezi Mungu mafanikio kila siku.

Katika mahafari hayo wahitimu walipewa zawadi mbalimbali kwa mshindi aliyeongoza kwa nidhamu, masomo, mazoezi kwa vitendo, uuguzi na ukunga, ambapo miongoni mwao alikuwa ni Sista Issabel Mdam, Mwasi Sostenes na Hadija Suleiman waliochukua ushindi wa jumla.

Jumla ya wahitimu 176 wametunukiwa vteti vyao katika mahafali hayo ya 10 tangu Chuo cha Uuguzi cha Mwika kilipoanzishwa.  

 

 

Read more...
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.