Menu
RSS

 

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

 

BARAZA la Maaskofu Katoliki Afrika Kusini (SACBC) limevipongeza vyama vya siasa nchini humo kwa jinsi vilivyopokea na kukubali matokeo ya uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.

 

Pongezi hizo zimo kwenye Waraka wa Kichungaji uliotolewa na SACBC kufuatia utulivu uliooneshwa na vyama vyote vya siasa nchini humo baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

 

Katika waraka huo, Maaskofu walisema, wamefurahishwa kwa namna vyama vya siasa vilivyopokea na kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo kisha uliofanyika uliofanyika Agosti 3, 2016 na kuridhia kuwa ulikuwa huru na wa haki.

 

Walisema, kitendo kilichooneshwa na vyama vya siasa katika uchaguzi huo kinadhihirisha kukomaa kwa demokrasia na kwamba huo ushindi kwa demokrasia yenyewe.

 

“Kitendo kilichooneshwa na vyama vya siasa katika uchaguzi huu kinadhihirisha kukomaa kwa demokrasia na kwa kweli huu ni ushindi kwa demokrasia yenyewe” walibainisha Maaskofu katika waraka wao huo.

 

Walisema, uchaguzi huo unatakiwa kutamalaki katika awamu mpya ya historia ya demokrasia nchini Afrika Kusini ukihusisha Serikali ya Mseto, upinzani wa kweli wa kisiasa na uwajibikaji mkubwa katika matumizi ya madaraka.

 

Waraka huo ulieleza kuwa uchaguzi huo umeonesha kupungua kuungwa mkono kwa chama tawala cha African National Congress (ANC), kilichokuwa kikihodhi siasa za nchi hiyo, na hiyo ni dalili kuwa wananchi wana hamu ya kuona mabadiliko yakitokea.

 

Maaskofu walisema, katika uchaguzi huo, wananchi wamezungumza kwa kura, wameonesha kuwa wanahitaji mabadiliko, wanataka huduma na wamechoka na rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na hawataki kupuuzwa.

 

“Katika uchaguzi huo, wananchi wamezungumza kwa kura, wameonesha kuwa wanahitaji mabadiliko, wanataka huduma na wamechoka na rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na hawataki kupuuzwa” walibainisha Maaskofu.

 

Katika uchaguzi huo, vyama vya upinzanai vya Democratic Alliance (DA) na the Economic Freedom Fighters, vilionesha upinzani mkubwa kwa ANC kiasi cha kupoteza umeya katika Jiji la Johannesburg.

 

Pakistan yateua Waziri Mkatoliki kuimarisha uhusiano

 

 

 

KARACHI, Pakistan

 

MJUMBE wa Baraza la Mawaziri wa Jimbo la Sindh nchini Pakistan, Anthony Naveed, amepandishwa hadhi kuwa Msaidizi Maalum wa Waziri Mkuu akipewa jukumu mahsusi la kusimamia ofisi ya maelewano kati ya dini mbalimbali. 

 

Naveed anakuwa mjumbe wa kwanza Mkatoliki kutoka Sindh kufikia wadhifa huo na anakuwa Mkatoliki pekee kwenye Baraza la Mawaziri la Waziri Mkuu Syed Murad Ali Shah.

 

Akizungumzia uteuzi huo, Naveed, anayetoka Chama cha Watu wa Pakistan (Pakistan People’s Party), alisema, atatumia nafasi aliyopewa kuimarisha maelewano kati ya watu wa Dini mbalimbali katika nchi hiyo inayokabiliwa na misimamo mikali ya imani.

 

Alisema, tangu mwaka 2012, Serikali katika Jimbo la Sindh imekuwa ikijitahidi kupigania maelewano kati ya Dini mbalimbali na kujenga jamii yenye kuvumiliana kwa watu wenye tofauti ya Dini, imani na madhehebu.

 

“Tangu mwaka 2012, Serikali yao katika Jimbo la Sindh imekuwa ikijitahidi kupigania maelewano kati ya Dini mbalimbali na kujenga jamii yenye kuvumiliana kwa watu wanaotofautiana kwa Dini, imani na madhehebu” alisema Naveed.

 

Alisema, ilikuwa kazi ngumu na haikuwa rahisi wala mchezo kuwakusanya na kuwaweka pamoja watu wa Dini na imani tofauti lakini jambo hilo limefanyika kwa mafanikio katika Jimbo la Sindh.

 

Naveed alisema, hatua inayofuata sasa ni kuandaa warsha na semina kwa ajili ya viongozi wa Dini wa madhehebu mbalimbali na kuunda vikundi katika ngazi ya wilaya ili kuwezesha kuwepo kwa maelewano ya kidini katika ngazi ya chini.

 

“Hatua inayofuata sasa ni kuandaa warsha na semina kwa ajili ya viongozi wa Dini wa madhehebu mbalimbali na kuunda vikundi katika ngazi ya wilaya ili kuwezesha kuwepo kwa maelewano ya kidini katika ngazi ya chini” alibainisha Naveed.

 

Naveed amekuwa mtetezi wa haki za binadamu wa aina ya pekee mwenye rekodi ya pekee katika jitihada za kulinda na kutetea haki za Wakristo nchini Pakistan.

 

Akiwa mwanasiasa, Naveed aliyekuwa pia mwanachama mkereketwa wa Tume ya Vijana Wakatoliki katika Jimbo Kuu Katoliki la Karachi kati ya mwaka 1998 na 2005, amejitesa kuhakikisha Wakristo walio wachache wanapata haki za msingi za kikatiba katika nchi hiyo yenye Waislamu wengi.

 

Kanisa lanusurika kulipuliwa

 

 

 

JAKARTA, Indonesia

 

JENGO la Kanisa Katoliki la Parokia moja nchini Pakistan limenusurika kulipuliwa baada ya milipuko aliyokuwa nayo mlipuaji wa kujitoa mhanga kushindwa kulipuka.

 

Msemaji wa Polisi nchi humo, Meja Jenerali Boy Rafli Amar alisema kuwa mlipuaji huo wa kujitoa mhanga aliingia na milipuko hiyo kanisani wakati kukiwa na umati mkubwa wa waamini walikokusanyika kwa ajili ya ibada ya Misa ya Dominika.

 

Meja Jenerali Amar alisema, mtu huyo kabla ya kutaka kufanya tukio hilo, Jumapili Agosti 28, 2016, alidhibitiwa ingawa alifanikiwa kumjeruhi Padri aliyekuwa akiadhimisha Misa Takatifu.

 

Alisema, tukio hilo lilifanyika wakati ibada ya Misa Takatifu ikiendelea katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu lililopo Medan, Mji Mkuu wa Jimbo la Kiserikali la Sumatra Kaskazini.

 

Meja Jenerali Amar alisema, wakati wa ibada hiyo, kijana mwenye umri wa miaka 17 anayejulikana kwa jina la Ivan Armadi Hasugian alisimama kwenye benchi alipokaa na kukimbilia altareni alikokuwa Padri.

 

Hata hivyo, Meja Jenerali Amar alisema, mabomu aliyokuwa nayo kijana huyo kwenye begi la mgongoni alilobeba yaliungua bila kulipuka kama ilivyokusudiwa.

 

“Hata hivyo, mabomu aliyokuwa nayo kijana huyo kwenye begi la mgongoni alilobeba yaliungua bila kulipuka kama ilivyokusudiwa” alisema Meja Jenerali Amar.

 

Alisema, kabla ya kudhibitiwa na waamini, kijana huyo alichomoa shoka alilokuwa nalo kwenye begi lake hilo na kumjeruhi mkononi, Padri Mwadhimishi Misa Albert Pandiangan mwenye umri wa miaka 60. 

 

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Usalama, Wiranto, aalisema, upekuzi uliofanywa katika simu aliyokutwa nayo kijana huyo, limo jina la Abu Bakr al-Baghdadi, kiongozi wa Kundi la Islamic State (IS), la Mashariki ya Kati.

 

Wiranto alisema, kijana huyo aliwaambia polisi waliokuwa wakimhoji kwamba yeye hayupo peke yake bali anafanyakazi na watu wengine ingawa hakutoa maelezo zaidi.

 

Masista wa Mama Teresa au Wamisionari wa Upendo

 

 

 

CALCUTTA, India

 

WAKATI Mwenyeheri Mama Teresa wa Calcutta akitangazwa kuwa Mtakatifu Jumapili Septemba 4, 2016, Dominika ya 23 ya Mwaka C wa Kanisa, Masista wa shirika alilolianzisha la Wamisionari wa Upendo {Missionaries of Charity}, wamemshukuru kwa kuanzisha shirika hilo.

 

Pongezi hizo zilitolewa na Mama Mkuu wa Shirika aliyechukua nafasi ya Mama Teresa, Sista Prema Pierick, alipokuwa akizungumzia namna Masista wa shirika hilo wanavyojivunia kazi iliyofanywa na mwanzilishi wao.

 

Sista Prema aliyekutana na Mama Teresa kwa mara ya kwanza miaka 36 iliyopita mnamo mwaka 1980, alisema, Mama Teresa ni kielelezo muhimu cha utendaji kazi katika shirika lao na Kanisa.

 

Alisema, Mama Teresa katika utume wake na katika maisha yake yote alijitoa kwa moyo wake wote kuwasaidia maskini kati ya maskini waliokithiri kwa umaskini.

 

Sista Prema alisema, utakatifu wa Mama Teresa umemfanya yeye na watawa wengine wa sshirika lao kujiona kuwa wakati wote mama huyo yupo pamoja nao katika utume wao.

 

Alisema, waliishi na Mama Teresa na kuichukulia hali hiyo kama ya kawaida na kujiona kwamba wakati wote mama huyo yupo pamoja na watawa na kuwasikiliza kwa makini.

 

“Tuliishi na Mama Teresa na tunaichukulia hali hii kama ya kawaida na kujiona kwamba wakati wote mama huyu yupo pamoja nasi na kutusikiliza kwa makini” alibainisha Sista Prema.

 

Alisema, wakati wa uhai wake, walifurahia uwepo wake na walitaka kufahamu kutoka kwake namna siku yake ilivyokuwa kila siku na namna alivyofanya kazi zake.

 

“Wakati wa uhai wake, tulifurahia uwepo wake na tulitaka kufahamu kutoka kwake namna siku yake ilivyokuwa kila siku na namna alivyofanya kazi zake” alisema Sista Prema.

 

Mama Teresa wa Calcutta alitangazwa kuwa Mwenyeheri, miaka sita baada ya kufariki dunia akiwa na umri wa miaka 87 na aliyekuwa Baba Mtakatifu wakati ule, Mtakatifu Yohana Paulo II, Oktoba 19, 2003.

 

back to top
Tumaini Media

Radio-TV Tumaini, also trading as Tumaini Media, is legally registered in Tanzania under the Business Registration and Licensing Agency (Brela), No 116952. It is a registered Tax payer with TIN 100-251-094 and VRN 10-012753-P. Tumaini Media runs radio and TV stations, and a newspaper namely Radio Tumaini, Tumaini Television and Tumaini Letu, respectively. Tumaini Media seeks to serve the Tanzania community regardless of their colour. race. religion and tribe.

  Jesus is the Patron of our Station

We Now Covering 7 Regions

Coverage has been expanded to include seven out of 21 regions of Tanzania, thus: Tanga, Pwani, Morogoro, Zanzibar, Dar es Salaam and some areas of Dodoma, Kilimanjaro, Iringa and Mbeya Regions.