- font size decrease font size increase font size

Kampuni ya Shell italipa fidia ya dola milioni 84 kufuatia kuvuja kwa mabomba ya mafuta nchini Nigeria, hatua inayoweza kufungua njia ya kufidiwa hasara zinazosababishwa na kampuni za mafuta duniani.
Wanavijiji 15,600 kwenye jimbo la Niger Delta watapata dola 3,300 kila mmoja, huku dola milioni 30 zikiingizwa kwenye mfuko wa jamii kwa ajili ya maendeleo ya vijiji vyao.
Hata hivyo, kampuni ya uwakili ya Leigh Day jijini London, Uingereza, ambayo ndiyo iliyofikia makubaliano hayo na Shell kwa niaba ya wakulima hao wa Nigeria, ilisema ni jambo linalokera kwamba imechukuwa miezi sita kwa kampuni tanzu ya SPDC kukubali kwamba ilifanya makosa na kufikia makubaliano ya fidia.
Pamoja na kukiri kwamba makosa kwenye ufungaji wa mabomba ulisababisha kuvuja kwa mafuta, Shell imeendelea kusisitiza kwamba sehemu kubwa ya uharibifu wa mazingira nchini Nigeria husababishwa na hujuma dhidi ya mabomba hayo, uchimbaji haramu wa mafuta na majaribio ya wizi.